Tatizo la Tanzania ni Uwaziri Mkuu?
Sakata la Zanzibar kujiunga na OIC na
G55 kudai Tanganyika irejeshwe lilisababisha Waziri Mkuu abadilishwe. Mchakato wa utoaji wa zabuni ya uzalishaji wa
umeme wa dharura kwa kampuni tata ya RICHMOND ulipelekea kujiuzulu kwa Waziri
Mkuu. Ugawanaji wa fedha za akaunti tete ya ESCROW unaweza kumuondoa Waziri
Mkuu.
Kwa nini Tanzania ilianzisha cheo hiki
cha Waziri Mkuu? Ilikianzisha ili iweje ilhali kuna Rais Mtendaji? Nini kilipelekea
hilo ukizingatia kuna Katibu Mkuu Kiongozi?
Majibu ya maswali haya yanaweza
kutusaidia kubaini kwa nini tunashindwa kutatua matatizo ya utendaji na ufisadi
nchini. Karibu kila mara kunapokuwa na mgogoro mkubwa wa kiutendaji au
kiufisadi suala la Waziri Mkuu linajitokeza. Pengine tatizo kubwa tulilo nalo
ni nafasi ya Waziri Mkuu. Kama ni hivyo ‘tuutatue’ Uwaziri Mkuu.
Tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu inaonesha
kuwa tumekuwa na Mawaziri Wakuu 10 toka sehemu moja ya nchi yetu ilipopata uhuru
mwaka 1961. Mawaziri Wakuu wawili wa kwanza – Julius Nyerere mwaka 1961 na Rashidi
Kawawa mwaka 1962 – hawakuwa chini ya Rais yeyote. Wao ndio walikuwa watendaji
na wawajibikaji wakuu wa Serikali.
Utaratibu wa kuwa na Rais ulipoanza baada ya kuwa na Jamhuri,
nchi ilikaa kwa miaka 10 bila kuwa na Waziri Mkuu. Hivyo, kati ya mwaka 1962 na
mwaka 1972 kulikuwa na Rais, makamu wake, na mawaziri pamoja na makatibu wakuu
wao. Siri ya kwa nini Tanzania iliamua kuwa na Waziri Mkuu aliitoboa Rais wa
kwanza wa Tanzania wakati alipokuwa akishinikiza kujiuzulu ama kufukuzwa kazi
kwa Waziri Mkuu mwaka 1994.
Hivi ndivyo Nyerere alivyoitoboa siri hiyo katika kitabu cha Uongozi
Wetu na Hatma ya Tanzania: “Narudia: kumbadili Waziri, hata Waziri
Mkuu, si jambo la ajabu. Anaweza kujiuzulu, anaweza kufukuzwa na nchi
isitikisike. Lakini huwezi kumtikisa Rais wa nchi bila kuitikisa nchi yenyewe.”
Ni dhahiri Uwaziri Mkuu ulikuwa ni wa kumkinga Rais.
Nyerere utaratibu huo ulimfaa. Japo humo anasema kuwa Kawawa hakufanya
kosa lolote ila akambadili tu kwa kumweka Edward Sokoine, muktadha wa wakati
huo unaonesha alifanya mabadiliko hayo kuzuia mtikisiko. Mwaka 1977 nchi
ilikuwa inajiandaa kuingia vitani ikiwa katika hali ngumu ya kiuchumi – Kawawa
akamhamishia Wizara ya Ulinzi kuchukua nafasi ya Sokoine. Na Sokoine huyo huyo
alimtoa kwenye Uwaziri Mkuu miaka mitatu baadaye, yaani 1980, na kumweka Cleopa
Msuya kisha akamrudisha tena Sokoine katika nafasi hiyo mwaka 1983 mara tu
baada ya jaribio la baadhi ya watu kumpindua Rais mwaka 1982 na wakati wa
operesheni dhidi ya wahujumu uchumi.
Lakini, je, nafasi hiyo bado inahitajika hasa katika kipindi
hiki cha mfumo wa vyama vingi? Katika
zama hizi za ufisadi nafasi ya Uwaziri Mkuu inausaidiaje Urais? Je, inausaidia
katika upambanaji na ufisadi au inaukinga na uwajibikaji dhidi ya ufisadi?
