“Mabadiliko haya
tuyatakayo yana sura ipi?” – Padre Privatus Karugendo

Siasa za Urais zimechukua sura ‘mpya’.
January Makamba ameibuka na kitabu kipya. Ni cha mazungumzo Kuhusu Tanzania Mpya aliyoyafanya na Padre Privatus Karugendo.

Ndani ya kitabu hicho kuna maneno
mengi tu matamu yanayoweza hata kumtoa nyoka pangoni. Jukumu langu katika uchambuzi
huu siyo kuyaimba kama kasuku. Kazi yangu
ni kudadisi na kuibua maswali zaidi ili tumfahamu kwa kina mgombea Urais
mtarajiwa.

Maadam kina maswali na majibu 40,
uchambuzi huu utajikita katika hoja mbalimbali zilizoibuka humo. Lakini kwa
kuzingatia maangalizo ya wanazuoni wawili, udadisi huu hautajibana tu kwenye
kitabu hicho na kuishia tu kujadili masuala ndani ya mabano aliyoyaweka
January. Bali kitapitia vyanzo vingine mbadala hasa vilivyopo mitandaoni.

Pia maadam mdadisi anasisitiza kuwa Tunahitaji
Viongozi Wenye U Tatu
, yaani “Utu”, “Uadilifu” na “Utaalamu” basi udadisi
huu utapima majibu ya January kwa kuzingatia U hizo. Kazi hiyo haitakuwa ngumu
sana maana majibu hayo yanajadili U nyingi – “Uthubutu”, “Uzoefu”, “Ujana”,
“Ujasiri”, “Ubora’, “Uadilifu” na kadhalika.

Lakini vivumishi vilivyojazana
kitabuni ni vinavyotokana na mzizi “-pya-”.
Humo kuna “upya”, “mpya”, “jipya”, “vipya”, “mapya” na “kipya”. Maneno
hayo yanayoashiria upya yapo 156 katika kitabu hicho chenye kurasa 196. Hivyo,
tuanze kwanza kuidadisi U hiyo.

Upya

Wachambuzi wa masuala ‘mapya’ huwa
tunashtuka tunapoona matumizi ya kivumishi chenye ‘-pya-’ hasa kwenye kichwa (kikuu)
cha habari. Kwa kawaida swali la kwanza tunalojiuliza lina muundo huu: “Ni nini
kipya kuhusu kinachosemwa kuwa ni kipya?”

Je, ni nini kipya katika “Tanzania
Mpya” anayoiongelea January? Anatuambia
hivi: “Rais ajaye ana kazi kubwa zaidi ya
kusimamia umoja wa nchi yetu na usalama, amani na utulivu kuliko viongozi waliopita.
Huu ni msitu mpya kabisa” (Uk. 3).

Kwa maana nyingine, Tanzania ya sasa
ina hatari zaidi kuliko ya enzi za majaribio ya mapinduzi ya miaka ya 60, vita
dhidi ya Nduli Idi Amin vya miaka ya 70, uhujumu uchumi wa miaka ya 80, na
machafuko ya kidini ya Mwembechai ya miaka ya 90.

Yaani, huyo Rais mpya ajaye wa awamu
ya tano atakabiliana na “msitu mpya kabisa” na hivyo kuwa na “kazi kubwa zaidi” (kuliko marais wa awamu ya kwanza hadi ya nne) ya kukabiliana na hatari iliyopo
“ya taifa letu kupasuka – kutokana na dalili za mpasuko wa kidini, mmomonyoko
wa maadili kwenye jamii, kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa Dola, ufa katika
Muungano na umasikini na tofauti kubwa ya kipato baina ya watu na hali ya
kukata tamaa miongoni mwa wananchi” (Uk. 2).

Kwenye suala mmojawapo katika huo
anaouita “msitu mpya kabisa”, January anasema hivi: “Changamoto ya Rais ajaye ni
kufufua ndoto na dhamira ya Muungano kwa kuupatia sababu mpya.” (Uk. 5). Lakini
kitabuni hatuoni hizo sababu mpya. Ni tamanio tu.

Tunachoona kitabuni ni hiki: “Muungano wetu
umetikiswa. Nimejiridhisha kwamba kiongozi ajaye lazima ahakikishe Muungano
wetu unajibu changamoto za umasikini na changamoto za kimuundo, mambo ambayo
yamezaa hoja na kelele za kuuvunja. Uhai wa Muungano utategemea sana ni kwa
jinsi gani unawasaidia Watanzania wa pande zote kwa kuwapa fursa ya kuendeleza
ndoto zao za kiuchumi na kijamii. Kinyume na hapo, Muungano utakuwa mali ya
viongozi na wanasiasa na hautadumu” (Uk. 5).

Maono mapya hapo ni matamanio tu
maana tunaendelea kusisitiziwa kuwa “Ubunifu unahitajika katika kuweka taasisi
na miundo itakayotoa fursa zaidi kwa wananchi wa Tanzania na haswa Wazanzibari
kuondokana na umasikini, na kuondoa mpasuko miongoni mwa jamii ya Wazanzibari” (Uk. 5). U nyingine hiyo ya Ubunifu ila uko wapi humo?

Ili walau tuone ubunifu huo mpya
kuhusu Muungano Wadadisi tunalazimika kurejea mchango wake kwenye Bunge Maaalum
la Katiba kama ulivyorekodiwa kwenye
video iliyopo mtandaoni
. Hayo aliyasema mwaka 2014 na maadam hajayakanusha
kwenye kitabu basi ndiyo angalau yanaweza kutupa picha ya maono yake kuhusu
hiyo miundo anayoiongelea kitabuni na inayomfanya aseme kuwa “Rais ajaye
afanikiwe kuwashawishi Watanzania kuhusu azma yake ya kusimamia Muungano
usivunjike kutokana na mashinikizo ya viongozi wachache wenye ajenda binafsi na
uchu wa madaraka” (Uk. 6).

Baadhi ya maneno aliyoyasema January
humo Bungeni ni haya: “Ndugu Mwenyekiti, waasisi wetu walitazama miundo yote,
walitafakari miundo yote kwa kina. Nilipata bahati ya kukaa na Mzee Lusinde,
Mzee Job Lusinde ambaye alikuwepo kwenye majadiliano ya kuamua aina ya Muungano
ambao tuwe nao. Dhana inayojengeka hapa ni kwamba wale wazee hawakuwa na
maarifa, walirukia tu kwenye muundo wa Serikali Mbili. Walitafakari miundo yote
ya Muungano iliyopo: walitafakari Serikali Moja, walitafakari muungano wa
Serikali Tatu, walitafakari Shirikisho na mingine mingi; na wakaamua, baada ya
tafakuri ya kina, kwa kutazama mazingira yetu, kwa kutazama mazingira mahususi
ya nchi zetu, kwamba muundo wa Serikali Mbili ndiyo ambao ungetufaa. Ndugu
Mwenyekiti, katika azma ile ya kuunda taifa lenye nguvu, ya kurasimisha udugu,
waliona kwamba wangeenda na Serikali Tatu, azma ile ingeisha, ingeishia
katikati, tusingefika mbali, tusingefika leo kwenye Muungano wenye umri wa
miaka 50”.

Sehemu ya hitimisho la utangulizi huo
wa hoja ya January ni hili: “Ndugu Mwenyekiti , kama tunataka kuvunja Muungano
wetu, kama tunataka kuvunja Muungano wetu – maanake lazima tuwe wakweli sisi ni
viongozi hapa – basi twende kinyume na ile busara; kama tunataka Muungano wetu
uvunjike ndani ya mwaka mmoja, ndani ya miaka miwili, tuingie kwenye Serikali
Tatu”.

Mti mwingine kwenye “msitu mpya
kabisa” wa January ni tishio la udini. Suluhisho lake analielezea hivi: “Tatizo
ni viongozi wachache, wa kisiasa na kijamii, ambao wanatumia dini kufanikisha
malengo yao ya kisiasa na kijamii kwa kuchochea chuki baina ya watu wa dini
tofauti. Watu hawa ni hatari sana ni lazima tuwabaini, tuwatenge, tuwadhibiti
na tuwaadhibu haraka sana. Serikali yetu inao wajibu katika hili lakini pia
jamii inao wajibu” (Uk. 132).

Pia anasema: “Kama kuna hujuma
inafanyika ili kutugawa kwa misingi ya kidini vyombo vyetu vya ulinzi na
usalama vifanye kazi ya kubaini hujuma hizo na kuzidhibiti” (Uk. 133). Na
anatoa wito huu pia: “sisi viongozi wa siasa tutimize wajibu wetu” (Uk. 132).

Rai nyingine anayoitoa January ni
hii: “Na wale wanasiasa wanaoomba nafasi za kisiasa kwa misingi ya dini nao
wanapaswa kuwekwa pembeni, kama ambavyo Mwalimu Nyerere alituasa” (Uk. 133).

Hakuna maono mapya hapo kuhusu suala
la udini. Sana sana tunachokiona ni kitabu ambacho kimeandikwa na Padre na
Alhaj na picha za January akiwa na viongozi wa dini mbalimbali, kitu ambacho
labda kinajaribu kutuambia kwamba January siyo mdini. Lakini uchambuzi wa picha
zilizopo kitabuni nao unaibua maswali ya kidadisi: Kwa nini kuna picha kadhaa akiwa na
viongozi wa dini ya Kikristo au akiwa kwenye taasisi mbalimbali za Kikristo ilhali inapokuja kwa Waislamu/Uislamu kuna picha
moja tu “akiwa kwenye Maulid jimboni Bumbuli” (Uk. 135).

Jibu pengine ni rahisi maana hizo picha
na viongozi wa Wakristo ni za kutoka kwenye madhehebu mbalimbali. Lakini kwani
Waislamu hawana madhehebu mbalimbali yenye viongozi wao? Picha kama ya “January
Makamba alipotembelea shule [ya] Sekondari ya Mtakatifu Maria Mazinde Juu,
Lushoto” (Uk. 99) inaweza kuelezewa kirahisi maana huko ndiko maeneo ya jimboni
kwake yalipo. Lakini tunapata shida kuelezea picha ya “January Makamba akisalimiana na
wanafunzi wa Sekondari ya Mtakatifu Agnes inayomilikiwa na Kanisa Katoliki la
Jimbo la Mahenge” (Uk. 44). Ni vigumu kuelezea picha ya “January Makamba
akihutubia katika mkutano wa vijana wa makanisa ya Pentekoste” (Uk. 96) ilhali
hatuoni picha zingine akiwa kwenye mikutano ya vijana wa dini zingine.

Pamoja na hayo hivi ndivyo January
anavyohitimisha maono yake kuhusu dini na uongozi: “Nchi yetu ili istawi na
kushamiri ni muhimu kwa viongozi wake na watu wake kumpenda Mungu na kufuata
mafundisho yake. Dini ya kiongozi haipaswi kuongoza nchi lakini imani kwamba
Mungu yupo ni muhimu kiongozi awe nayo. Mtu ambaye hamjui wala hamuogopi Mungu
hafai uwa kiongozi” (Uk. 134); “Kiongozi anaweza kuwa wa dini yoyote lakini cha
muhimu asiwe mdini. Watanzania wa dini yoyote wapo tayari kuchagua kiongozi wa
dini yoyote. Ambacho hawataki ni kiongozi mdini. Naomba nimalize kwa kusema,
Tanzania ni nchi yenye waumini wa dini tofauti ila misingi ya upendo, heshima,
amani, umoja, mshikamano, ujirani mwema ipo kwenye vitabu vyote vya Mungu
lakini pia ipo kwenye katiba na sheria zetu. Hivyo sisi kama viongozi
tutahakikisha kwamba misingi hii muhimu ya dini na katiba tunaisimamia” (Uk.
136).

Uadilifu

Kwenye “msitu mkubwa mpya” wa January
pia kuna U ya uadilifu. Hivi ndivyo anavyouhusianisha na uongozi: “Watanzania
hawatafuti mwanasiasa mkongwe kuwaongoza, wanatafuta kiongozi mahiri na mwadilifu
wa zama mpya” (Uk. 28).

Pia anasisitiza kuwa “Ukomavu wa kiongozi
haupo kwenye umri wake bali kwenye maarifa yake na busara zake na malezi yake
na uadilifu na uzalendo wake” (Uk. 30).

Uadilifu, kwa mujibu wa dhana ya
Udadisi wa Viongozi
Wenye U Tatu
, ni kigezo muhimu sana. Kigezo hiki kinaendana na U za ‘Ukweli’,
‘Uwazi’, na ‘Ujasiri’.  Japo majibu ya
January hayatuambii moja kwa moja kuwa ‘Mimi, January, ni mwadilifu’, uchambuzi
wa matumizi yake ya neno hilo yanayoonyesha kuwa anajibainisha/anajitambulisha hivyo.

Ni kazi ngumu sana kwa mwananchi
ambaye hamjui January binafsi kuthibitisha kuwa ni mwadilifu au la. Kwa kuanza
jaribio hili labda ni vyema kulirejea jibu lifuatalo na kisha kumuuliza
maswali ya nyongeza: “Kwa hiyo, wakati mwingine napata shida kidogo kutoka kwa
ndugu na jamaa na marafiki kwa sababu katika vitu ambavyo binafsi havinisumbui ni
haja ya kukusanya mali, majumba, magari ya kifahari na kadhalika. Falsafa yangu
ni kwamba hapa duniani tunapita tu kutimiza mapenzi ya Mungu na kwamba hakuna
mtu atakayekumbukwa kwa mali zake bali kwa mchango wake kwa jamii pana na labda
pia kwa uadilifu wa watoto aliowakuza na kuwalea. Hii haipaswi kuwa kauli-mbiu
tu ya kisiasa kwa ajili ya kufurahisha watu bali inapaswa kuwa imani ya ndani
ya moyo kabisa” (Uk. 21).

January, je, umeorodhesha mali zako
kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia maadili ya viongozi? Kama ndiyo,
je, mali hizo zina thamani ya shilingi ngapi? Na kama bado, kwa nini? Unaweza
kutuwekea wazi magazetini na vitabuni vielelezo tuthibitishe pasipo shaka?

Majibu yake ya maswali hayo ya
nyongeza yatatusaidia wadadisi kuelewa haya maelezo yake mengine kitabuni
kuhusu Kampuni/Shirika la Maendeleo la Bumbuli: “Shirika hili nililianzisha kwa mtaji wa fedha yangu ya
mfukoni ambayo ilikuwa ni mkopo wa magari ya Wabunge. Tumefanikiwa sana kwenye
mambo kadhaa lakini pia tumekabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo fedha za
uendeshaji wa shughuli zetu. Kwa kiasi kikubwa bado natumia fedha zangu
kusaidia shughuli za Shirika. Tulitegemea misaada kadhaa kutoka maeneo
mbalimbali lakini imechelewa” (Uk. 31).

