Wagiriki Wametimiza Ndoto ya Nyerere
*Wapiga kura kuyakataa masharti ya IMF
**Shivji asema tulichoshindwa Waafrika, Wakigiriki wamekiweza
Na Mwl. Sabatho Nyamsenda
Jumamosi, Julai 4, 2015, tulikuwa katika mabishano makali
kwa njia ya barua-pepe. Wanafunzi wenzangu wa shahada ya uzamivu walikuwa
wakitaka walipwe fedha ya kujikimu inayoendana na viwango vya nchi tajiri.
Iwapo viwango hivyo vitakubalika, basi mwanafunzi mwenye familia atakuwa
akilipwa kiasi cha dola 2,500 (sawa na shilingi milioni tano) kwa mwezi.
Mie nilikataa. Nilisema kuwa kiasi hicho ni kikubwa sana
kulinganisha na hali halisi ya nchi za Kiafrika. Hakuna chuo chochote hapa
Afrika kinachotoa kiwango hicho cha fedha. Zaidi ya hapo, fedha zote hutegemea
ufadhili, na iwapo ufadhili utakatika ndio utakuwa mwisho wa masomo. Kwa
vyovyote vile, ili ufadhili uendelee ni lazima tufumbie macho uporaji wa
rasilimali za Afrika unaofanywa na nchi za kibeberu. Tukiukataa unyonyaji na
uporaji huo, hakuna ufadhili! Nilitoa sababu nyingine: malipo hayo yatazalisha
wasomi walafi, ambao, kama walivyo wanasiasa wetu, wataenda kuwakamua wanyonge
ili wajilipe mishahara minono na “miposho” mikubwa.
Kwa kuwa wengi walichagua upande wa walafi, nilichofanya ni
kujiuzulu nafasi yangu ya ujumbe wa kamati ya uandishi wa sera ya fedha za
kujikimu. Nilisema nisingependa historia iniweke katika upande wa walafi.
Nikimnukuu Alexis Tsipras, waziri mkuu wa Ugiriki, nilisema siwezi kuwa
mwandishi wa “kila tokeo”.
Naam, Tsipras alisema kuwa hawezi kuwa “waziri mkuu wa kila
tokeo” (“I cannot be prime minister of every outcome”). Hii ilikuwa ni baada ya
“utatu mtaka-vitu” (Troika) unaoundwa na nchi za sarafu ya euro (Eurogroup),
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pamoja na Benki ya Biashara ya Ulaya (ECB)
kuilazimisha Ugiriki kukumbatia sera za uliberali mambo-leo zilizoisababishia
Ugiriki dhahama kubwa.
Hivi sasa karibuni asilimia 50 ya vijana wa Ugiriki hawana
ajira, huku serikali ikiwa imejiondoa katika utoaji wa huduma za msingi. Na
bado Troika wanailazimisha Ugiriki iongeze kodi kwa walalahoi, iondoe pensheni
kwa wastaafu pamoja na ruzuku kwa wanyonge. Masharti mengine ni pamoja na kutoa
misamaha ya kodi kwa kampuni za kigeni na kubinafsisha kampuni za umma.
Tsipras na serikali yake walikataa. Walisema kuwa sera hizo
ni za kijambazi na za kiuaji na zinainyima Ugiriki haki ya kujiamulia mambo
yake yenyewe. Serikali inayoongozwa na Tsipras ikajiondoa katika mazungumzo
kuhusu mikopo mipya, na ikagoma kuendelea kulipa deni inalodaiwa na Troika. Na
ikaitisha kura ya maoni ili wananchi wa Ugiriki waamue kama wanataka kufuata
masharti ya “Troika” ama la. Tsipras mwenyewe alitishia kujiuzulu iwapo upande
wake ungeshindwa, akisisitiza kuwa hakuwa tayari kutekeleza sera za kiuaji.
Japokuwa mwanzoni niliuunga mkono umamuzi huo wa Tsipras
baadaye nilianza kuutilia shaka. Chama cha SYRIZA kiongozwacho na Tsipras kina miezi
sita tu madarakani, na hakijapata wakati wa kujidhatiti ili kutekeleza sera
zake za kijamaa. Niliwaona SYRIZA wakichezea shilingi katika tundu la choo.
