Wako Wapi kina Anna
Calculator?

“Watu wananiona mimi kama
mwehu, lakini nina akili zangu timamu kabisa!” – Anna wa Mtwara

Jacqueline Mgumia

Usiku wa tarehe 17 Oktoba 2014 nilikuwa
Villa Park, Mtwara nikipata chakula cha jioni. Katika kuongelea burudani za mji
huo mmoja wa watu tuliowakuta mezani alitutaarifu kuwa walikutana na binti aliyeitwa
“Calculator” mwenye uwezo mkubwa wa hesabu aliyekuwa kivutio kikubwa. Nilishangazwa,
kwani mara nyingi vivutio vya wageni ni sanaa – sikuwahi kudhani hesabu nayo ni
sehemu ya sanaa. Kwa butwaa nikauliza, “sasa huyo binti ana uwezo gani”?

Mmoja wa mashuhuda akasema, “juzi
tulipokuwa tunakula huyo Calculator alipita, nasi kwa shauku tukataka kupima
uwezo wake, hivyo, weita akatuambia tumuulize swali lolote la hesabu atatujibu.
Tukamuuliza ‘kuna tisa ngapi katika mia moja?’ Kwa wapesi kabisa
akajibu kuna tisa ‘20′, wakati sisi tulidhani kuna tisa 19”. Calculator
aliwakumbusha kwamba 99 ina tisa mbili, kwa maelezo hayo wapimaji wakaingiza
mikono mifukoni mwao na kumpa fedha kidogo kama pongezi.

Kutokana na hamu ya kutaka kumfahamu
Calculator nilimuuliza mhudumu tunawezaje kumuona. Kwa haraka haraka akatujibu,
“yule! hayuko vizuri. Hakai sehemu moja anazungukazunguka tu. Labda mumjaribu
kesho jioni.” Jioni tuliyoambiwa haikuwa nzuri kwetu kwa kuwa tulikuwa
tunaondoka kurudi Dar es Salaam kesho yake alfajiri, hivyo, tukaamua kurudi
mchana kesho yake kumtafuta.

Nikamuuliza mhudumu tuliyemkuta iwapo
anamfahamu Calculator, yeye mara moja aligeuka na kuelekea counter, aliporudi
akatwambia, calculator haipo counter. Hakika alikuwa hamfahamu Calculator mtu
bali kitu, hivyo, tukasubiri mhudumu wa pili ambaye alituvunja moyo zaidi.
Alisema, “hakuna anayefahamu Calculator, anatokea wapi, anaishi wapi wala simu
yake.” Pia akatueleza kuwa hotelini hapo kuna wakati anafika na wakati mwingine
hafiki, kwani kuna wakati wanamfukuza iwapo anaonekana kuwasumbua wateja.

Ingawa uhalisia wa kumuona ulianza kufifia, ndani ya moyo nilishikwa na hamu ya kukutana naye labda kwa
sababu nilikuwa siamini kwa nini mtu mwenye uwezo kama yeye anafanya sanaa ya
hesabu hotelini, na pia kwa nini watu wamuone hana akili timamu?

Hivyo, nilipopanda bajaji kurudi nilipofikia, nikamuuliza dereva wa bajaji kama anamfahamu Calculator. Kwa
bahati nzuri alikuwa anamfahamu ila akasema itakuwa vigumu kumpata kwani
anazunguka sana mchana na hafahamu anakaa wapi. Tukakubaliana katika mizunguko
yake iwapo atakutana naye amuombe aje hotelini kwetu na atakapomleta tutamlipa
usafiri wake. Aliridhia na kutoa tahadhari kwamba anaweza asimpate kwani
Calculator ana mizunguko mingi sana pia “hapendi watu wanavyomuitaita na
kumshangaa.” Nikatoa salaam ampe: “mwambie sisi hatumshangai tunataka kutambua
uwezo wake.”

Saa moja baadaye, dereva wa bajaji
alipiga simu kwamba amempata. Nilitoka nje na kukutana na dada ambaye
alijitambulisha kwa jina la Anna! Swali langu la kwanza lilikuwa jina la
Calculator limetokea wapi. Alijibu, “napita huko njiani watu wananiuliza ngapi
jumlisha ngapi, ama ngapi gawa kwa ngapi, nawajibu. Wao wanaangalia kwenye
calculator walipoona sikosei wakaanza kuniita Calculator.”

Anna alimaliza darasa la saba mwaka
2002 ila baba yake alimwambia hakufanikiwa kuchaguliwa kuendelea na shule.
Hivyo, alienda kuishi na bibi yake mzaa mama kufuatia kifo cha mama yake. Leo
hii Anna ana umri wa miaka 27, anaishi na bibi yake na mama yake mdogo hapo
Mtwara. Toka alipomaliza la saba hakubahatika kuendelea na masomo wala kupata
kazi kutokana na ugonjwa wa kifafa
unaopelekea aanguke anguke hivyo kuwafanya waajiri wengi kukataa kumpa kazi.

Baada ya kufanya maongezi naye kwa muda
mrefu na kumuuliza hesabu za kujumlisha, kugawa, kuzidisha na kutoa kwa zaidi ya
nusu saa nilijiridhisha kwamba Anna hakika ni Calculator. Baadhi ya maswali
niliyomuuliza yalikuwa: Kuna mtu ana matofali 552. Akaamua kuwapa watu watano
kila mmoja matofali 72, je, yeye atabakia na matofali mangapi? Kwa haraka,
ndani ya sekunde tatu alijibu 192. Mimi kwenye calculator jibu lilikuja 190,
nikamwambia kakosea, akarudia hesabu hiyo na kusema kwamba jibu ni 192,
nikarejea tena kuhakiki kwenye calculator, ni kweli mimi ndiye nilikuwa
nimekosea.