Sijui wabunge wanakopeshwa shilingi ngapi, niliwahi tu
kuambiwa na Mbunge mmoja kuwa aliwahi kukopa shilingi milioni 30. Ila jibu la
January litatusaidia kujua ni namna gani huo mkopo – pengine na vyanzo vyake
vingine vya mapato ambavyo navyo ni haki yetu wananchi/wapiga kura kujua –
umetosha kupata fedha hizi zilizoelezwa kitabuni: “Hata hivyo, nafarijika
kwamba program tulizozianzisha zinaenda vizuri. Program kubwa ni ile ya ukopeshaji, ambapo hadi sasa tumekopesha karibu shilingi milioni 250 kwa
vikundi vya wajasiriamali Bumbuli, wengi wao wakiwa kina mama” (Uk. 31).

Hali kadhalika tungependa kujua gharama za kuchapisha hiki
kitabu zimetoka wapi maana japo kinauzwa shilingi 5,000 kwenye duka la vitabu
la TPH, kuna watu wengi sana ninaowajua – nikiwemo mimi mwenyewe – ambao
tumeletewa nakala za bure na pia kimetolewa kwenye magazeti na kwa
uelewa/uzoefu wangu mara nyingi huwa ni lazima ulipie kufanya hivyo au wamiliki
wenyewe wa gazeti wasamehe malipo. Je, ni nakala ngapi za bure zimetolewa?
Gharama zake ni shilingi ngapi? Nani anazigharamia?

Kwenye hili pengine rafiki yangu Padre Karugendo naye anaweza
kutusaidia kulijibu maana kwenye utangulizi wa kitabu hicho ameandika maneno
haya: “Nilifaidi mazungumzo yetu na nikaona makala peke yake haitatenda haki
juu ya kina na mapana ya mazungumzo yetu. Nilipenda watu wayapate kama
nilivyoyapata mimi bila ya kupunguza au kuhariri chochote. Nikaamua nichukue
muda, kwa kushirikiana naye, kutafuta uwezo wa kuchapisha hiki kitabu” (Uk. ix ). Uwezo huo mliupatapataje?

Kulinda maadili kunaendana na kuzuia migongano wa maslahi. Na tafsiri ya Udadisi ya mgongano wa maslahi, kama ilivyochambuliwa kwenye Fungate
la Uwekezaji na Migogoro ya Maslahi
pamoja na Lionel
Cliffe na Mgongano wa Maslahi Tanzania
, inagusa hata maslahi yasiyo ya
kifedha kama vile ‘umaarufu wa kisiasa’, au ‘kiki’ kama wanavyosema vijana wa
‘kizazi kipya’. Hivyo, ni vyema tukaelewa ni kwa misingi gani mtumishi wa umma
anaweza kutumia pesa zake kama kisa hiki kinavyoonyesha na
anazuiaje/anadhibitije kitendo hicho kisimpatie maslahi ya umaarufu wa kisiasa:
“Katika kampeni za uchaguzi za mwaka 2005, ambapo nilishiriki kama Msaidizi wa
Mgombea Urais wa CCM, Mheshimiwa Kikwete, nilishauriana naye na tukaamua
tuwashirikishe hawa wasanii kwenye mikutano yetu na shughuli zetu. Tukaanza na
Bushoke. Akabadilisha wimbo wake wa Mume Bwege na kuweka maneno mapya na ukawa
wimbo wa kampeni za CCM. Nakumbuka pesa ya kwenda kurekodi upya nilitoa mfukoni
mwangu. Baada ya hapo, wasanii wengine karibu wote nao wakaingia. Rais
akawapenda wote. Akawa anakula nao chakula, anapiga nao picha. Alivyoingia
madarakani, kwa mara ya kwanza kabisa, wanamuziki hawa tukawaalika Ikulu.
Mwanzo jambo hili lilistua wengi na kuzua mjadala lakini baadaye likaonekana ni
jambo la kawaida. Na Serikali nzima ikaona ni sawa kuwashirikisha kwenye
shughuli za kiserikali. Baadaye ikawa hivyo hivyo kwa wasanii wa filamu na
wengineo. Kwa hiyo, nilifungua mlango kwa wasanii vijana kuanza kutambuliwa na
Serikali na viongozi wa Serikali. Lakini pia nilikuwa mfadhili wa mwanzo kabisa
wa Tanzania House of Talent” (Uk. 138-139).

Hilo ni muhimu hasa ukizingatia kuwa kampeni ya Ubunge wa
January zilihanikizwa/zilitumbuizwa na wimbo wa Bumbuli Songa ulioimbwa na msanii Jobiso. Umuhimu
huo ni mzito zaidi sasa hivi ambapo January ni Naibu Waziri na ‘Rais Mtarajiwa’
ilhali anafanya vitu kama hivi vifuatavyo ambavyo hata kama kweli ni vya ‘nia
njema’ vina(fungua mianya ya) migongano ya maslahi: “Lakini vilevile kwa nafasi
yangu ya sasa, nimefanya vikao na wahusika, hasa makampuni ya simu, kuhusu
utaratibu wa malipo kwenye miito ya simu. Bado hatujamaliza lakini mambo yamebadilika kidogo na yataendelea kubadilika. Lakini pia nimeshiriki katika
kuweka presha ya mwanzo kwa vyombo vya habari, redio na televisheni, kuwalipa
wasanii pale wanapopiga nyimbo zao. Nilitambulisha kwa Waziri wa Viwanda na
Biashara Mheshimiwa Kigoda, vijana wenye teknolojia na utaratibu wa kuweza
kubaini nyimbo zote zilizopigwa na redio na luninga zote, au filamu zote
zilizoonyeshwa kwenye luninga, siku gani na kwa muda gani. Mazungumzo kati ya
COSOTA, wenye redio na TV na wasanii yamefanyika mara kadhaa na mradi mpya
umeanzishwa na Ndugu Rashid Shamte na unaosimamiwa na produsa mkongwe hapa
nchini, P-Funk, kwa ajili ya kufanikisha jambo hilo. Pia nimeendelea kuwasaidia
wasanii hawa mmoja mmoja kwa shida zao mahsusi. Nisingependa kuwataja na
kuzitaja hapa kwa sababu sio ustaarabu ila wasanii wengi wanajua kwamba mimi ni
rafiki yao na mtu wao na nitaendelea kuwa hivyo. Yapo mengi nimeyafanya kimya
kimya kusaidia tasnia hizi, ambayo siwezi kuyaorodhesha yote hapa” (Uk. 139).

Pia ni vyema tukaelezwa na tukaelewa jinsi ‘ushiriki/umiliki’
wa January katika Kampuni/Shirika la Maendeleo la Bumbuli hauleti mgongano wa kimaslahi
hasa ukizingatia yeye ni kiongozi wa umma ihali taasisi hiyo ina mwonekano
mwonekano wa ‘sekta binafsi’ na kutuletea hisia kuwa ni ‘kampuni binafsi’.

Ni vyema hilo likawekwa wazi mapema kabisa maana humo
kitabuni kuna majibu kama haya kutoka kwa January: “Pia tunatoa ushauri na
kushirikiana na Halmashauri ya Bumbuli kuiwezesha kupata mtaji wa shilingi
bilioni 5 kwa ajili ya kuwekeza kwenye shughuli za maendeleo” (Uk. 32);  “Shirika la Maendeleo la Bumbuli litaendelea
kubaki milele na kuwasaidia wananchi” (Uk. 36).

Sasa January akishinda Urais umelele huu utakuwaje? Je,
atamrithisha mtu mwingine (binafsi) kampuni/shirika? Atazuiaje upendeleo unaoweza kutokea
kwa kuwa yeye amekuwa Rais?

Ukweli

Ukweli ni nguzo muhimu sana ya uadilifu,
hivyo, itakuwa vyema January akatusaidia kujua kama baadhi ya majibu yake kwa
hakika ni ya ukweli – au ni ya uwongo (wa kisiasa). Pia ni vyema kujua kama
utata wa baadhi ya majibu yake unatokana na tatizo la uelewa – ama wa msomaji,
mwandishi au ‘mwandikwa’. Na pale ambapo inaonekana hakuna ‘uwazi’ kwenye
majibu yake, je, ni kwa sababu ya propaganda za kisiasa?

Tuanze na historia ya elimu. Kwenye
kitabu anatuambia hivi: “Nilipata daraja la kwanza kwenye mtihani wa kanda wa
mock wa kidato cha nne, nikiwa na uhakika wa kuendelea na A-Level katika Shule ya
Sekondari Kibaha, shule pekee iliyokuwa inafundisha mchepuo wa CBA hapa nchini.
Hata hivyo, nilifanyiwa hujuma kubwa kutokana na siasa zinazomhusu Mzee wangu
na kufutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne. Sikufa moyo, nilirudia
mtihani kama mtahiniwa binafsi na kufaulu na kuweza kusoma A-Level katika Shule
ya Sekondari Forest Hill Morogoro na nikapata Daraja la Pili kwenye mtihani wa
Kidato cha Sita” (Uk. 14-15).

Lakini kwenye tovuti yake
aliwahi kutuambia hivi: “So, we did our exams – and the day to go and look for
the result came. And, to the shock of friends and family and teachers, my name
was not there in the results sheet. I felt like collapsing. I went to another
result centre thinking that there was a mistake – again, nothing. Inquiries to
the reasons were not responded to immediately. Later we learnt that I was
mistakenly linked to a cheating scam that one of the teachers was involved in.
I was a pawn in a terrible mistake. A really long and painful story”.

Sasa swali la kiudadisi ni: Hiki kisa
cha mwalimu aliyeshiriki katika huo ufisadi wa  mitihani kina uhusiano gani na kisa cha siasa
za Mzee Makamba hadi uhusiano huo ukapelekea mtoto wake afutiwe matokeo? Ni watu
wangapi ‘huria’ ambao wamedhibitisha kuwa kisa cha kweli ni kipi hasa? Ni swali
muhimu kwa sababu kwa wale tuliosoma sekondari miaka hiyo tunakumbuka kuwa
uwizi wa mitihani (‘mafeki’) ulikuwa umeshamiri na kuna wakati hata wanafunzi
wenye akili nao walishiriki kuiba ili wasipitwe.

Kwa wale ambao tulikuwa tunafuatilia
sana mfumo wa elimu ya Vyuo Vidogo vya Jamii (Community Colleges) nchini Marekani katika miaka ya 90, tunafahamu
kuwa moja ya mbinu za Watanzania kufika Marekani na baadaye kupata udahili
katika Chuo Kikubwa Kiasi (College)
au Chuo Kikuu (University), hasa pale
matokeo yetu ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita yanapokuwa siyo mazuri, ni
hiyo ya njia ya ‘Community Colleges’. Hivyo, ni vyema pia January akawa muwazi
zaidi kwenye haya maelezo yake ya ziada ili kuondoa utata hasa kwa wale ambao
wanashuku ukweli kuhusu historia ya awali ya elimu yake ya juu, jambo tete ambalo
tunaona linatikisa sasa hata kampeni kali za Urais huko Nigeria: “Lakini
kilikuwa Chuo aghali kidogo, kwa hiyo nikaanza kusoma masomo ya awali kwenye
Chuo kingine kidogo katika jiji la Boston kinachoitwa Quincy College na baadae nikajiunga
na St. John’s University na kupata shahada ya kwanza ya sayansi ya masomo ya
amani (Bachelor of Science in Peace Studies)” (Uk. 15).

Ni vyema January atoe jibu thabiti na
vithibitisho ili wapiga kura wake tusije tukaona kwamba na yeye ni miongoni mwa
wale wale ambao Jenerali
Ulimwengu amewaelezea hivi
: “Tumeona…. jinsi kitoto kilichozaliwa katika
familia ya mafisadi kinavyolelewa kifisadi, kinavyosomeshwa kifisadi,
kinavyofanywa ‘kifaulu’ kifisadi, kinavyoajiriwa kifisadi, kinavyoozeshwa
kifisadi na kinavyokuwa kitu kingine cha ufisadi katika mwendelezo wa utamaduni
wa ufisadi kilimozaliwa. Sidhani kwamba tunaweza kuwa na matumaini ya kupata lo
lote la maana kutoka kitoto hicho kwa maana ya kuiendeleza nchi na kuwaendeleza
watu wake. Watu wa aina ya kitoto hicho hawawezi kuijenga wala kuiongoza nchi,
kwa sababu wao hawajajengwa wala kuongozwa katika misingi ya kujenga lo lote la
maana isipokuwa kuendeleza utamaduni uliowazaa na kuwalea”.

Ni ushuhuda kama huu ufuatao ambao
January ameutoa kuhusu safari yake ya kisiasa na vyanzo vilivyolipia shahada yake
ya umahiri ndiyo utatusaidia kuhisi hizo zinazotajwa kuwa zama mpya za kizazi
kipya cha viongozi zitazifunika hata zile zama za ‘ukweli na uwazi’ za awamu ya
tatu: “Nilipata wakati mgumu kulipa ada, kiasi cha kukaribia kufukuzwa shule.
Niliomba msaada kwa watu mbalimbali akiwemo Rais wa wakati ule Mhe. Benjamin William
Mkapa. Bahati nzuri, alikubali kusaidia kwa sharti kwamba nije kutumia utaalamu
wangu Serikalini nitakapomaliza masomo. Na ndivyo nilivyofanya. Baada ya masomo
hayo, nikajiunga na Wizara ya Mambo ya Nje….
Pale Wizarani, nilipata fursa ya kufanya kazi na
Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. Nahisi alipenda
kazi zangu na mara alipoamua kuwania nafasi ya Urais akanitaka nichukue likizo
isiyo na malipo Serikalini ili niwe msaidizi wake kwenye kampeni zile. Siwezi
kusahau maishani mwangu ile fursa kubwa kwani niliweza kuijua kwa kina nchi
yangu na watu wake. Baada ya Rais Kikwete kushinda aliniteua kuwa Msaidizi wake
Ikulu, nikiwa na jukumu la kumsaidia kuandika hotuba zake, pamoja na mambo
mengine mengi ya uendeshaji wa shughuli zake za kila siku” (Uk. 15-17).

January mwenyewe anasisitiza kwamba “Rais ajaye asiwe na chembe hata kidogo ya kuhisiwa kunufaika na fursa ya muda mrefu
wa uongozi katika Serikali” (Uk. 5). Wadadisi tunakubaliana naye. Ila tunapenda
kuifanyia ‘fomuleshini’ ‘mpya’ kidogo hiyo kauli ili isomeke hivi: ‘Rais ajaye
asiwe na chembe hata kidogo ya kuhisiwa kunufaika na fursa ya muda mrefu au
mfupi wa uongozi katika Serikali ama taasisi yeyote ya umma’.

