BEAUTY SALONS AND THE BEAST

(SALUNI
ZA UREMBO NA URIMBO
)

  

Mwisho
wa siku…sanaa ya umma…inahusu sanaa na umma. Na hilo litaendelea kuwa hivyo
pale ambapo huo umma siyo tu kikundi kidogo cha watu wanaojua na kufuatilia
sanaa, bali ni mchanganyiko wa taifa lenye matabaka, fursa tofauti, viwango
mbalimbali vya kuwa na muda wa kutosha; hivyo basi, sanaa ya umma hakika
itakuwa ni ya umma pale tu inapohusu vilivyo vya umma.’
(1) 

Mwaka
2008 nilishuhudia uzinduzi wa kile ambacho sasa kimekuwa tamasha maarufu sana
la sanaa duniani lijulikanalo kama Infecting The City, yaani ‘Kuliambukiza
Jiji
’. Hili ni tamasha linaloshirikisha aina nyingi za sanaa na maonyesho
katika jiji la Cape Town nchini Afrika Kusini na hivyo kutoa nafasi na fursa
kwa mtu yeyote kuzifikia na kuona kazi mbalimbali za sanaa. Kipindi hicho
nilikuwa ndiyo kwanza naanza mwaka wangu wa tatu wa masomo ya Shahada ya kwanza
ya Sanaa, hivyo, hata sikujua mwelekeo wangu kitaaluma na kisanii utakuwaje.
Lakini nakumbuka jinsi gani wazo la walioanzisha tamasha hilo lilivyonigusa na
kunifanya nitamani siku moja na sisi tuazime hata sehemu ndogo tu ya wazo hilo
ili kuwe na tamasha kama hilo katika jiji letu la Dar es Salaam, Tanzania. Pia
nilitamani niwe mmoja wa waandaaji wa tamasha la aina hiyo jijini Dar es Salaam
kwa kadri vionjo, uwezo na muktadha wetu utakavyoruhusu. Hatimaye mwaka huu,
ikiwa ni mwaka wa nane toka niupate ule uzoefu ulionigusa kwa mara ya kwanza,
nimefanikiwa kuifikia azma hiyo kupitia maonyesho ya Apexart Franchise
tuyaitayo “Beauty Salons and the Beast”, yaani, ‘Saluni za Urembo na Urimbo.’

Tamasha
la Saluni za Urembo na Urimbo ni zao la wasanii wawili – mimi mwenyewe,
Rehema Chachage, na Jan van Esch – ambao pia tupo kwenye menejimenti ya taasisi
ijulikanayo kama Nafasi Art Space, kituo pekee cha sanaa ya kisasa jijini Dar
es Salaam. Wazo la kuwa na tamasha hili liliibuka kufuatia hali tuionayo
Tanzania, yaani: kuhudhuria maonyesho ya sanaa kiukweli siyo utamaduni wa
Watanzania walio wengi. Hivyo, ukilinganisha na raia wa kigeni, hakuna
Watanzania wa kutosha wanaohudhuria maonyesho ya utamaduni pamoja na matukio
mengine ya kiutamaduni katika vilinge vya tamaduni jijini. Sisi kama waandaaji
wa takribani asilimia 50 ya maonyesho hayo, mara kwa mara tunajikuta
tukijiuliza umma wa Watanzania uko wapi na ni kwa namna gani tunaweza kufanya
iwezekane kwa umma huo kupata fursa ya kuona sanaa na kuwafikia wasanii.

Baada
ya kubunga bongo na kutafakari sana, tukahitimisha kuwa labda njia pekee ya
kuweza kuwafikia watu wengi zaidi ni kwa kuazima mbinu ya ‘Kuambukiza Jiji
na kujaribu kufanya maonyesho yanayoibuka ‘papo kwa hapo’ katika maeneo ya umma
ili kuvutia mkusanyiko mkubwa wa Watanzania. Tunasema,‘Kama hawataifuata
sanaa, basi tuiachie sanaa iwafuate wao;
’ na tupo kwenye mkakati wa
kuwafuata (umma wa) watazamaji wa sanaa popote pale walipo. Katika jaribio hili
la kwanza la maonyesho ya ‘papo kwa hapo’, tumeamua kutumia saluni kama maeneo
ya maonyesho baada ya kuona makala yaBeauty Salons and the Beast (yaani
Saluni za urembo na Urimbo)
iliyoandikwa na Erick Mchome. Makala hiyo
inaonyesha ni kwa kiwango gani saluni zimekuwa ni biashara zinazokuja juu kwa
kasi jijini Dar es Salaam ambapo tunaona kundi kubwa la watu wa matabaka ya
juu, kati na chini ya kiuchumi/kimaisha nchini Tanzania yakitumia muda wao wa
ziada humo, hasa mwisho wa wiki, yaani, wikiendi.(2) Hawa ndiyo aina ya watazamaji
ambao maonyesho yetu yanalenga kuwafikia.

