Katika waraka wa ‘Mmepotelea Wapi Makomredi?’ kuna kauli ya kwamba, “kuanzia miongo ya 1980 hadi 1990 mtikisiko utokanao na Uliberali Mamboleo uliathiri pia harakati za mrengo wa kushoto na hata kupunguza hamasa ya baadhi ya makomredi; na kwamba kufika miongo ya 2000 na 2010 hali ya kukuza ukomredi ikawa imepungua sana kasi yake ya zamani.”

Inawezekana tukawa na matamanio tofauti ya harakati na mafanikio yake. Mimi nina maoni tofauti kidogo juu ya hali ilivyokuwa katika miongo iliyotajwa, kwa sababu, hasa kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, harakati za UDASA katika miaka ya 80 na mapambano yao na uongozi wa Chuo, katika kutetea haki za wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo zilikuwa na nguvu, na kisiasa kulikuwa na msisimko wa kupinga uingiliaji wa siasa na matumizi ya nguvu za dola katika maisha ya Chuo. Hata hivyo, ni kweli kwamba uongozi wa Chuo na msukumo wa siasa na nguvu za ugandamizaji za dola iliyosalimu amri kwa uliberali mamboleo zilikuwa na athari hasi kwa harakati hizo.

Tunapoingia katika muongo wa 90 na 2000, mabadiliko ya siasa yaliyoruhusu vyama vingi yaliumbua vijana wengi Chuoni, walioacha kabisa kutumia akili na na taaluma katika kuchambua siasa katika enzi mpya ya vyama vingi. Walifikia kilele cha kuchanganyikiwa waliposhangilia viongozi kama Augustine Mrema na Christopher Mtikila kama wakombozi hadi kufika hatua ya kusukuma magari yao mithili ya wananchi walivyosukuma gari la Mwalimu aliporejea kutoka UNO (Baba Kabwela UNO). Na si wanafunzi tu; hata veterani mwanamapinduzi, Abdulrahman Mohamed Babu alisoma vibaya hali ya siasa za Tanzania akachukua fomu ya kuwania Umakamu wa Rais kama mgombea mwenza wa Mrema.

Wakati wa Kigoda Cha Mwalimu Nyerere juu ya Umajumui wa Afrika kati ya 2008 hadi 2013 kulikuwa na mwamko mpya na Chuo kilirejesha kiasi fulani hadhi yake kwa kuwavuta wanazuoni na wasomi maarufu kuja kutoa mihadhara. Wole Soyinka, Samir Amin, Micere Mugo, Bereket Habte Sellasie na Thandika Mkandawire walisisimua wanafunzi na kuleta mwamko walau wa kuhamasisha usomaji wa maandiko ya kimapinduzi. Vipindi vilivyofuata vya Kigoda vilibadili mwelekeo wake vikafanya mikutano yake kuwa nafasi ya kutoa elimu ya siasa kwa wanafunzi wa shule za sekondari.

Niunganishe hapa miaka ya 2014 hadi 2020 wakati wa Kavazi la Mwalimu Nyerere na mikutano iliyokuwa ikifanyika mara kwa mara kwenye ukumbi wa Costech na kuvutia wananchi wengi wasomi na wasio wasomi. Nafasi hizi zilipofungwa haikuwa rahisi tena kukutanisha watu. Ni kweli pia kwamba hali ilibadilika na kuwa ngumu zaidi wakati wa kipindi cha Rais Magufuli ambapo woga ulituingia sote na kwa sababu nzuri kabisa.

Maelezo ya kudorora kwa ukomredi wameyatoa; kwamba uliberali mamboleo ndicho chanzo kikubwa cha zahama hiyo. Lakini nafikiri pia kuwa hatuna budi, kujibu swali lifuatalo. Je, mfumo wa uliberali mamboleo, ndiyo sababu pekee ya kufanya harakati za mrengo wa kushoto kudorora na kufifia? Haiwezekani pia kuwa kufifia kwa harakati kulikuwa, na kunaendelea kuwa dalili ya udhaifu wa makomredi wa mrengo wa kushoto? Au je, mbele ya uliberali mamboleo hakuna la kufanya ila kuukubali? Naamini kuna haja ya kujikosoa, nguvu zetu ni ndogo, hilo liko wazi; lakini ni wazi pia kuwa ni ndogo kwa sababu hakuna jitihada za kutosha za kuzijenga hizo nguvu.