Tusogee kwenye hili jibu lake kuhusu suala
lingine: “Tumejenga Chuo Kikuu kikubwa cha Sayansi na Teknolojia na chenye
hadhi ya kimataifa pale Arusha ambacho kinafundisha wanasayansi na watafiti wa ubora
wa juu, waliojikita katika kutumia elimu ya sayansi kutafuta majawabu ya
matatizo ya msingi ya Watanzania. Kuanzia mwakani tutakuwa tunatoa wahitimu
watafiti wa sayansi, yaani PhDs, 500 kila mwaka na tutaendelea kuongeza” (Uk. 35 ). Hivi
kweli kuna chuo (kipya) na kidogo duniani kinatoa shahada za uzamivu – PhDs –
ambazo kwa kawaida zinachukua miaka 3 na kuendelea kwa wingi kiasi hicho kwa
mwaka? Hii ni kosa la uandishi au ndilo jibu halisi alilolitoa ‘mwandikwaji’ January?

Pengine kwa kutambua kwamba wengi hatupendi wanasiasa wahodhi sifa hasa pale ambapo wameshirikiana na wenzao kufanikisha
jambo fulani, January analijibu swali mojawapo hivi: “Umeuliza pia kuhusu
mafanikio ambayo tumeyapata Wizarani hadi tuaminiwe kwa nafasi za juu. Labda
niseme kwamba Wizara haiendeshwi na mtu mmoja au wawili. Kuna timu ya
watendaji, wataalam na watumishi wa Wizara pamoja na taasisi zilizo chini ya
Wizara. Na pia kuna wenzetu wengine ndani ya Serikali nzima ambao bila wao Wizara
moja haiwezi kutimiza majukumu yake. Mara nyingi sijisikii vyema pale Wizara
moja au Serikali inapotimiza majukumu yake, basi hujitokeza mtu mmoja kusema
yeye kafanya – kwamba ni mafanikio yake” (Uk. 32-33).

Lakini anapoelezea mafanikio ya
Kamati yake, kuna sehemu anasema hivi: “Kuhusu gesi, kabla Kamati yetu
haijaundwa, hapajawahi kuwa na mjadala Bungeni kuhusu masuala ya gesi. Niliunda
Kamati Ndogo ya Kamati yangu ili kulichunguza kwa kina suala la gesi. Kamati
ile ilifanya kazi nzuri na kwa kweli napendekeza watu waitafute ile ripoti ya
kizalendo na kuisoma” (Uk. 59).

Ukiisoma ripoti hiyo iliyopo kwenye tovuti ya Bunge na iliyowasilishwa na Mbunge wa Bukene, Selemni Jumanne Zedi
kwa niaba ya Mwenyekiti unakutana na maneno haya: “Mheshimiwa Mwenyekiti,
chimbuko la Kamati Ndogo ni hoja zilizojitokeza wakati Kamati ilipokuwa
inajadili na kuchambua Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na
Madini kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. Wakati wa mchakato huo Kamati ilipata
taarifa kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu mapungufu mbalimbali yanayolenga
sekta ya gesi katika mahusiano ya wadau wa gesi. Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 15 Julai, 2011 wakati Kamati ya Nishati na Madini inawasilisha taarifa
yake ya Bajeti ya Mwaka 2011/2012, Bungeni katika sehemu ya Maoni na Ushauri wa
Sekta ya Gesi, Kamati ilitoa hoja ya kuunda Kamati Ndogo kufuatilia suala hili.
Wabunge waliunga mkono hoja hii na Mheshimiwa Spika alikubaliana na ushauri huo
wa Kamati. Aidha, Katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ufasaha, Kamati
Ndogo ilipewa Hadidu za Rejea (Terms of Reference) na Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Nishati na Madini”.

Hata ukisoma ukurasa wa 67 wa Hansard ya 15 Julai 2011 unakutana na maneno haya aliyoyasema January akiwa Mwenyekiti:
“Kamati haijaridhishwa na ushiriki, ufanisi na uadilifu wa Kampuni ya Pan
African Energy Tanzania katika mchakato wa uendelezaji gesi nchini. Hivyo basi,
kufuatia utata huu uliopo, Kamati ya Nishati na Madini inaunda Kamati yake
ndogo ili kufuatilia utata huu na tutadhihirisha wazi mambo”.

Japokuwa kwa kawaida Wenyeviti wa
Kamati au Tume wanakuwa ndiyo vinara wa kushawishi maamuzi yaelekee upande gani,
ni dhahiri kuwa matumizi ya maneno yenye muundo wa ‘nilifanya hiki au kile na kile’ badala ya ‘tulifanya hiki au kile’ ni uwongo na kama siyo uwongo, basi ni
kile kilichobatizwa jina la ‘propaganda’ au ‘jibu la kisiasa’.

Kuhusu baadhi ya mafanikio kwenye
sekta ya elimu, January anasema hivi: “Katika miaka 46, yaani tangu uhuru mwaka
1961 hadi mwaka 2004, tulikuwa tumejenga shule za sekondari takriban 1,200.
Katika miaka nane tu, kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2013, tumejen[g]a shule zaidi
ya 3,500. Mwaka 2004, kulikuwa na wanafunzi wa sekondari kama 400,000 hivi leo
hii wanakaribia milioni mbili. Nakumbuka wakati nikiwa Msaidizi wa Rais Ikulu,
Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka D[e]semba 2005, moja ya vitu vya kwanza
alivyoagiza ni kupewa taarifa ya wanafunzi wali[o]faulu mtihani wa darasa la saba
na ni wangapi wamepata nafasi za kwenda Sekondari. Taarifa iliyokuja ilionyesha
kwamba karibu nusu ya wanafunzi waliofaulu hawakuwa wamepata nafasi na ilikuwa
ndio basi wanabaki nyumbani. Hakuridhika na hali hiyo, kwamba wapo watoto wenye
vipaji, waliofaulu, lakini kwa kuwa tu hakuna shule basi wanarudi nyumbani. Na
hawa ni watoto wa miaka 13 na 14. Hakuna aliyekuwa na jawabu kwamba wakibaki nyumbani wanafanya nini. Ndipo akaagiza kwamba yajengwe madarasa na shule mpya
haraka na kwa mtindo wa operesheni ili walau ifikapo mwezi Machi watoto hawa
wawe wamepata nafasi” (Uk. 97).

Hapa kwa kweli tunaona kana kwamba
historia inaandikwa upya japo siyo kwa usahihi (kamili). Pengine ni kwa sababu
za ‘ajali ya kisiasa’ ndiyo maana January hayasemi yale ambayo tunayakumbuka tuliokuwa
kwenye harakati za HakiElimu
miaka hiyo ya 2005 na 2006 tukihoji maagizo
tete/tata ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Kwa kumbukumbu tulizo nazo,
kama zilivyorekodiwa katika taarifa mbalimbali kama hii ya Raising
The Stakes: The Impact of HakiElimu’s Advocacy Work on Education Policy and
Budget in Tanzania
, maagizo
mawili ya kiongozi huyo aliyejiuzulu kufuatia kashfa ya ufisadi wa Richmond
ndiyo yaliyopelekea ujenzi wa shule nyingi za sekondari (hasa zijulikanazo kama za kata) na udahili wa wanafunzi
hao waliofaulu ila wakakosa nafasi. Hivyo, ni vizuri kuuenzi
ukweli kwa kueleza sehemu yake ya kufanikisha hayo anayoyasifia January.

Dalili hizo za uchakachuaji wa
historia ya elimu nchini zinazidi kuonekana tunapokutana na ‘vijembe vya
kampeni’ kama hivi ndani ya kitabu hicho cha mazungumzo na January: “Rais Ajaye
anatakiwa aje na majawabu kuhusu namna gani ataendesha mageuzi makubwa na
machungu katika sekta ya Elimu. Kauli za juu juu tu za kuboresha elimu tunazosikia
kutoka kwa baadhi ya watarajiwa hazitoshi. Lazima kwenda kwa kina zaidi” (Uk.
7); “Kuomba uongozi hakuanzii na kuishia na kauli-mbiu rahisi za afya bure,
elimu bure ambazo hazina ufafanuzi wala maelezo – ambazo ni rahisi kuvutia na
kuhadaa watu. Hazishii na kauli za juu juu kwamba tutaongeza ajira au
tutaboresha elimu. Kila mtu aweza kusema haya. Swali kubwa ni kivipi? Kwa
maarifa gani mapya?(Uk. 11)

Uwazi

Kuna baadhi ya majibu ya January
yanatuacha na maswali zaidi. Ni vyema akawa wazi ili ukweli uwe dhahiri. Hili
litazaidia kudumisha ukweli na kukuza uwajibikaji.

Wapo, kwa mfano, ambao tunapenda
kujua ni akina nani hawa na walifanya nini hasa hadi January akasema hivi
kuhusu shirika/kampuni ya maendeleo ya Bumbuli:
“Kuna baadhi ya maeneo watu niliowaamini kuendesha shughuli za
ukopeshaji wametuangusha na wamewaangusha wananchi kwa hiyo tunalazimika kurekebisha
hali hiyo” (Uk. 32).

Pia tungependa kujua ana maana gani
hasa anapohitimisha aya ifuatayo kwa kusema maneno yanayoonyesha kana kwamba
kuna wajumbe wa kamati aliyokuwa anaiongoza ambao walizidiwa na vishawishi: “Kama
Kamati tulipata changamoto nyingi mara kwa mara. Sekta ya Nishati ni nyeti na
kuna watu wengi wenye maslahi makubwa katika sekta hii. Sekta hii inahusisha
fedha nyingi na kumekuwa na historia ya rushwa na ubadhirifu. Kazi kubwa
tuliyofanya ni kuhakikisha wajumbe wote tunasimama pamoja na kuepuka ushawishi
unaoweza kutupeleka pabaya. Katika kipindi changu tulifanikiwa kwa kiasi
fulani” (Uk. 59).

Hili ni suala muhimu kwa sababu hitimisho
la hilo jibu lake katika aya inayofuata linatumia neno lenye muundo wa ‘inaonekana’
ambalo kwa kawaida katika tasnia ya uandishi huashiria kukosa uhakika au ‘kupotezea’: “Binafsi
nilipata changamoto kubwa za kuchafuliwa. Kwa kuwa nilikuwa mkali sana na
niliharibia baadhi ya watu mianya yao ya kula na kwa sababu nilibainisha
udhaifu katika utendaji na kwa sababu niliweza kuaminiwa sana na Watanzania, zikafanyika
jitihada kubwa kunichafua. Nakumbuka mojawapo ni watu walitengeneza
barua pepe ikidaiwa inatoka kwa dada yangu kwenda kwa mpenzi wake wa kufikirika
eti akiomba pesa kwa ajili yangu na kisha hiyo barua pepe ikazungushwa dunia
nzima. Barua pepe ile ilibainika kwamba ni ya kugushi. Wahusika wa ile barua
pepe hadi leo tunasalimiana lakini wanaamini siwafahamu. Kamati ile ilivunjwa
baada ya mimi kuondoka kwa tuhuma za rushwa dhidi ya wanakamati wachache, ingawa
baadae tuhuma zikaonekana za kusingizia” (Uk. 59).

Na kama tunavyojua, John Mnyika
ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa kamati ile iliyovunjwa aliendelea
kuashiria kulikuwa na vitendo vya rushwa kamatini na kutaka ripoti ya uchunguzi
wa tuhuma hizo ijulikanayo kama ‘Ripoti ya Ngwilizi’ iwekwe wazi. Zitto Kabwe
naye alikuwa ni miongoni mwa wabunge waliotaka iwasilishwe na ijadiliwe kiuwazi Bungeni.

Pengine tunamdai January mengi kwenye
hili la uwazi kuliko anayoweza kuyaweka kiuwazi hasa ukizingatia kuna sehemu
amekuwa muwazi kutueleza yafuatayo kuhusu usiri: “Kama Msaidizi wa karibu wa
Rais unapata fursa ya kujifunza kwa karibu jinsi siasa na uongozi wa nchi
unavyoendeshwa. Kila kiongozi huwa anapitia vipindi vigumu katika uongozi wake.
Na kwa Rais Kikwete ilikuwa hivyo hivyo. Zipo nyakati nyingi nilikosa usingizi.
Zipo nyakati tulipaswa kuandika hotuba ngumu kukabiliana na mazingira magumu na
masuala mazito yaliyokuwepo kipindi hicho. Kwa mfano, wakati wa ukame na njaa
kubwa iliyoikumba taifa mwaka 2007, kipindi cha kashfa za EPA na Richmond, na
pia kipindi ambacho taifa lilikumbwa na wimbi kubwa na kutisha la ujambazi.
Unapata fursa ya kujua siri nyingi za nchi na lazima uwe na ukomavu na uwezo wa
kuzitunza. Yapo mambo mengine niliyoyaona na kujifunza ambayo nitakwenda nayo
kaburini lakini yalinipa elimu tosha ya uongozi” (Uk. 68).

Uzoefu

Katika majibu yake January ametumia
nafasi, muda na nguvu nyingi kujibu madai – ama mashambulizi – kuwa hana uzoefu. Hoja
hii ya uzoefu imefungamana na hoja ya ujana na kwa kiasi kikubwa sana
amefanikiwa kuupangua ‘mfungamano’ huo kwa kutumia dhana ya rika. Tatizo lipo kwenye mifano anayoitoa
kushibisha hoja yake kuwa amekomaa na ana uzoefu wa kutosha.

Tuanze na mfano ulio karibu na
nyumbani kabla hatujaenda huko Ughaibuni. January anatuambia hivi: “Wakati
wazee wanamchagua Mwalimu Julius Nyerere kuwa Rais wa TANU mwaka 1954 ili aongoze
harakati za uhuru, ambazo ni ngumu na hatari kuliko hata uongozi wa nchi,
ukomavu wake haukutazamwa kwenye umri wake mdogo wa miaka 32” (Uk.
30).

Mahali pengine humo kitabuni anasema
hivi: “Wakati Mwalimu Nyerere anachaguliwa kuwa Rais wa TANU mwaka 1954, akiwa
na miaka 32 tu, ili kuongoza harakati za kutafuta uhuru wa nchi yetu, kama
kungekuwa na swali kwamba kwani kafanya nini hadi awe Rais wa TANU, kwamba kuna
wanaostahili zaidi Urais wa TANU kwa sababu wamefanya makubwa zaidi hata kabla
Mwalimu hajatia mguu Dar es Salaam, basi historia ya nchi yetu ingekuwa tofauti
na ilivyo leo” (Uk. 33).

