Labda wewe ni mmoja wa wengi ambao baada tu ya kusoma kichwa cha habari na jina la mwandishi, tayari hasira zimekupanda. Pengine unasoma haya makala siyo kwa sababu ya kutaka kujua kilichoandikwa, bali unasoma ili upate cha kukosoa na kunidogosha. Nikuombe ushushe pumzi! Kuwa mpole kidogo, ni vizuri kwa afya yako.
Alright! Najua wajua kuwa mijadala ya migogoro ya ndoa na ongezeko la talaka imeshika hatamu, huku waliojibatiza utaalam wa ndoa wakiwa busy kutoa uchambuzi na masomo kwa wanandoa hasa wanawake, na serikali ikianza kuhamasisha midahalo ya ndoa. Kwa baadhi yetu tunaona jambo hili linafanywa kuwa jipya ila si jipya. Labda ukubwa umeongezeka. Pengine watu wamekuwa wepesi kulizungumzia kuliko ilivyokuwa awali, lakini migogoro na kuvunjika kwa ndoa ilikuwepo na ipo.
Tuseme tu ukweli. Watu wanaumia kwenye ndoa jamani. Wanawake kwa wanaume.
Mpaka leo kuna familia kama mume mtarajiwa hana nyumba, hana gari, hana kazi nzuri, hawakubali aoe binti yao, hata kama wanapendana kiasi gani. Kaka zangu walio kwenye ndoa wanajua jinsi matarajio yalivyo makubwa. Kuwa mume bora ni kuwa na kipato kikubwa kuliko mume wa rafiki wa mke wako na kumpa mkeo, mashemeji na wakwe, kila wanachotaka hata kama hakipo kwenye uwezo wako.
Shida ya afya ya akili ni kubwa mno kwa ‘wakaka’. Hawasemi tu. Wanalazimika kufanya dili hatari. Wanaumizana kenye kutafuta kipato na ‘wanasnichiana’, ili mradi ‘makasiriko’ kama yote ili ndoa iende. Kimsingi, tumevurugwa.
Huku kwa dada zangu ndio mtume salale. Hakuliki wala hakulaliki. Tunastiriwa na make-up tu.
Ila kila mtu analia na lake. Huyu analia mume hana muda nae, kama hayuko safari kikazi, yuko baa na marafiki, akiuliza, anajibiwa, kwani umekosa nini? Yule analia mume hajigusi kwenye majukumu ya kifamilia kwa kuwa mke ana kipato kikubwa. Mke hakumbuki mara ya mwisho lini mume kumnunulia hata upande wa kanga, achia mbali kulipa ada au kununua bidhaa za nyumbani. Na akifungua mdomo kumuuliza anaambulia kipigo au matusi, eti anataka kumpanda kichwani mume kwa kuwa yeye ana hela kuliko mume.
Shangazi yangu mie analia machozi yasiyokauka. Kuamua kwake kuukimbia upweke na kuogopa dhambi ya kuzini kukamfanya akubali kuolewa mke mdogo sasa anafanywa mwizi wa penzi la Bi Mkubwa. Anajiona hana thamani na hastahili mapenzi wala faraja ya mume. Huo uadilifu unaosemwa haujui unafananaje.
Na jirani yangu anasema japo anafanya kazi ngumu na anachoka kama punda mbeba mizigo jangwani inabidi akirudi apike, afue n.k maana alishamfumania mumewe na mdada wa kazi. Tena mume akamkanya eti kama hatatimiza majukumu yake, ataoa dada wa kazi. Aibu ya kuolelewa dada kazi bora akomae na kufua majeans.
Halafu kuna wakina sie – Wasimbe.
Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa shida zote hizi zinakuja kwa sababu tumekataa kabisa kubadilisha taasisi ya ndoa, mfumo na matarajio ya wanandoa. Mpaka leo tunataka kuishi, kama wahenga walivyoishi kwenye zama za mawe za kale. Tunakwama. Ndoa zinakosa maana.
