Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania atakuwa Rais wa kwanza duniani kukutana na Rais Xi Jinping wa China tangu aongezewe muhula wa tatu kuongoza taifa hilo katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) uliomalizika wiki iliyopita.
Serikali zote mbili zimetangaza kwamba ziara hiyo itaanza rasmi Novemba 2 mwaka huu. Hii pengine – kwa maoni yangu – ndiyo itakuwa ziara muhimu zaidi kufanywa na Rais Samia nje ya Tanzania tangu awe Rais Machi mwaka jana.
Siamini kwamba jambo hili limetokea kwa ghafla tu bila muktadha. Nilikuwa mmoja wa waandishi wa habari waliokuwepo Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam wakati Rais Xi alipoifanya Tanzania kuwa nchi yake ya pili kuitembelea mara baada ya Urusi mnamo Machi mwaka 2013.
Urusi – wakati ikiwa sehemu ya uliokuwa Muungano wa Jamhuri za Kijamaa za Kisovieti (USSR) – ilitoa mchango mkubwa kwa China wakati wa mapambano yaliyokuja kukiweka madarakani CCP mwaka 1949. Kama kada kindakindaki wa chama hicho na muumini wa siasa za Kijamaa, ilikuwa rahisi kuona ni kwa nini Xi alianza na Urusi. Lakini Tanzania? Kwa nini?
Tanzania na China tangu zamani
Mtanzania wa kwanza kufanya mawasiliano rasmi na uongozi wa juu wa CCP alikuwa ni aliyekuwa mwasisi wa Chama cha Umma Party cha Zanzibar na mmoja wa wasomi na wanadiplomasia mahiri kuwahi kutokea nchini, Abdulrahman Babu. Kwenye maelezo yake yaliyochapishwa katika jarida la Review of African Political Economy (ROAPE), Babu alisema alikaribishwa rasmi na CCP mwaka 1959 nchini China na pengine kuwa mpigania Uhuru wa kwanza wa nchi za Afrika Mashariki na Kati kupata fursa hiyo kwa wakati huo. Alifanya mazungumzo na viongozi wakuu wa China kama Mao, Chou en Lai, Chen Yi, Chu Teh, na Deng Tsiao-Ping.
Kwa mujibu wa Profesa Horace Campbell, Babu ndiye aliyemtambulisha Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, kwa Waziri Mkuu Chou En Lau na kufanikisha ziara ya kwanza ya Rais huyo nchini China. Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa urafiki ambao hatimaye uliifanya China kuja kuwa rafiki wa kudumu wa Tanzania. China – wakati ikiwa bado taifa linaloendelea, ilifadhili mradi wa ujenzi wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Reli hiyo inayojulikana pia kama Reli ya UHURU inabaki kwenye historia kuwa mradi mkubwa wa kwanza kufadhiliwa na China nje ya taifa hilo. Kwa mujibu wa kitabu cha “A Monument to China-Africa Friendship: Firsthand Account of the Building of the TAZARA” kilichotolewa kuadhimisha miaka 50 ya uanzishwaji wa reli hiyo, utaona kwamba kimsingi China ‘ilijikamua mno’ kufanikisha hilo. Msaada huo ni aina ile ya misaada ambayo kaka au dada anaweza kumsaidia mdogo wake ama mzazi kwa mtoto.
Baadaye, wakati Dakta Salim Ahmed Salim – kwa sadfa tu mmoja wa vijana waliopikwa na kupikika na Babu, akiwa Balozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa (UN), aliongoza kampeni ya mataifa ya Kusini kuirejesha China UN hadi kufanikiwa mwaka 1971. Kuna vitu viwili ambavyo Wachina hawawezi kusahau kuhusu Tanzania; ufadhili wao TAZARA uliotumia pesa na uhai wa Wachina waliokufa kutokana na changamoto za kujenga reli hiyo na kujitolea kwa Tanzania kuhakikisha China inarejea UN.
Ujamaa, Guanxi na Dini
Kuna mambo mawili huwaongoza viongozi wa China – Mwongozo wa CCP na dini wanayoabudu Wachina walio wengi ya Confucianism. Uhusiano usio wa kawaida wa China na Tanzania unajengwa zaidi kwenye imani ya Confucianism pengine kuliko hata sera za kijamaa ambazo Mwalimu Julius Nyerere alijaribu kuzitekeleza nchini hasa kuanzia mwaka 1967 alipotangaza Azimio la Arusha.
Mwalimu wangu katika Chuo Kikuu cha SOAS jijini London, Profesa Stephen Chan, alinifundisha kitu kuhusu dini hiyo kwenye darasa la Siasa za Afrika wakati tukijifunza kuhusu uhusiano wa China na Afrika. Yeye ni raia wa New Zealand lakini wazazi wake ni wahamiaji kutoka China.