Hapo tatizo la kwanza ni hoja ya
awali kuwa harakati za uhuru zilikuwa ngumu na hatari kuliko hata uongozi wa
nchi (tena nchi changa). Hapa tunamwongelea Nyerere aliyetaka kupinduliwa na (wana)jeshi mwaka 1964 na kutaka kupinduliwa tena kwenye miaka ya 70 na miaka ya ya
mwanzo ya 80. Pia tunayemwongelea ni Nyerere aliyeongoza nchi kwenye vita dhidi
ya Nduli Idi Amin. Hali kadhalika huyu ni Nyerere aliyeongoza nchi katika
kipindi ambacho wengi wa viongozi wakuu wenzake wa nchi za Afrika walipinduliwa
ama kuuwawa – kina Patrice Lumumba, Sylvanus Olympio na Kwame Nkrumah. Baadhi
ya magumu haya January anayaelezea kwa ufasaha mwishoni mwa kitabu anapojibu swali
la 39 kuhusu Rais aliyeacha historia kubwa ila hapa mwanzo halitilii mkazo kwa kuwa (inaonekana) anajenga madai
kwamba kama ni uzoefu hata Nyerere wa 1954 hakuwa tofauti na January wa 2014.

Kisha tatizo la pili ni hiyo hoja
kuhusu Nyerere na uongozi wa TANU. Huyo ni Nyerere aliyekuwa ‘Mwenyekiti Mwanzilishi’ wa tawi la AA akiwa katika Chuo cha Makerere, hii ikiwa na maana
alikuwa anawaongoza wenzake ambao wengi wao ndiyo walikuwa wawe viongozi wa serikali
itakayopata uhuru kutoka kwa wakoloni. Huyo huyo Nyerere alikuwa ni ‘Mwenyekiti Mwanzilishi’ wa TAA ambayo ndiyo iliizaa TANU. Maswali hayo kuhusu uzoefu wa
Nyerere hasa ukimlinganisha na Abdulwahid Sykes yameshaulizwa na kama tujuavyo Mohamed Said amelishikilia sana
hilo bango katika vitabu na makala zake. Lakini sababu maalumu iliyopelekea
Nyerere kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti badala ya Sykes sote tunaifahamu.

Ukishajenga msingi wa hoja yako kwa
kusema kwamba kuongoza harakati za uhuru ni kazi ngumu kuliko kuongoza nchi
basi unajikuta unaacha kabisa kuongelea ni uzoefu gani Nyerere aliupata kabla
hajawa Waziri Mkuu na Rais tulipopata uhuru na kuwa jamhuri mwanzoni mwa miaka
ya 60 – ukifanya hivyo unaacha kuongelea yafuatayo:

Kwa mujibu wa mwanahistoria mmoja wa
nchi yetu, John Iliffe, kama kiongozi wa TANU, Nyerere
alishirikiana na wenzake kufungua matawi nchini kote na kufikia mwaka
1955 walikuwa wakipata wanachama wapya 100 kila siku; mwaka huo huo Nyerere alishiriki
kwenye Baraza la nchi zilipo chini ya Uangalizi wa Umoja wa Mataifa jijini New
York ambapo alitoa tamko liloipaisha TANU ndani na nje ya nchi; mwaka 1958 Nyerere alijiuzulu kwenye
Baraza la Kutunga Sheria kupinga mfumo ‘pendekezwa’ wa uchaguzi; mwaka huo huo
Nyerere alimshinda Kunambi kwenye uchaguzi kwa kura 2,628 dhidi ya 802 na wala
hakupita bila kupingwa tu kama baadhi ya wanasiasa wetu; mwaka  1960 Nyerere na wenzake walishinda uchaguzi
wa Septemba na kisha (w)akaunda Baraza lake la kwanza kabisa la Mawaziri.

Ukiacha kuongelea historia hiyo ya
kabla ya Urais wa Nyerere basi inakuwa siyo vigumu kudiriki kusema maneno haya
kitabuni: “Jingine ninaloweza kusema ni kwamba hakuna kazi yoyote inayomuandaa
au kumkomaza mtu kuwa Rais wa Tanzania. Kuna watu wanne tu hapa Tanzania ambao
tunaweza kusema kuwa wana uzoefu wa Urais: Mwalimu Nyerere, Mzee Ali Hassan
Mwinyi, Mzee Benjamin William Mkapa, na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kinachomfanya mtu awe tayari ni makuzi yake, maadili yake, busara yake, hekima zake, dira yake pamoja
na vipaji na talanta na karama alizojaliwa na Mungu” (Uk. 30).

Mifano ya ugenini ndiyo inaongeza
utata. Tunaambiwa hivi kitabuni: “Moja ya mijadala mikubwa kwenye uchaguzi wa
Marekani wa mwaka 2008 ilikuwa ni hili la uzoefu. Obama alikuwa Mbunge kwa
miaka mitatu tu, basi. Hajawahi kuwa hata Naibu Waziri. Viongozi wenzake na
wengine waliompinga wakasema hana uzoefu. Wamarekani wengi wa kawaida wakasema
kwamba sifa na ubora wa uongozi haupimwi kwa miaka mingi na nafasi za ndani ya
Serikali. Wakampa kura nyingi kuongoza taifa kubwa duniani” (Uk. 25-26).

Wadadisi tunagoma kukubali tu
tunachoambiwa na kupumbazika hivyo tunaingia mtandaoni kusoma historia ya Obama. Humo tunakuta yafuatayo: Mwaka 1992 Obama ni Mkurugenzi wa Mradi wa Kura
katika jimbo la Illinois na anafanikisha uandikishwaji wa wapiga kura 100,000
hasa kutoka kwenye jamii zilizoko pembezoni; Mwaka 1996 Obama anagombea kuwa
Seneta wa jimbo la Illinois na kushinda. Anachaguliwa tena mwaka 1998. Mwaka
1999 anagombea Ubunge na anashindwa kwa uwiano wa 2 kwa 1 baada ya
kutokuwepo wakati wa kutopitishwa muswada wa kudhibiti matumizi ya bunduki
maana alikuwa anamuuguza binti yake jimboni Hawaii, hivyo anaendelea na useneta na kufanikisha
kupitishwa kwa miswada ipatayo ishirini kuwa sheria.

Hapa inabidi tutulie na kutafakari
kidogo maana kuna madai kuwa huo Useneta wa Illinois ni sawa tu na Udiwani wa Bumbuli hivyo kumlinganisha January katika hilo ni sawa na kusema alipaswa kuwa Diwani
kwanza kabla hajawa Mbunge. Kwanza, siyo sahihi kwa kuwa kwa kiasi kikubwa jimbo moja la Marekani ni
kubwa kuliko Wilaya ya Tanzania na lina(hitaji) ugatuzi mkubwa wa madaraka  hivyo ni kama vile nchi/dola iliyo ndani ya
nchi/dola ambayo kwa kiasi kikubwa inajiendesha yenyewe. Pili, maneno hayo ni
dharau kubwa sana kwa Udiwani na sera/dhana nzima ya kugatua/kupeleka madaraka
zaidi mikoani, wilayani na vijijini.

Tukirudi mtandaoni tunaona kuwa mwaka
2003 Obama hatimaye anashinda Ubunge, hii ikiwa ni baada ya kushinda
Useneta kwa mara nyingine mwaka 2002. Hivyo, Obama hadi kufikia hapo alikuwa na
uzoefu mkubwa wa siasa za ushindani na siyo za kupita tu kwenye uchaguzi bila
kupingwa kwa sababu wagombea wamejitoa, wametolewa au wamelazimika kujitoa. Kwa kushirikiana na wenzake akiwamo mbunge wa kilichokuwa chama tawala nchini Marekani, mwaka 2006
Obama anafanikiwa kupitisha muswada kuwa sheria inayoruhusu Wamarekani kuingia mtandaoni na kuona matumizi ya kodi zao.

Huyo ni Obama aliyekuwa kwenye chama
kilichokuwa cha upinzani. Lakini akaweza kufanya ushawishi wa kimkakati mpaka
muswada wake ukapita na kuwa sheria ya nchi. January yuko chama tawala, analeta
muswada mwaka 2012, leo mwaka 2015 jibu lake kuhusu ulipoishia ni hili:
“Nilipowasilisha Muswada [wa Sheria ya Kudhibiti Shughuli za Upangaji wa Nyumba
(Rental Housing Act)] ulipokelewa vizuri na Wabunge wote. Serikali pia
iliupokea vizuri na ikaahidi kwamba kabla ya Sheria hii kutungwa basi lazima
kuwe na Sera ya Nyumba kwanza. Hivyo ndivyo alivyoahidi [aliyekuwa] Waziri,
Mheshimiwa Profesa Bungeni. Mimi
naamini swala hili litatekelezwa mapema” (UK. 123).

 Mapema ipi ilhali Bunge
karibia linavunjwa na lina viporo vingi vimeachwa baada ya mjadala mkali wa
ESCROW? Au utapitishwa atakapopata makazi ‘mapya’ Ikulu?

Mfano huu wa January kuhusu Tony Blair ambaye kumbe alikuwa Mbunge wa kugombea toka mwaka 1983 na Waziri Kivuli
pamoja na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kuanzia1994 baada ya kugombea/kushinda unafurahisha
zaidi: “Majuzi
kuna rafiki yangu alitumia nukuu ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair aliyoitoa mara baada ya kuchaguliwa kuongoza Serikali mwaka 1997. Tony Blair,
aliyechaguliwa kuongoza Uingereza akiwa na miaka 43 tu, alisema kwamba “wakati
nachaguliwa kama Waziri Mkuu, nilikuwa sijawahi kushika nafasi yoyote
Serikalini. Sikuwahi kuwa hata Naibu Waziri. Na Uwaziri Mkuu ndio kazi yangu ya
kwanza na pekee Serikalini”
”(Uk. 26).

January naye anatuambia anakijua
chama chake “vizuri sana” (Uk. 29). Kwa nini? Kwa sababu ya nyadhifa alizoshika:“Naweza kuelewa
kwamba, bila hata kujali umri, mtu ambaye hajawahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu au
Halmashauri Kuu ya Taifa anawezakupata changamoto ya uelewa wa namna ya
kukiongoza Chama chetu. Lakini kama umeshakuwa Mjumbe wa Sekretarieti, Mjumbe
wa Kamati Kuu, Mjumbe wa Halmashauri Kuu, kama ambavyo nimeshawahi kushika
nafasi zote hizo, utakuwa umepata uelewa madhubuti wa uendeshaji na uongozi wa
Chama” (Uk. 166).  Je, ni kwa muda gani na nini hasa alifanya katika kila kipindi? Hatuelezi
moja kwa moja, tunaambulia neno ‘kitambo’ maana kati ya mwaka 2010 na 2015
hajatulia kwa muda kenye wadhifa mmoja. Au ndiyo masuala ya kasi ‘mpya ya upya’?

Hebu tumsikilize: “Baada ya kitambo
kidogo, nikateuliwa kwenye Sekretarieti ya Chama nikiwa kama Katibu wa NEC wa
Siasa na Mambo ya Nje, na nikawa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya
CCM. Nilishika nafasi hizi katika kipindi kigumu sana kisiasa kwa Chama chetu
na nilijifunza mambo mengi  mchango wangu
kwenye kukijenga na kukiimarisha” (Uk. 17-18).

Pengine haya maandalizi ya “kitambo
kidogo”,  ama ‘voda fasta’ kama tukitumia
lugha ya vijana wa ‘kizazi kipya’ cha ’dot com’, ndiyo haya anayoyaongelea Mzee Mwinyi kwenye
Dibaji ya kitabu hicho: “Nilimteua Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mbunge na
Naibu Waziri akiwa na umri wa miaka 38 tu na baadaye Waziri wa Wizara muhimu ya
Maji, Nishati na Madini akiwa na umri wa miaka 40 na baadaye Waziri wa Fedha.
Sikufanya hivyo kwa sababu tu ya umri wake bali kutokana na kuamini katika
msingi wa kuandaa viongozi wa vizazi vijavyo kwa kuwapa majukumu katika Chama
na ndani ya Serikali” (Uk. vii-viii).

Ubunifu

Kuna tofauti kati ya uvumbuzi (invention) na ubunifu (innovation). Kwa tafsiri rahisi,
uvumbuzi ni ugunduzi wa kitu kipya na ubunifu ni ubadilishaji/uendelezaji wa
kitu kwa namna ‘mpya’ au nzuri zaidi. Kwenye kitabu cha January kivumishi
kitokanacho na mzizi ‘-bunif-’ kimetumika mara 22 na majibu yake
yamemtambulisha kama mbunifu.

Kwa mfano, kwenye ukurasa wa 89
January anatujulisha hili kuhusu kutuzwa na taasisi ya National Democratic Institute inayoongozwa na Waziri mstaafu wa Mambo ya Nje wa Marekani, Madeleine
Albright: “Tuzo niliyopewa mimi inaitwa Democracy Award ambayo nilishinda
kutokana na ubunifu wa kutengeneza mfumo wa kuwasiliana na wapiga kura wangu wa
Bumbuli kwa kutumia SMS. Tuzo hii nilishinda pamoja na Rais wa nchi ya Estonia na
mwanzishaji na mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Jack Dorsey. Nilipewa
heshima ya kuzungumza katika halfa hiyo iliyokuwa na viongozi wakubwa katika
Serikali ya Marekani. Ilikuwa heshima kubwa kwa sababu huko nyuma waliopata
kushinda tuzo hii ni pamoja na Kofi Annan na Desmond Tutu” (Uk. 89).

Anastahili pongezi kwa hilo hasa
kutoka kwa waumini wa ‘demokrasia ya kiliberali’ (liberal democracy). Wakati ubunifu huo
ulipofanyika kulikuwa na msisimiko na mvuto mkubwa mtandaoni miongoni mwa
watumiaji wa twitter nchini Tanzania. Tulipewa taarifa ya jinsi Wanabumbuli walivyokuwa wanautumia na hata kuwekewa nukuu kutoka kwenye SMS zao. Pengine
itakuwa vyema kama January atatueleza uendelevu wa ubunifu huo na kama umeweza
kufikia maeneo mengine ya Tanzania. Hili ni muhimu maana kuna vitu vingi sana
vizuri vimebuniwa ulimwenguni lakini kutokana na sababu mbalimbali
havitumiki.

