Kutumbuliwa Kwa Kitwanga Kunaashiria Kitu Kipi?

“Wale wasioweza kuyakumbuka yaliyopita wamehukumiwa kuyarudia” – George Santayana


“Uwendawazimu ni kuyarudia yale yale na kutegemea matokeo tofauti” – Albert Einstein

Chambi Chachage

Uamuzi wa Rais Magufuli kutengua uteuzi wa (aliyekuwa) Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, umepokelewa kwa msisimko katika mitandao ya jamii. “Hii”, anadai Mtanzania mmoja katika Twitter, “haijawahi tokea tangu Tanzania iumbwe”. Mhariri mfawidhi wa gazeti maarufu anaungana naye kwa kusema“Haijapata kutokea. Namba inasomeka kila kona #Tanzania”.

Mtetezi wa mchakato wa kuwapima watu kiuchunguzi kabla ya uteuzi wao (vetting)  anasisitiza kwamba kilicho muhimu ni ‘tiba’. Naye mwandishi mahiri wa vitabu vya ‘ushushushu’ amempongeza Mtumbua Majipu kwa ‘kutwanga’ baada ya kilio chetu ‘kumbipu’.

Hata mwanasiasa machachari na mbunge pekee wa chama kinachochipukia kwa kasi cha ACT-Wazalendo naye kaguswa:

“Uamuzi wa Rais kumfukuza kazi Waziri wa Mambo ya Ndani unatuma ujumbe mmoja – hataki mchezo. Rais amethibitisha kuwa anao uwezo wa kutumbua hata aliowateua. Ni maamuzi muhimu sana kwa Kiongozi wa aina yake.  Wale vijana waliokuwa wanatumwa kumtetea wasimame kumtetea. Rais kaonyesha Uongozi ‘ no nonsense ‘”

Hakika Rais anastahili pongezi nyingi. ‘Tusimbanie’. Hongera sana! 

Wakati tunaendelea kumpongeza pia tukumbuke ‘hapa kazi tu’ kwa wanahistoria ni kuyafukuafukua  makabrasha ili kujaribu kuelewa tumetokea wapi katika masuala fulani, tupo wapi na tunaelekea wapi ili tusije tukayarudia (makosa) yale yale kiuwendawazimu.

Historia ya kisiasa inaturudisha kwenye kampeni za uchaguzi za mwaka 2015. Pale tunakutana na maneno haya ya Magufuli:

“Mmemuona Kitwanga. Huyu ni rafiki yangu. Nataka niwaeleze: Chuo Kikuu nimesoma naye. Namfahamu kweli kweli. Na nataka niwaeleze nampenda. Ndiyo maana nimekuja hapa kumwombea kura. Ninaomba mumlete Kitwanga awe Mbunge wa jimbo hili.  Ninafahamu wapo watu wachache wanapiga piga ma ma nhe wanapiga piga maneno. Mwembe wenye matunda ndiyo unapondwa mawe na watoto…. Mtu anaweza akawa hapa mkamuona ninyi kuwa hafai lakini kumbe ndiyo faida ya Misungwi. Mkachukua hatua za kumwadhibu…. siasa saa nyingine zinaweza zikatumika kama baba asiye na busara…. majuto huwa ni mjukuu….”


Kwa wafuatiliaji wa kila kichesemwacho watakumbuka kuwa hata baada ya kuwa Rais, Magufuli alinena maneno kama hayo kuhusu wateule wake wengine alipokuwa akihutubia pale Kinyerezi:

“Na ndiyo maana Profesa Muhongo niliamua kukurudisha hapo. Na saa nyingine vitu vizuri vinapigwa vita. Hata Makonda alikuwa anapigwa vita, nikamwambia anabaki hapa hapa Dar es Salaam. Ili mbaya wao wamwone yuko hapo hapo tena bosi zaidi. Kwa sababu mwenye kuamua kuchagua ni mimi. Kwa hiyo nikishasali na kuswali na kumwomba Mungu ananiambia leo ni Makonda Dar es Salaam, ninampa! Na wenye chuki wajinyonge zaidi. Na ndiyo maana nilikaa nikasema Profesa Muhongo hapa hapa. Sichagui mwanasiasa. Mimi nataka mtu mchapakazi…. Na ndiyo maana ilibidi nichague watu ambao watachapa kazi kwa manufaa ya Watanzania wote bila kuwabagua vyama vyao. Na hiyo ndiyo dhana halisi ya ‘Hapa Kazi Tu….'”

Mbinu hii ya uteuzi na utetezi ni ya aina yake. Inaleta ugumu na ukakasi hasa kwa wadadisi wanaotaka kujua vigezo vyote ambavyo Rais wetu hutumia katika kuteua. Tukumbuke mwaka jana Udadisi iliwahi kuhoji majibu yafuatayo ya Rais na haki yetu ya kikatiba ya kupata habari/taarifa kuhusu masuala muhimu ya nchi yetu pale wanahabari walipojaribu kuhoji mantiki ya idadi ya manaibu waziri kwa kuzingatia uunganishaji wa wizara na vigezo vilivyotumika kuwarudisha mawaziri kadhaa kutoka kwenye Baraza lililopita:


Magufuli: Kafanye utafiti kwanza uangalie hiyo Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia sera, Bunge, ajira, vijana, walemavu, tumeunganisha Wizara ngapi… tumeweka Manaibu Waziri wawili. Utapata jibu lake.


Magufuli: Kwanza kwa sababu umekosea hata kupiga hesabu, kafanye hesabu vizuri. Kwa awamu iliyopita Mawaziri waliorudi ni saba sasa umesema kumi. Kwa hiyo, ukirudi huko ukapiga vizuri hesabu zako, utaelewa ni vigezo gani nilivyovitumia.

Baada ya kashfa nzito ya Lugumi kuibuliwa na mti wa Kitwanga kupondwa mawe na wapinzani, tumekuwa tunajiuliza kama vigezo vyote vya ‘vetting’ vilizingatiwa ilikuwaje akateuliwa kuwa Waziri na Mkombozi wetu wa kupambana na ufisadi nchini? Tunaoamini kuwa wanasiasa wa ‘mjengoni’ Dodoma wanajuana kwa vilemba, maneno haya aliyoaandika aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) yalituacha mdomo wazi:


“Namsihi Waziri Kitwanga amalize matatizo yake yeye mwenyewe. Yeye kama mmiliki wa Kampuni ya Infosys yenye mkataba na Serikali katika Wizara anayoongoza sasa anapaswa aone ni namna gani hana mgongano wa maslahi. Waziri Kitwanga asitafute watu wa kuwatupia lawama kwenye mambo yanayomhusu. Mimi binafsi sijawahi kugombana na Charles Kitwanga. Hajawahi kuwa rafiki yangu. Hajawahi kuni excite kama Kiongozi ( kimsingi nashangaa mtu kama yeye kuweza hata kuwa Waziri wa Wizara nyeti kama hiyo) . Zaidi ya yote Waziri Kitwanga sio ‘size yangu’. Kwa protokali za Uongozi, size yangu mimi ni Rais Magufuli, bosi wake. Naanzaje kuhangaika na Kitwanga? Ili iweje? Namsihi asijipandishe chati kwamba mimi nataka kumtoa. Ningetaka kumtoa wala asingejua maana ningeshughulika na aliyemteua. Nasema haya sababu amekaa na Waziri Mkuu na Wabunge kadhaa akilalamika kuwa nataka kumtoa Uwaziri. Asinipe dhambi, Uwaziri atatolewa na aliyemteua kwa madhambi aliyofanya. Asitafute bangusilo!” 

Lakini cha ajabu zaidi mnamo mwaka jana mtandao unaopigwa vita (na mafisadi) wa Jamii Forum ulitumika kuweka maneno haya:


“Ndugu zangu, mhe Rais amejipambanua kuwa atateua watu ambao ni wachapa kazi katika baraza lake la mawaziri. Naomba niwafahamishe tena kwa uhakika kuwa Charles Kitwanga aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ni mndani (msiri) wa mhe Rais.  Kitwanga alikwishaanza kujisifu kuwa atakuwa waziri wa wizara nyeti mapema kabisa na ushahidi upo. Lakini la pekee kubwa ni kuwa ni mtu asiyekuwa na rekodi ya utendaji wa kuwa waziri wa mambo ya ndani amepewa wizara hiyo sababu ya nepotism.  Muda utaamua na ni vema watanzania muelewe hata mhe Rais Magufuli na yeye pia kashindwa kuficha urafiki wa mtandao wake kinyume na kampeni zake.  Kitwanga atakuwa waziri wa kwanza kufukuzwa na bunge, ni suala la muda tu”


Je, ‘vetting’ haikuziona ishara hizo za nyakati? Kama haikuziona, hata Mungu wa Magufuli hakuyaona yote haya? Sikio lake la yeye awekaye na aondoaye watawala ni zito hadi asisikie maombi hayo?

Mwisho kabisa historia yetu inatukumbusha kwamba Rais wa awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alipigiwa kelele asiteue baadhi ya watu lakini akawateua tu. Matokeo yake Baraza la Mawaziri likavunjwa baada ya miaka miwili tu tena baada ya fedha nyingi kutumika kuwafanyia semina elekezi mawaziri kwenye hoteli ya kihafahari ya Ngurdoto. Kwa miaka kumi kazi kubwa ikawa ni kuweka/kuziba viraka ambapo katika Wizara moja tu mawaziri walibadilishwa zaidi ya mara tatu – kutoka kwa Naziri Karamagi kwenda kwa Ibrahim Msabaha kisha kwa William Ngeleja halafu Sospeter Muhongo hadi George Simbachewene – na Waziri wake mmojawapo, Shukuru Kawambwa, alihamishwa zaidi ya mara tatu.

Gazeti la Mwananchi linatukumbusha kwa miaka 10 Serikali hiyo ya ‘Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya (‘ANGUKA’) na ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’ ikaishia kutumikiwa na“mawaziri 120” huku JK akitema “mawaziri 60”. Unawezaje kuendesha Serikali endelevu, thabiti na sikivu katika mazingira hayo ya kupanga na kupangua kila kukicha? Hakika kuwajibika na kuwajibishana ni muhimu katika kujenga utawala wa kitaasisi unaodumu kuliko utawala kinyonga na tegemezi kwa kiongozi mmoja mmoja.


 Ila kinga ya ‘vetting’ si ni bora kuliko dawa ya kutumbua majipu?