Utangulizi

Miaka 20 imepita tangu Prof. Chachage S. L. Chachage atutoke duniani. Ni muda mrefu lakini bado anakumbukwa kwa namna mbalimbali na wanazuoni wenzake, ndugu, marafiki, na watu wengine wasio katika makundi haya. Katika kipindi chote hicho nimekuwa nikikutana na watu wa rika mbalimbali ambao wamekuwa wakimkumbuka kwa kujiuliza: ‘Sijui Chachage angekuwepo angefanya nini, au angesema nini?’

Swali hili kwa sehemu linaweza kujibiwa na namna Chachage alivyokuwa. Kwamba, jinsi alivyokuwa kama mtu na mwanazuoni ndio kunafanya watu wamkumbuke kwa namna mbalimbali.

Nitajaribu kumueleza Chachage, kadri nilivyomfahamu, kwa kujibu swali, Chachage alikuwa mwanazuoni wa namna gani?

  1. Je, alikuwa Mwanazuoni wa namna gani?

Chachage alikuwa na sifa zote zinazobeba majina au utambulisho ambao leo ungeweza kumweka matatani, pengine hata kufunguliwa mashtaka ya uchochezi au hata ugaidi. Hii ni kwa sababu Chachage alikuwa mwanazuoni Mchochezi, Mkosoaji, na Mkorofi. Na yeye akijitambulisha kama Mwanamapinduzi na sio Mwanaharakati.

Aghalabu alipenda kuwaita wenzake waliofanana naye kifikra na misimamo majina ya utani kama vile: Mlamoto, Mchochezi, na Mzushi!

Wakati mmoja tukiwa Zanzibar kwenye mkutano alitutangazia kuwa yeye sio mwanaharakati bali mwanamapinduzi. Uanaharakati haukuwa utambulisho wa maana kwa sababu watu wa itikadi na shabaha tofauti wanaweza kuwa wana harakati (activists).

Chachage alikuwa mchochezi. Uchochezi wake ulifanyika pale alipochochea wanafunzi wake na wenzake kufikiri, na hasa ufikiri tunduizi (critical thinking); pale alipowahimiza wanafunzi wake wajisomee ili kukuza maarifa, kuibaini kweli na kuepuka ujuha; pale alipoamsha fikira na mboni za waliosinzia na hivyo kutoona au kubaini uonevu, ukatili, dhuluma, unyonyaji, na ubaguzi. Aidha aliamsha ari ya kuunganisha nguvu za pamoja kuyapinga yote hayo.

Ukosoaji ilikuwa ni sifa kuu nyingine ya Chachage. Alikuwa mkosoaji mahiri wa mamlaka za kidunia, kidola, kiserikali, na zile za Vyuo Vikuu. Alipinga mipango na sera zao ambazo alibaini zilikuwa na madhara kwa watu na zilkuwa kinyume na haki za kijamii na ubinaadamu. Ukosoaji wa Chachage haukuwa wa kificho, ulikuwa wa wazi na dhahiri. Ukosoaji wake ulifanyika kwa njia mbalimbali zikiwemo:

  • Kuandika makala za kitaaluma.
  • Kutoa mihadhara.
  • Kuandika makala magazetini – ikiwemo barua kwa wasomaji.
  • Kushiriki mijadala katika Televisheni na kwenye makongamano.
  • Kutoa matamko – public statement hasa alipokuwa kiongozi wa UDASA.

Hakuna tukio la hovyo na lenye athari za kuvunja au kuminya haki za watu ambalo Chachage asingelifuatilia, kulitolea maoni au kulipinga. Kwa sifa hii Chachage hakuwa mwanazuoni asiyejali (the “indiferrent”). Kwenye ‘I hate the indifferent’ (Odio gli indifferenti) iliyoandikwa mwaka 1917, Antoni Gramsci anaeleza kuchukizwa kwake na wasiojali. Anawaeleza watu wa aina hiyo kama kizingiti kizito katika jitihada za kuleta mapinduzi na uhuru kwa binaadamu. Gramsci anaeleza zaidi kuwa kwa kutojali au kwa ukimya wao wasiojali huruhusu ukandamizaji (tyranny) na udhalimu (injustice) kushamiri. Katika jamii zetu kutojali (Indifference) kunazidi kuwa jambo la desturi. Na kama alivyosema Gramsci, ukimya na kutojali kumefanya ukandamizaji na udhalimu kupevuka na kushamiri duniani kote. Je, kwa hali ilivyo hivi sasa, Chachage angekuwa sawa na wengi wetu tulivyo, yaani kutojali, kuwa kimya? Sidhani!