Profesa Chan alinifundisha kuhusu dhana ya Guanxi ambayo ni mapokeo ya dini ya Confucianism. Dhana hiyo inaeleza aina tano tofauti za uhusiano zilizopo duniani. Uhusiano kati ya muumba na waja wake, mke na mume, mzazi na mtoto, mtawala kwa watu wake na wa mwisho kaka (dada) mkubwa kwa wadogo zake. Katika imani hiyo, uhusiano wa aina nne una wajibu na majukumu kwa kila upande, isipokuwa ule wa mkubwa kwa wadogo zake.
Muumba hutoa riziki kwa waja wake. Lakini wao wanatakiwa wasali na kutoa sadaka kwake. Mzazi atatoa huduma kwa watoto wake akitegemea labda naye watamhudumia uzeeni na kumwombea pepo pale atakapotangulia mbele ya haki. Mke na mume wanategemeana kwenye kupata watoto, mtawala atakuwa mwema kwa raia wake lakini raia nao watamtii. Kwa kaka au dada mkubwa kwa wadogo zake, kwa kawaida msaada wake hutolewa pasipo kutegemea chochote.
Ni uhusiano huu ndiyo ambao huifanya China wakati mwingine kutoa misaada na mikopo kwa nchi ambazo kimahesabu haziwezi hata kulipa. Nchi za Magharibi huleta maneno mengi kwa sababu kwao haiingii akilini kuona China inaikopesha nchi kama Zambia iliyopita wakati taasisi kama IMF na Benki ya Dunia ziliona haikopesheki
Kwenye ujenzi wa reli ya TAZARA, nchi za Ulaya na Marekani ziligoma kukopesha kwa maelezo kwamba haikuwa na faida zozote kiuchumi. Hata Benki ya Dunia na IMF zilikataa kwa sababu hizo hizo. Lakini China ilijitosa mpaka mradi ulipokamilika.
Ni wazi kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo China inaziweka katika kundi hili ambalo yenyewe inahisi wajibu wa kuzisaidia kiuchumi. Tofauti kubwa ya China na nchi za Ulaya na Marekani ni kwamba mpaka miaka 50 iliyopita, yenyewe nayo ilikuwa masikini kama nchi nyingi za Afrika zilivyo sasa.
Na kama kuna kiongozi anaujua umasikini, basi Xi anaufahamu. Kwenye miaka ya 1970, aliishi katika nyumba za mapangoni – Yaodong, kwenye mji wa Shaanxi wakati familia yake ilipoadhibiwa kwenye Mapinduzi ya Kiutamaduni (Cultural Revolution). Na Xi hawezi kuisahau Tanzania, nchi ambayo alishuhudia kujitoa sadaka kwa babu zake wakati alipotembelea makaburi ya Wachina kule Pugu, Dar es Salaam mwaka 2013.
Fursa ya Rais Samia
Sina shaka kwamba pamoja na changamoto zote inazopitia China sasa, roho ya Xi itakuwa inawaka kwa furaha. Ndiyo kwanza CCP imempa mamlaka na nguvu ambayo kiongozi wa mwisho kuwa nayo alikuwa ni hayati Mwenyekiti Mao. Namwona Rais Samia akiwa anatembelea China kukutana na ‘kaka yake’ mwenye furaha na aliye tayari kusikiliza.
Ninafahamu kwamba Kenya ni nchi muhimu kwa Tanzania kibiashara na Rais Samia alienda huko kwenye ziara yake ya kwanza kama Rais. Ninafahamu pia uhusiano wa Tanzania na Msumbiji ni wa kihistoria na ilikuwa vema kwamba Rais alikwenda Msumbiji kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Chama cha FRELIMO.
Nimemwona Rais Samia akiwa nchini Marekani kufanya promosheni ya filamu ya Royal Tour inayotarajiwa kuzimua sekta ya utalii kwa nchi yetu ambayo iliumizwa sana na janga la ugonjwa wa UVIKO-19. Nimemwona pia na viongozi kadhaa wa IMF na Benki ya Dunia.
Lakini hii ya Xi ni funga kazi. Akiwa China, Rais Samia atakutana na kiongozi ambaye jarida la Forbes lilimtangaza kama mtu mwenye nguvu na mamlaka zaidi duniani kwa sasa. Anakutana na kiongozi ambaye amekuza Pato la Taifa lake maradufu katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na kuondoa watu milioni 100 kutoka kwenye umasikini wa kutupwa kwenye kipindi cha miaka nane tu iliyopita.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Samia kufanya ziara rasmi ya kiserikali na kukutana ana kwa ana na kiongozi ambaye kwa yakini anaongoza taifa lenye hadhi ya Superpower. Sina shaka kwamba duniani kuna watu watakuwa wanatazama ni kwa vipi Tanzania na Samia wamepata fursa hii.
