Kwa sababu za kisiasa na mitazamo yao, kuna watu wanasema CCM ife. Wapo pia wanaosema, na hata kunuia kabisa, CHADEMA ife. Wengine wanataka vyama vya upinzani vidhoofishwe au vididimizwe kabisa.
Lakini kuna jambo moja la msingi ambalo hoja hizi zinaonekana kulisahau.
Hizi ni taasisi za kisiasa zenye wajibu kwa umma, na baadhi yake hupokea ruzuku inayotokana na fedha za walipakodi. Yaani, your tax money! Sasa tunaposhabikia taasisi hizi kufa, tunadhani ndiyo tumepata mwarobaini wa matatizo yetu?
Kwangu mimi, haya ni maono finyu mno, tena ya kichoyo mno!
Taasisi hizi zinaendeshwa na watu wanaotoka miongoni mwetu, waliokabidhiwa dhamana mbalimbali. Tatizo haliishii kwenye majina ya vyama vyao. Lipo pia katika fikra, mitazamo, maadili na mifumo inayowaongoza. Na tusijiondoe kwenye picha: mara nyingi fikra hizo zinashabihiana kabisa na fikra za baadhi yetu sisi wananchi.
Imekuwa kana kwamba ugomvi ni wa zamu. Leo wako hawa, kesho wanaingia wengine wenye akili zilezile, mitazamo ileile na tabia zilezile, wakitumia mfumo uleule. Kinachobadilika ni wahusika na nafasi zao, lakini namna ya kufikiri na kuendesha mambo inabaki palepale.
Same system. Garbage In, Garbage Out!
Kwa lugha ya teknolojia, kubadilisha watumiaji wa mfumo pekee hakutoshi ikiwa system software yenyewe ina kasoro. Hiyo ndiyo inayohitaji kuandikwa upya. Yaani, mindset lazima ibadilike!
Ukiangalia kwa makini, utaona vyama vikigombania wanachama wenye mawazo yaleyale, huku watu wenye fikra tofauti, uwezo, maadili na mitazamo inayoweza kuleta mabadiliko wakikosa nafasi. Wengine wanatengwa, wanabaguliwa au wanachujwa na mifumo ambayo haivumilii kuhojiwa.
Tunataka wanachama wengi, lakini je, tunataka pia mawazo mapya? Tunatafuta watu wa kutuunga mkono tu, au watu wenye uwezo wa kutuambia tunapokosea?
Wapo watu wengi katika Taifa letu wenye akili nzuri, maadili safi, uwezo mkubwa na nia njema. Lakini uwepo wao pekee hautoshi. Bila mazingira yanayowaruhusu kusimamia wanachoamini, wanaweza kuingia katika taasisi wakiwa na dhamira ya kuzibadilisha, halafu taasisi hizo zikawabadilisha wao.
Mfumo unawapokea, unawameza, unawazoesha au unawasukuma pembeni.
Hili linaonekana hata katika comments za wananchi, mijadala yetu ya kila siku na matamshi ya baadhi ya viongozi. Mara nyingi tunashangilia kwa kutazama nani amesema, anatoka upande gani na amemshambulia nani. Hoja yenyewe, mantiki yake na manufaa yake kwa Taifa vinakuwa vya pili.
Mtu wa upande wetu akikosea, tunamtafutia sababu. Wa upande mwingine akisema jambo la maana, tunamtafutia kasoro. Halafu tunatarajia viongozi wetu wawe na utamaduni tofauti na huo tunaoulea sisi wenyewe!
Sauti zinazotaka kutuelekeza kwenye fikra mpya, maadili na maslahi mapana ya Taifa zinapoibuka, mara nyingi hupuuzwa, hudharauliwa au hunyamazishwa. Wakati mwingine wenye sauti hizo huchoka na kuamua kukaa kimya.
Na hapo ndipo tatizo letu kubwa lilipo.
Kwa mtazamo wangu, tunachohitaji si kushabikia kufa kwa taasisi hizi. Tunahitaji mapinduzi ya fikra ndani yake na katika jamii yetu kwa ujumla.