Kwa uanazuoni wake, Chachage alikuwa mtafiti mahiri na wa kimapinduzi. Katika hili Chachage

  • Alipenda kufanya na kuhimiza tafiti za msingi (Basic research).
  • Alitafuta taarifa na maarifa toka kwa watu wa kawaida – Vijana na watu wa kawaida ambao hawakuwa wasomi kama yeye.
  • Alisoma magazeti yote: Ya wateule (elite) na ya Udaku
    • Huko alijua nini kinatokea na kinaendelea mitaani, ipi ilikuwa misamiati mipya, na yepi yalikuwa masuala yaliyowasibu!

Chachage hakuwa mwanazuoni aliyejitutumua na mwinua mabega, alikuwa ‘mdogo, lakini mkubwa katika udogo wake.’ Hakuwa mwanazuoni mteule (elite intellectual) bali mwanazuoni aliyejitanabahisha na kujifungamanisha na watu na hasa wavuja jasho, yaani ‘an organic intellectual of the working people.’

Sifa nyingine ya Chachage ni kutokuwa mwanazuoni mamluki (A mercenary intellectual). Wakati wote alikuwa na alibaki na msimamo ulioongozwa na mtazamo wake wa kimapinduzi. Hakukubali kutumika kwa ajili ya maslahi ya watawala au wenye fedha. Alijitahidi sana kutowasaliti watu, na kutoisaliti haki na kweli! Hapa nitatoa mifano miwili:

  • Mosi, alipofanya Ushauri Elekezi – na matokeo ya kazi yake kutofautiana na matarajio ya aliyempa kazi, na mshauriwa kuelekeza au kutaka taarifa ya ushauri elekezi ichujwe ili kukidhi mahitaji na maslahi yake, Chachage hakukubali, alisimamia ukweli wa matokeo ya yale aliyoyakusanya kwenye utafiti uliozaa taarifa ya ushauri elekezi. Mfano mzuri ni kuhusu taarifa ya ushauri elekezi kuhusu Mradi wa Kamba kule Rufiji– ambao sehemu ya ghiliba za wenye pesa anazisimulia katika Riwaya yake ya Makuadi wa Soko Huria (tazama Uk: 262-267).
  • Pili, ni kitabu kiitwacho Environment, AID and Politics in Zanzibar. Kitabu hiki kilikuwa ni matokeo ya Utafiti ambao yeye aliufanya kati ya mwaka 1997-1999. Utafiti ulikuwa ni Mradi wa Utafiti uitwao: Finnish Aid in Tanzania and Nepal. Chachage alijitoa kwenye mradi na kuamua kumalizia mradi huo yeye mwenyewe. Anatoa sababu za kujitoa kwemye mradi huo mwaka 1999 kwa maneno yafuatayo:

“Niliamua kuasi dhidi ya hali ambamo wasomi na watafiti wengi wa nchi za kusini hujikuta … Siku zote huwekwa katika nafasi za chini huku wakitakiwa kufuata masharti yanayoamuliwa kiimla dhidi yao … kwa muhtasari uhusiano huo hauna usawa” (Chachage 2000: ix).[1]

Wengi wetu hatuna ujasiri, hata huu mdogo, wa kukataa kutumika. Inasikitisha zaidi pale ambapo miongoni mwetu, na katika zama hizi, hatuoni haya kuwa mamluki na baadhi yetu hujivuna kwa kutumika kwa ajili ya mamlaka za nje au za ndani, mashirika ya kinyonyaji – ya kiserikali au binafsi, na wawekezaji wa ndani na wa nje. Sina shaka kuwa Chachage angesingekubali hata katika nyakati hizi zenye mikanganyiko mingi na mikubwa kuwa mwanazuoni mamluki.

