Siku moja kabla ya uchaguzi wa Septemba 22, 2022 wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania, nilipata taarifa za kushangaza kwangu kuhusu kile ambacho kingeenda kutokea bungeni mjini Dodoma kesho yake.

Niliambiwa kwamba aliyekuwa mgombea kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Mashaka Ngole, alikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kumshinda aliyekuwa mgombea kutoka Chama cha ACT Wazalendo, Ado Shaibu. Nilishangazwa na taarifa hizo kwa sababu zilikuwa kinyume cha kile kilichokuwa kichwani kwangu.

Niliamini katika mambo makubwa mawili niliyodhani yanampa Ado nafasi kubwa zaidi. Kwanza uhusiano “mzuri’ kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK). Kwa kawaida, katika mambo yenye maslahi ya kitaifa, Wazanzibari hupiga kura ya pamoja (block vote). Kwa dhania yangu kuwa hali ni shwari baina ya ACT Wazalendo na CCM, nikadhani Ado atapata kura za jumla kutoka wabunge wote wa CCM Zanzibar.

Dhana ya pili ikawa kwamba kama CCM Zanzibar haina shida na Ado, CCM Bara haitakuwa na sababu ya kuwa na shida naye. Kubwa zaidi, niliamini kwamba katika siasa za Tanzania za sasa, ACT Wazalendo – hasa kupitia Kiongozi wake, Zitto Kabwe, kimefanya makubwa kusaidia uwepo wa utulivu wa kisiasa nchini baada ya vifo vya vinara wawili wa siasa wa vyama hivyo – hayati Rais John Magufuli na hayati Maalim Seif Shariff Hamad.

Kifo cha ghafla cha Magufuli kilisababisha nchi kuingia katika mazingira ambayo haikuwahi kuyapita, yaani ya kufanya mabadiliko ya Rais bila uwepo wa Rais anayemaliza kipindi chake. Na kwa sababu ya ukweli kwamba Rais Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani katika wakati ambapo kulikuwa na uhusiano mbovu zaidi kuwahi kutokea nchini baina ya chama tawala na vile vya upinzani, kulihitajika upinzani ulio tayari kwa maridhiano ya kisiasa.

Naamini kuwa kama kuna kiongozi wa upinzani na chama kilichobeba ajenda hiyo ya maridhiano basi ACT Wazalendo na Zitto pengine wamefanya makubwa zaidi kuliko vyama vingi vilivyopo nchini – kuliko hata CCM yenyewe. Kifo cha Maalim Seif kingeweza kutikisa Maridhiano ya Zanzibar lakini Zitto na wenzake ndani ya ACT Zanzibar wameendelea palepale alipoachia Mwenyekiti huyo za zamani wa chama hicho. Kwa sababu ya vitendo hivyo vya Zitto na ACT, nikajenga imani kwamba CCM wanaweza kumpa mgombea wa chama hicho kiti kwa sababu – katika muktadha wa siasa za Bara na Zanzibar kwa sasa – pengine ACT Wazalendo ni muhimu kwao kuliko vyama vingine.

Mchana ule wa Septemba 22, nikapigwa na bumbuwazi. Mwenendo wa kura ulionesha kwamba Ngole atashinda kwa kura nyingi – kwamba angezidi kwa mbali mno kiasi kwamba kusingekuwa hata ana ushindani mkali. Nini kimeleta matokeo haya? 

Hali si shwari Zanzibar
Katika mazungumzo na vyanzo vyangu ndani ya CCM, nilibaini kwamba hali ya uhusiano ndani ya SUK baina ya vyama washirika si nzuri. Kabla ya uchaguzi, CCM Zanzibar ilishaamua kwamba haitompa kura mgombea kutoka chama cha ACT.

Mgombea ambaye CCM Zanzibar ilimtaka ni Habibu Mnyaa kutoka chama hicho hicho cha CUF. Bahati mbaya ni kwamba inaonekana uhusiano baina ya Mnyaa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, umelegalega na hivyo bingwa huyo wa uchumi alikuwa anataka Ngole ndiye apate nafasi hiyo.

Kwa nini hali si shwari Zanzibar? Ninafahamu sasa kwamba mambo mawili yamechangia; mosi, ni namna baadhi ya viongozi mashuhuri wa ACT Wazalendo wanavyoikosoa SMZ hadharani na kuipunguzia umaarufu CCM. Wahafidhina ndani ya CCM wanataka ACT Wazalendo isiseme mabaya yake hadharani – jambo ambalo viongozi wa upinzani hawalitaki; na Ismail Jussa Ladhu, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT, amewahi kuzungumzia hili hadharani kwamba wataendelea na ukosoaji.

La pili linahusu hofu ya kuipa nguvu ACT Wazalendo kama mpinzani pekee wa CCM Zanzibar. Mazungumzo yangu na marafiki zangu wa Zanzibar yananipa picha kuwa kuna mkakati wa kuiongezea nguvu CUF hasa Zanzibar ili kigawe kura za upinzani Zanzibar – hasahasa Pemba. Ndiyo sababu, kwa CCM Zanzibar, mgombea mwafaka alikuwa Mnyaa kutoka Pemba.

Kwa wasiofahamu, katika miaka mitano ya maisha ya mbunge wa EALA, mapato yakeyanaweza kufikia wastani wa takribani dola 700,000 (zaidi ya shilingi bilioni 1.5 za Tanzania). Kama mgombea kutoka Pemba kama Mnyaa angeamua kuwekeza dola 200,000 tu (takribani shilingi milioni 450), kiasi hicho kingefanya ‘fujo’ nyingi katika eneo kama Pemba ambapo CUF ingali ina ufuasi.