Baada ya hapo nikamuuliza hesabu hizi
za kuzidisha na kugawanya kwa haraka haraka: (i) 920 x 5= 4600, (ii) 927 x 4 =
3708, (iii) 48 x 49 = 2352, (iv) 97 x 95 = 9 515, (v) 2300/7 = 328.571, (vi)
322/5= 64.4, (vii) 1950/6 = 325, (viii) 9580 x 250 = 2,355,000. Katika hesabu
zote hizi, alikosea namba (iv) lakini alipopewa nafasi ya kusahihisha,
alitoa jibu sahihi ambalo ni 9215. Kila swali aliweza kutoa jibu lake ndani ya
sekunde 10, mengi akijibu ndani ya sekunde 3. Hata watu waliokuwa jirani
walikuja kumsikiliza na  walistaajabu.

Hakika tulistaajabishwa na uwezo wake
na hata kumfanya rafiki yangu aliyekuwa karibu, Chambi Chachage, kumuuliza
alijifunza wapi hisabati. Anna alijifunza hesabu kupitia shule ya msingi, kama
vijana wengi wa Kitanzania. Anakumbuka mbinu za kukumbuka urahisi wa mahesabu
kupitia MAGAZIJUTO (Mabano, Gawanya, Zidisha, Jumlisha, Toa). Pia kichwani kwake kuna kumbukumbu ya table nzima ya
kuzidisha. Anasema alizikariri hesabu hizo kwa ufasaha alipokuwa shule ya
msingi. Anapofanya hesabu anaziona kirahisi tu kichwani japo kuna wakati
kinamuuma.

Kwa uwezo huo, nilidhani Anna angefanya
vizuri kwenye hesabu alipokuwa shuleni. Lakini akasema hapana, alipokuwa shule
alikuwa anapata na kukosa, kwani kuna wakati alipokuwa anaumwa alishindwa kujua
mbinu gani wenzake walijifunza na hivyo kukosa hesabu mpya. Anna aliendelea
kujifunza hesabu alipotoka shule, kwani yeye kichwani huwa anaziona namba kwa
urahisi pale anapotembea barabarani na huwa zinamvutia. Pia hujifunza namba kwa
kuangalia magazeti na kujibu maswali ya watu anaokutana nao.

Kwa kuwa nafahamu kwamba tunapofika
darasa la saba watu wengi tunakuwa hatufahamu trilioni na bilioni, nilimuuliza
yeye namba hizo alizijuaje baada ya kuziandika kwa usahihi kwetu kwenye
karatasi tuliyompa. Alisema namba nyingi anajifunza kupita matangazo ya Tigo na
Voda, kwani wanatoa zawadi za mamilioni na hivyo yamemsaidia kujua bilioni 1
ina milioni elfu 1, na trilioni ina sifuri 9.

Katika kuelezea uwezo wake alisema
hesabu zote ambazo ni chini ya elfu moja ziwe za kutoa, kujumlisha, kugawanya
ama vipeo na vipeuo huwa hazimchukui muda kuzifanya. Anaweza kuzijibu hizo
ndani ya sekunde zisizozidi tatu. Lakini hesabu zinazoanzia na maelfu kwenda juu
na ambazo zina mchanganyiko wa namba nyingi huwa anazifanya kuanzia sekunde 5 mpaka
10.

Pia huwa anakosea hapa na pale hasa
hesabu inapokuwa na namba zilizochanganyika sana au zinapokuwa na jibu lenye
desimali baada ya kugawanya. Moja ya hesabu hizo ni 950 x 2443, alitoa jibu la
2,318, 850 ambapo alikosea namba mbili, jibu sahihi likiwa 2,320, 850. Katika
maswali ya kugawanya hukosea desimali namba inapokuwa kubwa sana, kwa mfano,
nilipomuuliza 9568/869 ni ngapi,  alitoa
jibu la 11.011 badala ya 11.010.

Sasa Anna anakitumiaje kipaji hiki?
Kwa kuwa hana kazi na watu wamekuwa wanavutiwa na uwezo wake, anafanya sanaa ya
hesabu. Watu wanapomuita akiwajibu maswali magumu kwa furaha huwa wanampa fedha
kidogo. Wengi wa watu hawa ni wageni, hivyo hufikia mahotelini. Lakini kwa kuwa
ana ugonjwa wa kifafa amekuwa akianguka mara kadhaa mbele ya watu na hivyo
wenye hoteli humfukuza kwa hofu anaweza kuangukia wateja mahali pao pa azi.

Sasa mimi nabaki kushangaa tu! Ni watu
wangapi wana uwezo kama wa Ana na hawajulikani kabisa ama wamebaki kufanya
sanaa ya hesabu? Je, ni nini kifanyike mtu anapokutana na kipaji kama hicho?

Najiuliza, ni sahihi kweli kumuita mtu
mwehu kwa kushindwa kujua uwezo wake? Ni kweli alifeli darasa la saba au kifafa
kilimfanya asiendelee na shule? Nini hatma ya kina Ana Calculator wa Tanzania?

Tunawatambuaje? Tunawasaidiaje? Tunawatumiaje?