Kuna msemo mmoja mashuhuri wa wahenga wetu kwamba kwenye mafanikio ya mwanamume, kuna mwanamke pembeni yake. Kama kuna mahali msemo huu umesadifu ukweli huu, basi ni kuhusu maisha ya aliyekuwa pengine bilionea maarufu zaidi nchini Tanzania, Reginald Abraham Mengi na mkewe wa kwanza, Mercy Anna Mengi.

Wawili hao sasa wametangulia mbele ya haki. Mercy alikuwa wa kwanza kufariki dunia mnamo Oktoba 31, mwaka 2018 na aliyekuwa mumewe akafuatia miezi sita tu baadaye yaani Mei 2, 2019. Kwa sababu ya tabia zao tofauti, Mengi alikuwa mtu mashuhuri na sura yake ikijulikana na karibu kila mtu mzima Mtanzania aliyejua kusoma na kuandika au angalau kumiliki televisheni – lakini mkewe Mercy hakuwa maarufu kwa sababu ya tabia yake ya kupenda kufanya mambo yake mbali na kamera za waandishi wa habari.

Matokeo ya tofauti hizi za kitabia ni kwamba Mercy alipofariki dunia alikuwa hajulikani na wengi zaidi ya wale waliowahi kuguswa na maisha yake moja kwa moja iwe kwa kufanya naye kazi, kuishi katika jumuiya moja au kufanya shughuli zinazofanana.

Hadithi ya maisha ya Mercy na Reginald Mengi ni hadithi ya maisha ya wanaume wengi waliofanikiwa kwenye maisha yao. Tatizo kubwa ni kwamba jamii zetu huwa hazina tabia ya kuonesha upande wa pili wa maisha ya wenza waliofanikiwa. Leo, takribani miezi miwili kabla ya maadhimisho ya miaka minne ya kifo cha Mercy Anna Mengi, pengine huu ni wakati wa kuangalia nafasi yake – na kwa kioo hicho, kuwasilisha ukweli halisi katika jamii yetu kuhusu nafasi ya wenza hususan wanawake katika mafanikio yao kama washirika kibiashara.

                       (From Humble Roots – https://reginaldmengi.com/biography/)

Hapo mwanzo, Mengi hakuwa bilionea
Mengi na Mercy walioana Novemba 27, mwaka 1971. Wakati huo, Mengi hakuwa maarufu nchini wala hakumiliki mali. Ndiyo kwanza alikuwa amerejea nchini baada ya kumaliza masomo yake ya uhasibu huko Uskochi na kipindi kifupi cha kufanya kazi nchini Uingereza. Mercy tayari alikuwa ameajiriwa katika lililokuwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (East Africa Airways).

Kimsingi, wakati huo, ungeweza kusema Mercy alitoka ‘matawi ya juu’ kumzidi Mengi maana alizaliwa kwenye koo za kichifu katika jamii ya Wachaga. Mercy ni mtoto wa Chief Abdiel Shangaliwa Machame. Mengi alizaliwa katika familia ya kawaida na kwa maana hiyo, ndoa yake na Mercy ilimfanya kuwa mmoja wa wanafamilia katika mojawapo ya koo mashuhuri katika jamii yake.

Ingawa Mengi hakuwa na damu ya kichifu, lakini alikuwa mtu mwenye akili na maarifa. Wakati akimaliza masomo yake ya uhasibu ughaibuni, Tanzania haikuwa na wahasibu wengi wa hadhi yake. Kama angetaka, angeweza kubaki Uingereza na kufanya kazi huko lakini aliamua kurejea nyumbani alikoona kuna fursa zaidi.

Simulizi za watu waliowafahamu wawili hawa tangu wangali vijana, zinaeleza kuhusu wapenzi waliotengeneza ‘kombinesheni’ ya kipekee. Mengi alikuwa mchapakazi, mwenye maarifa na mpambanaji huku Mercy alikuwa mwenye maono, mchapakazi, msimamizi, mlezi na aliyekuwa tayari kufanya maamuzi magumu ikibidi.