Katika
jaribio hili la kwanza la maonyesho ya ‘papo kwa hapo’, tumeona ni vyema
tujaribu kwanza kutumia saluni zilizoko katika maeneo ya karibu na tulipo,
hivyo tumechagua eneo la Msasani ambalo kiutawala ni kata katika Wilaya ya
Kinondoni. Msasani pia ipo kati ya Peninsula (yaani maeneo ya
Masaki/Oysterbay), ampapo wanaishi wageni wengi pamoja na Watanzania wengi wa
daraja/tabaka la kati na la juu kiuchumi/kimaisha, na Kijiji cha Msasani
ambacho zamani kilikuwa ni kijiji cha wavuvi na mpaka sasa kina mkusanyiko
mkubwa wa watanzania wa tabaka la chini kiuchumi. Hali kadhalika ni rahisi kwa
watu wengine kutoka maeneo mengine ya Wilaya ya Kinondoni (wengi wao wakiwa ni
mchanganyiko wa tabaka la chini na la kati kimaisha/kiuchumi) kupafikia Msasani
maana biashara nyingi zinazowahudumia ziko hapo. Hivyo mazingira hayo yanatupa
fursa ya kuwafikia Watanzania wengi na wa aina nyingi ambao kwa kawaida
hatuwaoni kwenye maonyesho ya wazi ya usiku tuyafanyao katika kituo chetu cha
Nafasi Art Space.

Kama
walivyo wasanii wengi wanaongezeka leo, wasanii waliochaguliwa kwa ajili ya
maonyesho ya Saluni za Urembo na Urimbo wanapendelea sanaa ya umma na
kuhoji nafasi zao katika jamii kwa kutumia sanaa kuwasiliana na jamii husika
kuhusu masuala muhimu ya kijamii. Wanatumia maonyesho haya kama mbinu ya kuitoa
sanaa kwenye kuta nne za kituo cha sanaa walichokizoea na kuzipeleka nje kwa
watu ambao siyo kawaida yao kuja kwenye vituo vya sanaa. Kwa kuwafikia watu
hao, wasanii hawa pia wanapata fursa ya kusikiliza maoni mbadala kuhusu ujumbe
wao wa kisanii na hivyo kuwawezesha kukuza maono na usikivu wa vionjo na
tafsiri za Kitanzania kuhusu sanaa ya kisasa. Kupitia kitendo hiki, wasanii
wanataka kuwapa changamoto watazamaji na wao wazingatie na watazame kwa undani
zaidi mazingira waliyopo – yaani, muktadha ambao sanaa yao inapokelewa nao na
mitazamo inayoibuka humo ni masuala muhimu katika maonyesho haya. Kwa namna
fulani, wasanii hawa wanachukua nafasi ya watetezi (kupitia sanaa) wa mitazamo
mbadala inayohoji tafsiri, imani na misimamo ya jamii.

Kuna
njia nyingi za kutafsiri mitazamo na maana ya mchango wa kila msanii. Sisi kama
wasimamizi wa maonyesho haya ya Saluni za Urembo na Urimbo, tumetoa
fursa kwa mtazamo na tafsiri yoyote ile ambayo wasanii wataiongezea kwenye wazo
letu la kuwa na maonyesho haya. Japokuwa kila mada ya msanii katika nafasi yake
imejikita kwenye taaluma au mfumo fulani wa sanaa, mnyanganyiko wa uzoefu wa
 ndani na wa nje wa wasanii wote, kwa pamoja, ni mpana na unaakisi uzoefu
wa nchi yetu na siasa zake katika mapana yake.

Maonyesho
yaliyojumuishwa katika Saluni za Urembo na Urimbo ni yale ambayo
yanagusa fikra zetu na kugusia kipindi hiki na mazingira yetu ya sasa nchini.
Mengi yanagusia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 na kurejea miaka 5+ ya Uhuru na
miaka 20+ ya mfumo wa demokrasia ya kiliberali pamoja na mikanganyiko yake,
mmojawapo ukiwa ni namna ya kuzuia rushwa/ufisadi na matumizi mabaya ya
madaraka. Kwa kuzingatia upigaji kura, wasanii kwa pamoja walikubaliana tuanze
na mfumo wa maswali ya kuchagua kama mbinu ya kwanza na mada mtambuka – kama
namna ya kutathmini ambapo watu wanaulizwa wachagua jibu au majibu kutoka
kwenye orodha ya majibu, mtu hugudua kuwa mara nyingi jibu linakuwa ni majibu
yote, yaani kuna mengi ya kuchagua.