Tusisahau pia kuwa neno “makomredi” lilitumika na linaendelea kutumika bila kujali sana mwamko na imani ya kiitikadi ya wahusika, kama ilivyokuwa kwa neno “Ndugu,” ambalo, bila kujali tofauti za kimtazamo, lilijumuisha wanachama wote wa TANU-AFRO na CCM, wenye mielekeo ya siasa ya kuanzia kushoto kabisa hadi kulia kabisa. Wote waliitana Ndugu licha ya kuwa walifahamiana vyema katika nafasi zao kwenye wigo wa itikadi ya ujamaa.  Kwa mfano, Komredi Ngombale Mwiru ambaye alikuwa kushoto hata kwa Mwalimu Nyerere kiitikadi, bado aliwaita wajumbe wengine katika vikao vya Chama, ndugu, licha ya kwamba wengi wao hawakuamini hata kidogo siasa, wala maisha ya kijamaa.  Msamiati wa “Ndugu” waliukubali kwa sababu uliwafichia siri. Haishangazi kuwa baada ya kulitupilia mbali Azimio la Arusha, na Mwalimu kuachia ngazi zote za mamlaka katika Chama na serikali, viongozi hawakutaka tena kuitwa Ndugu, na badala yake wakalazimisha waitwe Waheshimiwa.

Kupungua kwa vuvumko la harakati miongoni mwa makomredi kuna sababu nyingi. Wakati wa uongozi wa Mwalimu, mikutano ya kisiasa ilikuwa ya kawaida, katika jamii nzima, ndani ya Chama na nje ya Chama. Majadiliano yalikuwa wazi na ya kidemokrasia; hakukuwa na vitisho vyovyote. Vyuo Vikuu vilikuwa vitovu vya mijadala mikali, na kuongezeka kwa idadi ya vijana wanafunzi na wanazuoni wote wenye sifa za mrengo wa kushoto.

Wahitimu wa Chuo Kikuu waliendeleza majadiliano na mikutano ya kusoma fikra za kimapinduzi. Ushawishi wao ukawa ukipenyeza katika Wizara, viwanda na taasisi za umma. Lakini baada ya miongo miwili mitatu makada hao wamepungua sana na wale waliopo wanapambana na hali za utu uzima na athari zake kwa afya zao za mwili, na ukali wa maisha, wengi wakiishi bila pensheni au njia nyingine za hakika za kuendeshea maisha yao.

Changamoto za kiuchumi baada ya vita vya Kagera na kutekelezwa kwa sera za Benki ya Dunia na IMF kwa maoni yangu kulisababisha sana kuvurugika kwa maisha ya kitaaluma. Kwa kweli Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na kusema kweli wanafunzi na walimu wao ndio walikuwa kitovu na waliotoa msukumo (inspiration) kwa harakati za mrengo wa kushoto.Umaskini ulikithiri. Maprofesa waliacha kazi za kufundisha na utafiti wakatumia muda mwingi katika kufuga kuku na nguruwe ili mradi walishe familia zao. Wengine walihama wakaishia katika vyuo nje ya Tanzania, hasa kusini mwa Afrika ambako walishamiri.

Wanazuoni wengine walirubuniwa kuwa mamluki wa Benki ya Dunia na IMF, wakawa wakilipwa ada kubwa za huduma za ushauri na kuwa watetezi wa sera gandamizi zao. Kwa kulenga kuua Chuo Kikuu walilenga kufukia chemchemi ya fikra za mapinduzi na unaharakati na kuifanya Afrika iwe bara la walala hoi, na vituo vya manamba. Sina shaka mnakumbuka kuwa Benki ya Dunia iliwahi kupendekeza kuwa Afrika haihitaji Vyuo Vikuu na kwamba ilichohitaji ni shule za msingi na za ufundi, na kwamba wataalamu wangeweza kuajiriwa kutoka nje walipohitajika.

Sehemu muhimu ya Azimio la Arusha – miiko ya viongozi – ilifutwa na Azimio la Zanzibar. Uchumi wa soko huria ulifanywa kibwagizo cha sera na utamaduni wa uongozi wa taifa, kama kilivyo sasa kibwagizo cha Sekta Binafsi. Uliberali mamboleo ulizaa utamaduni wa ubinafsi wa kupindukia. Ubinafsi huo ulitenga watu, na makomredi walisahauliana; wale walioendelea kushika itikadi ya ujamaa walichukuliwa kama watu wasio na ndoto za mafanikio katika kutafuta utajiri. Baadhi ya makomredi waliukana kabisa.

