Escrow – Vita vya Panzi au Tembo?

Chambi Chachage

Wakati tunasherehekea kuingia mwaka mpya kadhia ya –
ama sakata la – Escrow linazidi tu kuchukua sura mpya. Majibizano na vijembe vya hapa
na pale
vinaendelea huko na kule. Kulikoni?

Baada ya Hotuba
ya Rais Kikwete
, vinara wa kulilipua skandali hilo wameibuka
na hoja nzito
dhidi ya kile alichokisema. Na baada ya gazeti
la Nipashe linalomilikiwa na Bwana Mengi kuwauliza maswali mazito watetezi wa
Waziri Muhongo
, Wizara ya Nishati na Madini imejibu
mapigo
. Mtandaoni nako kumesambazwa barua
inayosemekana ilitoka kwa Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) kwenda kwa
aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dakta Rashid
. Yote haya
yanaonekana kuthibitisha kile
alichokisema Mbunge Lusinde kuwa kuna makundi kadhaa
kwenye vita vya
Escrow.

Lakini wahenga waliosema “vita vya panzi furaha ya
kunguru” ndio hao hao waliosema “wapiganapo tembo ziumiazo nyasi.” Swali la
kujiuliza hapa ni, je, wananchi – yaani umma – ni nyasi au kunguru katika
mpambano wa Escrow? Na, je, wanaojipambanua kama wanaopigana kwa niaba – na
ajili – ya (fedha za) umma ni panzi au nao ni tembo?

Kama mawingu yaashiriavyo mvua, kuviziana ilikuwa ni
dalili ya vita. “Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Kamati” anayoongoza “ya
PAC kuwasilisha Bungeni Taarifa Maalumu kuhusu ukaguzi maalumu wa akaunti ya
Tegeta Escrow,” Mbunge Zitto aliujulisha umma, “kumekuwa na
kampeni za chini chini zinazoendeshwa kwenye korido za Bunge na kwenye mitandao
dhidi” yake “binafsi na baadhi ya wabunge waliosimama kidete dhidi ya wizi wa
fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania akaunti ya Escrow”.

Mwenyekiti wa PAC pia
alitujulisha
kuwa “Waziri mmoja ambaye ni mtuhumiwa wa wizi wa fedha za
Tegeta Escrow” alikuwa “anazunguka kwa wabunge akisema tuhuma hizi kupikwa kama
njia yake ya kuhamisha mjadala kutoka uporaji wa Tshs 200 bilioni kwenda kwenye
masuala binafsi.” Kisha Mwenyekiti huyo akazijibu ““Tuhuma hizi zenye kichwa cha habari “Zitto
na Filikunjombe wanatumiwa na Kenya na Uingereza kuvuruga na kudhoofisha
Uwekezaji nchini mwetu””.  Baadhi ya
tuhuma hizi zilipotolewa Bungeni aliyekuwa
Waziri mmojawapo alioneshwa runingani akigonga meza huku akicheka kwa furaha na kejeli.

Wakati anajibu
bloguni tuhuma namba 6 kuwa
“Uingereza imekuwa inamfadhili Zitto kwa miaka
mingi kwa mambo yake ya kisiasa kwa hiyo sasa hivi Ubalozi wa Uingereza
unamlipa Zitto na Kafulila kuhakikisha kwamba Standard Chartered ya Uingereza
inalipwa deni lake lisilotambulika kisheria nchini mwetu”, Mwenyekiti
wa PAC akasisitiza kuwa
“kuna propaganda ambazo haziangalii hata diplomasia”
na kuhitimisha kuwa “Kurudia kurusha tuhuma kwa Ubalozi wa Uingereza nchini ni
kudhihirisha kwa mara nyingine kiburi cha kuwa na mamlaka…walichonacho wanaotuma
tuhuma hizi.”

Tuhuma hii ina uzito wa pekee kwa kuwa hiyo
barua inayosemekana iliandikwa na Standard Chartered Bank (Hong Kong)
mwaka
2009 ina
maneno haya
: “Regrettably, the courts will not take notice of the fact that
the Bank has appointed a Receiver over the shares (the Shares) held by (both Mechmar
and) VIP in IPTI. The Bank has exercised its rights under Share security given
to it by both Mechmar and VIP and now controls the Shares absolutely, through
its Receiver. The Bank asserts that it has the power to, and it will if so
advised, sell the Shares to a third party and pass good title to them…. The
Bank has proposed to your legal advisers that the Government of Tanzania
immediately consider Nationalisation of IPTL. This would be with the support of
the Bank and with the express objective of implementing the Agreed Plan…. If Nationalisation
were to be agreed upon and implemented…. The whole process could be conducted
through the Tanzanian Parliament. There would be no need to involve the
courts….”

