Tutaishije bila Falsafa
Mpya ya Kifo?
(*Buriani Esther Lameck
Mwamukonda*)
Chambi Chachage
Ninaogopa kufa. Kifo kweli hakina
huruma! Lakini mbona kinaonekana kana kwamba kina upendeleo wa wazi kabisa?
Kifo kimeuandama mtaa niliokulia. Nikiutazama
uwanja wetu wa mpira wa utotoni pale Ubungo Flats ninamwona golikipa mahiri
Angelo, mshambuliaji hatari Abdallah na kiungo mshereheshaji Juma. Wote hawa
wametutoka katika kipindi cha hii miaka mitatu.
Wote walikuwa hata hawajitimiza miaka
40. Bado walikuwa vijana. Pia uwanjani namwona Bugwema aliyekuwa mmoja wa vinara wetu darasani. Namwona na
Masanja aliyekuwa mjasiriamali toka akiwa shuleni. Hali kadhalika namwona Eric
aliyekuwa na kipaji cha ufurahishaji toka utotoni. Hao nao wametutoka hivi
karibuni. Wengine 7 niwakumbukao walitangulia zamani. Jumla: Watu 13.
Inakuwaje katika nchi ambayo
tunaambiwa na wanatakwimu kwamba kwa wastani tunategemewa kuishi zaidi ya miaka
40 mtaa mmoja upoteze watu wote hao uliowakuza mapema hivyo ili walitumikie taifa wanapokuwa wakubwa. Wanasiasa wa aina
mpya wanatusisitizia kwamba sisi ni Taifa la vijana sasa inakuwaja shule moja iliyowapa msingi ipoteze vijana wabichi wote hao na zaidi?
Je, Mungu ndiye ametaka iwe hivyo?
Kama anajua nani atakufa lini, je, ndiye anapanga nani afe lini? Ndiye anaamua
watu wa mtaa au kijiji fulani wafe zaidi? Ama ndiye huamua vifo vya ajali za
mabasi vitokee zaidi nchi fulani? Wapi alisema kwamba wakati wa kujifungua mama
wajawazito na watoto wachanga wafe zaidi katika bara fulani? Ndiko kutimizwa kwa mapenzi yake huko?
Gautama Siddartha (Buddha) aliyekuwa
mwanafalsafa maarufu huko barani Asia (inasemekana) aliwahi kumpa funzo mtu mmoja aliyejiona
kama yeye peke yake ndiye amefiwa. Alimwambia aende katika kila nyumba ambayo
haijawahi kufiwa na kuomba kitu kama mchicha hivi ambacho hupatikana katika kila kaya. Hakufanikiwa kukipata na hivyo akajifunza kwamba kumbe kifo hutugusa sote.
Vivyo hivyo nasi tunapaswa kujifunza
kwamba japo kifo huwajia watu wote, hiyo haimaanishi tubweteke tu na kutofanya
jitihada za makusudi kabisa za kupunguza na kuzuia vifo hasa pale inapokuwa
ndani ya uwezo wetu kama wanadamu. Mbona wenzetu wengi wameweza? Kama ushindi dhidi ya kifo ulishaanzishwa kwa nini tusubiri tu
siku ya kuimba “Uko wapi Ewe
mauti uchungu wako?”
Mwanafasihi na ‘Mwanafalsafa’ Ngugi
wa Thiong’o analalama kwa huzuni kuu kwamba thamani ya maisha ya Mwafrika duniani ‘imedogoshwa’
ukilinganisha na ya wengine. Vifo vitokanavyo na mashambulizi ya Ki-Xenophobia
huko Afrika Kusini, kuzama kwa wahamiaji huko Afrika Kaskazini, vita vya
kigaidi huko Afrika Magharibi pamoja na kupigwa risasi huko kwenye Diaspora ya Afrika
ni ushahidi tosha kwamba hakika kufa ‘kunaafrikishwa.’
tunaenda mbali zaidi, sasa ‘tunatanzanisha’ kifo. Ni kama vile tunataka
kuionesha dunia kwamba kufa ni kawaida zaidi hapa kwetu kiasi cha kwamba leo kuna
aina ya vifo vinapatikana Tanzania tu kama ilivyo Tanzanite. Hivi albino wa
Tasmania au Tajikstan akiaambiwa aje ‘kuishi’ hapa Tanzania atakubali kweli?