Tusisahau pia kuwa mwaka 1989 na 1990 Umoja wa Jamhuri za Kisoshalist za Kisovieti ulisambaratika, kukawa na kuvunjika moyo kwa watu wote wa mrengo wa kushoto duniani kote. China nayo ilipoamua kutumia mbinu ya ubepari wa mitaji binafsi kujenga uchumi wa uzalishaji bidhaa viwandani, watu wengi ambao awali walichukuliwa kama watu wa mrengo wa kushoto, ni kama walipata kisingizio walichokuwa wakitafuta; kuwa kumbe, hakuna haja tena ya kushikilia itikadi hiyo. Wengi wao walijitosa katika ubepari, ambao huku kwetu ulikuwa wa kikomprador; wa wizi wa mali za umma au waliingia katika siasa za ulaghai na usanii wa kijinai.

Lakini licha ya changamoto hizi, kuna makomredi waliokataa kukata tamaa. Asasi nyingine za Sheria na Haki za binadamu, Bara na Zanzibar, TGNP na TAMWA, TAWLA kwa masuala ya Haki za wanawake na nyinginezo kwa kiasi chao ziliendelea kupambana. Hao makomredi wachache waliendeleza mapambano kupitia njia mbaimbali; waliandika, walikutana kunywa kahawa pamoja na kubadilishana mawazo. Na kama Lenin alivyowahi kusema, “Better few but better”— “Bora wachache lakini bora.”

Mijadala yetu leo ni mifano hai ya ninachokisema. Kumbe bado tupo. Sina shaka kuwa tutaendelea kuchambua na kutafakari changamoto zote zilizo mbele yetu. Naamini pia kuwa tutajifunza na kupongeza jitihada za makomredi ambao wamekuwa imara katika muda wote, wakifanya kazi katika hali ngumu kueneza fikra sahihi. Jithada zao zimezaa matunda, wamefundisha wafanyakazi katika sehemu mbalimbali mijini na vijijini na kuwawezesha kutetea maslahi yao dhidi ya wanyonya jasho lao. Wanastahili kupongezwa sana.

Kabla sijamaliza ninataka kukumbusha kuwa njia ya harakati za kuleta dunia mpya yenye maisha mema kwa wote, yenye fursa za binadamu kuishi kiasi cha uwezo wao na vipaji vyao; na dunia isiyo na tabaka si njia iliyoonyoka. Kuna wakati miaka mingi nyuma wakati Chama cha Kikomunisti cha Marekani kilipokuwa kimeingiliwa na FBI, ilibainika kuwa wanachama wengi zaidi katika chama hicho walikuwa maajenti wa FBI. Kwa hiyo njia hiyo ni ya milima na mabonde; ni ya kwenda mbele na kurudi nyuma, ili mradi bado kuna utashi wa makomredi wa mrengo wa kushoto kutokata tamaa, na kupambana hadi kufikiwa kwenye lengo, hata kama inachukua miaka 100. Hawa ndio makomredi.

Kwa kumaliza nataka kupendekeza pia kuwa ukomredi usiishie kwenye mikutano. Wengi wetu hatujui nani anaishi wapi na anaishi vipi. Bado hatuwatendei makomredi waliotutoka kwa kuwakumbuka katika shughuli maalum za kumbukizi na kutambua mchango wao. Hatuna budi kukutana na kufahamiana zaidi. Itikadi peke yake bila upendo wa kimapinduzi haitoshi.

Tukutane, tule, tunywe pamoja. Tucheke tufurahi, tusaidiane inapohitajika. Tufarijiane katika nyakati ngumu. Vizazi vitatu vyenye kusoma na kujielimisha juu ya itikadi ya ujenzi wa ujamaa wa kweli, na vinavyoendelea kukosoa mifumo gandamizi na uchumi wa manufaa kwa wachache si haba. Sisi wa kizazi cha tatu nyuma bado tupo na tuko tayari kushikamana nanyi. Natumai majadiliano yetu yatafungua njia na jitihada mpya katika malengo yetu ya pamoja.