Mafichoni Hotel

17-07-2020

 

Mpendwa Mchepuko, 

 

Yah: Kusitishiwa Huduma za Uchepukaji

 

Nimeshtushwa na taarifa picha iliyonifikia kutoka kwa besti angu. Umeonekana wilayani ulikozaliwa ukiwa ofisi za Chama cha Siasa ukichukua fomu ya kuwania ubunge. Picha ya pili ndio imenikalisha chini na kuanza kujipepepea na baridi na mvua hizi. 

 

Ume-post huko Twitter uko na mkeo ‘kipenzi’ alipokusindikiza kuchukua fomu. Kwa ujasiri ukaiwekea kapsheni matata, “Nguzo mama, imesimama”. Haki hata sijui kama uliwahi soma hicho kitabu!

 

Yaani kumbe safari za kwenda nyumbani kila mara ilikuwa ni haya maandalizi? Mwenyewe ulikuwa unaniweka sawa eti kwanza unakarabati nyumba ya wazee wako. Mara unaanza kujenga nyumba yako. Mara mkaanza kuongozana ama kupishana na Mama Neema kwenda kijijini. 

 

Kwa hilo ulisema walau yeye ataweza kusimamia ujenzi uende haraka. Kwa taarifa zilizonifikia hivi punde, Mama Neema alikuwa anapita chini kwa chini kwenye vikundi vya akina mama akajiunga navyo na kuviongezea mitaji. Na wewe mwenzangu, ulikuwa hukosi kwenye kila tukio la kijamii na michango kama yote. 

 

Yaani bado najipepea na nakunywa maji baridi. Baba Neema wewe wa kunificha mie? Unajua sipendi siasa za vyama vingi kwa sababu siamini kwamba ni kiashiria wala mkondo wa kubeba demokrasia. Lakini mambo mangapi tunatofautiana na bado tumeendelea kushiriki pamoja shughuli za ujenzi wa taifa katika uchumi wa kati! 

 

Na tumeongelea sana suala la utaifa na jinsi ambavyo taifa letu lina sifa mbele ya mataifa kuwa ukaazi waweza kushinda uzawa na rangi kwenye siasa za vyama. Tena tulikubaliana kwamba bado mfumo wa vyama unatumia wanawake kama madaraja ya kupandia kwenye siasa za kitaifa bila kubomoa mfumo dume wa siasa wala kufanya mapinduzi kwenye ukombozi wa mwanamke. Ulikuwa unanichora au? 

 

Umenishirikisha mengi kuhusu ndoa yako kwa takribani miaka 10. Japo sipendi kujipa sifa nilidhani nilikusaidia sana kimawazo mlipokuwa na migogoro na Mama Neema kuhusu kuwekeza kwa kununua viwanja, kufungua biashara kadha wa kadha, mambo uliyoyapinga kama ni unyonyaji na ulimbikizaji mali. Tena ukawa unamponda Mama Neema wa watu eti anapenda sana mali. Mi nikawa nakwambia sio mali anaangalia, (Mungu aepushie mbali) Mungu akikuchukua watoto atawaleaje? 

 

Sasa hivi sijui la kuamini na la kutokuamini maana Mama Neema huyo huyo ulokuwa unasema anakufanya unachukia kurudi nyumbani maana anakaa anadai pesa za hiki na kile saa hii ndio ‘nguzo mama’. Mama Neema uliyekuwa unamuacha nyumbani kwa sababu alikuwa anajiona hayuko huru kuhudhuria hafla kubwa kubwa mnazoalikwa akijilinganisha na watu wengine leo kapata matumizi kulingana na uzao na elimu yake: kwenda vijijini maeneo aliyozaliwa kukujengea mtandao wa wapiga kampeni na wapiga kura. Yangu, mabesti zangu na familia yangu sijui kama kuna nililokuficha, wayajua. 

 

Bado najiuliza, ulichoshindwa kunishirikisha ni nini? Unaogopa sitakubaliana na maamuzi yako? Unahisi nitamuonea wivu Mama Neema na nianze visanga vya ukewenza? Kwani mimi ni mgombea mwenza?

 

Linalonijia kichwani ni moja, wewe ulikuwa rafiki yangu hivyo nilikuamini mia kwa mia. Lakini mimi sikuwahi kuwa rafiki yako. Ulinihitaji tu kwa shughuli za ujenzi wa taifa, kupumzika na kupata tu mtizamo wa kisiasa unaokufikirisha na saa nyingine kukukasirisha.

 

Ulipoanza kunipotezea wiki hizi za karibuni mi nilijua tu ni wingi wa kazi maana mchakamchaka wa kumaliza muhula chuoni si mdogo. Nilikuwa najua unakimbizia kuandika na kumaliza mradi fulani na makala mbili tatu. Kwa hiyo kama iliyo ada ya uchepukaji, nikajiambia tulia mzee baba apunguze kazi. Likizo ndefu ikija tutaendelea tena na shughuli za ujenzi wa taifa na mengineyo. 

 

Yaliyojiri, yashajiri siwezi kuyabadilisha. Lakini kutokana na hali ya kutoaminiana kati yetu, navunja rasmi uchepukaji huu. Tafadhali, sio unafika mbeleni unaanza kunipigia simu, “Tukutane Mafichoni saa kumi na moja”, sijui ka-email nikusaidie ku-review nini, koma. Nakutema kama ulivyonitema. 

 

Barua hii naiacha hapa hapa mafichoni, namuachia dada wa mapokezi maana najua ndio kijiwe chako ukitoka kazini. 

 

Wasalaam, 

 

Kinky

 

*Hii ni tungo ya kisanii/kiubunifu ya Diana Kamara, haihusu maisha yako halisi ewe mpendwa ndugu msomaji.