Ayub Rioba aliwahi kujaribu kuchambua baadhi ya misemo na methali zetu ambazo alisisitiza zinahitajika kuangaliwa upya kwa kuwa zinajenga falsafa zinazoathiri maendeleo yetu
kama jamii. Pengine sasa ni muhimu tuanze kuziangalia kwa kina zile ambazo
zinaongelea kifo maana labda zinachangia kwa kiasi kikubwa sana ‘kukikawaidisha’ kifo.
Tuanze kwanza na hili la ‘kufa kufaana’ na ‘kifo cha
wengi harusi.’ Maana ya ndani ambayo imelengwa inaonekana ina mantiki nzuri sana ambayo, kitafsida, wala
haizungumzii kifo kama kifo. Lakini ukiitazama maana ya nje unakuta inajenga falsafa ya
kwamba kifo kinaweza kutufaa na hasa kifo kinapokuwa kimetamalaki. Na kwa
kawaida falsafa ya maisha ndiyo hutuongoza kivitendo maishani.
Lakini tunapokufa wengi kwenye ajali
za mabasi hayo ni matanga, siyo harusi. Na tunapowaua ndugu zetu albino na
ajuza hatuwafai, hivyo, hatufaani nao. Kufa kutofaana. Kifo cha wengi matanga.
Halafu kuna ‘hujafa hujaumbika.’ Mama
mjamzito anapopoteza himila kwenye tumbo la uzazi hospitalini au mimba changa kabisa inapotolewa ni kweli mtoto anakuwa bado hajaumbika kikamilifu. Kilicho muhimu ni
kuhakikisha kwamba tunazuia upotezaji holela wa maisha wakati mgumu wa ujauzito na ajali
zingine ili tusiwe na kisingizio/sababu ya kutumia falsafa hiyo kujifariji na kuwafariji waliokumbwa na majanga. Maafa mengi tunayaumba wenyewe.
Je, kweli ‘kufa ni wajibu’? Ni wajibu
wangu kufa kwa malaria au ni wajibu wangu ‘kuwaua’ hawa mbu wengi wanaoning’ata
ninapoandika haya na kununua chandarua hasa chenye dawa? Hivi ni wajibu wangu kufa tu kwa UKIMWI ama ni wajibu wangu
kujikinga na maambukizi ya VVU au kutumia dawa za kurefusha maisha na kuhakikisha
napata matibabu ya magonjwa nyemelezi?
Sam Cooke aliwahi kuimba wimbo wenye maneno haya ya simanzi: “Nimechoka kuishi lakini naogopa kufa.” Kuna wakati
tunachoka kabisa kuishi kutoka na sababu mbalimbali zinazoyafanya maisha (matamu) yawe machungu
– umaskini/ufukara, maradhi/magonjwa na kadhalika. Lakini kwa kawaida binadamu anaogopa sana kufa. Dwight Nelson yeye anasisitiza kwamba mbinu ya kukabiliana na
kifo chako bila hofu na kwa kukiongelea kijasiri kabla
hakijatokea.
Remmy Ongala, yule Mwanamziki na ‘Mwanafalsafa’,
naye aliwahi kuimba wimbo maarufu wenye falsafa yake tata ya kifo. Unasema “Kifo
hakina huruma.” Mtenda(ji) ni kifo na mtendwa(ji) ni mtu. Mama Mjamzito anakufa
mtoto akiwa tumboni, wimbo unakilaumu kitendo cha kifo na siyo kitu ambacho mtu huyu, huyo ama yule alikifanya au kutokifanya na hivyo kusababisha kifo.
hakukiona wakati ule ni kwamba wale waliojiandaa kukabiliana nacho hawaishi tu kwa kutegemea rehema/huruma ya
kifo na kuinung’unikia kudra ya Mungu. Kama jamii wao hupunguza kasi ya kufa na wengine hufanikiwa kabisa
kutokomeza vifo vinavyozuilika. Na ndiyo maana kuna nchi ambazo zimefanikiwa
kutokomeza magonjwa kama malaria.
Ongezeko la jitihada za kulinda
maisha ni moja ya sababu kuu ya kwa nini takwimu zinaonesha kwamba kiujumla kuna
nchi/jamii zinaishi maisha marefu kuliko zingine. Kwa mfano, huko Marekani
tafiti zinaonesha kwamba, kwa wastani, Waadventista Wasabato (wengi) huishi
muda mrefu zaidi kutokana na kuzingatia kanuni jumuishi za kutunza afya.
Kanuni hiyo imejikita kwenye neno NEWSTART lenye maana ya ‘Mwanzo Mpya’, ambapo
kila herufi inawakilisha hitaji fulani ambalo mtu anatakiwa ahakikishe analipata vya
kutosha kiuwiano, yaani Nutrition (Lishe), Exercise (Mazoezi), Water (Maji), Sunshine
(Mwangaza), Temperance (Kiasi), Air (Hewa), Rest (Mapumziko) na Trust (Imani).