Kingine kilichonipa mashaka ni pale vyama vya kibepari
vilipoungana na “Troika” kuihujumu serikali ya SYRIZA. Walitunga mbinu nyingi kuwahadaa
wananchi kuwa iwapo upande wa “hapana” ungeshinda basi Ugiriki ingetimuliwa
katika ukanda wa sarafu ya Euro na isingepata mikopo, hivyo kungekuwa na
ufukara wa kudumu.
Serikali ya Ujerumani ambayo ndiyo “kaka mkubwa” wa ukanda
wa Euro, ndiyo hasa iliyoongoza kampeni dhidi ya SYRIZA. Siku moja kabla ya
kura ya maoni, mashabiki wa SYRIZA nchini Ujerumani waliukatisha mkutano wa Kansela
wa nchi hiyo, Angela Markel, wakiwa wamebeba mabango ya OXI (hapana). Baada ya
“wavamizi” hao kuondolewa, Merkel, kwa mbwembwe, akawataka Wagiriki kupiga kura
ya NAI (ndiyo).
Mpaka siku moja kabla ya kura ya maoni, vyombo vya habari vya
kibwanyenye viliripoti kuwa wananchi wa Ugiriki wamegawanyika sawa kwa sawa
kuhusu kura ya maoni, na kulikuwa na uwezekano wa upande wa “ndiyo” kushinda.
Majuma machache kabla ya Serikali ya SYRIZA kujiondoa katika
mazungumzo, Tume ya Kuchunguza Uhalali wa Deni la Ugiriki ilitoa taarifa yake
ya awali. Kwa ufupi taarifa ya Kamati
hiyo inasema kuwa serikali ya Ugiriki iliyokuwa ikiongozwa na vyama vya
kibepari, ilipanga njama za kukopa fedha kwa kushirikiana na “Troika” huku wakijua
kabisa kuwa Ugrikiri isingeweza kulipa
madeni hayo. Zaidi ya asilimia 90 ya fedha hizo zilichukuliwa na benki na
kampuni za kibepari, huku kiasi kilichoenda serikalini kwa ajili ya matumizi ya
wananchi wa kawaida ni pungufu ya asilimia 10.
Taarifa hiyo inazidi kubainisha kuwa tangu Ugiriki ilipoanza
kufuata sera za uliberali-mamboleo miaka ya 1980, deni la serikali lilianza
kupaa. Kupaa huko hakukutokana na matumizi makubwa ya serikali, bali kulitokana
na riba kubwa zilipwazo kwa wakopeshaji pamoja serikali kutoa ruzuku za mitaji
kwa benki na kampuni binafsi. Ukopaji wa fedha hizo ulikiuka taratibu za
kisheria na ulienda kinyume na matakwa ya wananchi.
Taarifa hiyo ikaweka msimamo:
“Ushahidi wote tunaouwasilisha katika taarifa hii unaonyesha
kuwa Ugiriki haina uwezo wa kulipa deni hili, lakini pia haipaswi kulilipa kwa
sababu deni hilo litokanalo na mipango ya ‘utatu mtaka-vitu’ (Troika) ni
ukiukwaji wa haki za msingi za watu wa Ugiriki. Kwa hiyo, tumefikia hitimisho
kuwa Ugiriki isilipe deni hilo kwa sababu ni la kilaghai, haramu na la kionevu”
(tafsiri yangu).
Taarifa hiyo inaungwa mkono na wabunge walio wengi katika
Bunge la Ugiriki, pamoja na Chama cha SYRIZA, ambao wote wanaitaka serikali igome
kabisa kulipa deni hilo.
Sasa sauti za wananchi wa Ugiriki zimepigilia msumari.
Matokeo ya kura ya maoni iliyopigwa Jumapili, Julai 5, 2015 yamethibitisha
matakwa ya wengi. Asilimia 61.3 ya waliopiga kura wamesema “HAPANA”, huku
waliosema ndiyo wakiwa ni asilimia 38.7 tu. Wengi wape. Wagiriki wameamua
kuzikataa sera za kiuaji za uliberali mambo-leo.
Yalipotangazwa matokeo nilijikuta nikitoka nje kushangilia.
Muda mfupi baadaye, nikapokea ujumbe wa simu kutoka kwa Profesa Issa Shivji,
ambae hakuficha furaha yake: “Hili ni jambo jema sana. Watu wa Ugiriki
wameukataa uendawazimu wa sera za uliberali-mamboleo. Tulichoshindwa kukifanya
Afrika kama bara, wamekifanikisha kama nchi” (tafsiri yangu).