Maadam January tayari ni kiongozi
mkubwa wa Serikali katika sekta ya mawasiliano ni vyema pia akaufanyia na
majaribio ya awali na huu ubunifu mwingine anaouelezea ili angalau tupime kama unafanya kazi
kweli/kiuhalisia badala ya kusubiri mpaka atinge Ikulu ndiyo tufanywe kuwa
sehemu ya maabara ya majaribio: “Nimefarijika kuanza kuona kwamba kuna makampuni
kadhaa yameanza shughuli za kuweka rekodi za ukopaji, yaani Credit Reference,
kwa ajili ya matumizi ya mabenki na taasisi nyingine. Hili ni jambo jema. Lakini
mimi naamini kwamba kuna fursa ya ubunifu zaidi. Kwa mfano, karibu kila
Mtanzania anatumia simu ya mkononi na kila siku anatumia airtime au anahifadhi
pesa kwenye simu na kuhamisha na kufanya manunuzi mbalimbali. Simu ni kama
akaunti ya benki siku hizi. Na kwenye simu kuna taarifa muhimu ya kujua nguvu
ya kiuchumi ya kila mtumiaji simu. Makampuni ya simu, kwa ruhusa ya watumiaji, yanaweza
kutumia taarifa hizi kama credit reference na kuwezesha watu wasio kwenye sekta
rasmi lakini wenye nguvu ya kiuchumi kuweza kukopesheka na kupata mikopo nafuu
ikiwemo ya ununuzi na ujenzi wa nyumba au mikopo ya biashara” (Uk. 124).

Au kwa kuwa hatuna Waziri wa Ardhi
kwa sasa pengine Rais amteue January kuziba nafasi hiyo ili afanye na hili
jaribio lake la kibunifu tuone kama litawezekana: “Asilimia zaidi ya 60 ya
wakazi wa Dar es Salaam wanaishi kwenye makazi yasiyo rasmi na wanalipa kodi
kubwa kuliko hali ya nyumba wanazoishi. Jawabu ni kujenga nyumba zaidi. Jawabu
la haraka ninalolifikiria ni kubadilisha kabisa maeneo yanayoonekana kama ni
mabaya – Manzese, Tandale, Mbagala, Vingunguti na kwingineko – kuwa mazuri. Kwa
mfano, ukienda Manzese ukaainisha eneo lenye nyumba duni la ukubwa wa uwanja wa
mpira wa miguu, ambalo linaweza kuwa na familia kama 200, halafu ukazungumza na
wakazi hao na kuwashawishi wakubali kuhama na kuwalipia makazi ya muda kwa miezi
kumi na nane ili kuliendeleza. Wakihama, lile eneo unalivunja na kujenga nyumba
za ghorofa tatu au nne zitakazochukua familia si chini ya 800, kuweka mifereji,
bustani, maduka, na shule. Ukimaliza unazirudisha zile familia 200 katika
nyumba hizi mpya bora zaidi na unakuwa umepata nafasi mpya kwa familia 600
zaidi katika eneo lile lile. Halafu unaendelea kwa kukata kipande kingine tena
sawa na uwanja wa mpira wa miguu ambapo utapata familia nyingine 200 na safari
hii huna haja tena ya kuzihamisha familia za eneo hili kwenye makazi ya muda
kwa miezi kumi na nane, kama ulivyofanya mwanzo, kwa sababu tayari una nafasi za
familia 600 – kwa hiyo utatoa nafasi 200 na kubakiwa na nafasi 400. Kwa hiyo
utajenga kwenye eneo hilo na kupata nafasi nyingine mpya za familia 800
halafu ukijumlisha na zile 400 utakuwa na nafasi za familia 1,200. Familia 400
za kwanza zilizohamishwa zitalipa kodi sawa na waliyokuwa wanalipa zamani na
nafasi mpya zilizobaki zitauzwa au kukodishwa kwa gharama nafuu. Ukiendelea
hivi na mpango huu katika maeneo yote tunayoyaita ya uswahilini katika miji
yetu utapunguza sana tatizo la makazi, utapendezesha mji na utawezesha watu
wanaoishi kwenye miji kuishi kwenye nyumba zenye hadhi zinazohifadhi utu wao”
(Uk. 119-120).

Inaonekana bila madaraka makubwa au fursa
ya kuwa karibu na wenye madaraka makubwa inakuwa vigumu kutekeleza
kilichobuniwa pengine ndiyo maana ni muhimu mtu awe Rais au awe karibu na Rais.
Mfano ufuatao unaonekana kudhihirisha hilo: “Kwa kifupi sana, nimefanya mambo
kadhaa: kwanza, ingawa hili halijatangazwa sana, lakini watu wa TRA, BASATA,
COSOTA na wengineo wanafahamu kwamba kuanzia mwaka 2008 nikiwa Msaidizi wa
Rais, niliitisha vikao vya wadau wa muziki na filamu, ikiwemo wasambazaji wote
wa filamu, ili kuangalia namna ya kuisaidia tasnia hizi. Katika kikao
nilichoongoza, ndipo wazo la stika za TRA tulipolibuni kwa mara ya kwanza. Hata
hivyo, suala hilo lilihitaji utafiti kidogo, na utafiti huo ulihitaji pesa.
Nikaenda kumuomba Rais Kikwete pesa hizo, akakubali kutoa shilingi milioni 20,
ambazo zilipelekwa TRA ambao ndio waliosimamia utafiti huo. Dhana nzima ya
kuanzisha stika ilikuwa ni kwamba kazi za wasanii lazima zitambuliwe rasmi na
kuwe na taasisi Serikalini inayosimamia uchakachuaji wa kazi hizo kwa kuwa huko
nyuma ilikuwa ni holela tu na ilionekana kama halali kufanya uharamia kwenye
kazi za wasanii. Tukaona kwamba, kwa kuwa, ukiwa na sigara feki, mvinyo feki au
konyagi feki, unakamatwa na Serikali, basi tuweke utaratibu kwamba ukiwa na CD feki
basi pia ukamatwe na Serikali. Na kwa kuwa sigara, konyagi na mvinyo zinawekwa
stika ili kuzitambua halali na feki, basi na kwenye kazi za wasanii na kwenyewe
tuweke stika za TRA ili Serikali iwe na wajibu wa kusimamia kazi hizi. Bahati
nzuri tukaanza utekelezaji. Imechukua muda na mwanzo tumeanza kwa kusuasua na
kukiwa na changamoto za hapa na pale lakini naona sasa TRA wameamka na kuanza
kukamata kazi feki. Kwa hiyo, naona fahari kwamba

 hili ni jambo nililianzisha, kwa maelekezo ya
Rais, nikiwa Ikulu na likaingizwa kwenye mfumo wa Serikali na kupelekwa Bungeni
na sasa ni utaratibu rasmi” (Uk. 137-138).

Masuala mengine kama haya inaonekana hayahitaji mpaka mtu uwe na (ukaribu na) madaraka ya Kiikulu/Kirais: “Nilishawahi kwenda pahala kwenye
shule ya sekondari nikapewa kero ya maji, kwamba yapo mbali na sio masafi.
Lakini nikaangalia ile shule ina majengo makubwa zaidi ya 9. Nikauliza hali ya
mvua huwa ikoje. Nikaambiwa huwa zinanyesha sana, hasa wakati wa masika
na vuli. Tukaanzisha harambee ya kujenga kata za kukinga maji na
matenki ya kuhifadhi maji. Siku hizi naambiwa kwamba mvua zinakuta bado maji
ya msimu uliopita yapo na wanakijiji pia wanayatumia. Kwa hiyo, kwanza,
katika masharti ya kutoa vibali vya ujenzi, kuwepo na kanuni mahsusi za
kulazimisha uwepo wa miundombinu ya kukinga maji katika majengo na kuyahifadhi” (Uk. 157).

Kwenye suala la “majimbo ya kiuchumi”,
January anasema anaamini “kwamba kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukitazama
mgawanyo wa maeneo ya nchi yetu katika misingi ya kiutawala au kiuongozi zaidi
kuliko kiuchumi” (Uk. 45). Tatizo linakuja kwenye uchambuzi wake wa kihistoria
ambapo anasema “Mfumo wa uchumi wa kikoloni uliitazama nchi yetu kama eneo la
uzalishaji mali, kama vile shamba tu la Malkia. Wakoloni hawakujali maendeleo
ya watu wetu. Ndio maana kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu yalitengwa tu kwa
ajili ya kutoa manamba kwenye mashamba, na kuna baadhi ya maeneo yalitoa askari
tu katika jeshi la mkoloni. Miundombinu yote iliyojengwa na mkoloni ilikuwa ni
kwa ajili ya kusafirisha bidhaa ghafi kuja bandarini kwa ajili ya kusafirishwa
nje ya nchi” (Uk. 45).

 Lakini huo ndiyo mfumo wa ‘siasa uchumi’ wa
kikoloni ambao ulijikita katika majimbo 9 ya kiutawala/kiuchumi wakati wa ukoloni wa
Mwingereza. Wakati tunapata uhuru mwingereza mmojawapo, Kathleen Stahl,
alitembelea majimbo hayo na kuandika kitabu cha Tanganyika: Sail in the Wilderness ambapo alijaribu kuelezea
uchumi wa kimajimbo. Tulipopata uhuru ilibidi tuamue kubaki na mfumo huo au kujaribu kujenga mwingine wa mikoa hasa kwa kuzingatia kuwa uchumi
unaingiliana na siasa.

Sasa wazo la January ni lile lile la
wakati wa ukoloni ila safari hii limebeba hoja kwamba majimbo/kanda ziwe 6 na, kwa
kuzingatia maneno yake yafuatayo kuhusu jimbo/kanda ya Dar es Salaam, pia
maendeleo ya jimbo mojawapo yasififishe ya lingine: “Cha msingi ni kwamba
maendeleo na uwekezaji katika ukanda huu yasiwe na yasionekane kuwa na athari
kwa maendeleo na uwekezaji kwenye kanda nyingine za kiuchumi. Maendeleo na
uwekezaji kwenye kanda hii yawe ni sapoti kwa maendeleo ya nchi nzima” (Uk.
56).

Hayo mawazo yake pia ni mwendelezo wa
sera ya majimbo ya chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, ambacho hata nacho
kinayaangalia majimbo kiuchumi na si kiutawala tu. Ukiyasoma maandishi ya
wanasiasa vijana wenzake, John Mnyika na Zitto Kabwe,  hasa waliyoyaandika kabla ya 2014, kuhusu
majimbo au mikoa fulani ndani ya majimbo na kuyalinganisha na haya ya January
ni kana kwamba kuna ‘kuegelezeana’.

Kwa mfano, mnamo tarehe 11 Januari 2013 Mnyika aliandika hivi kwenye makala yake yenye kichwa cha habari Sera
ya Majimbo ya CHADEMA Siri ya Maendeleo
: “Mwaka 2005 wapinzani wa
hoja hii walitoa hoja kwamba lipo jimbo ambalo halina rasilimali na walitolea
mfano wa jimbo la kusini. Hawa ni watu ambao pengine walikuwa hawafahamu kwamba
Tanzania ina rasilimali kila mahali. Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa
mikoa ya kusini haina maendeleo.Wakati huo tuliwaeleza ukweli ni kwamba tafiti
zinaonyesha mikoa ya kusini ina rasilimali na mali asili nyingi sana tatizo
kubwa ni miundo mbinu. Tuliwapa mfano kuwa Jimbo la Pwani ya Kusini kwa mfano
lina mikoa ya Lindi, Mtwara na maeneo mengine yana rasilimali kama madini,
bandari, uvuvi, nishati ya gesi, kilimo cha korosho, mikoko pamoja na utalii. CHADEMA
imeendelea kuwaeleza wananchi umuhimu wa mfumo mpya wa utawala kwani kila jimbo
lina rasilimali za kutosha ila kwa kuwa serikali ya CCM imekuwa ikiwahadaa
wananchi na kuwafanya wabweteke kisaikolojia ili wasijiletee maendeleo, imekuwa
ikipinga vikali serikali ya majimbo. Baada ya ugunduzi wa ziada wa gesi, sasa
hoja imebadilika kutoka kusini haina rasilimali; sasa lugha ni kuwa kusini
haipaswi kudai manufaa ya rasilimali hizo kwa kuwa ni za nchi nzima”.

Linganisha na haya ayasemayo January
kitabuni mwaka 2014/2015: “Kanda nyingine ni Kanda ya Kusini yenye mikoa ya
Mtwara, na Lindi. Kwa miaka mingi mikoa hii imeonekana kama imesahauliwa
kimaendeleo ingawa inazo fursa nyingi za kiuchumi zinazoweza kutumika kuinua
kipato cha watu wake. Kutokana na historia ya mikoa hii Serikali ina wajibu
kufanya juhudi za maksudi za kuhakikisha maendeleo ya mikoa hii inapatikana.
Mwanga mpya umepatikana kutokana na uvumbuzi wa gesi ambayo inapaswa
kuwanufaisha wananchi wa mikoa hii na taifa kwa ujumla…. Mikoa ya Lindi na
Mtwara pia sasa imepata fursa mahsusi ya kiuchumi kutokana na upatikanaji wa
gesi. Fursa za kuwepo kwa gesi ikiwemo viwanda vya kuchakata gesi kwa ajili ya
kuiuza nje ya nchi ni muhimu pia ikatumika kuipa Kanda hii mwamko mahsusi wa
kiuchumi wa kuweza kubadilisha maisha yawatu wa kawaida. Ni muhimu kutengeneza
maarifa mahsusi ya kuwashirikisha wananchi katika uchumi huu” (Uk. 48).

Baada ya CHADEMA kushindwa kuiuza sera yao ya majimbo mwaka 2005-2010 kwenye Ilani yao ya Uchaguzi ya 2010-2015
wakaja na gia ya maeneo maalumu. Hivi ndivyo inavyosema kuhusu eneo hilo: “Mikoa
ya Mtwara na Lindi ni mikoa ambayo bado haijachangia inavyostahili katika masuala
ya uchumi na imekuwa bado ikikimbiwa kutokana na kile kinachoaminika kuwa ni
ugumu wa maisha na umbali uliopo na maeneo yaliyofanikiwa zaidi. Chini ya
serikali ya CHADEMA hili halitakuwa hivyo kwani mikoa hii ndio itaunda kile
ambacho tunakiita kuwa ni “Makao Makuu ya Mapumziko Afrika” (Africa’s
Vacational Capital). Lengo ni kuhakikisha kuwa miji hii inavutia uwekezaji mkubwa
katika masuala ya mapumziko (Leisure). Katika kutekeleza azma hii, Serikali ya CHADEMA
itachukua hatua zifuatazo…. Serikali itaanza ujenzi wa barabara za kisasa ndani ya
mikoa hiyo na za kwenda nje ya mikoa hiyo ili hatimaye kuinganisha mikoa hiyo
na mikoa ya Morogo[ro], Pwani, na Ruvuma….” (Uk. 90)

January naye anasema hivi: “Moja ya sehemu zenye fukwe nzuri zaidi katika ufukwe mzima wa Bahari ya Hindi kutoka Djibouti hadi Cape
Town ni kipande cha kutoka Kilwa hadi Mtwara. Kipande hiki hakijaendelezwa sana
kiutalii. Inawezekana kabisa kujenga mahoteli makubwa ya kitalii na viwanja vya
kisasa vya mchezo wa gofu na uvuvi wa kitalii (sports fishing) kwenye kipande
hiki lakini cha kwanza ni kuboresha miundombinu ya kufika huko, ikiwemo
barabara na viwanja vya ndege. Ajira na

kodi na manufaa mengine
yatakayopatikana kutokana na kufunguka kwa eneo hili kutabadilisha kabisa hali za
maisha za watu wa kanda hii” (Uk. 50).