Nikimnukuu kiongozi mmoja wa CCM Zanzibar; “Wanaopenda ACT wana mapenzi na chama chao, waliopenda ile CUF ya zamani ya akina Maalim Seif, wao walikuwa na mahaba na chama chao”. Kwa hiyo, njia inayotafutwa Zanzibar ni kukuza nguvu ya CUF ili kuikata makali ACT na mojawapo ya njia ilikuwa ni kumnyima kura mgombea wa ACT EALA.

Zanzibar ikitaka lake inapata
Nimekuwa nikiandika mara kwa mara kwamba kinyume cha mtazamo wa wengi, mara nyingi CCM Zanzibar imekuwa ikitaka jambo wakati linapoletwa kwenye Muungano hasa kama haliingilii maslahi mengine ya Tanzania Bara.

Nimekuwa nikitoa mifano ya namna CCM Zanzibar ilivyomkataa Dk. Salim Ahmed Salim hata kama alikuwa chaguo la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kumrithi kama Rais wa Tanzania mnamo mwaka 1985. Nimekuwa nikitoa mfano wa namna jina la CCM lilivyoingia neno Mapinduzi ingawa huku Bara hakukuwa na mapinduzi bali Zanzibar.

Hata kuondolewa kwa Aboud Jumbe Mwinyi kama Rais wa Zanzibar mwaka 1984 kulikuwa ni kwa sababu ya taarifa zilizotoka Zanzibar kwenyewe – kutoka kwa wale waliokuwa hawafurahishwi na vitendo na CCM Bara iliingia kuzifanyia kazi taarifa zilizoletwa na Wazanzibari wenyewe.

Kama Ado Shaibu hakuwa anatakiwa na CCM Zanzibar, ilikuwa wazi kuwa asingeweza kukubaliwa na CCM Bara hata kama angefanya kampeni nzuri kiasi gani au angezungumza kwa ushawishi mkubwa kiasi gani mbele ya wapiga kura wabunge.

Kuhusu Ado na Mashaka Ngole
Kuna msemo wa Waswahili wa Dar es Salaam kwamba wakati unapomsifia mwizi kwa mbio, unatakiwa pia kumsifia na anayemkimbiza. Itakuwa ni mapungufu ya kiuchambuzi endapo sitazungumzia kuhusu uwezo wa Ngole.

Inawezekana Ngole si maarufu miongoni mwa wengi mitandaoni na kwa wanaofuatilia taarifa kwenye vyombo vya habari. Ado ni mashuhuri kwa sababu ni Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo na ana matukio mengi ya kuandikwa.

Nguvu kubwa ya Ngole ilikuwa ni kufahamiana na wabunge wengi wa CCM kutokana na kazi zake za kisheria. Ngole pia ni mpambanaji na ninafahamu wajumbe ambao yeye mwenyewe alifunga safari kuwafuata majumbani kwao kuwashawishi wampe kura.

Hata kwenye mazungumzo ya kuomba kura, alijieleza vizuri na kuonesha ni mtu aliyejiandaa kwa muda mrefu kupata nafasi hiyo. Ado alijieleza vema pia lakini nguzo kuu yake aliyoitegemea ilihusu mahusiano yake na wanasiasa wanataaluma kama Spika Tulia Ackson na wabunge kama Palamagamba Kabudi na Bashiru Ally, aliowahi kufundishwa au kufanya nao kazi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Hata hivyo, kama Ado angeandaliwa vizuri zaidi, maombi yake ya kura kwa wajumbe yangejikita kwenye kuwafanya wabunge wa CCM waone haya kumnyima kura – kwa kuzingatia uhusiano wa vyama hivyo viwili katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Huenda asingeshinda kwa sababu hiyo lakini angeweza kupenyeza ujumbe muhimu kwa wapiga kura na jamii ya Watanzania kwa ujumla. Hata hivyo, kama nilivyosema awali, inaonekana hata kama angezungumza kwa kutoa hoja nzito na muhimu tupu, bado ungebaki kuwa uchaguzi ambao angeshindwa.

Kuelekea 2025
Kuna dalili zote kwamba SUK bado haijamaliza kutoaminiana na tofauti za kimsingi baina ya CCM na ACT Zanzibar. Matokeo ya uchaguzi wa EALA yanatoa picha kwamba uchaguzi ujao wa Zanzibar hautakuwa tofauti na ‘chaguzi’ nyingine zilizopita.

Jambo pekee ninaloliona sasa ni kwamba kama ACT Wazalendo walikuwa wameanza kufikiri kushambulia kwa kutumia glovu za mabondia, sasa wana sababu ya kuzivua na kuanza kupiga kavukavu. Kama CCM imewawekea ngumu kwenye EALA, ACT Wazalendo haitakuwa na sababu ya kutoyapigia kelele yale wanayoona hayaendi sawa serikalini.

Ndiyo kile ambacho huandikwa kuwa; kama mmemwaga ugali, sisi tutamwaga mboga. Baada ya Katibu Mkuu wa chama chake kuzidiwa kwa kura zaidi ya 100 kwenye uchaguzi na mgombea kutoka chama kinachoonekana kiko chini yake kwenye umashuhuri, simwoni Zitto akipiga kelele za maridhiano ndani ya Zanzibar.

Kama ulikuwa umefichika, ufa sasa umeonekana miongoni mwa vyama washarika katika SUK Zanzibar. Ufa huu unaweza kuzibwa kisiasa mapema kabla ya 2025. Lakini kama utaachwa, naona dalili ya kujenga ukuta mzima kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.