Waandishi Wanawalinda
Wanasiasa Wanaokopa Wananchi?

  

Chambi Chachage

“Na ninyi waandishi wala hamuendi… mkawaanika hadharani” – Rais Magufuli

Matukio matano yamenichochea
kuandika makala haya. Kwanza, ni harakati za kulinda ‘Uhuru wa Kujieleza’.
Pili, semina ya Kavazi la Nyerere iliyotolewa na Profesa Carlos Nuno Castel-Branco kuhusu‘Deni la Taifa’. Tatu, taarifa ya gazeti la Tanzania Daimakuhusu uwezekano wa chama cha ACT Wazalendo
kufilisiwa. Nne, tangazo la Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, kuhusu madeni yake. Tano, mahojiano ya Rais John Magufuli na wahaririyaliyogusia madeni ya wanasiasa.

Kwa wachambuzi wa tasnia ya
habari, halikuwa jambo la kushangaza kuona Tanzania Daima ikichapisha katika
ukurasa wake wa mbele kwamba ‘Zitto, ACT-Wazalendo Hatarini Kufilisiwa.’ Gazeti hilo
linajulikana kama ‘kinywa’ cha chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho
kilimvua uwanachama Zitto. Hivyo, siyo jambo la ajabu kuona likipata ujasiri wa
kujaribu kuanika habari za Naibu Katibu Mkuu huyo wa zamani wa chama hicho.
Ndiyo maana mwana-ACT, Dotto Rangimoto, amehoji kwenye Jamii Forums kama ‘Mbowe anasaka “Kiki” kwa jina la Zitto?’

Siku hiyo hiyo ya tarehe 27
Desemba 2016, Zitto alitoa tamko lililosajiliwa na “Wakili na Kamishna wa Viapo”,
Emmanuel Mvula. Tamko hilo lililowekwa katika vyanzo mbalimbali mtandaoni
tarehe 30 Desemba 2016 linatoa ufafanuzi kuhusu deni ambalo gazeti la Tanzania
Daima lilikuwa linajaribu kulianika na kulijengea hoja kwa kutumia taarifa ya
madai ya madeni inayomhusisha mdai Soraya Souleymane. Hilo nalo halishangazi
kwani baada ya kuwasisitizia watimize ahadi yao ya kutoa taarifa za gharama za
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ACT-Wazalendo walizitoa mtandaoni tarehe 15-16
Februari 2016 ambapo jina la mdai huyona wengineo yaliwekwa wazi.

Hivyo, kitu kilichotuacha na
butwaa baadhi yetu ni taarifa hii katika tamko hilo la mwaka huu: “NINA DENI LA
TZS 191,060,094. HILI DENI LINATOKANA NA MKOPO KUTOKA NSSF.” Kwa nini
linashangaza? Mosi, ni kwa sababu tamko hilo halituambii ni lini fedha hizo
zilikopwa. Pili, ni kwa sababu katika tamko lake la aina hiyo la tarehe 29 Machi 2015 deni hilo halikuorodheshwa. Tatu,
kutokuwepo kwa taarifa hizo kunatufanya tusijue kama zilikopwa wakati Zitto
alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo ‘inaisimamia’ NSSF.

Utata huo umepelekea wadadisi
wa mambo tuikumbuke hoja hii ya Rais Magufuli wakati wa mahojiano na wahariri wa
vyombo vya habari tarehe 4 Novemba 2016:

“Kinachotokea na ambacho kilikuwa kinatokea, benki zetu hizi zilikuwa [zinakopwa] na wanasiasa. Nenda NSSF wamekopa wanasiasa wa kila aina, wa UKAWA wamo, wa CCM wamo. Wamekopa benki zingine mpaka…zimeingia mufilisi. Hawarudishi. Kuna benki moja hapa, nilipokuwa nimeingia madarakani, niliwaambia ina-sound negative by 11 percent. Hatua hazikuchukuliwa. Sasa [z]imekuja kuchukuliwa na benki, ina-count 22 percent negative. Lakini angalia majina yaliyokopesh[w]a humo, ni wanasiasa tu – wengi. Na ninyi waandishi wala hamuendi kwenda kuchambua, mkawajua hao, waandishi mkawaanika hadharani. Ndiyo challenge ya nchi yetu,mnawa-protect. Wanazungumza kweli,wana mamidomo kweli, utafikiri they are so clean. Najaribu kuwaeleza hili kwa sababu Tanzania ni yetu. These are the challenges ambazo ninaziona.” 

Wadau wa ‘hashtag’ ya #UhuruWaKujieleza tunapaswa kuifanyia kazi changamoto hiyo. Bila ajizi Rais
amesisitiza kwamba waandishi tunawalinda wanasiasa waliokopa katika taasisi
zetu za umma. Bahati nzuri mwanasiasa mmojawapo amekuwa muwazi kwa kiasi chake
kuhusu madeni yake ya NSSF na haya mengine: “NINA DENI LA TZ 176,315,106.21.
HILI NI DENI LINALOTOKANA NA MKOPO KATIKA BANK YA CRDB.” Je, tutegemee tu
utashi na uadilifu wa wanasiasa au turasimishe uwazi na uwajibikaji wao?