Katika misimamo yake hiyo thabiti kuna wakati Chachage alivutiwa na kuingia madarakani kwa Rais Jakaya Kikwete. Chachage, kama ilivyokuwa kwa watu wengi, alijenga matumaini na utawala wa Rais Kikwete juu ya mustakabali wa nchi na watu wake. Kikwete, kwa mujibu wa Prince Bagenda alikuwa ni ‘Tumaini Lililorejea.’ Chachage hakufanikiwa kuuona mwisho wa utawala wa Kikwete wala mwisho wa mapambano ya kudai Chuo Kikuu tukitakacho yaliyochochewa na ubaini kuwa uongozi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ulikuwa umekwishaandaa Charter ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam bila kushirikisha waalimu, wanafunzi, na wafanyakazi waendeshaji. Na kabla hajaaga dunia aliandika makala ambayo, kwa walioisoma na kuikosoa, waliona ilikuwa ikihalalisha tabia ya dola dhidi ya vyama vya upinzani. Bahati mbaya wakati ukosoaji huo ukitokea Chachage hakuwepo kujitetea. Na kabla hajaondoka hapa duniani alishaanza kuwa na shaka juu ya matumaini yake kwa utawala mpya wa Rais Jakaya Kikwete. Na hayo yalijibainisha, kama ilivyokuwa kawaida yake ya kuumba maneno yanayobeba sifa za jambo, alipoibuka na neno ANGUKA likiashiria hatma ya ‘Ari Mpya, Nguvu Mpya, na Kasi Mpya!

  1. Chuo Kikuu na Uhuru wa Wanazuoni

Katika Makala The University: the site for the pursuit of truth, the whole truth, Wamba dia Wamba anabainisha kuwa: Mosi, Kwa asili vyuo vikuu vilianza kama chama (guild) cha wapenda kutafuta Ukweli (pursuit of Truth) enzi za zama za kati huko Ulaya. Mwanzoni vyama hivi vilikusanya watu kutoka mataifa mbalimbali (universalistic) wakiunganishwa na mapenzi yao juu ya ukweli. Na baadae vilipokuwa vyuo vikuu vikabaki kuwa huru nje ya uthibiti wa dola na kanisa. Lakini pindi utafutaji ukweli, ukweli kamili ulipoanza kutishia wenye mamlaka ya dola na kanisa – dola na kanisa vikaanza kuthibiti vyuo. Na kilichofuata ni kukaanza kuundwa vyuo vya dola na vya kanisa; na pale watu wengine walipotaka kuanzisha vyuo walipaswa kuomba na kupata ithibati ya dola. Jambo moja dhahiri katika mtiririko huu wa asili ya vyuo vikuu na mahusiano yake na dola ni kwamba pale tu ukweli unapouma kwa watawala basi huingilia uhuru wa wapenda na watafuta ukweli – vyuo vikuu kwa maana ya wanafunzi na waalimu wao (kitivo au faculty). Na shabaha ya kufanya hivyo kwa dola na kanisa ni kuthibiti ukweli.

Hali hii imekuwepo katika nchi zetu za Afrika ikiwemo Tanzania. Na kwa sababu za kihistoria, vyuo vikuu, mathalani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vimekuwa na mahusiano ya moja kwa moja na dola tokea kuanzishwa kwake. Na kwa hivyo vimekuwa vikikabiliana na hamu ya dola kuongeza uthibiti wake kwa muda mrefu. Lakini tokea miaka ya 1980 mpaka sasa vyuo vikuu vya Afrika vikiwemo vya Tanzania vimekuwa vikipata shinikizo kubwa zenye maana na athari mbalimbali.

Moja ya matokeo ya mashinikizo hayo ni vyuo vikuu kupoteza uhuru (autonomy) katika maeneo mbalimbali yakiwemo:

Mosi, maamuzi mengi kuhusu uendeshaji wa vyuo kufanywa na Serikali (ikiwemo miundo ya chuo, ajira, uhamisho, na mikataba ya utumishi).

Pili, msukumo wa kushinikiza vyuo vizingatie mahitaji ya soko kwa hoja kuwa bila kufanya hivyo vitapoteza maana (relevancy).