Kwa tafsiri rahisi ya kimuhtasari, benki hiyo inaonekana
haikupendezwa na maamuzi/mitizamo ya mahakama za Tanzania na katika
kipande hicho kilichonukuliwa hapo juu
inaziona mahakama zilikuwa hazizingatii
kuwa benki ilimteua mkusanyaji wa hisa za Mechmar na VIP katika IPTL. Tukumbuke
kuwa, kwa
mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu
akaunti ya Escrow
, benki hii ilinunua madeni ya IPTL, jambo ambalo pia
limegusiwa katika barua hiyo. Pia tukumbuke kuwa Mechmar na IPTL ndio walikuwa
wanahisa wa kwanza kabla hisa za Mechmar hazijauzwa kwa Piper Link na kisha PAP
katika mazingira ya kutatanisha yaliyochangia kutolewa kwa fedha kwenye akaunti
ya Escrow kabla ya kutatua utata huo.

Tukumbuke pia, kwa
mujibu wa ukurasa wa 50 wa Taarifa ya CAG
, benki hiyo na huyo mkusanyaji
wake wametajwa katika baadhi ya kesi hizi ambazo hazikuchambuliwa kwa undani
humo: “v. Standard Chartered Bank dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania- ICSID Case No. ARB /10/12, vi. Standard Chartered Bank
(Hong Kong) Limited dhidi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) ICSID
case No ARB/10/20, vii. Martha Kaveni Renju the Administrator Receiver
of IPTL dhidi ya IPTL Shauri Na.124 ya 2003, viii. Martha Kaveni Renju
the Administrator Receiver of IPTL dhidi ya IPTL na VIP Engineering and
Marketing ltd Shauri Na.98 la 2013, ix. Shauri la Mapitio Na.1 la 2012
kati ya Standard Chartered Bank (hong Kong) dhidi ya Mechmar Corporation, VIP
Engineering and Marketing, IPTL, The Liquidator of IPTL, The Bank of Tanzania,
TANESCO na TRA katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Pengine kwa kutambua kuwa hii ni tuhuma nzito
inayohitaji majibu mazito, Mwenyekiti wa PAC alisema maneno yafuatayo
kwa uchungu sana wakati anawasilisha majibu/ majumuisho ya Taarifa ya Kamati yake/yao
tarehe 28 Novemba 2014: “Mheshimiwa Spika, Mheshimwa Waziri wa Nishati na Madini
ukurasa wa ishirini amezungumzia suala la kwamba TANESCO haina mashtaka na
ICSID ila mashtaka ni ya Standard Chartered. Napenda nimkumbushe Mheshimiwa
Waziri kwamba IPTL kabla haijawekwa kwenye muflisi ilifungua kesi kupinga
kitendo cha TANESCO ku-dispute zile invoices. Kesi ilipoendelea kule mahakamani
ICSID baadaye IPTL ikawekwa chini ya muflisi na mahakama zetu za Tanzania baada
ya maombi ya mbia mmoja, Ndugu James Rugemalila. Na wabunge wengi, wengine wameingia
humu mara ya kwanza ndio maana wamediriki hata kunitukana, hawanifahamu. Nataka
niwakumbushe na Waziri wa Mambo ya Ndani ni shahidi yangu. Fedha hizi zilitaka kuanza
kuibwa toka mwaka elfu mbili na nane [2008], elfu mbili na tisa [2009]. Mahakamani
Jaji akaenda akaondoa amri ya kuiweka IPTL kwenye muflisi wakati  tuna kesi ambayo kwa kujenga hoja kwamba hii
kampuni iko kwenye muflisi ile kesi tungeweza kushinda.”