Tunaiona pia Ilani ya CHADEMA ya 2010-2015 ikisema
hivi: “Mkoa wa Kigoma utapewa kipaumbele cha kuwa kiunganish[i] cha Tanzania na
nchi ya DRC. Hivyo, mikakati ya makusudi itafanyika kama ambavyo tumedokeza
awali lakini vile vile pia kuhakikisha kuwa mji huu unafikika kirahisi kutoka
maeneo mengine ya Tanzania. Kipaumbele kikubwa kitakuwa ni katika kuboresha
usafiri wa Reli ya Kati na Ujenzi wa barabara za kisasa za kuunganisha mkoa huo na Tabora na Shinyanga na kuunganisha na Mwanza kupitia Shinyanga Magharibi.
Serikali ya CHADEMA …. Itahakikisha…. Kunakuwa na mapunguzo ya kodi mbalimbali za
viwanda ili kuchochea ujenzi wa viwanda mbalimbali hasa vile vya kuhifadhia
chakula, nyama na matunda. Tutahakikisha kuwa kilimo cha mawese kinapata mwamko
mpya na kuwa chanzo kikubwa cha mapato” (Uk. 91).

Halafu tunamwona January akisema hivi
kitabuni: “Kigoma inaweza kuwa kituo kikubwa cha biashara na uwekezaji kinachohudumia
nchi jirani za Burundi na Kongo. Moja ya njia ya kufanya hivyo ni kuipanua
Bandari ya Kigoma ili iwe bandari huru na bandari kubwa ya mizigo – na uchukuzi,
kwa nchi za Burundi na Kongo, kwa kuwa Kongo ya Mashariki inategemea upande wa
Tanzania kwa karibu bidhaa zote. Hili lazima liende sambamba na kuimarisha reli
ya kati ili iwe ya kisasa ikiwa na treni ya abiria na mizigo karibu kila siku…. Mkoa
wa Kigoma pekee unaweza kuzalisha mafuta ya kula ya kutosha ya kulisha nchi
nzima kutokana na kilimo cha mawese. Kwa hiyo, lazima kuanzisha kilimo kikubwa
cha mawese na viwanda vya kusindika mawese na bidhaa … nyingine za mawese,
ikiwemo sabuni na umeme kutoka katika kanda hii. Kilimo hiki pia kinaweza
kumaliza tatizo la ajira katika kanda ya magharibi….” (Uk. 52-53)

Utaalamu

Kwa kiasi kikubwa utaalamu ambao ni
pembe mojawapo katika dhana ya Udadisi wa Viongozi
Wenye U Tatu
 imejadiliwa kwenye sehemu ya uzoefu na ubunifu hapo juu na
kugusiwa kwenye sehemu zingine. Hapa tunajikita kwenye kuhoji baadhi ya majibu ya
January yanayogusa taaluma/utalaamu mbalimbali. Msingi hasa wa hoja hapa siyo
kuonyesha alichosema ni ukweli au uwongo bali kudadisi kama kina ‘mashiko’ kitaaluma.

Tuanze na sekta ya Wizara yake, yaani
mawasiliano. January anatujulisha kuwa “Ndio sekta inayoongoza kwa kukua kwa
kasi na kwa muda mrefu – kwa kiwango cha wastani wa asilimia 20 katika kipindi
cha miaka saba. Hakuna sekta yoyote ya uchumi iliyokuwa kwa kasi hiyo na kwa
kipindi kirefu kama hicho” (Uk. 33 ). Sasa sijui hii ni taarifa ya kisiasa tu au vipi maana
hatuambiwi mchango wake hasa kwenye uchumi ni kiasi gani ukilinganisha na hizo
sekta zingine anazodai (bila kusema moja kwa moja hapo) kuwa hazikui/hazijakua
kwa kiasi/kasi hiyo katika kipindi hicho.

Shida inaanzia pale unaposoma maneno
haya ya Mchumi Aidan Eyakuze kwenye jalada la kitabu cha January: “Ni jambo la
nadra sana kwa wanasiasa wa Tanzania kutoa ufafanuzi wa kina wa mipango na
maono yao ya kiuchumi kwa uwazi na kwa kujiamini. Katika kitabu hichi, January
Makamba amefanikiwa kufanya yote haya, tena kwa ujasiri mkubwa”. Maadam ‘mchumi mahiri’ kanena na wewe ni ‘mchumi kanjanja’ basi unaenda walau kutafuta machapisho ya
mchumi huyo uone anasema nini kuhusu sekta zetu za uchumi zilizopo katika muktadha wa ‘uliberali mamboleo’.

Huko kwenye kabrasha la ‘The State of East Africa 2013’ (yaani ‘Hali ya Afrika Mashariki Mwaka 2013’)
ambalo mmoja wa watunzi wake wakuu ni huyo Aidan Eyakuze unakutana na picha/grafu nzuri yenye kichwa cha habari “Evolving Structure of Tanzania’s Economy (2005-2012)”
yaani ‘Mabadiliko ya Muundo wa Uchumi wa Tanzania’ iliyoambatana na maneno haya: “In 2012 the service industry in Tanzania accounted for 49 per cent of the
economy, a 3 per cent increase from 2005, while agriculture’s share shrank from
28 per cent to 24 per cent during the same period. Industry grew its share of
the economy from 20 per cent to 22 per cent in 2012” (p. 71). Unajiuliza nafasi
ya sekta ya mawasiliano katika muundo huo iko wapi? Au bado kulikuwa hakuna takwimu?

Au pengine ni kwa sababu sekta yenyewe imejifichaficha kwenye sekta nyingine na hivyo (labda) kupelekea January aielezee hivi baadaye humo kitabuni: “Zipo sekta kadhaa – ambazo zenyewe
ni shughuli za uchumi lakini pia ni viwezeshi, yaani
huduma, kwa shughuli nyingine za uchumi. Sekta hizo ni uchukuzi, kwa maana ya bandari, reli, barabara na usafiri wa anga; huduma za fedha, kwa maana ya
upatikanaji rahisi na kwa unafuu wa mikopo ya biashara; nishati, kwa maana ya
upatikanaji wa umeme wa uhakika na gesi viwandani kwa bei nzuri; mawasiliano,
kwa maana ya huduma bora za simu na miundombinu ya TEHAMA; na huduma za
utawala, kwa maana uwezo na weledi wa serikali kuwezesha biashara kuanzishwa na
kuendeshwa bila vikwazo vya rushwa na urasimu, pamoja na usimamizi bora wa
uchumi au sound economic management, ikiwemo sera wezeshi na rafiki kwa
biashara na uwekezaji. Sekta hizi zinazohudumia uchumi ni muhimu sana ziwe bora
na imara” (Uk. 81)?

Unatoka hapo unaenda kutafuta
makabrasha ya mchumi mwingine mahiri, Profesa Benno Ndulu ambaye ni Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BOT), huko unakutana na taarifa hizi kutoka kwenye kabrasha ‘aliloliandika’ na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, na kuliwasilisha kwa
Mkurugenzi wa IMF, Christine Lagarde tarehe 18 Desemba 2014: “The structure of
the economy is broadly unchanged with agriculture being the largest sector (23.8
percent) followed by trade (10.1 percent), construction (9.6 percent) and
manufacturing (7.6 percent)” (Uk. 11). Unajiuliza kama sekta ya mawasiliano
imekuwa kwa kasi kubwa kiasi kile kwa miaka 7 inakuwaje wachumi wanatuambia
bado sekta kubwa nchini ni kilimo, ikifuatiwa na biashara, ujenzi na uzalishaji
viwandani?

Ama hiyo sekta ya biashara iko juu
kwa sababu ya sekta ya mawasiliano ndiyo maana January anatuambia “Kwamba sasa
hivi karibu kila mtu ana simu ya mkononi na anaweza kumudu kuitumia sio jambo lililotokea
lenyewe tu kwa ajali – ni matokeo ya uamuzi wa Serikali, ni matokeo ya Sera za
Serikali, ni matokeo ya Sheria na Kanuni tulizoziandika Serikalini. Maisha ya
Watanzania yamebadilika kwa kiwango kikubwa sana kutokana na sera muafaka
tulizoweka, zilizowezesha uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya mawasiliano ikiwemo
kwenye mitandao ya simu za mikononi. Huduma ya fedha, kutuma na kupokea fedha,
sasa inapatikana kwa Watanzania karibu wote – hata wale wasio na akaunti za
Benki. Biashara za aina zote zimeshamirishwa kutokana na urahisi wa mawasiliano
– jambo lililowezeshwa na uwekezaji wa Serikali kwenye kujenga mkongo wa
mawasiliano wa taifa” (Uk. 33)?

Pengine kwa kutambua kuna tatizo
katika kuthibitisha ni kwa kiasi gani hasa sekta ya mawasiliano inachangia pato
la taifa, January anatupiga ‘chenga ya mwili’ na ‘kuitupia mpira’ wizara
nyingine kama ifuatavyo japo humo humo kitabuni anadai Serikali ni timu: “Kumekuwepo
na mashaka kwamba Serikali haipati mapato stahiki kutoka kwenye makampuni ya
simu. Suala la usimamizi wa kodi na mapato ni suala la Wizara ya Fedha sio la
Wizara za kisekta. Hata hivyo, mwezi Oktoba 2013, tumefunga mtambo wa kisasa wa
kufuatilia mapato ya makampuni ya simu na sasa mapato ya Serikali yameongezeka
kwa kiwango kikubwa. Pia, kutokana na usimamizi mzuri wa sekta hii, ajira zimeongezeka
sana – kwanza kwenye makampuni yenyewe lakini pia kwa Watanzania wengi hasa
kina mama walioingia kwenye biashara za kuuza vocha na huduma za kuhamisha
fedha. Karibu katika kila kona ya nchi yetu wapo watu wanaofanya biashara hizi
– na hizi ni ajira nyingi sana zinazowasaidia Watanzania wa kawaida” (Uk.
33-34).

Msomaji unazidiwa kuchanganyikiwa –
ama kuchanganywa – pale unapokutana na majibu haya ya January kwa swali mahsusi
la Padre Karugendo kuhusu uchumi wa Tanzania: “Kwanza, shughuli za uchumi
zilizokua kwa kasi katika miaka kumi na tano iliyopita ni zile ambazo
hazijawagusa au haziwahusishi watu wengi – kwa maana ya ajira na kipato. Kwa
mfano, mtaji uliowekezwa kwenye sekta ya madini ni mkubwa na mtaji huo
umejumlishwa kwenye mchango wa Pato la Taifa, hivyo kuleta taswira ya ukuaji wa
kasi wa uchumi, lakini ajira, kodi na manufaa mengine hayakuwa makubwa sana.
Kwa kifupi ni kwamba uchumi wetu umepanuka katika sekta ambazo haziwagusi
wananchi wengi moja kwa moja. Shughuli ambazo zinawagusa au zinawahusisha watu
wengi ni kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi – shughuli ambazo zaidi ya asilimia
70 ya Watanzania wanajihusisha nazo. Lakini ukitazama kasi ya ukuaji [wa] shughuli
hizi, bado sio ya kuridhisha” (Uk. 79-80).

Unabaki unajiuliza hivyo hizo sekta
zilizotajwa hapo juu na wachumi kuwa ndiyo sekta kubwa katika muundo wa uchumi
– hasa hizo ya biashara na ujenzi – au hiyo ya huduma inayosemekana kukua kwa
kasi, je haziwahusishi/haziwagusi watu wengi? Kwa nini? Na inakuwaje hata hiyo
ambayo ‘imefagiliwa’ sana na January – yaani mawasiliano – kuwa imekuwa kwa
kasi kubwa na kugusa watu karibia wote Tanzania haina jipya hapo?

Unabaki kujiuliza January aliona nini hasa kuhusu hayo yote wakati anafanya hivi: “Majuzi
nilikuwa natazama
kitabu cha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa na nikaona takwimu kwamba
mwaka 2013, tumeuza nje huduma na bidhaa za thamani ya dola bilioni 6 na tumeagiza kutoka nje bidhaa na huduma za thamani ya dola bilioni 11” (Uk. 83).

Chambuzi za kitaalamu za January pia
zinaibuka na hili ambalo pia tungeweza kulijadili kwenye sehemu ya upya na ya
ubunifu: “Ukiwa unamiliki mashirika haya haupaswi kushindwa kununua vitabu vya
watoto mashuleni, haupaswi kukosa madawa kwenye zahanati na hospitali. Lakini
ili tufanikiwe lazima tubadili mfumo wa umiliki na usimamizi wa mali za Serikali.
Kwa sasa mwenye mali ni Msajili wa Hazina lakini anayesimamia uendeshaji wa
mashirika ni Wizara za Kisekta. Huu ni mkanganyiko wa kwanza. Shirika moja lina
mabwana wawili. Suala hili aliwahi kulizungumzia kwa ufasaha zaidi rafiki yangu
Ndugu Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya
Umma. Ni vyema basi tukaanzisha Kampuni kubwa tanzu, kwa Kiingereza wanaita a
Holding Company, itakayomiliki na kusimamia uendeshaji wa Mashirika ya kibiashara ya
Serikali kwa weledi, maarifa ya kisasa na kanuni ya kibiashara bila kuingiliwa
na siasa. Singapore wamefanya hivyo na wamefanikiwa sana. Msajili wa Hazina ameelemewa
na majukumu mengi, ikiwemo kushiriki kwenye bodi za mashirika zaidi ya 100. Pia
baadhi ya Wizara za kisekta zimeishia kuwa waendeshaji na wasemaji wa mashirika
yaliyo chini ya Wizara hizo badala ya kutoa uongozi wa ujumla wa kisera na
kimkakati wa maendeleo ya sekta husika” (Uk. 183).