Tatu, msisitizo mkubwa katika mafunzo ya stadi (skills) badala ya uelimishaji wenye shabaha ya kunoa ubongo wa wanafunzi kuwa na fikra tunduizi. Kwa Chachage,  mwelekeo huu haukuwa na maana nyingine bali kuvigeuza Vyuo Vikuu kuwa vyuo vya amali (Vocational Training School) au glorified High Schools. Kwa muda mrefu Benki Kuu ya Dunia imekuwa ikihimiza mafunzo ya amali dhidi ya elimu ya vyuo kwa misingi na asili ya kazi za vyuo vikuu. Huko nyuma msukumo huu wa Benki ya Dunia ulipata upinzani mkubwa japo katika miaka ya karibuni imefanikiwa kwa kiasi kikubwa baada ya vyuo vikuu vingi vya umma, hapa Tanzania, kubadili mitaala kwa kuzingatia hitaji la mafunzo ya amali.

Aidha katika mwelekeo na msukumo huu kazi ya vyuo vikuu sasa inaonekana kama ni kutoa shahada na vyeti vya kuhitimu (yaani mkazo mkuu uko kwenye meritocracy). Vyuo vinatoa na wanafunzi wanakuja kuchukua, jambo ambalo Chachage alilifananisha na kuvifanya vyuo kuwa kama Supermarket. Na mantiki ya mwelekeo huu msisitizo mkubwa ni ufaulu wa wanafunzi na sio kunoa ubongo ili ufikiri kitunduizi na kutafuta ukweli. Na miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mashambulizi makubwa dhidi ya vyuo vikuu vikilaumiwa na kubezwa kwa kutotoa wahitimu ambao hawako tayari kuajiriwa au kujiajiri. Hili limehusishwa sana na vijana wengi kukosa ajira huku lawama zikielekezwa kwa vyuo kwa kufundisha na kutoa wahitimu wasio na vigezo vya kuajirika. Pamoja na matatizo ambayo vyuo vikuu vya Afrika vinapitia – ikiwemo kukosa rasilimali za kutosheleza mahitaji ya uendeshaji shughuli za kitaaluma, havistahili lawama za aina yoyote kuhusiana na ajira kwa vijana na wahitimu. Chachage alipingana na mtazamo na msukumo huu wa kuvinyima vyuo uhuru.

  1. Uhuru wa Wanataaluma na Wa-Kidemokrasia havitenganishwi

Historia ya demokrasi na ile ya uhuru wa wanataaluma vinalandana na ile ya vyuo vikuu (rejea makala ya Wamba dia Wamba hapo juu). Hii maana yake ni kwamba haiwezekani kutenganisha uhuru wa wanataaluma, wa vyuo vikuu, na ule wa wananchi wote, na hasa wavujajasho. Hii maana yake ni kwamba mapambano ya kudai uhuru wa wanazuoni na vyuo vikuu hayatenganiki na mapambano ya kudai demokrasia kwa watu. Na mara nyingi pale uhuru wa watu unapokuwa umebinywa, ule wa vyuo vikuu nao huathirika na kinyume chake.

Lakini katika dhana hii ya mahusiano ya uhuru wa wanazuoni/wanataaluma, ule wa vyuo na wa watu, si kila mwanataaluma na mwanazuoni atakuwa na ataongozwa na mtazamo huo. Kwa sababu hiyo yapasa kutofautisha wanazuoni wa aina mbili yaani wanazuoni wa mfumo (synthetic intellectual) na wanazuoni wa watu (organic intellectual).

Wanuzoni wa mfumo (synthetic intellectual) wana sifa zifuatazo:

  • Hawana hisia za kiutu na hivyo hawajali wala hawajihusishi na matatizo ya watu wanaoonewa na kunyanyaswa.
  • Wanapenda na kutaka uhuru wa kitaaluma au wa kizuoni, ili kulinda hadhi na heshima zao.
  • Wanahudumia mfumo kwa uaminifu na hufanya hivyo kwa matarajio ya kuzawadiwa heshima, hadhi, na marupurupu (prestige and privileges).
  • Wanaweza kulalamika pale waonapo mfumo (system) hauwapi utambuzi, hadhi, na marupurupu yabebayo vitambulisho vya hadhi zao.
  • Hujitofautisha na kujiweka mbali na mapambano ya jamii inayotaka mapinduzi.

