Fungate la Uwekezaji na Migogoro ya
Maslahi Escrow

Ufisadi wa Escrow ni ishara kuwa sasa tumemaliza rasmi
fungate la uwekezaji Tanzania. Harusi tuliyofunga kwa chereko na nderemo nyingi
na wawekezaji katika miaka ya 90 imegeuka shubiri. Kama wahenga wetu walivyonena,
“kukopa harusi, kulipa matanga”.

Kwa hisani ya wafadhili wetu tulijiingiza kwenye sera
za Serikali kukopa, kukodi, kununua, kuuza, kuwekeza na kuingia ubia kwa
kutumia fedha za (mashirika ya) umma bila kuzingatia kwa kina dhana
ya mgogoro wa maslahi katika mapana yake
. Hivyo, kupitia Azimio la Zanzibar
lililolizika rasmi Azimio la Arusha tumeishia kuwa na wanasiasa ambao wanavaa
zaidi ya kofia moja. Japo sio vibaya
kuwa na nyadhifa au shughuli zaidi ya moja ni hatari pale zilizo binafsi zinapogongana
na za umma.

Mtu anaweza kuwa mwanasheria wa Serikali na wakati huo
huo akapata ‘gawiwo’ litokanalo na hisa zilizopo kwenye kampuni inayochunguzwa
na Serikali. Pia mtu anaweza kuwa mbunge, mmiliki wa kampuni binafsi na
mwanasheria wa kampuni ya umma inayochunguzwa na Kamati ya Bunge. Kama hili
haliwekwi wazi na kutatuliwa lazima mgongano wa maslahi unaoleta au unaoulinda
ufisadi kama wa Escrow utokee.

Ni katika muktadha huu swali la kama fedha
zilizochotwa katika akaunti ya Escrow ni za umma au za binafsi linapokuwa na
uwili usio na tija. Ziwe za umma ama zisiwe za umma ukweli ni kuwa uchotaji
wake ni zao la mgogoro mkubwa wa kimaslahi na kiuchumi. Hata kama Serikali
itaweza kutumia uprofesa wa hali ya juu kututhibitishia pasipo shaka kuwa ni za
binafsi, bado haiwezi kuepuka ukweli kuwa fedha hizo hawajapewa watu binafsi tu
bali na wale ambao wana dhamana katika mihimili mikuu mitatu ya Serikali.

Hata hao watu binafsi wamegawiwa fedha hizo katika
mazingira holela ya utoaji fedha na uhujumu uchumi. Inawezekana kabisa kuwa
‘utakatishaji wa fedha haramu’ na uingizaji huo wa fedha nyingi kiasi hicho kwa
kasi hiyo katika mzunguko wa fedha wa nchi ndio umechangia kwa kiasi kikubwa
kuongezeka zaidi kwa mfumuko wa bei katika kipindi hiki. Kama alivyosema
mchangiaji mmoja katika mtandao wa kijamii, hali hii inafanana na Mansa Musa wa
Mali alivyopitisha dhahabu nyingi Misri na kudidimiza thamani yake nchini humo.
Tofauti ni kuwa hakuwa Mmisri na wala hakuwa mtuhumiwa wa ufisadi.

Tatizo linalojitokeza katika mjadala wa Escrow ni
wachangiaji wengi pia kugawanyika katika uwili huo – za binafsi au za umma. Na
ni uwili huo huo unaopelekea kwa kiasi kikubwa ‘mashabiki’ wa kila upande
kuvutia kwao na kupata tabu kukubali hata hoja yenye ‘mashiko’ kutoka upande
mwingine. Pengine tutumie mfano wa Mbunge wa Jimbo la Mtera ambaye hoja na
vioja vyake vimeacha gumzo kubwa mitaani na mitandaoni.

Pamoja na kuwa uwasilishaji wake uliomfanya ajulikane
kwa jina la utani la ‘Kibajaji’ wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa
jimbo la Arumeru Mashariki unawakera watu wengi wenye staha, tunahitaji uvumilivu wa
kutuwezesha kuchambua na kutenganisha mchele na chuya. Hapo chuya 
ni lugha yake isiyo ya ‘kistaarabu’. Mchele hapo ni hoja yake ya msingi kuwa
kuna makundi kadhaa yenye maslahi katika mjadala wa Escrow.

Waziri mmoja anayetajwa kuwa miongoni mwa wenye nia ya
kugombea Urais mwakani aliguswa na bainisho hilo na kujenga hoja kuwa mgombea
Urais hapaswi kuwajengea zengwe wagombea wengine waondoke kwenye kinyang’anyiro
bali anapaswa kuwa tayari kushindana na wenzake katika uchaguzi. Lakini hilo ni ‘tamanio’ tu la kisiasa, hali halisi inaonesha kuwa mbinu nyingi hufanyika ili
kuhakikisha wagombea, hasa wale wenye nguvu ya umma au ya ufisadi, hawapati
fursa ya kupitishwa kuwa wagombea na hivyo kutumia nguvu hizo kushinda uchaguzi
wa kuteua mgombea katika vyama vyao.

Lakini kundi mmojawapo lililotajwa na Kibajaji ambalo
pengine ndilo linaloelezea kwa ufasaha dhana ya fungate la uwekezaji na
migogoro ya maslahi ni lile linalohusiana na ufanyabiashara. Hapa tunaona
makampuni na hata nchi ambazo baadhi ya makampuni hayo yanatokea zikijaribu
kujipenyeza kwenye michakato na mijadala inayohusiana na uwekezaji katika sekta
ya umeme kulinda maslahi ya nchi zao na raia wao. Ndiyo maana mabenki kadhaa ya
nje yamekuwa sehemu ya mjadala wetu wa sakata la Tegeta Escrow.

Ili kuelewa hii hoja iliyojifichajificha katika vioja
vya Kibajaji na dhana
ya CSC katika uwekezaji
ni vyema turejee maneno ya Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mahesabu ya Serikali
wakati anajumuisha hoja
kuhusu Escrow. Ameitaja kwa jina benki mojawapo kubwa ya nje na kusema kuwa
iliwahi kuja na balozi wa nchi yao [ambayo ni mfadhili mkubwa wa bajeti ya nchi
yetu] ‘kulobi’, yaani kushawishi, ili “tuwaachie” tu “wachukue hela za Escrow”, ikabidi ampigie
aliyekuwa Waziri wa Sheria kuhusu uvunjaji huo wa protokali/taratibu za kidiplomasia.

Sasa tujiulize kwa makini sana ni wanasiasa na
viongozi wangapi wanaofuatwa na taasisi hizi za kifedha/kibiashara zinazohusika
kwa namna moja au nyingine na uwekezaji katika sekta zetu za umma?Mara ngapi? Wangapi
hukubali ushawishi wao badala ya kuhoji uvunjaji huo wa taratibu zetu na
mgongano wa maslahi? Tutegemee tu ujasiri na kuamini(a) tu uadilifu wao wa moyoni
utakaowapelekea kuvijulisha vyombo vyenye dhamana ya kulinda sheria au uzito na
‘ujeuri/ukali’ wetu wa kitaasisi na kidiplomasia wa kuzuia uingiliaji wa taasisi
zetu za umma?

Fungate la uwekezaji hakika limeisha. Harusi ya wanasiasa na
wawekezaji imezalisha migogoro mingi ya maslahi. Wakati wa ku(wa)tenganisha (wana)siasa
na (wafanya)biashara ni huu.