Mdadisi wa historia ya Ujamaa na
Ubepari nchini unajikuta unajiuliza hiyo kampuni kubwa tanzu ina/itakuwa na
tofauti gani hasa na Shirika la Maendeleo la Taifa ambalo Idrian Resnick
alilielezea hivi katika kitabu chake cha mwaka 1981 kijulikanacho kama The Long Transition: Building Socialism inTanzania: “A new parastatal organization (state-owned corporation), the
National Development Corporation (NDC) was created in 1964 to manage
government’s holdings in manufacturing and primary product companies…[it] grew
enormously during its first five years, becoming the channel through which
imperialism made substantial gains…. By 1966, the NDC wholly owned or held
shares in thirty-seven companies” (Uk. 52). Kwa tafsiri rahisi ya kimuhtasari, shirika hilo lilianzishwa umnamo mwaka 1964 kama kampuni kuu ya kumiliki
makampuni mengine na lilikua kwa kasi sana na kuwa sehemu ya kuuwezesha ubeberu kupenya
nchini ambapo kufikia mwaka 1966 likawa na hisa au umiliki kamili wa makampuni
37.

Kivumishi mtambuka ndani ya kitabu
cha January kinaonekana kwa mara nyingine tena pale anapotuambia hivi: “Kwanza
kabisa, ni muhimu kubadilisha mtazamo na kuondokana na dhana ya ajira au dhana
ya kuajiriwa. Tuchukue dhana mpya ya kipato. Kimsingi watu hawatafuti ajira
bali wanatafuta kipato cha kujiendeleza kimaisha. Kuajiriwa ni moja tu ya njia
ya kutafuta kipato. Tukiwa na dhana ya kipato itaweza kutusaidia kupanua wigo
wa mawazo na fikra kuhusu mambo tunayoweza kuyafanya” (Uk. 38-39). Lakini
mipango yake mikubwa – kama wa “Muswada na Mpango Mahsusi” wa kutenga shilingi
trilioni 3.6 kwa miaka 3 ili kuwezesha vijana – umejikita katika kuongeza ajira. Hapa tunapata
utata kuhusu upya wa dhana yake maana kwa kawaida dhana ya ‘kipato’ (income) na ‘ajira’ (employment) zimefungamana hasa mtu anapoitazama ajira katika upana
wake, yaani, ajira za kuajiriwa na za kujiajiri, ambapo kwa mtazamo huu ajira
inaweza kutafsiriwa pia kwa Kiingereza kama ‘income generating activities’, yaani ‘shughuli za kujipatia kipato’. Tungependa kuulewa huu utalaamu unaodai
unatuletea dhana mpya itakayotupanulia mawazo (mapya).

Pia tafiti mbali mbali za biashara
barani Afrika na kwingineko zinaonesha kuwa siyo kila mfanyabiashara wa kati
(au hata mdogo) anataka kuwa mfanyabiashara mkubwa hasa ukizingatia kuwa kuna
wafanyabiashara ambao lengo lao ndilo hilo la ‘kati’ au ‘udogo’ ili mradi lina
tija kwa familia zao na kwa taifa. Lakini January anatuambia kuwa “Rais ajaye lazima
awe karibu na aongoze jitihada za dhati za kuwasaidia wafanyabiashara wa kati,
wengi wao waliopo huko mikoani, wengi wao wakiwa wasafirishaji, wanunua mazao,
wenye viwanda vidogo vidogo, ili nao wawe wafanyabiashara wakubwa” (Uk. 10).
Hivyo, tungependa kujua pia utaalamu huu wa biashara unaopelekea kuwa na
hitimisho hili msingi wake ni nini hasa isije ikawa ndiyo itikadi/sera zile
zile za kuua biashara ndogo ndogo ili kufungua njia kwa biashara kubwa kubwa
tu. Hili ni muhimu maana January mwenye anakiri kwamba “Kote duniani, biashara
za kampuni ndogo na za kati ndio injini ya uchumi wa nchi” (Uk. 43).

Suala hili tutalijadili zaidi kwenye
sehemu ya ‘uitikadi’. Lakini ni dhahiri kuwa kwa kiasi kikubwa utaalamu huu wa
January unapata ushawishi mkubwa kutoka kwenye taasisi kubwa za kifedha duniani
kama haya maneno yake kitabuni yanavyoonesha: “Kwa mujibu wa takwimu za Benki
ya Dunia, asilimia 20 tu ya biashara na kampuni ndogo zikiongeza mfanyakazi mmoja kwa
mwaka, ajira 400,000 zitazalishwa. Je asilimia 80 za biashara hizi zikiongeza
watu watatu kwa mwaka?” (Uk. 43); “Asilimia zaidi ya 80 ya biashara za jijini
ni biashara ndogondogo zinazoajiri watu wasiozidi wawili. Kwa mujibu wa takwimu
za Benki ya Dunia, asilimia 20 tu ya biashara hizi zikiongeza mfanyakazi mmoja tu,
ajira zitakazopatikana ni 400,000 kwa mwaka. Kwa hiyo kuna haja kwa Serikali
kuhakikisha kwamba biashara ndogo katika miji yetu zinapanuka na kuwa biashara
kubwa na za kati na kuongeza watu wanaojishughulisha na biashara” (Uk. 120).

Kabla ya kumaliza kuudadisi utaalamu wake uchumi, mdadisi unayasoma kwa kina maneno haya ya nguli wa ‘sayansi ya siasa’ kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam/Mkwawa, Profesa Bernadeta Killlian, yaliyopo kwenye jalada la kitabu cha January kujaribu kubaini nini hasa kilimgusa humo: “Je, uchumi wa Tanzania unaweza kuwafanya Watanzania waondokane na umaskini? January Makamba ameainisha mawazo yake makubwa na mapya ya kiuchumi pamoja na mipango yake madhubuti ya maendeleo katika kitabu hiki ambacho kimejaa matumaini juu ya uwezekano wa Tanzania Mpya”.

Maneno ya Profesa yanakufanya ujiulize wataalamu wetu kutoka kwenye vyuo vikuu vyetu wana nafasi gani, kitaalamu na kiitikadi, katika safari (fupi na ya haraka) ya January ya kuuelewa uchumi. Unarudi kitabuni na kukutana na shuhuda hizi: “Kwa mfano, kutokana na kazi ile [ya Msaidizi  wa Rais], nililazimika kwa haraka sana kujifunza kuhusu masuala ya
uchumi kwa kusoma na kuongea na manguli wa uchumi, ili kuweza kumsaidia Rais
kuwasiliana na wadau mbali mbali kuhusu malengo yake kwa uchumi wa nchi. Kwa
hiyo uelewa wangu kwenye masuala ya uchumi na maendeleo kwa ujumla umepanuka
kutokana na mazingira ya kazi ile. Na huo ni mfano wa uchumi tu, nimejifunza
mambo mengi ya kisera na kimkakati kwenye sekta mbali mbali kama kilimo, afya, miundombinu, na mambo ya ulinzi na usalama” (Uk. 66).“Kwa upande wa wahadhiri na wakufunzi
wa vyuo vikuu, nako nina marafiki wengi ambao pamoja na kujadiliana nao kuhusu mustakabali wa taifa letu, tumekuwa pia tunazungumzia changamoto
zinazowakabili katika kazi zao….” (Uk. 102)

Uitikadi

January anatuambia hivi: “Katika
kipindi chote ambacho nimekuwa kiongozi, nimekuwa naamini kwamba elimu haina
itikadi, inagusa maslahi ya kaya moja moja na maslahi ya taifa” (Uk. 6). Kisha
anasema: “Katika awamu zijazo, elimu itakuwa ndio siasa” (Uk. 7).

Lakini hakuna siasa ambayo haina
itikadi. Itikadi yako ikiwa ni ya mrengo wa kushoto, kulia au wa katikati basi
elimu unayotoa kwa kiasi kikubwa itafuata mrengo husika. Ni dhahiri kuwa
itikadi ya January ni mchanyato – kama siyo mkanganyiko – wa pande mbali mbali.
Pengine huo ndiyo wajihi wa viongozi wengi
wa kizazi kipya na zama mpya ambazo Mzee Mwinyi amesema dibajini nazo zina
“mitume wake” (Uk. viiii).

Huyu January anayetuambia “Serikali inao wajibu wa kuona fahari ya kutengeneza
mabilionea wa Wakitanzania ambao watawekeza fedha zao hapa, watatengeneza
ajira, kulipa kodi, kuendeleza nchi yao” (Uk. 87)” ndiye huyo huyo anasema
hivi: “Mimi ni muumini wa falsafa za Mwalimu Nyerere na kama kiongozi kijana najitahidi
niwezavyo niige mfano wake, mfano wa maisha yake, mfano wa msimamo wake, mfano
wa uadilifu na uchapakazi wake” (Uk. 186).

Pia ndiye January anayesema hivi bila
kutuelezea huo urasimishaji unatofautianaje na tulioletewa na Hernando de Sotokupitia MKURABITA ili eti tuhuishe mitaji yetu mingi japo ni mfu na kutuwezesha na sisi tuwe na Ubepari wenye tija kwa
wamiliki wa rasilimali na biashara: “Juhudi za kurasimisha sekta isiyo rasmi lazima
zifanyike kwa kasi mpya na maarifa mapya” (Uk. 10).

Ukigeuka kidogo tena unamkuta January
anayesema tuendelee tu na haya ambayo kwa kiasi kikubwa ni ya Kinyerere: “Vilevile, kuendelea na harakati za
kuwezesha kuwepo mfumo wa uchumi na biashara duniani wa haki na usiokandamiza
nchi changa; kuendelea na harakati za kujenga msingi wa nchi maskini
kushirikiana zaidi ikiwemo kufanya biashara zaidi baina yetu; lazima tuendelee
na harakati za kurekebisha taasisi za utawala wa siasa za kimataifa zizingatie
matakwa na maslahi ya mataifa mengi zaidi; lazima kuendelea kupambana na
ukoloni-mamboleo ambao kila kukicha unachukua sura mpya ikiwemo kuhusisha
misaada kwa nchi yetu na maslahi ya kibiashara ya mashirika ya nchi zinatoa
misaada hiyo, kupewa masharti ya kupata misaada isiyo na msingi, na mashinikizo
ya kufuata sera na kuchukua misimamo isiyo na manufaa kwa nchi yetu” (Uk. 92).

Tena anasisitiza kwamba “Rais ajaye
lazima athamini mchango [wa misaada kwa “mataifa tajiri na makubwa duniani”] lakini pia ajue kwamba nchi wahisani sio wajomba
zetu na lazima aongoze mkakati madhubuti wa taifa letu kujitegemea kibajeti na
kubadili mahusiano yetu na nchi kubwa kutoka kwenye ufadhili kwenda kwenye ushirika
wa kibiashara na uwekezaji” (Uk. 11).

Ila malengo yake ya Urais/Uongozi wa kizazi kipya yanalenga kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo “Bila
kufuta mipango mizuri iliyopo sasa….” (Uk. 74) na moja ya mipango hiyo
anaielezea hivi:  “Jitihada nyingi
zimefanyika tangu uhuru katika kilimo, lakini kutokana na ukubwa wa sekta hii,
matokeo bado ni finyu. Serikali ya Rais Kikwete imeweka kipaumbele kwenye
kilimo kupitia sera kubwa kuliko zote toka uhuru wa nchi yetu ya Kilimo Kwanza
inayojumuisha miradi mikubwa kama vile mradi wa kisasa kabisa SAGCOT. Sera hii
ya Kilimo Kwanza imeundwa kutatua matatizo yote katika sekta za kilimo, ufugaji
na uvuvi na kuongeza tija ya shughuli za kilimo kwa wakulima na uchumi wa taifa
letu kwa ujumla” (Uk. 74).

SAGCOT hiyo hiyo ambayo wanaharakati wa HakiArdhi na wengineo tunaidadisi kuhusu ‘uporaji wa ardhi’ (land grab) kubwa sana ya wananchi na
kuwapa wawekezaji/wabia wakubwa hawa kutoka nje wakiwamo ambao wanatiliwa mashaka katika nchi mbali mbali: “Diageo,DuPont, General Mills, Monsanto, SAB, Syngenta, Norfund, Unilever, USAID, YaraInternational, the Irish Embassy, AGRA and FAO”. Lakini January yeye ana jibu la haraka tayari – eti anasema: “Ardhi ambayo haijapimwa ndio chanzo kikubwa cha migogoro. Tumejaribu kupima
maeneo mengi nchini lakini kasi ni ndogo na bajeti haitoshelezi. Napendekeza
matumizi ya teknolojia ya satellite katika kupima na kupanga matumizi ya ardhi
nchini. Kila kipande cha ardhi katika nchi yetu kiwe kimepimwa, kina hati na
matumizi yake yanajulikana” (Uk. 75).

Ndiyo maana siyo jambo la kushangaza
kuona kuwa miongoni mwa wajumbe wa bodi ya Kampuni/Shirika la Maendeleo la
Bumbuli aliowataja
mtandaoni
na kuelezea nyadhifa zao mbalimbali katika taasisi kadhaa yupo Profesa Andrew Temu ambaye pia ametambulishwa
kama mjumbe wa bodi ya SAGCOT. Yupo Betram Eyakuze ambaye ametambulishwa
kama mmoja wa wamiliki wa Serengeti Advisers Limited ambaye pia anashiriki
katika mradi mkubwa wa kilimo cha kibiashara. Tunamwona pia Dakta Paul
Armington ambaye tunaambiwa amewahi kuwa mchumi wa IMF na Benki ya Dunia.
Kinara  wa – au kichwa cha – sera za
uchumi wa soko na mtetezi mkuu mmojawapo wa sekta binafsi nchini Tanzania,
Balozi Juma V. Mwapachu naye yupo ‘bodini’. Hali kadhalika Edward V.K.
Jaycox ambaye tunajulishwa kuwa aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia
katika ukanda wa Afrika 
‘ya Kusini mwa Jangwa la Sahara’. Wanabodi wengine
waliotajwa ni Dakta Najim Msenga, Askofu Dakta Stephen Munga, Bi. Grace C.
Rubambey na January Makamba mwenyewe. Ukiiweka kwenye mizani ya itikadi ya
Nyerere, bodi hii inaangukia kulia badala ya katikati achilia mbali kushoto.

                                                       

Utu

Wahenga wetu walinena kuwa “mnyonge
mnyongeni lakini haki yake mpeni”. Na sisi wachambuzi/wadadisi tunahojiwa pale
tunapojikita tu kwenye kuibua mabaya na kufukia mazuri. Hivyo, maadam simjui
January kwa undani kama mtu binafsi, ni dhahiri kuwa kwenye kitabu chake
ameelezea vitu ambavyo vinakidhi kigezo kikuu kimojawapo cha dhana ya Udadisi
wa Viongozi
Wenye U Tatu
. Kiukweli sijui kama hayo anayosema (w)aliyafanya ni kwa
ajili ya maslahi ya kisiasa au la lakini kimaandishi – yaani kwenye karatasi – walau yanaonesha utu. Jukumu la kupima utu, kama dhana ya U Tatu inavyoeleza, ni la
wananchi wanaomjua fika ambao hasa hasa ni wale walioko jimboni na mtaani
kwake.