Jan
van Esch
na Aika Kirei, kwa mfano, wanatumia ‘mbinu ya
kutathmini kwa kutumia maswali ya kuchagua’ kuuliza maswali kuhusu namna
ambavyo wajasiriamali wadogo wadogo na wa kati wanavyopata au kukosa fursa. Na,
kama ilivyokuwa kwa baba yake aliyekuwa Profesa wa Sosholojia na Mchambuzi wa
masuala ya Kijamii  na ambaye anasemekana kuwa mtu wa kwanza kuyachezesha
kikejeli maneno ya kaulimbiu ya chama tawala ya uchaguzi wa mwaka 2005, Rehema
Chachage
naye anayachezea kisanii maneno hayo ya ARI, NGUVU, KASI ambayo
kiuhalisia yamekuwa kinyume chake na kuwa A, -NGU, -KA (ANGUKA) kutokana na
chama hicho kushindwa kutekeleza mambo mengi waliyoahidi. Vivyo hivyo, japo kwa
mbinu tofauti, Gadi Ramadhani anatumia mwendelezo wa maonyesho yake ya Blindfolded
(Kufungwa Macho) kuonyesha, kwa mtazamo wa kisanii, ni jinsi gani leo sisi kama
jamii tumefungwa kitambaa machoni hivyo ni kama vile tunatembea bila
kujua/kuona jinsi ambavyo mfumo tawala (wanasiasa, vyombo vya habari n.k.)
unatuhadaa.

Kwenye
suala la maamuzi na kuchagua, Delphine Buysse  anatumia madoli 50
yanayoning’inia kichwa chini miguu juu na ambayo yamepakwa rangi ya kijivu kwa
asilimia 50, kuonyesha na kuchambua mtanziko wa maisha na ugumu utokanao na
kuamua/kuchagua. Eneida Sanches naye analitazama suala hilo hilo ila kwa
namna tofauti. Kwa kutumia michoro ya wanaume ambao hawapo (tena) katika maisha
yake, sanaa yake inaonyesha mikanganyiko na tafakuri kuhusu wanaume hao na
uchaguzi/uamuzi wao wa kumwacha… swali lake kuu likiwa ni; wako wapi na nini
kiliwafanya waondoke/wamwache?

Cloud
Chatanda
anakuja na mtazamo chanya zaidi kwenye mada hii kwa
kutumia mchanganyiko tete wa uchoraji na uchongaji kuonyesha jinsi viumbe vya
zamani visivyojulikana ambavyo kwa muda mrefu vimegana kwenye Mlima Kilimanjaro
vinaamka na kukuta Tanzania iliyo katika hali tata na kuamua kupambana na
matatizo ili kulirudisha Taifa kwenye hali yake ya asili. Hali kadhalika Amani
Abeid
naye anakuja na mtazamo chanya kwa kuonyesha shujaa anaejitokeza
(kutoka Tanzania) kuikoa dunia kutoka kwenye majanga baada ya mashujaa maarufu
na wapendwao wa nchi za magharibu kushindwa kufanya hivyo.

Onyesho
la Vita Maluli, ambalo limejikita zaidi kwenye kejeli, linatumia ‘kango
moko’, yaani kipande kimoja cha kanga chenye vijimaneno au vijembe, ambapo
tunaona kanga ikiwa imepata uhuru zaidi hivi karibuni baada ya kuacha utamaduni
wa kuwa tu vazi la kuvaliwa nyumbani kwa matumizi ya ndani na kuwa pia vazi
linaloonekana mitaani, likiwa limevaliwa na wanawake mchana kweupe.

Kila
msanii anajaribu, kwa namna yake ya pekee, kupaza sauti yake kuelezea yale
yanayomgusa. Kama Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Afrika, Tanner Methvin
anavyosema, “propaganda ni kusema hatuna mamlaka ya kujieleza kwa Uhuru. Eti
sauti zetu zinahitaji ruhusa kutoka kwa mtu au kitu fulani chenye mamlaka hayo.
Kuwa walimu wetu, wakuu wa taasis za elimu, mabosi wetu, na maofisa wa Serikali
ndiyo wanaturuhusu kucheza muziki, kuimba, kuchora, kupiga picha, kuandika, au
hata kuongea tu. Wanatuambia lini tumechaguliwa au tumeteuliwa na hapo ndipo tu
tunaposimama…Hili kwa hakika ni hekaya lakini ambayo tunashiriki kuitunga na
kuikuza kila mara tunapojibana wenyewe na kuzikimbia fursa za kuelezea visa
vyetu wenyewe.”(3)   