Hii haimaanishi kuvipa vyama kinga dhidi ya kukosolewa au kuwajibishwa. Taasisi lazima zihojiwe. Viongozi lazima wawajibike. Lakini tujiulize: tunataka kurekebisha kasoro zinazoturudisha nyuma, au tunataka tu wanaozisimamia waondoke ili nafasi zao zichukuliwe na watu wetu?
Tatizo si uwepo wa CCM, CHADEMA au vyama vingine. Tatizo ni fikra, maadili na mifumo inayozalisha viongozi na tabia zilezile, hata watu na vyama vinapobadilika
Watu wenye fikra mpya, maadili, uwezo na dhamira ya kujenga Taifa wanahitaji nafasi ya kuingia, kushiriki na kuathiri maamuzi ndani ya taasisi hizi. Nafasi hiyo haiwezi kutegemea ukaribu na viongozi, ushabiki au uwezo wa kunyamazia makosa. Inapaswa kujengwa kwa hoja, uwezo, uadilifu na utayari wa kubeba dhamana.
Vilevile, hatuwezi kuendelea kuwatenga wenye fikra huru, halafu tukalalamika kwamba hatuna viongozi wazuri. Hatuwezi kuadhibu wanaohoji, kuwazawadia wanaosifu kila jambo, halafu tukashangaa taasisi zetu zinapokosa uwezo wa kujisahihisha.
Lengo lisiwe kubomoa taasisi ili kujenga nyingine zenye kasoro zilezile. Lengo liwe kubadili utamaduni wa uongozi, namna tunavyochagua na kulea viongozi, mifumo ya uwajibikaji na jinsi tunavyoshughulikia tofauti zetu.
Na mabadiliko hayo hayawezi kuwa jukumu la chama kimoja, serikali pekee au kundi fulani la wananchi. Yanahitajika ndani ya vyama, serikalini, katika taasisi zetu, kwenye jamii na hata ndani ya familia zetu.
Kwa sababu viongozi hawa hawatoki sayari nyingine. Wanatoka miongoni mwetu. Wanabeba sehemu ya fikra, tabia, maadili na mapungufu ya jamii iliyowazalisha.
Mtoto anayekua akiona mwenye nguvu hasahihishwi, mkubwa haulizwi na mwenye fedha husamehewa kila kosa, anajifunza nini kuhusu uongozi na uwajibikaji? Sisi tunaokubali au kushangilia tabia hizo katika maisha ya kawaida, tunapata wapi matarajio kwamba zitatoweka mtu akiingia kwenye siasa?
Hatuwezi kuendelea kulea fikra zilezile, kuimarisha mifumo ileile na kuchagua kwa misingi ileile, halafu tukatarajia matokeo tofauti.
Tusipokuwa makini, hata wale tunaowaona leo kuwa mbadala wa matatizo yetu wanaweza kesho kuwa sehemu ya matatizo yaleyale. Si kwa sababu matumaini yote ni bure, bali kwa sababu matumaini bila mabadiliko ya fikra na mifumo yanaweza kuturudisha tulipoanzia.
Ndiyo maana naamini mapinduzi tunayoyahitaji zaidi hayaishii katika kubadilishana zamu za madaraka. Yanahusu namna tunavyofikiri, tunavyoongoza, tunavyowajibika na tunavyolitazama Taifa letu.
Taasisi zinaweza kudumu kwa vizazi vingi. Watu hupita. Lakini tukirithisha mifumo mibovu ya fikra kutoka kizazi kimoja kwenda kingine, hata taasisi mpya zitabeba matatizo ya zamani.
Kwa mwendo huo, kama Taifa, tutaendelea kuimba sana, kugombana sana, kulaumiana sana na kubadilishana zamu sana, lakini hatutoboi!
Ni yaleyale, kwa sura tofauti.
Tunahitaji kubadili fikra na mifumo inayozalisha matatizo, pamoja na kuwawajibisha watu wanaoyasimamia. Kubadilisha wahusika pekee hakutoshi.
Leave A Comment