Unapomwacha Adui yako Fisadi Nyuma
Chambi Chachage
Filamu ya Shaka Zulu ina ujumbe muhimu katika vita
dhidi ya ufisadi. Kama tulivyoona katika makala ya Tunahitaji Viongozi Wenye U Tatu, tulipopata Uhuru tuliambiwa kuwa maadui zetu wakuu wa maendeleo walikuwa
watatu – ujinga, umaskini na maradhi – ila baadaye tukajulishwa kuwa
ameongezeka wa nne,yaani rushwa. Sasa rushwa imekubuhu na kuwa ufisadi ambao
kwa hakika ni adui mkuu maana anakuza hao wengine watatu.
Katika filamu hiyo tunamuona Shaka akisema hivi: “Never
leave an enemy behind or it will rise again to fly at your throat.” Maneno
haya, kwa tafsiri ya haraka haraka, yanamaanisha: “Usimwache adui yako nyuma la
sivyo ataibuka tena na kukurukia akukabe koo.” Shaka alisisitiza pia kuwa hiyo
ndiyo pekee ya kumkabili adui.
Tatizo kubwa katika vita dhidi ya ufisadi ni kuwa
maadui, yaani mafisadi, huachwa nyuma hivyo huibuka tena na tena kutukaba koo.
Unakuta mtuhumiwa yule yule wa kupokea fedha za ufisadi wa rada ni mtuhumiwa
huyo huyo wa kupokea fedha za ufisadi wa Escrow. Na unakuta mtuhumiwa yule yule
wa ufisadi wa mgodi wa Kiwira ni mtuhumiwa huyo huyo wa kupokea fedha za
kifisadi za Escrow. Tunamuacha tu.
Wahenga walinena, “akuanzaye mmalize”. Na kuna njia nyingi za kummaliza adui
aliyeanza kukufanyia ufisadi unaokuongezea ujinga, maradhi na umaskini pamoja
na ufisadi zaidi. Katika nchi inayofuata utawala wa sheria, njia kuu ni
kumshitaki na kumuadhibu vilivyo pale inapothibitika pasipo shaka kwamba
amefanya ufisadi.
Lakini, je, ukimuadhibu kwa faini na kumfunga jela si atakulipa
tu vijisenti na atatoka na kukukaba koo tena? Siyo rahisi hasa kama adhabu hiyo
imejumuisha kumfilisi mali zake na kuvunja mtandao wa ufisadi unaoweza
kumwezesha kulipiza kisasi. Ni vigumu kama utakuwa umemkata mabawa yanayoweza
kumfana akurukie tena na kukukaba koo.
Si anyongwe? Hapana. Ya Uchina tuwaachie Wachina.
Tuendelee na harakati zetu za kuondokana na adhabu ya kifo inayoondoa haki ya
msingi kabisa ya mwanadamu yoyote yule, yaani kuishi. Tujikite kwenye kutunga
na kutekeleza sheria zenye adhabu kali zaidi dhidi ya ufisadi, yaani,
zitakazotufanya tuogope ufisadi kuliko hata tunavyoogopa kifo.
Mwanakijiji ameliweka
hivi: “Kashfa ya akaunti ya Escrow ni miongoni mwa kashfa zinazotokana na
watawala kuwadhania, kuwachukulia na kuwatenda Watanzania kwa ujinga. Kashfa kama
hizi zinaishia mawaziri kung’oka, watu kushtakiwa na hata baraza la mawaziri
kuvunjwa lakini chama kilichounda Serikali kinaendelea kwa kuruhusiwa kuingiza
sura mpya. Tungekuwa na mfumo wa kumwajibisha Rais pale mawaziri wake
wanapovurunda basi Baraza la Mawaziri linapovunjwa na yeye mwenyewe anaondoka
nao na haruhusiwi kugombea na anapoteza mastahili yote ya ustaafu! Wangekuwa
wanaogopa hata kudokoa ndotoni! Hata mawaziri wanaojiuzulu wangekuwa wananyang’anywa
mafao yao na mali yote yenye utata kufilisiwa. Wangeona hela za umma chungu!”
Hakika ufisadi ungegeuka shubiri ambayo tusingetaka kuichukua pima.
Ujumbe huo wa Shaka unawahusu pia wanasiasa na
wanaharakati wapambanaji ambao aghalabu wanawaonea huruma baadhi ya mafisadi na
kuwaach(i)a kutokana na sababu
mbalimbali. Kushughulikia baadhi ya mafisadi na kuwaachia wengine, kwa
kisingizio kuwa makosa au maslahi yao ni madogo zaidi na/ama walijitahiditahidi
kuzuia ufisadi ila wakazidiwa nguvu na wakuu wao wa kazi hivyo ufisadi huo
ukatokea, ni kumwacha adui nyuma na kumpa nafasi ya kujipanga upya ili je kukukaba
koo tena. Ni kubariki ufisadi.
Mafisadi wao hawana hulka ya kumuacha adui nyuma. Ndio
maana mfuatiliaji mmoja wa ufisadi aliniasa hivi kwa Kiingereza, “it pays to
watch your back.” Ila hatutakuwa na haja tena ya kutazama tazama nyuma kwa hofu
na sisi tukiacha kuwaacha nyuma mafisadi.