Mwenyekiti wa PAC akaendelea kujibu kama
ifuatavyo
: “Leo kuna baadhi ya wabunge wanahoji kuwa labda tunatumwa na
Uingereza. Huyu Chikawe ni shahidi. Balozi wa Uingereza alikuja na delegation
yake ya watu wa Standard Chartered kuniona kama Mwenyekiti wa POAC ku-lobby
kwamba tuwaachie Standard Chartered wachukue hela za Escrow. Nikatoka nje ya
kikao nikampigia simu Chikawe, wakati huo ni Waziri wa Justice, nikamwambia
Chikawe hawa wanavunja diplomatic protocol, hawawezi kuja kwa Mwenyekiti wa
Kamati hawana kibali cha Wizara ya Mambo ya Nje, wanakuja ku-lobby. Chikawe ni
shahidi yangu akatae hapa, anikane. Hamna kingine kilichonituma kufanya hivyo,
ni uzalendo kwa nchi yangu. Kwa hiyo, siwezi kuwajibu watu ambao kwa njia moja
ama nyingine wameniparuraparura, siwezi kuwajibu; siwezi kuwajibu hata kidogo
kwa sababu hawajui nini nilichokifanya kwa nchi hii. Mheshimiwa Spika, shauri
lile kule ICSD tukashinda kwa kuhoji ya kwamba IPTL iko chini ya muflisi.
Mahakama ikairuhusu Standard Chartered waingie kwa nafasi ya IPTL kwa sababu
wanaidai IPTL. Kwa hiyo ikaingia mahakama. Na hoja pale ilikuwa ni Capacity
Charges, kwamba tumekuwa overcharged. Tumeshitakiwa sisi kwamba kwa nini tuna-dispute
invoices. Kesi imekwenda. Mwezi Februari mwaka huu shauri limeamuliwa kwamba, kwanza,
ni kweli tumekuwa overcharged na, pili, ifanyike recalculation. Mheshimiwa
Spika, maamuzi ya kesi haya hapa na nayawasilisha mezani kwako. Serikali leo
inakuja kukataa maamuzi ambayo sisi tumeshinda na imeamuliwa recalculation,
kwamba bei mpya ya umeme, bei mpya ya Capacity Charges iangaliwe kulingana na
uwekezaji ambao wale watu wameweka. Sasa tunakujaje kukataa kitu ambacho sisi
tumeshinda?”

Kisha Mwenyekiti wa PAC akahitimisha hivi: “Sasa
ngoja niwaambie madhara yake. Mkataba ule baada ya maamuzi ya mwaka 2001,
Capacity Charges zikashushwa mpaka dola milioni mbili nukta sita kila mwezi,
kama tulivyoeleza kwenye Taarifa ya Kamati. Usipofanya recalculation maana yake
ni kwamba mpaka sasa hivi, hivi mwezi huu wa Novemba unakwisha, huyo anayesema
ni mmiliki mpya analipwa Capacity Charges ile ile. Tungefanya recalculation,
hata kama huyo mtoto mpendwa Seth angeachiwa hiyo mitambo, Capacity Charges
ingekuwa chini. Hivi tunafikiria namna gani kama nchi?”

Pamoja na majibu hayo, Rais
ametoa Hotuba
inayoonekana imeegemea zaidi upande wa Utetezi
wa Serikali uliowasilishwa Bungeni na Waziri wa Nishati na Madini tarehe 27
Novemba 2014
. Na pengine Hotuba hiyo ndiyo imeipa Wizara hiyo ujasiri wa
kutoa Tamko
la kuijibu Nipashe
linalojumuisha jibu hili: “Waziri wa Nishati na Madini
ndiye msimamizi mkuu wa masuala yanayohusu sekta za Nishati na Madini nchini.
Mtambo wa IPTL ulijengwa kwa ajili ya kufua umeme unaotumiwa na jamii ya
watanzania. Kuwepo kwa mgogoro kungeweza kuondoa azma ya uwepo wa mtambo huo ya
kufua umeme ili kuliepusha Taifa kuingia katika mgawo wa umeme kutokana na upungufu
wa upatikanaji wa nishati hiyo, hivyo lilikuwa ni jukumu lake kuona kuwa
mgogoro wa wawekezaji wa mitambo ya IPTL unakwisha ili mitambo iendelee kutoa
huduma ya umeme kwa Taifa. Jukumu la Waziri ni kusimamia Sera, Sheria na
taratibu katika sekta anazozisimamia.”