Si wengi wanaofahamu kwamba ni Mercy aliyekuwa wa kwanza kukubali kuacha ajira yake kwenye shirika la ndege ili kuanzisha na mume wake na kusimamia biashara ya familia.  Na ingawa Mercy aliamua kuacha kazi ili ajikite zaidi huko, walikubaliana Mengi aendelee na ajira.

Biashara ya kwanza kwa familia ya Mengi – iliyokuja kuwa msingi wa mafanikio yao yote yaliyofuata – ilikuwa ni ile ya kutengeneza kalamu. Biashara hiyo ilianzia sehemu ya kula chakula (dining room) nyumbani kwao, Upanga jijini Dar es Salaam, kwa vile hawakuwa na uwezo wa kumiliki ofisi wakati huo.

Kazi ya kutengeneza kalamu wakati huo haikuwa rahisi kama ilivyo sasa. Waliowafahamu miaka hiyo walishuhudia jinsi ilivyolazimu kuingiza wino katika bomba la ndani la kalamu moja moja kwa kutumia aina fulani ya sindano. Hatua hiyo ilifuatiwa na kuingiza bomba la wino ndani ya kasha la kalamu, kufunga ncha ya mbele na vizibo vyake. Kazi hiyo ilifanywa kwa kalamu moja baada ya nyingine hadi boksi zima la kalamu likamilike.

Mercy aliamua kufanya uamuzi mgumu wa kuacha ajira yake ili aweze kutunza familia changa, ikiwa ni pamoja na mume wake, na kufanya kazi hizo za kufunga kalamu na kushughulikia mambo mengine ya biashara yao kama kupokea mizigo inapoagizwa, mambo ya benki, na kadhalika. Wakati Mengi akiwa kazini na watoto shuleni, jukumu lote hilo lilimwangukia Mercy.

Kuondoa miaka ya baadaye wakati walipopata uwezo wa kuajiri watu wa kuwasaidia kazi, shughuli hiyo ya kufunga kalamu ilikuwa ikifanywa wakati wote na Mercy peke yake.  Mengi aliungana na mkewe kwenye jukumu hilo jioni alipotoka kazini. Watoto wao; Regina na Rodney Mutie ambao walikuwa wangali wanasoma shule ya msingi walifundishwa kazi na kushiriki kidogo walipotoka shule mchana.

Katika kitabu cha historia ya maisha ya Mengi kiitwacho I Can, I Must, I Will kilichotolewa mwaka mmoja kabla ya kifo chake, tajiri huyo alieleza kwamba ni kwa kupitia biashara hiyo ndipo walipotengeneza zaidi ya shilingi bilioni moja. Jambo moja la kuzingatia hapa ni kwamba ni Mercy ndiye aliyekuwa akifanya shughuli hizo tangu awali, kwa muda mwingi zaidi na pia ndiye aliyefanya maamuzi magumu ya kuacha kazi ya kuajiriwa!

Pamoja na mafanikio hayo, bado Mengi aliendelea na ajira yake kwenye moja ya kampuni mashuhuri za kimataifa za ukaguzi wa kihasibu.

Mmoja wa marafiki wa karibu wa Mzee Mengi aliyezungumza nami miezi michache baada ya msiba wake alinieleza kwa mara nyingine kuwa Mercy ndiye alimshawishi Mengi kuacha ajira yake katika kampuni iliyokuwa inajulikana kama Coopers & Lybrand (na sasa inaitwa PricewaterhouseCoopers [PwC]) ili kuongeza nguvu kwenye biashara zao.

Hatimaye Mengi alisikiliza ushauri wa mkewe na kuacha kazi ili kuendeleza makampuni na biashara za familia. Biashara hizo ni kama Anche Mwedu – kiwanda kilichokuwa kinatengenza sahani na vikombe. Kampuni ya IPP ilizinduliwa rasmi, na waliunganisha nguvu ya biashara na makampuni ya awali na kuendeleza uanzishwaji wa makampuni mengine vikiwamo vyombo vya habari kama runinga za ITV na EATV na magazeti ya The Guardian na Nipashe.