Nami nilimjibu: “Huwezi kujua furaha niliyonayo. Nimekuwa nikiufuatilia
mjadala wa Ugiriki kwa karibu sana. Wagiriki wameandika historia. Nikitumia
maneno ya mwanamapinduzi Lenin, ukuta wa uliberali mamboleo umeoza na unatweta.
Tunachotakiwa kufanya ni kuusukuma ili uanguke”.
Wagiriki wametimiza ndoto ya Mwalimu Nyerere. Kinachotokea
Ugiriki hivi sasa hakina tofauti na kilichoikumba Tanzania miaka ya 1980 ambapo
IMF kwa kushirikiana na Marekani na Uingereza waliilazimisha Tanzania kuachana
na sera za kijamaa ili kukumbatia sera za uliberali mamboleo. Mwalimu aliigomea
IMF huku akiuliza, “When did the IMF
become an ‘International Ministry of Finance’? When did nations agree to
surrender to it their power of decision making?” (Kwa tafsiri isiyo rasmi,
“Tangu lini IMF imegeuka kuwa Wizara ya Kimataifa ya Fedha? Tangu lini mataifa
yalikubali kusalimisha mamlaka yao ya kujiamulia mambo yao kwa IMF?)
Na hapo ndipo Mwalimu alisisitiza kuhusu msimamo wa
Tanzania: “Tanzania haiko tayari kushusha thamani ya fedha yake eti kwa sababu
hili ndilo suluhisho la kimapokeo la ‘Soko Huria’ kwa kila kitu bila kujali
maslahi yetu. Tanzania haiko tayari kusalimisha haki yake ya kudhibiti bidhaa
ziagizwazo toka nje, kwa hatua zilizolenga kuhakikisha kuwa tunaagiza dawa za
hospitali badala ya vipodozi, au mabasi badala ya magari ya watu binafsi kwa
ajili ya vigogo. Serikali yangu haiko tayari kuachana na jukumu letu la msingi
la kutoa elimu ya msingi kwa kila mtoto, huduma za matibabu ya msingi na maji
safi na salama kwa ajili ya watu wetu wote”.
Katika hotuba hiyo, iliyotolewa katika hafla ya kuukaribisha
Mwaka Mpya 1980 iliyoandaliwa kwa ajili ya mabalozi, Mwalimu alisisitiza: “Na
juu ya yote hayo tutaendelea na jukumu letu la kujenga jamii ya kijamaa”.
Mwalimu hakufanikiwa katika harakati zake za kuizima IMF na
kuzizika sera za uliberali mamboleo. Ndani ya Chama chake na serikalini
kulikuwa na kundi kubwa lililoshirikiana na wahujumu uchumi kuuteketeza ujamaa.
Kundi hili lililoungwa mkono na IMF na nchi za kibeberu lilipata nguvu zaidi.
Mwalimu alipoondoka maradakani, serikali ya Mwinyi ilisaini
mkataba na IMF, na kisha zikaanza zama mpya za ubinafsishaji wa mashirika ya
umma, uporaji wa machimbo na ardhi ya wachimbaji wadogo na wakulima, serikali
kujiondoa katika utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi wake, na ufisadi
mkubwa wa kutisha.
Duniani kote hivi sasa wanyonge wameunganisha nguvu kuzikataa
sera hizi. Katika bara la Amerika ya Kusini, wanyonge wa nchi hizo wamevichagua
vyama vya kijamaa kuongoza katika nchi za Cuba, Ecuador, Nicaragua, Venezuela
na Bolivia. Nchini Brazil, Argentina na Uruguay vipo vyama vya mrengo wa kati,
lakini vyenye kupinga uliberali mamboleo. Huko Ulaya, baada ya SYRIZA kuingia
madarakani, vuguvugu la kijamaa limepata nguvu kubwa sana katika nchi za Italia
na Hispania.
Vuguvugu hili la kuubomoa ubepari litafanikiwa. Kama alivyopata kusema Mwalimu mwaka 1972, “Mabeberu na wabaguzi wa rangi watatoweka; Vorster na wenzake kama yeye watazuka na watatoweka. Kila beberu na mbaguzi wa rangi ni mnyama wa aina fulani; na aina hizo za unyama hazina nafasi ya kudumu. Hatimaye zitatoweka! Afrika lazima ikatae kusukumwasukumwa na kunyonywa.”