Changamoto iliyobaki kwetu ni
kuwabana wanasiasa wengine nao wawe wakweli na wawazi au, kama alivyosema Rais, waandishi tuwachambue na kuwaanika hadharani bila kupepesa macho. Pia kwa ambao wamejitahidi kuwa wawazi
tusiishie kuwapongeza tu. Tunatakiwa pia kuweka mapenzi na ushabiki wetu kwao pembeni na
kuwauliza maswali magumu kuhusu namna walivyopata mikopo na jinsi ambavyo watalipa
madeni ili Watanzania wote tufaidike.

Zitto ameonesha mfano.
Kaonesha na ujasiri wa kujibu maswali yaliyoibuka kuhusu tamko lake ambapo amesisitiza kuwa anaamini “kwamba
uwazi ni moja ya silaha madhubuti ya kupambana na ufisadi”. Hivyo, kawasilisha
“muswada bungeni kutaka uwazi huu liwe sharti la sheria za nchi yetu.”
Kupitia tamko lake rasmi
pia:

“[A]Namsihi sana Rais John Pombe Magufuli kusaidia kufanya mabadiliko makubwa ya Sheria ya maadili ya Viongozi ili kurejesha na kuboresha Miiko ya Viongozi katika kuimarisha vita dhidi ya ufisadi nchini. Rais aliahidi kuweka wazi Mshahara wake alipokuwa anazungumza katika kipindi cha 360 cha Clouds TV. Ninamkumbusha afanye hivyo na pia aweke wazi Mali, Madeni na Maslahi yake ya Kibiashara ili awe mfano kwa Viongozi wengine Nchini.”

 Sasa ni jukumu la waandishi kumuuliza Zitto
naye atoe ufafanuzi kuhusu baadhi ya zinazoonekana kama tofauti kati ya taarifa yake ya mwaka jana
na ya mwaka huu. Kwa mfano, taarifa ya mwaka huu haionekani ikiyataja makampuni
ya Gombe Advisors Limited na Kigoma Development Initiatives (KDI) Limited
ambayo mwaka jana aliyaorodhesha. Je, ameacha kumiliki hisa katika makampuni
hayo ambayo amekuwa anasisitiza kwamba siyo ya kupata faida? Kama na yenyewe
yalikopa, je, madeni hayo yameshalipwa? Na kama umiliki wake umebadilika, nani
ni mmiliki wake? Maswali kama haya ni muhimu hasa ukizingatia kwamba tarehe 10
Desemba 2016 aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Leka Dutigite ambayo ilikuwa ina uhusiano wa kihisa na GombeAdvisors, Habib Mchange, alitoa taarifa kwa umma kuhusu ‘KUJIVUA UANACHAMA WA ACT WAZALENDO NA KUTOSHIRIKI
SIASA’ ili apate “muda mwingi zaidi kufanya na kusimamia shughuli” zake “za kijasiriamali.”

Jambo jingine linalostahili kuhakikiwa
na waandishi wa kiuchunguzi ni taarifa ya malipo ya madeni. Katika tamko la mwaka
huu Zitto anatuambia:
“NIMEPUNGUZA MADENI NILIYOKUWA
NADAIWA TOKA TAMKO LA AWALI LA MWAKA 2015 NILILOTOA TAARIFA YA DENI KIASI CHA
TSH 560,000,000/=”. Ukilirejea tamko la mwaka jana unakuta deni la NMB ambalo mwaka huu halipo, ikiashiria
kwamba ameshalilipa lote. Ama? Pia tunakuta taarifa hii: “Nina mkopo wa Tshs.
24,624,046.88 katika Benki ya CRDB. Huu ni bakaa la mkopo wa Tsh. 200,000,000
niliouchukua mwaka 2010 na 2011.” Lakini mwaka huu tamko linasema ana deni la TZ
176,315,106.21 la CRDB. Je, hili ni deni la bakaa ile ile? Au ni mkopo
mwingine?
 

Deni la Taifa, kama
alivyosisitiza Profesa Castel-Branco
katika semina yetu kavazini, huchangiwa pia na mabenki ‘kukopesha madeni’. Huu
‘ufedhazishaji’ pia hupelekea madeni binafsi kugeuzwa kuwamadeni ya umma. Kwa nini? Kwa sababu taasisi za umma zilizokopesha watu binafsi
zinapofilisika mzigo hubebwa na wananchi wote.

Badala ya kulindana tuanze
kuanika madeni ya umma na kusisitiza wahusika walipe.


La sivyo tutakuwa hatuutendei haki #UhuruWaKujieleza.