Zaidi ya yote, Rais Samia anakwenda kukutana na kiongozi ambaye kwa yakini anaiona Tanzania kama kaka au dada mdogo ambaye anahitaji kutazamwa kwa jicho la kipekee na kaka yake. Lakini ili kutumia nafasi hii vizuri, kuna jambo ambalo Rais wetu anatakiwa kulifanya; kumjua na kumgusa Rais Xi.
Xi kwa mujibu wa Henry Kissinger
Nimetazama mahojiano kupitia mtandao wa You Tube yaliyofanyika takribani wiki tatu zilizopita kati ya mwadiplomasia na msomi mbobezi, Henry Kissinger na taasisi moja ya masuala ya usalama ya Marekani. Swali moja aliloulizwa baada ya kuwa amekutana na Xi ni kuwa Rais huyo ni mtu wa namna gani.
Kissinger – ambaye amekutana na viongozi wote mashuhuri wa China katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, alisema vitu viwili; Mosi, kwamba ni mtu makini na pili, anaamini katika nguvu na ushawishi wa taifa lake duniani. Lakini watu walio karibu naye waliohojiwa na vyombo vya habari wakati akiingia madarakani kwa mara ya kwanza, wanamweleza kama mtu ambaye kwa yakini anachukia umasikini. Hiyo yote ni kwa sababu ameuishi kwa sehemu kubwa ya ujana wake.
Na nini ambacho Xi alifanya kwanza kwenye kupambana na umasikini? Wakiandika katika jarida la Globetrotter wiki iliyopita, waandishi Vijay Prashad na Tings Chak walisema Xi aliagiza makada 800,000 wa CCP kuwatuma katika vijiji takribani 128,000 nchini kwake kuzungumza na wanavijiji, kukusanya kero na kuziwasilisha kwenye chama. Huo ndiyo msingi wa mipango ya Xi ya kupunguza umasikini. Huyu ni mtu anayefanya kazi kupitia taarifa halisi kutoka chini.
Hii maana yake ni kwamba kufaidika na lolote kutoka kwenye fursa hii, ni muhimu kwa ujumbe wa Tanzania utakaofuatana na Rais kwanza kuandaa vitu vitakavyoibua roho hiyo ya ‘’Kaka Mkubwa’’ ya China kwa Tanzania na kuwa na mipango ya nchi kupambana na umasikini iliyojaa takwimu halisi.
Kama ni kukuza biashara – ni biashara zipi ambazo China ikifanya na Tanzania zitasaidia kupunguza umasikini kwa watu wetu? Kama ni suala la Reli au Bandari – ni kwa vipi hili litachangia kupunguza umasikini? Kama China ilisaidia TAZARA wakati nchi za Magharibi zikigoma, pengine huu ni wakati wa kusaidia reli nyingine – ya SGR kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kama ilivyokuwa miaka 50 nyuma?
Katika dunia hii ya sasa ya kulegalega kwa uchumi na amani duniani, fursa ya kukutana na wakubwa wa duniani ni fursa ya kukumbatiwa kwa mikono na miguu. Mwenyekiti Mao alipata kusema huko nyuma kwamba ‘’Jasho jingi wakati wa amani, huepusha damu nyingi wakati wa vita’’. Maandalizi mazuri ya kuijua China, Dunia na Xi kabla ya mkutano naye yatafanya safari hii ya kipekee ya Rais Samia iwe safari yenye manufaa kwa nchi yetu.
Ni fursa kubwa ya kisiasa, kiuchumi, kiulinzi na kidiplomasia. Mpira uko mikononi kwa Rais na wasaidizi wake.
Hapa nimesoma vema mwandiko wako
Nachoona sasa ni kwamba maombi mazuri sana juu ya uboreshaji wa Tazara au Bandari lakini kwenye Tazara ili iwe SGR vita inapigwa sana na wafanyabiashara wa Malori
Naitamani sana hiyo Reli kwani biashara ya Bandari wateja wakubwa ni Congo Zambia na Malawi hakina Rwanda na Uganda tayari wamerahisishiwa na SGR japo Kwa ufupi lakini itaendelea kitengenezwa
Suala ni kuingia mikataba ya kuboresha miundombinu Samia ndo aliangalie nje ya hapo hakuna maana ya ziara yake
Tuangazie suala la bagamoyo Corridor ni muhimu sana Kwa kizazi kijacho maana kazi zitakuwepo zaidi ya miaka kumi ndo ikamilike
Bado tunauhitaji mkubwa wa ufadhili kutoka china
Good piece Kamwaga