Zama hizo walizoishi wao waliyofanya yali-make sense. Kwa mfano, japokuwa wanadini wanaamini ndoa ilianza na Adam na Hawa/Eva, wataalam wa historia na sayansi ya jamii watakwambia ndoa kama taasisi ilianza pale ambapo jamii zilianza kukaa pamoja na kumiliki Rasilimali. Kabla ya hapo, kwa mujibu wa wataalam hao, watu walikuwa wanajamiiana ila si kwa taratibu za kindoa kama tunavyozijua sasa.
Enzi zile upatikanaji wa mali ulitokana na uwezo wa watu kutumia nguvu, iwe kuwinda, kutengeneza zana (za mawe au chuma), kulima, kuvua n.k. Wanafamilia wenye nguvu kazi kubwa (watu wengi) walikuwa na uwezo mkubwa wa kufanikiwa zaidi. Kutokuwepo na mbinu za uzazi wa mpango kuliwafanya wanawake wengi, wawe aidha wana mimba au mtoto mchanga muda wote. Si mnaujua ule msemo wa ‘masika mimba, kiangazi mtoto’? Ewaaa, ndivyo ilivyokuwa!
Na hapo ndipo mgawanyo wa majukumu ulipotokea na shughuli na tamaduni za kuozeshana zilipoanza. Wanawake wakitolewa mahari ili wawe wazalishaji wa nguvukazi (watoto). Nguvukazi hiyo ilipewa ubini wa baba au wajomba kama alama ya umiliki. Pale ambapo walizaliwa watoto wa kike, basi baba au mjomba alipokea ‘mali’ (mahari) na kuwatoa mabinti zake wakazalishe nguvukazi kwenye jamii nyingine.
Uhitaji wa nguvukazi kubwa kwa haraka ulilazimisha wanaume waoe wake wengi. Ndoa za mitala zilikuwa ni jambo la kawaida kabisa. Kabla ya ujio wa dini zilizokataza au kuweka ukomo ya idadi ya wanawake wa kuoa, kwenye jamii nyingi za kale ukomo wa idadi ya wake ilitegemea ukomo wako wa kulipa mahari.
Katika jamii hizi, ndoa zilikuwa na kazi maalum, kuzalisha nguvu kazi, kuwa sehemu ya utambulisho wa mtu, kuwa taasisi ambayo mali na rasilimali zinamilika na kusaidia jamii kuendelea kwa maana ya mgawanyo wa kazi – pale ambapo wanaume walitoka kwenda kutafuta rizki, muda mwingine iliwachukua siku kadhaa, wanawake walibaki kijijini na kwa umoja wao wakilea nguvukazi na kufanya kazi za nyumbani ikiwa ni pamoja na kuzalisha chakula. Ndoa hazikuwa kuhusu mapenzi na mahaba, bali kutimiza mahitaji ya jamii (practical purposes).
Leo tuko mwaka 2022, tunausogelea mwaka 2023, rizki na mali kwa sehemu kubwa hasa huku mijini, hazitafutwi tena kwa kutumia nguvu na misuli, bali akili na maarifa. Maboresho katika sekta ya elimu na kupanuka kwa huduma za uzazi wa mpango kumeongeza ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za kiuchumi. Maendeleo ya teknolojia yameleta matarajio tofauti hasa kwenye sekta ya mahaba.
Ukuaji wa uchumi na kukua kwa miji kumevunja mshikamano wa Kijamii. Ubepari umeleta umimi na ubinafsishaji wa mali. Sasa mafanikio ya familia yanategemea zaidi ubora na si wingi wa wanafamilia. Katika muktadha huu tulitarajia kama jamii tuanze mchakato wa kubadilisha matarajio na labda mfumo wa ndoa.
Niliwahi kuongea na rafiki yangu mwanaume na kumuuliza kwa nini hataki kuoa tena baada ya kuachana na mtalaka wake? Jibu lake lilikuwa, “naogopa mgogoro wa mali, hiki nilichokichuma nataka kirithiwe na wanangu, ndoa zetu ni ‘all inclusive’, chake changu na changu chake, sasa kwa sisi ambao tuna watoto ukioa tena unatafuta majanga kuliko furaha.” Majibu yake yalinifanya nimvutie waya swahiba wangu, msimbe mwenzangu, nimpe hizi habari njema kuwa kuna wakaka ambao wanataka kuwa na mahusiano/ndoa ila wanaogopa migogoro ya mali, mana huyu swahiba wangu kila siku alikuwa anasema, yeye hafuati mali kwenye ndoa, ana zake. Kiherehere changu kilizimishwa na majibu yake mafupi ila mazito, aliniambia, “Mishy, wakaka wengi kama hao wako emotionally unavailable, wanataka tu kuwa na independent women but they have no idea, what to do with them.” Hapa alikuwa anamaanisha kuwa wanaume wa aina hiyo hawana muda wa kuwa pamoja na wewe vilivyo kihisia, wanataka tu kuwa na wanawake walio huru na wanaojitegemea lakini hawajui wafanye nini na wanawake hao wanapokuwa nao.
