By Richard Mabala (@MabalaMakengeza)

Siri ya mtungi aijua kata?
Nakaa huko mtungini, nikitulia gizani
Kila kilicho ndani, naona bila miwani
Mabaki yake majani, mende alofia chini
Hata nyufa ukutani naziona, hamzioni

Sasa hebu shangaeni, kata asiye na soni.
Eti siri za ndani, yeye ndiye namba wani
Atajua kitu gani, si mkazi mtungini
Aingia kwa idhini ya kuchota tu kazini

Nastaajabu hiyo kata, inavyopenda kubwata
Eti siri azipata, Kwa mimi kunifuata
Juujuu anachota, hanidumbukii hata
Kwa kweli anadata, kwa aibu atafyata

Awadanganya jamani, hadi methali tungeni
Siri yake mtungini, eti kata amebuni
Kiburi chake mwishoni mtakuja kubaini
Siri yake mtungini ni ya maji ya ndani

Tuingie mfanoni, tunapokaa sokoni
Hali yetu ya ndani, wanaojua ni nani?
Ni wakazi au wageni, mtambao magarini
Mwasimama jukwaani, kufoka na kulaani

Hamtaki kueleza, akili kuchokoza
Kwa elimu tutaweza, panga na kutekeleza
Mwaweza kusikiliza, tutakavyopendekeza?
La! Mwapenda kujikweza, amrisha na elekeza

Akili zetu timamu, ya maisha tuna hamu
Pamoja na kujikimu, kotekote ni muhimu
Uwiano ni mgumu, uhai na kujikimu
Tuishinde hiyo sumu, maisha yetu kudumu

Nimegusia sokoni, lakini pia nyumbani
Pamoja na mitaani, kwetu sisi mtungini
Siri zote za ndani, najua mimi na jirani
Hebu tusikilizeni, pamoja tupangeni

Taaluma mnaweza, nadharia kueleza
Kutafsiri tunaweza mwapaswa kusikiliza
Sisi tukipendekeza ndipo COVID tutaweza
Lakini mkitubeza, virusi vitatumeza

Comments Off on Siri ya Mtungi aijua Kata?