Nukuu mmojawapo yenye mguso wa utu ni
hii: “Kwa kuzingatia mazingira magumu ya hali ya hewa ya baridi kali, Shirika hili
limeanzisha programu ya kugawa viatu vya shule kwa wanafunzi wote wa Shule za
Msingi katika Jimbo la Bumbuli kila mwaka. Tumeanza mwaka huu kwa kugawa pea
45,000 na tutaendelea kufanya hivyo kila mwaka. Pia tumeanzisha programu za
kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha nne kufanya vyema katika mitihani yao ya
taifa” (Uk. 32).

Tuhitimishe hili la utu kwa
kusisitiza kuwa watu wanaowasiliana na January mara kwa mara na kwa undani ndiyo wenye nafasi
kubwa zaidi ya kuthibitisha utu wake kuliko siye wengine tunaomjua kupitia vitabu,
magazeti na mtandao. Hao – wakiwamo anaojadiliana/anaobishana nao kwenye
mitandao ya twitter n.k. – ndiyo wanaweza, mathalan, kuthibitisha hili alilolisema
kitabuni kuhusu mahusiano yake na watu ambao ndiyo msingi hasa wa utu: “Kama ni
kukomaa kwa maana ya busara, hekima na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, jibu
pia ni ndio, nimekomaa. Sina rekodi ya kuropoka, kutukana, kuhamaki,
kushambuliana na watu na kufanya maamuzi ya papara. Najua uzito wa dhamana ya
uongozi” (Uk. 29 ).

Ujasiri

Kwenye jalada la kitabu husika, Mzee
Yusuf Rajab Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu, anamuelezea hivi mwanaye: “Nimemfahamu January katika kipindi chote cha uhai wake kama mtu mwenye msimamo
na pia kama kijana mwenye hekima na busara inayozidi umri wake. Lakini sikuwa nafahamu kwamba ana uelewa na ufahamu wa mambo mengi na kwa kina hadi
niliposoma kitabu hiki”.  Naye January
anamuelezea hivi babaye: “Lakini pia kuna mambo mengi mazuri ambayo nimejifunza
kutoka kwake ikiwemo haja ya kuwa na msimamo usioyumba katika unayoyaamini na
haja ya kutokumuogopa mtu yoyote” (Uk. 18).

Hivyo, siyo jambo la kushangaza kuona
January anatuelezea visa viwili vinavyojaribu kutudhihirishia kuwa ana ujasiri
na kutuambia kuwa kuna vingine vingi tu. Kisa cha kwanza ni hiki kuhusu kubaini
“wizi mkubwa wa chakula cha wakimbizi”: “Sasa siku moja, tukiwa katikati ya
kugawa, kambi nzima ikiwa imesimama kwenye foleni nikabaini kitendo cha wizi.
Nilikasirika sana. Nikalazimika kufanya uamuzi wa aidha kuendelea tu kugawa
chakula ili tumalize huku nikijua kuna watu wanaiba au kusimamisha zoezi ambako
kuna gharama na usumbufu mkubwa. Nilichofanya nilienda kituo cha polisi
kambini, nikatoa shitaka la wizi na nikaomba askari waje kwenye eneo na wakaja
na gari lao pale kwenye uwanja wa kugawa chakula. Nikawatangazia wakimbizi
kwamba tunasimamisha zoezi kwa muda kwa jambo lenye manufaa kwao na kwamba
watulie. Nikawaambia askari kwamba naomba wafanyakazi wangu wote wakamatwe na
kupelekwa ndani kwa tuhuma za wizi. Walijua ni mzaha. Na nikawaambia kwamba
wana nusu saa wataje wezi miongoni mwao la sivyo kila mmoja anafukuzwa kazi
papo hapo. Wakati huo huo nilikuwa natafuta vibarua wengine wa muda wa
kuendelea kugawa. Chini ya nusu saa wakatajana. Waliohusika wakabaki polisi.
Wasiohusika wakaja kuendelea kugawa chakula. Tangu siku hiyo tukakomesha wizi
wa chakula cha wakimbizi. Hiyo ilikuwa mwaka 1997 na nilikuwa na miaka 23 tu. Nilijifunza
tangu zamani, tangu nikiwa kiongozi mdogo, kwamba, kuna baadhi ya mambo ya
msingi, kama wizi au dhuluma, ambayo hakupaswi kuwa na suluhu. Wengine wanaweza kusema huu ni uamuzi mgumu
lakini mimi naamini ni katika kutekeleza wajibu (Uk.114).

Kisa cha pili ni kuzuia uchakachuaji
wa mafuta uliowahi kushamiri nchini na January anatuambia kwamba: “Matokeo yake, na
kama ukiwa unasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze ukihesabu idadi ya
vituo vya mafuta aidha vilivyofungwa au vilivyoishia katikati kwenye ujenzi,
utaona ni vingi mno kwa sababu vilikufa kutokana na shughuli ya uchakachuaji
kukoma. Tulipendekeza na kusimamia uamuzi ambao haukuwa maarufu wakati ule
lakini majuzi nimesikia watu ambao hawakuunga mkono suala hili wanapongezana
kwa kumaliza tatizo la uchakachuaji” (Uk. 114).

Pia tunaonyeshwa picha yenye maneno
haya: “January Makamba akiongoza mkutano aliouitisha kwa ajili ya kutafuta
utatuzi wa matatizo katika Kampuni ya Simu ya TTCL. Mkutano huo ulipelekea
kusimamishwa kazi kwa baadhi ya maofisa wakuu wa kampuni hiyo. Mafanikio ya
mageuzi katika TTCL yameanza kuonekana” (Uk. 171).

Lakini kuna haya maneno yake humo
kitabuni yanayotufanya tuutilie mashaka ujasiri wake: “Kuna tatizo kubwa la
usimamizi wa miradi ya Serikali. Hapa tunapoteza fedha nyingi sana kwa wajanja
wachache. Kwa mfano, daraja ambalo linapaswa kujengwa kwa shilingi milioni 100,
linatengenezewa BOQ, yaani mahitaji, ya shilingi milioni 300 na hatimaye
linajengwa kwa shilingi milioni 30 na linavunjika baada ya miaka miwili na
zinatafutwa fedha nyingine za ujenzi. Au kwenye mradi wa maji, panapostahili
bomba la inchi 6 linawekwa bomba la inchi 2 na baada ya muda linapasuka na maji
hayatoki tena. Haya nimeyashuhudia kama Mbunge ambapo niliwahimiza watu wa
Bumbuli kukataa kupokea mradi uliojengwa chini ya kiwango. Cha ajabu kulikuwa
na presha kubwa sana kutoka kila pahala kwamba tuupokee. Cha ajabu zaidi
hakukuwa na adhabu yoyote kwa waliohusika. Cha ajabu zaidi mkandarasi huyo huyo
akaendelea kupewa kazi nyingine zaidi za ujenzi. Haya yanatokea kila siku, kila
mahali kwenye maeneo yetu” (Uk. 182).

Kabla sijakisoma kitabu cha majibu ya
January Mtandao wa Wazi wa Wanazuoni ulifanya mjadala mkali mtandaoni wenye
kichwa cha habari Kisa
Cha Vitabu Viwili Vya Urais?
 ambacho ulichochewa na picha za kulinganisha
kitabu cha Jakaya Mrisho Kikwete: Tumaini Lililorejea kilichoandikwa mwaka 2006 na Prince Bagenda na
hiki kinachohusu mazungumzo ya January na Padre Karugendo. Niliwauliza
wanazuoni haya: Kwenye mjadala wa Escrow tumeona IPTL ilianza lini na hatua
gani zilichukuliwa, umeona ‘uzoefu’ gani? (Kumbuka Rais Mtarajiwa aliwahi kuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, je, alizuia ufisadi sekta-ni (rejea
hii Taarifa
ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Gesi(Ripoti ya Pan African Energy)
 au
baada ya kuwa Naibu Waziri wa Wizara nyingine hakuweza kuendelea na harakati
zilizotajwa humo ripoti-ni? Au aliendelea tu ila nyuma ya pazia?)

Baada ya kupata majibu kadhaa kutoka
kwa Wanazuoni nikauliza maswali haya ya nyongeza:  “Na ndiyo maana kabla mgombea hajaulizwa ‘utafanya nini?’ inabidi aulizwe ‘ulifanya/umefanya nini?’ Kwenye ule ‘uzoefu’ dhidi ya ufisadi maswali yanakuwa ni marahisi tu, natumai Prof. Kitila Mkumbo
et al. watawauliza maswali kama haya kwenye hiyo midahalo ya ITV na UDASA:
Ulifanya/Ulisema nini EPA ilipotokea? Ulifanya/Ulisema nini RICHMOND
ilipotokea? Ulifanya/Ulisema nini ESCROW ilipotokea? Utaishughulikiaje ESCROW
ukiingia IKULU?

Hivyo, nilipata shauku kubwa
nilipoona swali nambari 21 la Padre Karugendo kwa January likiuliza hivi: “Wananchi
wanalalamikia sana ufisadi. Mikakati ya sasa inaelekea haijafanikiwa kiasi cha
kuridhisha wananchi. Je, wewe una mbinu zozote mpya za kupambana na tatizo
hili? Je, unaongeleaje ufisadi wa Richmond, EPA na IPTL” (Uk. 108).

Lakini majibu ya moja kwa moja ya
January kwa swali hilo hayakuonyesha uzoefu na mchango wake katika masakata
hayo. Tunachokiona ni maneno kama haya yafuatayo ya kikaulimbiu yanayovut(i)a
hisia: “Rushwa ni kansa mbaya sana ambayo inaweza kuitafuna jamii. Moja ya dhambi
kubwa unayoweza kufanya kama kiongozi ni kutumia dhamana uliyopewa na wananchi
kujinufaisha mwenyewe na ndugu, jamaa na marafiki zako. Ni zaidi ya ujambazi” (Uk. 108);
“Tatizo limekuwa kubwa sasa na watu wanakula mali ya umma waziwazi, bila woga –
wanavimbiwa na kujitapikia kwenye viatu vyao. Na wadogo wanawaiga wakubwa” (Uk.
108).

Pia yapo majibu kama haya ambayo
hayaonyeshi uchukuaji wowote wa hatua za kijasiri: “Umeuliza pia kuhusu masuala ya
Richmond, EPA na IPTL. Hizi skendo zimetudhihirishia kwamba bado tunayo safari
ndefu na kazi kubwa ya kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. Zimetuonesha
kwamba miongoni mwetu wapo ambao kwa tamaa binafsi wapo tayari kuhujumu uchumi
wa taifa letu. Lakini vilevile zimetufundisha kuhusu haja ya kuimarisha mifumo
ya uwajibikaji kwa watendaji na viongozi wa umma. Inashangaza kwamba kiongozi
amebainika kuhusika na ubadhirifu lakini bado anasubiri msukumo wa bunge au
jamii kuwajibika. Lazima tujenge utamaduni wa uwajibikaji lakini vilevile kwa
viongozi waliobainika kutumia madaraka vibaya au kujihushisha na ubadhirifu, kujiuzulu
au kuondolewa kwenye nafasi zao hakutoshi. Lazima jamii ishuhudie wakipewa
adhabu kali ili kuzuia matukio ya namna hii kujirudia. Ushauri wangu ni kwamba
maswala ya uwajibikaji yasichanganywe na siasa. Kwamba pale kunapotokea wizi na
ubadhirifu, wahusika ni watu binafsi, sio vyama na kwamba wabunge na viongozi
wa vyama vyote wanapaswa kuungana kulaani na kuchukua hatua bila kuingiza siasa
za vyama. Skendo za EPA, IPTL na Richmond zimeandikwa sana kwenye magazeti
lakini kila siku kuna wizi mkubwa zaidi unaoendelea katika utekelezaji wa
miradi ya maendeleo ambao hausikiki” (Uk. 110).

Lakini alishatumbukusha kuwa “Kulizungumzia
na kulipigia kelele suala la rushwa pekee hakutoshi” na kutuambia “Ziko namna
mbili za kukabiliana na hili tatizo” (Uk. 110). Lakini January hatuambii uzoefu
wake katika kutumia hizo njia mbili kuukabili ufisadi wa RICHMOND, EPA na IPTL.
Hilo linatufanya tuhoji ujasiri wa kukabiliana na ufisadi. Pia hatuambii moja
kwa moja atafanya nini kukabiliana na ESCROW (kama) akiwa Rais.

Ila ndiye aliyetoa msisitizo huu: “Katika
kutafakari, nimebaini kwamba Rais ajaye ana mtihani mkubwa wa kurejesha imani haswa ya wananchi wengi masikini kuwa anaguswa na hali yao, na kuwa anachukua
jitihada za kuwakwamua kutoka katika hali yao. Hayo yatadhihirika si tu kwa
maneno bali hatua atakazochukua dhidi ya viongozi wabadhirifu, wala rushwa na
matumizi ya serikali yake. Hapaswi kuhisiwa wala kutuhumiwa kwamba yeye ni
miongoni mwa hao” (Uk. 5).

Uchaguzi

Tanzania ina changamoto kubwa. Wale
maadui wakuu watatu wa awali – maradhi, ujinga na umaskini – bado wapo na
Mwalimu Nyerere alituambia ameongezeka wa nne, yaani, rushwa. Lakini adui
rushwa sasa amekubuhu na kuwa ufisadi, yaani, ‘rushwa (m)kubwa’.

Hivyo, nakubaliana na maneno haya ya
January: “Katika tafakuri yangu nimejiridhisha kwamba lazima Rais wa Awamu ya
Tano awe ni mtu mwenye kuzitambua changamoto hizo na kuwa na mkakati wa kuzitatua.
Changamoto hizi ni za kiuongozi na utatuzi wake utategemea tu kiongozi
mwenyewe, hulka yake, mtazamo wake na usahihi wa maamuzi yake. Na yote hii
inategemea wajihi, yaani character, wa kiongozi mwenyewe. Hivyo, wajihi wa
mgombea unapaswa kujibu maswali yanayoletwa na changamoto hizi” (Uk. 3). Ila kuchagua
ni kuamua. Na kama January anavyosema: “Cha msingi ni kwamba wenye kuamua
kiongozi awe nani ni Watanzania wenyewe – kwa msaada wa Mungu” (Uk. 30).

Mungu na atusaidie tufanye uchaguzi/uamuzi sahihi ili, kama vijana wa ‘kizazi kipya’ wanavyosema, tusije tena ‘tukapigwa changa la macho’ na ‘kuuziwa mbuzi kwenye gunia’.

Nimeamua kumchagua mtu mwenye uthubutu,
ujasiri na uzoefu wa utu, uadilifu na utaalamu.

Wewe je?