Kimsingi, alinieleza yeye anataka kuwa na mwenza atakayekuwa mwandani, msiri, na mfariji wake. Mwenza wa kumuonea huruma, wa kumtia moyo, wa kufurahi na kuhuzinika nae. Kwa kizungu tungesema soulmate maana kwa mujibu wake, japo anaweza kukimbizana na maisha, na anajua kuitafuta pesa haswa, ila kuna hitaji la moyo la kupendwa na kujaliwa.
Shida ni pale huyo mwenza, na jamii inayomzunguka, bado wanapokuwa na matarajio yaleyale ya mke wa zama za mawe za kale. Ndoa haitakuwa ‘yeye (mke) anataka nini’ bali ‘mume anataka nini’. Hakuna hata kauuchochoro ka kusema, basi tupange wote tunataka nini – utaambiwa wewe sio wife material, sio kama bibi zetu. Hawakumbuki kuwa bibi zetu hawaishi maisha yetu. Kigumu ni kipi hapo kuelewa?
Anyways, kwa hapa tulipofika, ndoa siyo tena sehemu ya kuanza au kupata maisha. Siku hizi wadada na wakaka wote wanaweza kuyatafuta maisha nje ya ndoa na wakafanikiwa. Siyo tena sehemu pekee ya kupata watoto maana zamani kuzaa nje ya ndoa dunia ingeweza kukumeza mzimamzima. Ila siku hizi wala. Mpaka baadhi ya makanisa yana utaratibu wa kurejesha watu kundini japo sijawahi kuona wakaka wanarejeshwa kundini kwa kuzaa nje.
Ndoa sasa zinaacha kuwa kipimo pekee cha mafanikio na heshima, japo ka-pressure bado kapo hasa kwa wadada. Ila nawajua wadada na wakaka wengi wanaoana ili ‘watoe nuksi’ basi ‘waridhishe wazazi’ na maisha yanaendelea kuwa bukheri baada ya talaka. Mjini wanasema heshima pesa, mengine yanaongeleka.
Maana pekee iliyobaki ni ya kiimani. Katika jamii zetu ambazo dhambi haziogopwi kivile tena, siku si nyingi maana hii nayo itapotea. Kama alivyoniambia kaka yangu senior bachela, kuliko kujibebesha stress za kuandaa harusi za gharama, kuishi maisha ya kuwafurahisha wakwe na kudeal na mke na shida zake, bora aendelee kuwa na rafiki tu, atatubu.
Kama kweli, tunataka ndoa ziendelee kuwepo, basi tuzitafutie maana mpya na mifumo mipya inayoakisi mahitaji ya wanandoa wa karne hii ya ishirini na moja. La sivyo tutaendelea kuhesabu talaka, single mothers and fathers na ongezeko la kutisha la ukatili wa kijinsi(a) pamoja na mauaji baina ya wenza. Ni muda sasa wataalam wa sayansi wa jamii kuanzia wanasosholojia hadi wanasaikolojia kufanya kazi yao ipasavyo au tuendelee kutia ndoa doa.
This is a best article for me to read in this year. Truth should be told. And we should all hear to understand not hear to reply. I love it sister.
very interesting views and opinion
Binti na vijana wa kiume wasome hii kabla au wakiwa ktk mahusiano.