Baada ya Mengi na mkewe kuingia kwenye biashara kwa miguu yote miwili, huo ndiyo ukafungua milango ya utajiri mkubwa kiasi cha kwamba kufikia katikati ya miaka ya tisini, Mzee Mengi, aliyekuwa Mwenyekiti wa makampuni ya IPP alikuwa akionekana kama Mtanzania mweusi mwenye ukwasi zaidi nchini kwake kuliko wengine.

Mercy aliendelea kubaki kwenye kivuli cha mumewe. Tabia ya Mercy ya kutotaka kutajwa au kutangazwa ilikuwa ikijulikana hadi kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Azania Front alikokuwa akisali. Wakati wa ibada ya msiba wake iliyofanyika kanisani, baadhi ya waombolezaji walikumbusha kuhusu mambo mawili aliyokuwa akijulikana nayo mke huyo wa kwanza wa Mengi.

Mosi, wakati wa Sikukuu za Mavuno, siku ambayo waumini huwasilisha sadaka zao za mavuno na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Mercy alielezwa kushiriki bila kuwa na mbwembwe wakati wa minada iliyokuwa ikifanyika kanisani. Hata hivyo, lililokuwa linajulikana kwa viongozi wa Kanisa ni kuwa yeye alikuwa akiwasilisha sadaka yake mapema bila watu kujua. Mchango wake alitaka uwe siri yake na Mungu wake.

Jambo la pili ambalo waumini walisema wanakumbuka ni tabia yake ya kutopenda ‘kujionesha’ kama kukaa kwenye viti vya mbele. Pamoja na umaarufu wake kama mke wa mfanyabiashara tajiri – huku naye tayari akiwa ana ukwasi wa kutosha, Mercy alipenda kukaa kwenye viti vya nyuma na usingeweza kumbaini kwamba ni mtu wa daraja tofauti.

Naamini kwamba kama ilivyokuwa kwa kitabu cha mumewe, kuna siku tutasoma historia kamili ya Mercy Mengi kupitia maandishi ili mchango wake naye uweze kutanabaishwa bayana. Watanzania na wengine waliosoma kitabu cha Mengi wamepata upande mmoja tu wa shilingi kwa sababu kwa bahati mbaya kitabu hakikueleza sana kuhusu uhusiano wa utajiri wao na ushiriki wa kila mmoja wao katika kutafuta na kumiliki mali zote walizochuma pamoja.

Itakuwa si haki iwapo kumbukumbu pekee ya Mama Mercy itahusu mambo mengine yaliyotokea katika uhusiano wake na mumewe huyo kwa kuwa historia hiyo inadogosha mchango mkubwa wa mwanamama huyu katika utajiri wa familia yake na mumewe.

Bahati mbaya ni kwamba hadithi hii ya Mercy Anna Mengi ni hadithi ya wanawake wengi katika historia ya bara la Afrika. Ukisoma historia ya viongozi wakubwa na makubwa yao – kwa kiasi kikubwa, utasoma historia ya wanaume.

Kama ukitazama orodha ya mabilionea na mamilionea wa Afrika, utakachoona ni utajiri wa wanaume na hakuna maelezo yoyote kuhusu wake zao. Kama utasikia habari za wanawake wa watu mashuhuri, utakachosikia zaidi ni habari kuhusu wanavyopenda maisha ya anasa, wasivyojua kutafuta pesa na pengine migogoro ya mali baada ya vifo vya waume zao.

Ukizungumza na watu binafsi na taasisi ambazo zilifaidi misaada ya Mercy Mengi wakati angali hai, utapata picha ya watu wanaotamani mama huyo akumbukwe kwa kumcha Mungu, kwa upendo wake, kwa upambanaji wake, kwa malezi na kwa misaada yake. Pamoja na kulea watoto wake, alilea pia sehemu kubwa ya wanafamilia wa Mengi na wa Shangali katika kipindi chote cha uhai wake. Ukizungumza na wale waliosaidiwa naye, utaona matamanio yao ya kutaka shughuli alizokuwa akisaidia nje ya kamera za vyombo vya habari zisikome na badala yake ziendelee.