Hawa hawawezi kuona uhuru wa wanazuoni na ule wa vyuo kama sehemu (integral part) ya uhuru wa watu, wavujajasho.

Wanazuoni wa watu (organic intellectuals) wao wanazo sifa zifuatazo:

  • Japo si lazima wawe wavujajasho lakini wana jinasibisha na wavujajasho.
  • Wana utu, na wanaamini katika itikadi ya kitabaka – yaani itikadi ya wavuja jasho (working people ideology).
  • Wanaamsha utambuzi (consciousness) wa kitabaka na kimapinduzi kupinga mfumo wa kinyonyaji na kikandamizaji.
  • Wako tayari kujitolea na kuunganisha maarifa na nguvu zao kwa ajili ya kupigania mustakabali wa haki za watu.

Hawa ni waasi (yaani rebels) wa mfumo uliopo.

Chachage alikuwa ni organic intellectual. Na ndio maana katika jitihada zake za kupigania haki na uhuru aliunganisha nguvu za makundi mbalimbali yakiwemo yale ya wanafunzi, vyama vya wafanyakazi, vyombo vya habari, asasi za kiraia na vyama na vikundi vya wazalishaji wadogo wadogo. Kwa namna hiyo Chachage alishiriki katika mapambano mengi nje na ndani ya  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na ndani na nje ya Tanzania. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilikuwa ni ngome tu lakini mipaka ya uwanja wa mapambano ilikuwa mipana.

Hapa nitatoa mifano minne, mmoja ni wa kesi iliyomkabili mwandishi wa Habari Adamu Mwaibabile ya mwaka 1997. Adamu Mwaibabile alifunguliwa kesi ya kukutwa na nyaraka ya serikali kinyume cha sheria. Akahukumiwa miezi 12 jela. Alikata rufaa dhidi ya kesi ile ya kubambikiwa. UDASA, chini ya uongozi wa Chachage, ilishiriki kikamilifu katika suala lile  kwa kuzileta pamoja asasi mbalimbali za vyombo vya habari, wanasheria, na watu waliojali. Mwaibabile aliachiwa huru baada ya kushinda rufaa yake.

Aidha Chachage, akiwa kiongozi wa UDASA, alishiriki katika kupinga maamuzi mbalimbali ya serikali kuhusu madai ya uboreshaji maslahi ya wanataaluma. Mwaka 2005 UDASA kwa muungano na vyama vingine vya kitaaluma walifanikiwa kuishinikiza serikali kujadili suala hilo na kufikia makubaliano ya kuboresha mishahara ya wanataaluma, mishahara iliyoanza kulipwa kwa awamu kuanzia Januari 2006.

Na mwaka 2002 Jenerali Ulimwengu alipotangazwa na serikali ya Tanzania kuwa si raia, Chachage na wenzake hawakukalia kimya au kuliacha jambo hili lipite kimyakimya. Petition iliandikwa ikipinga uamuzi wa kumtangaza Jenerali kuwa si raia.

Na mfano wa mwisho ni wa mwaka 1998 wakati wanakijiji wa Kazimzumbwe walipochomewa na kubomolewa nyumba zao kwa tuhuma za kuvuka mipaka na kuvamia hifadhi ya Kazimzumbwi. Hatua zilizochukuliwa na serikali dhidi ya wanakijiji hazikuwa za kiutu. Chachage na wenzake wakiwemo viongozi wa DARUSO na waandishi wa Habari walisafiri hadi Kazimzumbwi kuujua ukweli juu ya hatua zilizochukuliwa na serikali dhidi ya wanavijiji na maana yake nini.