True that, though missing some insights from the Law of Marriage Act of 1971 (URT)
Mdahalo mzuri Sana, nakuomba utafute tafsir ya Surat Ruum 30:21 Na baqrah 2:187. also look for ahadith of Rasul (saw) that says “the best among you are those who are good to their Ahl(family) stress in on wife. these will provide u a solid appreciation of the institution of marriage. in summary, the man has failed in his role of KAWAM. leadership
Inaelekea kuna Demokrasia kwenye taasisi ya ndoa kufuata Sera ya 50/50… Kiongozi anapigiwa kura sijui kwa namna gani maadam mko Wawili tu kwenye ndoa ♡
Ukweli huu ni mchungu sana ila ndio ukweli halisi taasisi hii inahitaji marekebisho makubwa ya kifikra na kisaikolojia. Huko mitaani hali ni mbaya na kibaya zaidi watu wanaona aibu kusema kwa hiyo wanaugulia ndani kwa ndani.
Wengi hawapendi kuusikia ukweli huu. Bitter truth da Mishy.
Kwa kweli hongera sana dada Mishy; nimependa udadafuzi wa ages na maana za ndoa kwayo. Naunga mkono mifumo ya ndoa tuliyonayo haiakisi maendeleo ya mwanadamu tuyaishiyo sasa. Kongole for a piece.
Mtume s.a.w ameshatufunda hzo ndoa unazozihitaji Leo hili ila wengi wetu hatuzifati.
Makala nzuri, umezungumzia hali halisi iliopo kwenye jamii inayotuzunguka. Jamii kiukweli ina matatizo yaliyo mengi na hivyo kupelekea mambo mengi kuharibika. Suluhisho pekee la matatizo haya ni watu kurudi katika mstari ulionyooka na mstari huo ni Dini ya Uislamu, vyenginevyo tutaendelea kupiga kelele mpka siku ya mwisho. Maharibiko haya yanaletwa na watu kuacha misingi na malengo ya kuumbwa kwao.!
Full package
This a close and candid ‘conjecture’. Naona umeongea vizuri sana kuhusu janga linaloikumba jamii yetu. Ukapapasa madhila yanayowakuta wanaume then ukajikita kwenye kusema yale yanayowakumba wanawake. Ninakuelewa. Katika jamii yetu, Tanzania, Afrika au kwengineko suala la wanawake kukatiliwa na wanaume limeangazwa kiasi kwamba yanayowakuta wanaume kwenye ndoa inapapaswa kama ulivyofanya hapa.
Matarajio ya jamii imekuwa jambo la kubadilika kwenye kila kizazi.
Kwenye misaafu ndoa ni sheria ya uumbaji (creation ordinance). Na misaafu tuliyo nayo haijatokana na mila na desturi za Kiafrika. Kwa Wakristo tunaamini sheria ya uumbaji kwa imani ya Wayahudi. Waislam kwa upande wao wanaamini sheria ya uumbaji kwa imani ya Waarabu. Mtazamo huu kwa wengi itakuwa usaliti au tusi kwa dini. Kuna mtazamo mwengine wa imani mambosasa (contemporary beliefs). Kwenye hili watu wnafanya wanafanya na kusema wanavyoona inastahili.
Kile ambacho hatujafanya kama jamii ya wanadamu ni kujiuliza misingi ya utu tumeacha wapi? Nani anapaswa kuwa au kuonesha utu kwa mwenzake? Kwa nini tumefika mahali hapa ambapo tunasema ndoa hazina maana? Au kusema kuna mila au dhana ndani ya jamii iliyopitwa na wakati? Kwa nini tukubali au kukataa mtazamo huu?
Ume simplify The Origin of family state and private property kwa lugha nyepesi kabisa. Na katika muktadha wa sasa,iwe kimila ama kupitia dini zetu mbalimbali kuna mambo basic tunafundishwa ila basi tu hatuyazingatii matokeo yake ndio hizi talaka,mafarakano,visas nk.