1. Jay Pather, Curator’s Note in Infecting the City: Public Arts Festival, March 10-15, 2014, Cape Town City Centre, exhibition catalog, p. 3.
2. Eric Mchome, “Beauty Salons and the Beast,” Mail & Guardian, Dec. 12, 2011: http://mg.co.za/article/2011-12-12-beauty-salons-and-the-beast.
3. Tanner Methvin, Introductory Note in Infecting the City: Public Arts Festival, March 10-15, 2014, Cape Town City Centre, exhibition catalog, p. 2.


© Rehema Chachage (Msimamizi wa maonyesho, Beauty Salons and The
Beast
Saluni za Urembo na Urimbo)


TAARIFA KWA WANA HABARI:
UZINDUZI WA MAONYESHO YA BEAUTY SALONS AND THE BEAST (SALUNI ZA UREMBO NA
URIMBO)

FOR IMMEDIATE RELEASE.

Uzinduzi wa Beauty Salons and
the Beast (Saluni za Urembo na Urimbo); maonyesho ya sanaa yaliyopangwa
kufanyika katika saluni za kiume na za kike maeneo ya Msasani (Mtaa wa
Makangira, karibu na Edo Chips), Dar es Salaam, Tanzania. Maonyesho haya
yatahusisha kazi za sanaa zilizotayarishwa na wasanii wafuatao:

Amani Abeid (Tanzania)

Delphine Buysse
(Tanzania/Ubelgiji)

Rehema Chachage (Tanzania)

Cloud Chatanda (Tanzania)

Eneida Sanches (Brazil)

Jan Van Esch (Tanzania/
Uholanzi)

Aika Kirei (Tanzania)

Vita Malulu (Tanzania)

Gadi Ramadhani (Tanzania)

  

Muhtasari:

Maonyesho ya “Beauty Salons
and the Beast” yaani, “Saluni za Urembo na Urimbo” yamelenga kuwatambulisha
Watanzania kwenye sanaa iliyo mpya, ya kisasa na ya majaribio. Lengo kuu ni kuchochea
mwamko, na mazungumzo zaidi juu ya umuhimu wa sanaa nchini Tanzania. Maonyesho
haya yatagusia mada ya ‘uwezo wa kuchagua’, iwe ni rafiki, mpenzi, mke, raisi,
ajira, makazi, n.k. na yataonyesha kazi za sanaa kutoka kwa wasanii wa
Kitanzania na wa Kimataifa. Kwa kutumia kazi zao, wasanii hawa wataangalia
maswala mbalimbali ya kijamii na kuhoji sehemu ya msanii na sanaa yake katika
jamii. Wasanii watatumia mbinu mbalimbali za kutengeneza sanaa zao ili
kuhakikisha kwamba jamii nayo inapata nafasi katika ukamilishaji wa kazi zao za
sanaa.

Watayarishaji wamebuni
maonyesho haya kutoka kwenye msemo huu; ‘kama hawatofuata sanaa, basi acha
sanaa iwafuate wao’; hii ni baada ya kugundua upungufu wa jamii ya kitanzania
(ukilinganisha na jamii ya wageni wanaoishi Tanzania) katika maonyesho na
matukio mbali mbali ya kisanii nchini, hivyo, watayarishaji wa maonyesho haya
wameamua kuwapelekea wananchi sanaa kwani imeshindikana kwa wananchi kuifuata
sanaa wenyewe. Watatumia njia ya “kuliambukiza” jiji na matukio mbalimbali ya
kisanii kama vile maonyesho na majadiliano ya umma kuhusu sanaa na kuhamasisha
jamii kujihusisha na kujua zaidi kuhusu sanaa kwa ujumla.

Uzinduzi
huu utafanyika siku ya tarehe 7 Februari 2015 kuanzia saa 8.00 mchana. Kutakuwa
na kazi za sanaa  zikionyeshwa ndani ya
saluni nne (4) za kike na za kiume katika mtaa wa Makangira (Pia hujulikana
kama mtaa wa Msasani, karibia na Edo Chips) Dar es Salaam Salaam. Uzinduzi utakuwa
na vitumbuizo tofauti vya burudani, pamoja na hotuba fupi kutoka kwa waandalizi
wa maonyesh, wasanii, na wafadhili wa mradi; taasisi iitwayo apexart kutoka New
York, USA.

Maonyesho yameandaliwa na
Rehema Chachage na Jan van Esch.