  1. Chachage Angekuwepo Leo?

Nimejaribu kumweleza Chachage kwa mapana na marefu kadri nilivyomfahamu kama mwanazuoni. Na kwa namna hiyo yawezekana nimeshajibu swali la ‘angekuwepo angefanya nini?’ lakini kabla ya kujielekeza moja kwa moja kwenye swali nililoanza nalo ni vyema tukajiuliza, je, muktadha uliopo ni uleule aliouacha au umebadilika? Na kama umebadilika umebadilika kwa kiasi gani? Kuna mambo machache ya kimuktadha ambayo nitayabainisha:

Kwanza, Julai 2006 Rais wa Marekani alikuwa George W. Bush na Machi 2003 aliamuru majeshi ya nchi yake kuipiga Iraq. Tuliandamana kupinga uvamizi wa Iraq tukiongozwa na UDASA na vyama vingine vya kiraia. Na baadae tukiwa Chuo Kikuu katika moja ya mikutano ya UDASA chini ya uenyekiti wa Chachage lilipitishwa azimio la kupinga ziara ya Balozi wa Marekani Chuoni Kikuu – Mlimani kama kielelezo cha kupinga unafiki wa Marekani wa kutaka kuonesha kujali na kuunga mkono shughuli za kitaaluma kwa upande mmoja na kwa upande mwingine kuhusika na ubomoaji na uteketezaji wa urithi mkubwa wa kitaaluma katika Iraq. Ikumbukwe kwamba katika operesheni zake nchini Iraq, Marekani ilibomoa na kuteketeza nyaraka za kale katika Chuo Kikuu cha Mustansiriya mjini Baghdad na maeneo mengine ya kihistoria kama vile Maktaba Kuu na Makavazi ya Taifa ya Iraq. Kufuatia upingaji huo Balozi wa Marekani alisitisha ziara yake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Muhimu katika matukio haya ni kwamba serikali ya Tanzania haikuzuia maandamano dhidi ya Iraq kufanyika, na utawala wa Chuo japo haukupenda, haukuweza kuzuia upingaji wa UDASA dhidi ya ziara ya Balozi wa Marekani.

Mwaka huu tunaomkumbuka Chachage ni 2026. Rais wa Marekani ni Donald Trump. Huyu kafanya vitendo vingi vya uvunjifu wa amani na utu – kapiga mabomu Iran, kateka na kumkamata Rais wa Venezuela, kaizuia Cuba kupata mahitaji yake muhimu na ya msingi kwa maisha kama vile mafuta. Katika haya – tumeufyata! Japo kumekuwa na jitihada chache, lakini kwa sehemu kubwa sote tumeufyata.

Na kwa kuongezea, kwa takriban miaka mitatu sasa Israel imeendelea kuua watu wa Palestina – tumekuwa kimya! Lakini wachache waliojaribu kufurukuta hawakuruhusiwa, walizuiwa na mamlaka.

Tofauti ya sasa na mwaka 2006 na miaka ya nyuma kidogo kulikuwa na uhuru mkubwa kuliko hivi sasa. Ndio maana yakaweza kufanyika hayo niliyoyataja kwa jinsi nilivyoyaelezea.

Pili, mwaka 2006 ndio rais Jakaya Kikwete alishika madaraka ya serikali na dola. Kama nilivyoeleza awali kulikuwa na matumaini ambayo hayakudumu kwa muda mrefu. Dola ilianza kuongeza kiwango cha kutaka watu  watii mamlaka bila kuhoji. Hali hii imeendelea kuongezeka kidogo kidogo na kufikia kiwango cha juu sana hivi sasa. Matokeo ya haya ni ukimya, hofu, mashaka, na wasiwasi kutamalaki!

Tatu, tuko katika zama ambazo uongo unalazimishwa kuwa ukweli na ukweli unalazimishwa kuwa uongo. Haya yananikumbusha tamthiliya ya Kivuli Kinaishi ambamo watu waliolishwa unga wa ndele huuangalia ukweli kinyume na uongo hali kadhalika.

Nne, wakati Chachage anaondoka duniani hapakuwa na AI. Lakini kulikuwa na maendeleo makubwa katika matumizi ya kompyuta na Internet. Mwaka 2003, anasimulia Chachage katika moja ya Makala zake, aliombwa kuandaa mhadhara juu ya Uhuru wa Wanazuoni na Wajibu wao katika Jamii. Aliiamuru kompyuta imwandalie mhadhara haikuweza, badala yake ikawa imemuuliza maswali yasiyoeleweka. Chachage alishangilia kwa furaha pale alipobaini kwamba yeye ni bora kuliko kompyuta na kwa maneno yake mwenyewe hivi ndivyo alivyosema: I am happy to announce that I am superior to a computer or any scientific gadget, because I can think!” Leo kuna AI unadhani Chachage angesema au angefanya nini? Sina shaka kuwa pamoja na AI kuweza kuandaa mhadhara bado haiwi bora zaidi ya binadamu, bado binadamu ana uwezo wa kufikiri kuliko AI!