Wapo wanaoona kuwa muundo huu ni kichaka cha kuficha na kukuza
ufisadi. Katika mjadala wa Waking’oka
na yeye ango’ke? kwenye mtandao wa kijamii, mtoa mada anasema hivi: “Kashfa ya akaunti ya
Escrow ni miongoni mwa kashfa zinazotokana na watawala kuwadhania, kuwachukulia
na kuwatenda Watanzania kwa ujinga. Kashfa kama hizi zinaishia mawaziri
kung’oka, watu kushtakiwa na hata baraza la mawaziri kuvunjwa lakini chama
kilichounda Serikali kinaendelea kwa kuruhusiwa kuingiza sura mpya. Tungekuwa
na mfumo wa kumwajibisha Rais pale mawaziri wake wanapovurunda basi Baraza la
Mawaziri linapovunjwa na yeye mwenyewe anaondoka nao na haruhusiwi kugombea na
anapoteza mastahili yote ya ustaafu! Wangekuwa wanaogopa hata kudokoa ndotoni!
Hata mawaziri wanaojiuzulu wangekuwa wananyang’anywa mafao yao na mali yote
yenye utata kufilisiwa. Wangeona hela za umma chungu.” Kweli zingekuwa shubiri.
Ila mtoa mada huyo, ambaye amewahi kutuhariria na kutuwekea mtandaoni
chapisho lote la Nyerere lililonukuliwa hapo juu, anaonekana kusahau maneno
haya yaliyomo humo: “Ni vizuri jambo
hili likatamkwa wazi wazi na likaeleweka sawa sawa. Maana watu wengine
wananong’onanong’ ona kuwajibika kwa Rais kana kwamba ni jambo la mchezo mchezo
tu. Kulazimika kumchukulia hatua Rais wa nchi ni mkasa na balaa kwa nchi yoyote
ile. Ndiyo maana tunatakiwa kuwateua na kuwachagua marais wetu kwa uangalifu
mkubwa; na ndiyo maana wakishakuchaguliwa, wanatakiwa wajiheshimu na kuwa
waangalifu sana.” Ndiyo, tuwe waangalifu mno kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
Chapisho hilo la Nyerere linaendelea kusisitiza kuwa: “Ni
jambo muhimu kabisa, kwa kweli la kufa na kupona, kufanya kila jitihada ili
kujenga na kuimarisha utaratibu na mazoea ya kuchagua na kubadili Rais wa Nchi
yetu kwa njia ya kupigiwa kura, baada ya Rais anayetoka kumaliza kipindi chake
kimoja au viwili kwa mujibu wa Katiba. Utaratibu mwingine wowote haufai, na ni
lazima tufanye kila lililo ndani ya uwezo wetu kuuzuia. Mnapolazimika kuutumia,
ni jambo la kufanyaje, si jambo la kurukia.”
Escrowgate inatosha kutufanya tulazimike kuutumia utaratibu
huo? Bunge na wabunge wana mori na
motisha wa kulirukia, achilia mbali utashi na ujasiri wa kulifanya, jambo hilo?
Nchi na wananchi wapo tayari kumtua Waziri Mkuu zigo la kashfa zote za ufisadi utokanao
na uzembe wa watendaji na viongozi wakuu wa Serikali na kumtwika Rais?
Au ni yale yale yaliyopelekea nchi isitikisike baada ya
aliyekuwa Waziri Mkuu wa awamu wa nne kwa miaka miwili kunena
haya bungeni na kuachia ngazi bila kumwathiri Rais aliyemteua na Bunge lililompitisha:
“Nadhani tatizo ni Uwaziri Mkuu. Kwamba ionekane Waziri Mkuu ndio amefanya
haya, tumwondolee heshima au tumwajibishe”?
Gharama za demokrasia hakika ni kubwa. Lakini matokeo ya
demokrasia yanapaswa, si kurudisha gharama hizo tu, bali pia kuzalisha faida,
yaani, maendeleo yetu ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Kuwa na Serikali ambayo
inalazimika kuvunja baraza la mawaziri na kubadili viongozi mara kwa mara
katika kipindi kifupi cha miaka 10 tu ni demokrasia ghali. Kodi za wananchi
wenzao zinawagharimia chakula, mavazi na malazi pamoja na posho za ujuzi
wanaoupata katika semina elekezi na ziara za mafunzo ila hata kabla hatujaona
matunda ya utendaji wao wanatoka kutokana na ufisadi wao au wa wengine.
Basi imetosha. Tusiwe na Waziri Mkuu. Rais awajibike
mwenyewe. Katiba isimike hilo.