Kuhusu hizo tuhuma za Waziri kuwa “Dalali wa Fedha wa
Escrow”, Kanusho
hilo la Wizara
linaendelea kwa kusema kuwa: “Katika kufanya hivyo, Waziri
hukutana na wadau na kujadili masuala kwa uwazi bila kificho kwa nia ya kujenga
nchi na kuhakikisha kuwa maslahi ya Taifa ndiyo kipaumbele. Kwa hiyo mikutano
na Wadau ikiwa ni pamoja na wawekezaji hufanyika si kwa udalali. Suala la fedha
za akaunti ya Escrow lilihusu uamuzi wa mahakama iliyojiridhisha kuwa mnunuzi
wa hisa zote za VIP na MECHMAR ni halali na alitakiwa kukabidhiwa mali na
madeni ya IPTL. Mali ni pamoja na kiasi cha fedha stahiki kwenye Akaunti ya
Escrow ambazo hata hivyo ilidhihirika kuwa hazitoshi kukidhi deni halali. Akaunti
hiyo ilikuwa na Sh. 182 bilioni wakati malipo yaliyokubalika kwa pande zote
(IPTL na TANESCO) kwa mujibu wa maamuzi ya ICSID I yalikuwa Sh. 306 bilioni.
Kumwita Waziri wa Nishati na Madini kuwa ni dalali ni kupotosha ukweli.”

Lakini siku moja tu baada ya Hotuba ya Rais,
Mwenyekiti wa PAC aliandika maneno haya katika Ukurasa wake wa Facebook:
“Kuweka rekodi sawa, PAP (sio IPTL) wamelipwa tshs 306 bilioni. Alizosema Rais
ni zile zilizokuwa Benki kama taslimu na dhamana za Serikali. Ambazo hakusema
ni zile ambazo zililipwa na TANESCO baadaye. Ifahamike hadidu rejea (Terms of
References) kwa CAG kufanya uchunguzi zilitolewa na PAC, hivyo PAC ndio yenye
mamlaka ya kuzisemea, kuzielezea na kuzitolea ufafanuzi. Kwenye eneo hili Rais
hakuwa sahihi na Ikulu inapasa kurekebisha. Jumla ya fedha ambayo PAP wamelipwa
kutoka akaunti ya ‪#‎TegetaEscrow Ni
tshs 306 bilioni.”

Pia akarejea na kuiboersha hii hoja yake ya awali na
kusisitiza kuwa hili ni “Muhimu sana”:  “Mamlaka
ya Kutafsiri Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali haipo kwa
mkaguliwa (Serikali) Bali kwa Bunge. Bunge hufanya kazi hiyo kupitia Kamati ya
PAC”. Hili tumelidadisi katika makala ya Hotuba
ya Rais na Hatma ya Udhibiti na Ukaguzi wa Fedha za Serikali
. Tulichoona ni
kuwa migongano ya kimamlaka katika suala la Escrow inachangia kuleta utata
hivyo ni vyema tukaondoa miingiliano ya aina hii ila tuhakikishe pia kuwa
kikundi kimoja au mtu mmoja – Bungeni ama Serikalini – asiwe na nguvu sana na madaraka
makubwa kupita kiasi ya kitafsiri na kimaamuzi.

Wakati ‘Serikali’ inaonekana kuendelea tu kushikilia ‘tafsiri
yake’ kuhusu fedha hizo iliyopelekea kuiweka wazi kwa mara ya kwanza Taarifa
Maalum ya CAG magazetini na mitandaoni ili tuisome, tarehe 31 Desemba 2014 Mwenyekiti
wa PAC aliibukia huko Mtwara na Hotuba
yenye jibu hili (kinzani) la nyongeza
: “Katika shilingi bilioni 306 zilizokuwa na
zilizopaswa kuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow kuna fedha za Umma. Serikali
inasema hazikuwa 306 bilioni bali 202 bilioni! Hii sio hoja ya msingi. Hoja ya
msingi ni kwamba hata zingekuwa bilioni moja, bado ndani yake kuna fedha za
umma na ilipaswa utekelezaji wa hukumu ya kupunguza kiwango cha tozo ya
uwekezaji kufanyika ili kujua kiasi cha fedha za umma. Tapeli Harbinder Singh
Seth alilipwa hizo zilizokuwemo katika akaunti na akaendelea kulipwa bakaa na
TANESCO kiasi kwamba shirika hili linalofilisika linamlipa kila siku bwana huyu
shilingi milioni 400. Kila siku inayokwenda kwa [M]ungu tunamlipa mtu ambaye
hajawekeza hata senti tano nchini mwetu. Alikuja na briefcase tu. Kule Kigoma
kuna neno jipya siku hizi, linaitwa umazwazwa. Ni kama ujuha hivi. Huu ni
umazwazwa ambao wananchi hawapaswi kuukubali.”