Tano, desturi nyingi za Chuo Kikuu – hasa hiki cha Dar es Salaam – zinakufa kama hazijafa kabisa! Desturi ya kupenda mijadala na kukosoana katika mijadala imefifia sana. Wanataaluma na wanafunzi hawana ari ya kuhudhuria na kushirki katika mijadala, na mijadala yenyewe hutokea kwa nadra sana. Na zipo jitihada za wazi na za chini chini zinazojaribu kuthibiti aina ya mijadala inayofanyika Chuoni. Na kama ilivyo nje ya chuo, wanazuoni na wanafunzi nao hawajiamini, wana hofu na mashaka juu ya wakisemacho!

  1. Chachage angekuwepo Leo!

Sasa turudi kwa Chachage, katika muktadha huu angefanya nini? Mara nyingi tokea mwaka 2006 nimekuwa nikikutana na watu ambao huvuta kumbukumhu nzuri za Chuo Chao – Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Chuo kilichochangamka kwa mijadala, kilichochochea fikra mpya na za kiukombozi, Chuo kilichokosoa Sera na Mipango ya kinyonyaji na kikandamizaji – na kuasi sera na mipango hiyo – dhidi ya Serikali za nje na za ndani, na mashirika ya kimataifa ya kiserikali na binafsi. Na wakumbukapo Chuo Chao huwakumbuka wale waliofanya hayo yatokee au yawe. Na miongoni mwao ni Chachage. Hawa wenye kukumbuka Chuo na kumkumbuka Chachage wako katika makundi matatu:

i. Wanaovutiwa (admirers) – watu waliopendezwa na Chachage na kuvutiwa na:

Namna yake ya kufikiri na kuwasilisha mawazo na hoja zake.

Ujasiri wa kukosoa mamlaka na wenye madaraka.

Misimamo ya kimapinduzi ya jamii na imani yake katika kweli na kutoisaliti.

ii. Wafuasi: wapo ambao waliojitanabahisha kama wafuasi wake – ama waziwazi au kwa kificho.

iii. Makamarade: wako, wachache, ambao walikuwa Makamarade wenzake katika mapambano.

Chachage hayupo nasi, alishafanya yake akiwa hai na katuachia mengi ya kujifunza katika matendo na maandishi yake. Pengine tujiulize tunaposema, ‘sijui angekuwepo angefanya nini leo’, tunamaanisha nini? Mimi nadhani tunamaanisha angalau mambo matatu:

  • Mosi, hatuna social agency, yaani hatuna cha kufanya kwa yanayotokea na kutusibu kama jamii.
  • Pili, katika shida na madhila yetu tunahitaji ukombozi, na ili utokee tunahitaji mkombozi (messiah!)
  • Tunahitaji kiongozi mwasha na mbeba mwenge kwa sababu hatuoni, mbele kuna kiza kinene.

Lakini katika mafunzo yote anayotupa Chachage ni kwamba ukombozi uko mikononi mwetu – na njia kuu ya kuupata ni kujenga umoja na mshikamano wa wale wote wanaoamini kuwa ubinaadamu haugawanyika, yaani humanity is indivisible! Na kama anavyotukumbusha Mwalimu Nyerere kwamba: ‘Utu wa mwanadamu hauwezi kutolewa kwa hisani ya watu wengine. Hauna budi kupiganiwa na wengi wanagandamizwa na hawa lazima wawe tayari kujikomboa kutoka katika minyororo ya unyonyaji’. Na mapambano huanzia tulipo!

[1] Chachage Seithy L. Chachage (2000): Environment, AID and Politics in Zanzibar, Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press (DUP), ix.

MUKTADHA

Mhadhara huu ulitolewa kwenye: Chachage Memorial Dialogue 2026 Friday, 14 2026, Council Chamber, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam