Siku Bunge Lilipopitisha Sheria ya Kucheka

Na Francis Salehe Mbuzi


Ilikuwa bado mapema, ndio kwanza saa moja na dakika zake changa lakini mandhari ya nje hayakuakisi muda. Mionzi ya jua ilichachamaa. Ule ukimya wa usiku ulishatoweka; mchuuzi wa mboga alipita akinadi ‘spinachi, majani ya maboga, mchicha, tembele’; mara mwingine na kipaza sauti chake alisikika akisajili laini; yote tisa, sauti ya Mzee muuza samaki ndio iliyomuamsha Iddi kutoka usingizini, ‘wapya, wabichi, bado wanarukaruka, wa leo leo samaki hao…’

Jumamosi haikuwa na maana tena ya mapumziko kwake, dirisha lake lililokuwa kando kabisa na barabara lilimfanya ayasikie yote yanayoendelea duniani. Iddi alisalia kitandani akiwa ameulalia mgongo, macho yake kayafunga lakini alikuwa macho akitafakari. Alikaa hivyo kwa muda na taratibu usingizi ukaanza kumuita tena. Ile anauaga ulimwengu na kuingia katika sayari ya njozi, ilisikika sauti ya Vyuma, jina la kijana aliyekuwa akinunua vyuma chakavu, akisema kwa kurudia rudia, “nanunua vyuma chakavu, kwako uchafu, kwangu dhahabu.” Vyuma alifahamika mtaani kote kwa sababu ya ukali wa sauti yake aliyoipaza na kusikika hata mtaa wa tatu toka mtaa aliopo.

‘Hivi nini maana ya wikiendi kama nashindwa hata kupata muda wa kupumzika,’ saa hii Iddi alilalama huku akiwa amesimama anakunja shuka na kisha kutandika kitanda. Huyo alitoka chumbani akapita uani kwenda kunawa kabla ya kuelekea sebuleni. Alifungulia mziki mkubwa na aliingia jikoni kujiandalia chai. Leo majirani walijua Iddi yupo, kutokana na kazi yake kuwa Mombasa, Fimbo ya Mboto yeye akitokea Tegete Nyaishoni, ilimlazimu kudamka mapema sana, hivyo yeye alikuwa wa kwanza kuondoka na wa mwisho kurudi. Alionekana wikiendi na siku za sikukuu tu.

Tayari ameshapata chai, sasa Iddi alikuwa kajilaza kwenye kochi, huyo na simu yake akaanza kutembelea mitandao ya kijamii. Moja kwa moja akaingia twita. Hakuwa mtandaoni tangu alhamisi usiku alipoingia kulala, hivyo jumbe zilikuwa nyingi sana. Ni mengi yalimpita kwa kutokuwepo siku moja. Ile anaambaa ambaa, mara huku mara kule, alishangazwa kuona kila mtu akiongelea juu ya suala la kucheka na haki ya kucheka. Gumzo lilikuwa #HakiYaKucheka.

‘Kucheka kumefanyaje? Haki ya kucheka… kwani suala la kucheka nalo ni la haki za binadamu?’ Alikuwa na maswali mengi. Kutokana na utitiri wa jumbe, aliamua kutembelea tovuti ya Miadi ya Akyo maana aliamini huko angeweza kuelewa kinaga ubaga juu ya habari hiyo. Alijiambia ni lazima Akyo atakuwa ameliongelea hilo suala kwa kina katika kipengele pendwa na kikuu cha tovuti.

Haikumchukua hata sekunde 10 kuipata habari hiyo, alikaribishwa nayo ikiwa imeshikiliwa mwanzo kabisa, “Bunge lapitisha Sheria ya Kucheka”. ‘Makubwa haya, sheria ya kucheka tena!’ Alijisemesha huku akiwa amebonyeza kufungua kuisoma habari nzima. 

Bunge la Jamhuri ya Changanyika, leo hii tarehe 20 Februari 2020, limepitisha Sheria namba 20 ya mwaka 2020 inayofahamika kama Sheria ya Kucheka. Sheria hii imepitishwa katika wakati ambao asilimia 92 ya wabunge wa kambi ya upinzani wakiwa nje ya bunge, wakisusia vikao vya bunge, jambo ambalo Spika wa Bunge, Mheshimiwa Kazi Ndugu, alisema haliwezi kuingilia shughuli za bunge. Hatua hiyo ya wabunge wa upinzani imeshuhudia sheria hii kupitishwa bila kupingwa.

Katika majadiliano na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Mbunge wa Jimbo la Sukarini, Mheshimiwa Patrick Limwezilikali, amesema sheria hiyo imekuja katika wakati mzuri na sheria hii inaunga juhudi ya Serikali ya Awamu hii. Mheshimiwa Limwezilikali ameeleza miongoni mwa mambo mengine kuwa, sheria hiyo inaunda TUME YA VICHEKO CHANGANYIKA (TUVICHA) ambayo ndio itakayokuwa na wajibu wa usimamizi wa sheria hii.

Sheria hii pia inaeleza kuwa mtu yeyote atapaswa kulipia leseni kama anataka kucheka, ambapo katika kuikata leseni hiyo, lazima mtu aeleze atakuwa anacheka kwa ajili gani, anachekea wapi na atacheka kwa muda gani. Pia tume hiyo itakuwa inatoa vibali maalum kwavajili ya wachekeshaji, hawa watasema wanataka kuchekesha nini, watakuwa wanamchekesha nani, wapi, kwa muda gani na malipo ya vibali hivyo itabidi mchekeshaji alipe kwa ajili ya leseni ya wale wote anaokusudia kuwachekesha.

Mheshimiwa Limwezilikali, ameeleza pia kuwa sheria hiyo itakuwa ni chanzo cha mapato kwa serikali. Naye aliyasema haya, “Hizi leseni ni hela. Pia kuna faini kwa wale watakaokuwa wanavunja sheria hii. Sheria hii ni ubunifu mujarabu wa Mheshimiwa Rais Yusufu Manguvu na sisi kama wabunge tumeipitisha ikiwa ni sehemu ya kukuza uchumi wetu kama taifa.

Mbunge huyo, Limwezilikali, aliendelea kueleza kwa hisia kali kuwa sheria hiyo pia ni sehemu ya kuendeleza ajenda na kaulimbiu ya PIGA MZIGO! iliyoasisiwa na Mheshimiwa Rais wetu. “Sasa hatuwezi kusema PIGA MZIGO! alafu tukaendelea kuwa na jamii inayocheka cheka. Sasa kama watu wanataka kuendelea kucheka cheka, wacha waendelee kucheka kwa manufaa ya taifa, na hiyo ni kwa vicheko vyao kuchangia katika uchumi wa nchi.”

“Makubwa!” Iddi alibaki akistaajabu tu, hakuamini yale aliyoyasoma. ‘Kweli tumefika huku.’ alijiuliza maswali rundo pasi kuwa na jibu hata moja. Sasa alielewa zile kelele za kule twitani. “Haki watu wana haki ya kuhoji… leseni ya kucheka na hapo hapo lazima pawepo na msajili wa vicheko. Sio mazuri haya ila yanachekesha,” alizidi kujiongelesha huku sasa akiwa anaenda katika kundi lake la Whatsapp la Vibonzo kuona watu wana maoni gani na sheria hiyo.

Huko nako watu walilaani sheria hiyo. Wengi wao ni wachekeshaji, wao hata hivyo walikuwa wanalaani kuwa vibali hivyo vilivyowekwa vilikuwa ni vya gharama za juu sana. Majonzi na masikitiko ya huko akayaona jau, hivyo akarudi twita na huko akaendelea kuona mtanange kati ya #MabadilikoChanganyika na #MACHAGA – Make Changanyika Great Always.

Huku na kule, Iddi akapata wazo la kibonzo. Akachukua picha ya Maalim Salif akiwa amevalia bonge la suti, suti bwanga, huku akiwa ameshika mkoba wake naye anarudi nyumbani na mtoto wake anamkimbilia, kwenye picha akaandika – “Pale Msajili wa Vicheko anaporudi nyumbani”, pembeni ya picha hiyo palikuwa na picha yake Iddi akiwa anacheka.

Kibonzo hicho hakikuchukua masaa na kikawa gumzo mtandaoni kote. Usiku huo huo, Iddi akapokea simu ya wito kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi. Iddi hakuwa na budi na aliitikia wito huo na hapo hapo akafunguliwa mashtaka ya jinai ya ukaidi na uvunjifu wa sheria ya kucheka, uchochezi wa kifamilia dhidi ya familia ya msajili wa vicheko na uhujumu uchumi kwa kulipotezea taifa shilingi milioni 200 kwa kibonzo alichokituma.

Watu wengi walimuonea huruma Iddi kwa kuwa mtu wa kwanza kuwa mhanga wa sheria hiyo. Wengine walienda mbali na kumlaani, wakieleza kuwa kwa yote yaliyomsibu alikuwa amejitakia na ni matokeo ya ujinga wake. Hapo ndipo zikaanza tambo mtandaoni za #UsiweKamaIddi na #UjingaWaMtotoIddi na wengine wakiimba:

Mtoto Iddi kajizulia balaa… Mtoto Iddi kajizulia mikosi… Mtoto Iddi alijawa na sifa… Anahitaji kuadabishwa!