Kana kwamba inalifufua Azimio
la Songea
la enzi za sakata la Buzwagi kupitia Azimio la Mtwara, Hotuba
hiyo
inaendelea kwa kusema hivi: “Watu watatu tu ambao ni raia wa kigeni
walichora wizi huu kwa miaka mitatu. Mtu mmoja anaitwa Bwana Baharuddin kutoka
Malaysia, Bwana Issa Ruwaih kutoka Oman na Bwana Singh kutoka Kenya na anaishi
Afrika Kusini. Walidanganya nyaraka za kuuziana makampuni, bwana Baharuddin
akauza hisa za IPTL kutoka Mechmar kwenda kwa Bwana Issa wa kampuni ya
PiperLink na Bwana Issa naye akauza hisa hizo zikiwa zimezuiwa na Mahakama kwa
Bwana Seth wa kampuni PAP.  Mabwana hawa wanajua Watanzania ni mazwazwa na
hawafanyi uchunguzi wa kina, yaani ‘due diligence’ kwani hata kwenye EPA fedha
ziliibiwa kwa kutofanya due diligence na kwa kutumia kitu kinaitwa ‘deed of
assignment’. Mabwana hawa wanajua kuwa Watanzania wenye ofisi za umma wana njaa
na watawahonga kidogo tu na kupitisha kila kitu. Ndivyo ilivyofanyika. Kama
viongozi wetu wangefanya ‘due diligence’ kwenye manunuzi ya makampuni haya kama
Sheria ya Kodi ya Mapato inavyowataka, tusingekuwa na skandali ya Tegeta
Escrow. Mfumo uliganzishwa kwa rushwa. Ukitazama miamala ya malipo kutoka
akaunti ya Bwana Seth katika akaunti ya StanBic utaona fedha zimekwenda benki
za UAE na baadaye Oman na Malaysia. Fedha hizo zilikwenda kuwalipa mabwana Baharuddin
na Issa.”

Hotuba
hiyo inayoutangaza 2015 kuwa “Mwaka wa Kuwajibishana”
inahitimisha jibu (mbadala) hilo kwa msisitizo huu: “Serikali lazima ichukue hatua mara moja kuhakikisha fedha
zilizokuwamo kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zinarudi, uamuzi wa mahakama ya
kimataifa unatekelezwa na fedha za umma zinarejeshwa TANESCO na zile za binafsi
zinalipwa kwa wamiliki halali. Tanzania haiwezi kuwa nchi ya kubariki utapeli
wa kimataifa na kuchafua sura ya nchi yetu mbele ya jamii ya kimataifa. Baraza
la Taifa yaani Bunge, kupitia wawakilishi wa wananchi, tayari wameamua na
kupitisha maazimio. Kilichobakia ni maazimio hayo kutekelezwa na Serikali.
Hakuna mjadala katika maazimio ya Bunge, maana katika maazimio hayo Serikali
nayo imo; ilishiriki kikamilifu katika kuyandaa na hatimaye kupitishwa na
Bunge. Hakuna namna ya kukwepa kutekeleza maazimio ya Bunge kwa ukamilifu wake;
nasema hakuna, ni utekelezaji tu.” 

Mtaalamu mmoja aliyebobea katika kufuatilia kwa undani sakata la
Escrow anashauri kuwa, kimkakati, kwa sasa suala la Standard Chartered Bank siyo muhimu
kulishikilia bango maana kwa kufanya hivyo mwanaharakati unaweza kujikuta
unatumiwa na mafisadi hata bila kujijua. Kilicho muhimu, kwa mujibu wa mfuatiliaji
huyo, ni kulivalia njuga suala kuu tu nalo ni la PAP/VIP kuchota kilichokuwa Escrow ili fedha zetu zirudi na gharama za umeme zipungue. Wito wake
unaonekana una mashiko ukizingatia kuwa matamko
ya
VIP yaliyotolewa
katika gazeti la Serikali la Daily News
yamejikita katika kuishambulia
Benki hiyo ya Standard Chartered kuwa ndiyo iko nyuma ya harakati dhidi yao.

Lakini baadhi ya wananchi wadadisi tuko njia panda.
Kwa nini tuangalie tu upande mmoja wa shilingi na sio mkanda mzima? Kama hao wote ni tembo – yaani
VIP/PAP na Standard Chartered Bank (ya Uingereza au hiyo ya Hong Kong) –
tunaoumia si ni sisi nyasi? Au hao ni panzi tu ilhali sisi na wapambanaji wetu
ndio kunguru? Kama ni hivyo, je, na hili lililonenwa na wahenga  wetu nalo linatuhusu pia: “kunguru mwoga hufukuza
mbawa zake”?