Makala nzuri na uandishi mzuri. Tujitafakari
Asante kwa makala yenye kufikirisha, “Ndoa Bado Zina Maana” (Tena sana), ndoa ni jambo jema sana kuwahi kutokea kwenye uhai na maisha ya mwanadamu, changamoto iliyopo ni ukosefu wa maarifa na matayarisho kabla kuingia kwenye mahusiano ya ndoa. Bila maarifa sahihi na matayarisho ni vigumu kuingia kwenye ndoa au mahusiano yoyote makini. Wengi wanaingia kwenye ndoa kwa kubahatisha huku wakitarajia automatically wapate matokeo mazuri, haiwezekani, lazima watakwama. Wengi wanaanguka kwenye ndoa na huishia kulalamika na kulaumu, lakini kiuhalisia hawana maarifa, hawana pa kushika, hawajui wafanyeje, ni sawa na mtu aliyepewa gari aliendeshe lakini limemshinda anabaki kulalamika kuhusu aina ya gari, barabara, nk. Kama umeshindwa kuendesha gari, unapaswa uende kujifunza kuendesha pamoja na kanuni zake na si kulalamika na kulaumu, vivo hivyo kabla au kama uko kwenye ndoa au mahusiano yenye changamoto unapaswa ujifunze MAARIFA ya jinsi ya kuimudu ndoa au mahusiano yako.
Ndoa sio jambo la kubahatisha, si kamari ya kupata na kukosa, maarifa lazima yatafutwe vinginevyo wengi wataendelea kusaga meno,kulalamika na kulaumu.
Content ni nzuri na inaakisi uhalisia katika jamii yetu ya leo ila head iko so conclusive. Nadhani kuna mambo yanaweza kufanywa na taasisi ikawa poa!
Ni hivi, kama ndoa yako ni ya Kimungu inatakiwa kuendeshwa as such. Kama ni ya dunia inavyobadirika basi nayo ibadirishe kama makala inavyopendekeza. Hii kitu ina misingi yake, ukiichezea tu lazima uishie wengi wanakoishia. Wengi waliobadirika nayo nayo imebadirika nao. Hili wazo halina tofauti na kuhasa wanadamu wabadirike kufuata upepo na matendo ya dunia, kwa mfano na ushoga…nk ili tuweze kuishi na hawa watu vizuri. Ndoa sio issue ya kila mtu. Ukiona unaweza miiko yake fanya. Ukiona hauko tayari miiko yake ni migumu hauko tayari, acha. Na hapo ndio utakuwa umebadirka na wakati in my opinion.
Mishy, kwanza asante. Mada ni yenyewe hasa na ni muafaka. Mtindo wa uandishi ni mzuri sana – kama kawaida yako. Heko. Niseme mawili matatu.
Kwanza- nakiri kwenye ndoa wapo wengi wanaotekeseka (wanaume kwa wanawake). Kila upande ukikupa madhila yao na ukawa mkweli kujaribu kuelewa kwa muktadha wao hutashangaa shida ya akili uliyozungumzia. Kwa hiyo ni muhimu kujadili haya mambo kwa uwazi, kwa mapana yake, na kwa nia njema.
Pili- kuhusu asili ya taasisi ya ndoa, mali binafsi na mahusiano kati ya dola na familia/mali. Lakini mimi naelewa haikuwa lengo lako kufanya uchambuzi wa aina hiyo. Hoja yangu ni kwamba bila kuzingatia misingi ya ndoa – kisheria, kidini, na kimila na kujadili uleo wa misingi hiyo itakuwa ngumu kupiga hatua mbele.
Tatu – naona umehitimisha kwa kukata tamaa na kurusha mpira kwa wasomi. Nadhani tusikate tamaa. Hebu tufungue mjadala uje kwetu walaji a “bidhaa” hii (ndoa) kisha wataalam watakuja kutusaidia tu. Ila ngoma hii tuicheze kwanza sisi wenyewe. Mwanzo mzuri ni kuvunja ukimya.
Narudia tena, kongole kwa mchango wako maridhawa.
Daniel
Asante sana kwa makala nzuri Dada Mishy, kusema kweli kabla ya kusoma makala hii nilikuwa mmoja wa wale tulioweka mbele kukosoa hata kabla ya kusoma na kuelewa kilichoandikwa. Kwa hili naomba unisamehe sana.
Kusema kweli andiko hili limeweka bayana uhalisia mzima wa dhana ya ndoa katika jamii yetu. Uhalisia ambao wengi wetu tumekuwa tukijificha nao. Naungana na wewe na kuhimiza wengine kuendelea kuibua mijadala hii ya taasisi ya ndoa ili tuweze kupunguza ama kuepusha; magonjwa ya akili, ukatili na hata vifo vitokanavyo na misukosuko ya mahusiano na ndoa.
Asante sana!