Uchambuzi wa matabaka/madaraja pia unahitajika
tunapotafuta falsafa ya kukabiliana na kifo. Sidhani kwamba ni jambo la kawaida
tu kwa mtaa wa Ubungo Flats katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupoteza vijana
wake 13+ ilhali kuna mitaa mingine katika Chuo hicho haijapoteza hata mmoja.
Haijatokea tu kibahati bahati, inaonekana kuna sayansi fulani au siri ya kitabaka/kidaraja.
Daraja/Tabaka na tofauti zake ilikuwa ni moja ya
misingi mikuu katika ubunifu na ujenzi wa Chuo Kikuu hicho. Na kama kuna mtaa
ambao ulidhihirisha hilo ulikuwa ni Ubungo Flats. Wakati tunakua mitaa ya
Kileleni na Kilimahewa ndiyo ilikuwa ‘Oysterbay’ na ‘Masaki’ ya chuoni ikifuatiwa
na mitaa mingine kama Koroshoni, Darajani, Lamboni, Miembeni na Ng’ambo.
kiasi kikubwa ilikuwa imekusanya matabaka yote makuu ya Chuo Kikuu. Jengo la
mapolisi halikuwa lilivyo sasa – lilikuwa linaongoza kwa kubanana na uchafu,
huku ikisemekana familia mbili tofauti zilikuwa zinaishi kwenye nyumba ndogo ya vyumba
viwili. Pia kulikuwa na majengo ya wafanyakazi wa kawaida na upande mwingine
kulikuwa na majengo ya wahadhiri ambao wengi wao walikuwa kwenye michakato ya
kuomba wahamishiwe mitaa ya ‘uzunguni’/‘unaizesheni’ ya humo chuoni Mlimani.
Baada ya miaka mingi jirani yangu wa
utotoni aliniambia kila jioni taa zikiwashwa walikuwa wanaangalia upande
majengo yetu yalipo na kutuona sisi ndiyo tumefanikiwa sana na kutamani kuhamia
kwetu na kuwa kama sisi. Nasi tulikuwa tunatamani kuhamia walipokuwa wanaishi
zaidi vingunge wa chuo na wahadhiri wageni kutoka nje ya nchi. Jirani yangu huyo yeye alifanikiwa kuhama.
Pamoja na hayo Ubungo Flats ya enzi
hizo za miaka ya 80 haikupoteza watoto wake wengi kama ilivyowapoteza sasa
baada ya kuwakuza. Msiba mkubwa wa kwanza wakati huo ulikuwa wa mdogo wangu,
Atuhalile, aliyeumwa Degedege na kupoteza maisha njiani wakati jirani yetu
Dokta Minja anajitahidi kadri ya uwezo wake wote kumwahisha hospitalini Muhimbili baada ya jitihada
zingine kushindikana. Ilikuwa siku ya majuto na majonzi mtaani.
Enzi hizo kifo hakikuonekana ni kitu
cha kawaida. Hata utamaduni wa kuomboleza misibani unaonekana ulikuwa tofauti na wa siku hizi.
Majuzi Bibi yangu, Mkunde, alikubaliana na hoja tete kwamba zama hizi misiba
mingi mijini imekuwa ni kama sherehe – ni kana kwamba sasa tumekizoea kifo kwa kuwa kipo karibu mno; kinatokea kila kukicha hapa, hapo, pale na si kule tu. Kama hili
ni kweli, je, linatokea kwa sababu falsafa yetu ya kifo imebadilika?
Falsafa yetu ya kifo ni ya kusubiri tu siku zetu za kufa kwa kuwa eti zimeshapangwa/zimeshaandikwa kabla hatujazaliwa? Au ni ya kuzuia vifo vinavyozuilika? Hata misahau si inasema kwa nini tufe kabla ya siku zetu? Si inasema tunaweza kuongeza siku za kuishi?







Pole sana kwa misiba hii mingi ya watu wa karibu. Na kama mambo yanaendelea hivyo, hali itaendelea kuwa mbaya zaidi. La msingi ni kujiweka kwa Mungu na kukumbuka tumaini lenye baraka kwamba siku moja Yesu atakuja kutuchukua atupeleke katika nchi ile aliyotuandalia mahali amabako hakutakuwa na vifo, wala vilio, wala machozi, wala maombolezo.