DEREVA WANGU WA TEKSI[1],
RICHARD WAGNER NA MAPAMBANODHIDI
YA KUTAWALIWA AKILI[2]
Ngugi wa Thiong’o
Heshima
mliyonipa leo imefungamana na kipindi muhimu katika maisha yangu. Mwaka elfu
moja mia tisa na themanini na nne nilialikwa na Chuo Kikuu cha Auckland,
New Zealand, kutoa mihadhara mine kuhusu Siasa za Lugha Katika Fasihi ya
Afrika. Wakati huo nilikuwa nikiishi London, baada ya kulazimika kuishi nje ya
nchi yangu kutokana na udikteta wa serikali ya Kenya. Pamoja na Wakenya
wenzangu, ambao nao walikuwa wakiishi
uhamishoni, na pia watu wa mataifa mingine waliokuwa wanatuunga mkono, nilikuwa nimeshughulika na
siasa za harakati za kupinga ukandamizaji nchini Kenya.
Tulikuwa
tukifanya kazi mchana na usiku ili kuwaelimisha na kuwahamasisha watu wa
mataifa mengine duniani kuhusu yaliyokuwa yakitendeka Kenya – nchi ambayo nchi za Magharibi
zilikuwa zikiisifu kuwa ni mfano
mzuri wa demokrasia na utulivu katika bara la Afrika.
Kwa
hivyo, ingawa nilikuwa nimeukubali mwaliko huo wa Auckland, miezi mitatu kabla
ya kusafiri kwenda New Zealand, sikuwa nimeanza hata kuwa na fikira yoyote
kuhusu mihadhara hiyo, na sikuwa nimeandika hata mstari mmoja! Sikuwa nimepata
wakati wala makini ya kulifanya hilo. Nikaanza kubabaika: Nikazungumze nini?
Nianzie wapi?
Miezi
miwili niliyokuwa katika Chuo Kikuu hiki ndiyo iliyoniokoa! Nilikuwa nimealikwa
hapa kuwa Profesa kwa muda mfupi. Mambo mchanganyiko yaliifanya ziara yangu
hiyo hapa Bayreuth kuwa ni mahali muwafaka pa kupatia ilhamu. Kwani hapa
kulikuwa na kazi iliyokuwa ikifanywa
kuhusu lugha za Afrika, na fasihi iliyotokana na lugha hizo:
Kulikuwa
na “Iwalewa-Haus”, iliyokuwa ikiongozwa na Ulli Beier – mtu aliyefanya kazi
muhimu kuhusu Fasihi ya Afrika iliyoandikwa kwa lugha za Ulaya. Ulli Beier
alikuwa ni mmojawapo wa waasisi wa vituo vya waandishi vya Mbari huko Nigeria;
na pia mhariri wa jarida lililoitwa Black Orpheus. Jarida hilo na vituo hivyo vilikuwa ni
miongoni mwa asasi zilizotangulia kuchapisha maandishi ya waandishi wa Afrika yaliyoandikwa kwa
lugha za Ulaya, katika miaka ya Sitini ya karne iliyopita. Na asasi hizo
mbili zilichangia katika kufanikiwa kwa Kongamano la Waandishi wa Kiafrika
Wanaoandika kwa Kiingereza, lililofanyika Chuo Kikuu cha Makerere,
Kampala, mwaka elfu moja mia tisa na
sitini na mbili.
Lakini
jambo muhimu zaidi lililonitokelea hapa Bayreuth ni lile la kuwa karibu na
Jumba la Masrahi laTamasha la Bayreuth
– jumba alilolijenga Richard Wagner. Msije mkanielewa visivyo! Chuo Kikuu cha
Bayreuth hakikunipa tiketi ya kwenda kwenye tamasha la kila mwaka katika jumba
la opera. Bali niliambiwa kwamba mtu ilimbidi kununua tiketi miaka kumi kabla,
au awe ameirithi kutoka kwa bibi au babu yake.
Lakini,
kwa nini Wagner? Kuna
nyakati chache katika maisha yangu ya uandishi ambapo ilinibidi kupata ilhamu
kutokana na muziki wa kutoka Ujerumani. Baina ya mwaka elfu moja mia tisa na
sitini na tano, na mwaka elfu moja mia tisa na sitini na saba, nilipokuwa Chuo
Kikuu cha Leeds, Uingereza – ambako
ndiko nilikoiandika riwaya yangu,A Grain ofWheat – nilipokuwa nimekwama
katika uandishi, nilikuwa nikijikwamua kwa kusikiliza sehemu ya mwanzo ya “Fifth
Symphony “ ya Beethoven.
Safari
moja nilimwelezea habari hii dereva wangu wa teksi huko Marekani, anayeitwa
Danny Durant. Hapo hapo, nikagundua kwamba kumbe alikuwa ni mpigaji mahiri wa
fidla (au vailini), na pia nikafahamu kwamba alikuwa akielewa mambo mengi
kuhusu historia ya muziki. Basi tangu wakati huo, anapokuwa ananiendesha kutoka
Irvine, ambako ndiko ninakosomesha, na
kunipeleka Los Angeles, ambako ndiko
ninakopandia ndege ninaposafiri, mazungumzo ya Danny Durant huwa ni kuhusu
muziki kwa jumla – lakini hasa kuhusu
ubingwa wa muziki kutoka Ujerumani, na muziki wa Bach. Kwa sababu ya mapenzi yake
ya muziki, Danny pia anajua habari nyingi mno kuhusu maisha ya kimuziki ya
Leipzig, ingawa hajapatapo kufika huko.
Miaka
mitatu iliyopita – tarehe kama ya leo – mimi niliuzuru mji wa Leipzig. Lakini
si kwa sababu ya kwamba Richard Wagner alizaliwa katika mji huo, au kwamba
alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Leipzig, bali ni kwa sababu ya
Abdilatif Abdalla, mmojawapo wa washairi maarufu wa Kiswahili duniani.
Abdilatif,
ambaye kwa miaka kumi na tano alisomesha
Lugha ya Kiswahili na Fasihi katika Chuo Kikuu cha Leipzig, alikuwa anastaafu.
Na Chuo Kikuu hicho kiliandaa kongamano la kimataifa la siku mbili kwa heshima
yake. Nilipokuwa huko Leipzig nikasikia kwamba kila Jumamosi huwa kuna aina ya
tamasha kwenye Kanisa la Mtakatifu Thomas, ambako, karne kadhaa zilizopita,
Johann Sebastian Bach alikuwa akiongoza kwaya. Nikayakumbuka mazungumzo ya
Danny Durant kuhusu Sebastian Bach. Lakini Jumamosi hiyo walikuwa wanapiga
muziki wa Vivaldi. Hata hivyo, nikasema , “Haidhuru!” Kwa vile Danny Durant alinielezea kuhusu
Kanisa hili, nikajiambia ni lazima nilizuru.
Pamoja na Abdilatif; na kaka yake, Sheikh Abdilahi Nassir; na
rafiki yetu, mchapishaji vitabu, Walter Bgoya; na Khamis Ramadhan, aliyekuwa
akipiga filamu, tukaelekea Kanisani. Tulipofika, Kanisa lilikuwa limeshajaa
tele, na sehemu yote ya mbele ilikuwa imeshakaliwa!
Kaka yake Abdilatif ni miongoni mwa
mashekhe na viongozi maarufu wa Waislamu nchini Kenya. Alikuwa amevaa mavazi ya
Kiislamu – kanzu na kofia. Tulipoingia kanisani na kutembea masafa marefu hadi
sehemu ya nyuma kabisa ya Kanisa ili kutafuta nafasi ya kukaa, nilikihisi
kihangaiko na wasiwasi uliokuwa umewatanda wale waliokuwa wakitutazama tulipokuwa
tunaingia. Hatimaye, tukapata nafasi karibu na sehemu alipozikwa Bach. Kidogo nilijihisi sikuwa na utulivu moyoni
mwangu nilipoona kwamba kiu yangu kuhusu Bach ilisababisha fazaa na wasiwasi
kanisani. Shughuli yenyewe ilipomalizika kwa salama, nilifarijika! Tukatoka
nje, na kupiga picha karibu na sanamu la Johann Sebastian Bach.
Sikuuhisi msisimko kama huo kuhusu
Wagner nilipokuwa hapa Bayreuth mwaka elfu moja mia tisa na themanini na nne.
Lakini miaka miwili kabla, nilipokuwa bado niko Kenya, nilitaka kutumia Ride of the Valkyries, ambayo ni sehemu
ya opera ya Wagner, The Ring Cycle, katika
tamthilia yangu ya pili niliyoiandika kwa Kikikuyu, Maitu Njugira; yaani “Mama, Niimbie”.
Hebu fikiria: Wagner akishindana na
ngoma za kiafrika, katika tamthilia ya lugha ya kiafrika, inayoigizwa na
wanakijiji nchini Kenya. Lakini, hilo
halikufanyika. Kwani serikali iliizuia tamthilia hiyo kuigizwa katika mwaka
elfu moja mia tisa na themanini na mbili – mwaka ambao nililazimika kuishi
uhamishoni.
Kwa hivyo, mkusanyiko wa mambo haya
matatu – mwaka elfu moja mia tisa na themanini na nne, Bayreuth, na Wagner –
yalinikumbusha yaliyonikumba Kenya miaka michache kabla, kwa sababu ya harakati
zangu na mapambano kuhusu Lugha – ambayo ndiyo iliyokuwa mada ya mihadhara
yangu huko Auckland, New Zealand.
Wagner akawa ni kiungo baina ya Limuru,
mahali nilikozaliwa; London, nilikokuwa uhamishoni; na New Zealand, nilikokuwa
ninakwenda. Kwa hali yoyote ile iwayo, ukweli ni kwamba ni wakati nilipokuwa hapa
kwenye kijiji cha St. Johannis, Mei 15, mwaka elfu moja mia tisa na themanini
na nne, ndipo nilipouandika mhadhara wa kwanza, ambao baadaye ulikuwa ni sehemu
ya kitabu changu maarufu cha nadharia, Decolonising
the Mind.
Katika
kitabu hicho nilijishughulisha zaidi na uhusiano baina ya mkoloni na
aliyetawaliwa na mkoloni – uhusiano ambao matokeo yake yalikuwa ni lugha za
Ulaya kuyatawala maisha ya bara la Afrika kiuchumi, kisiasa na kitamaduni.
Wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni, Waafrika wa tabaka la kati walizitumia
lugha za Ulaya kuwa ni mbinu za kuzipa uwezo lugha za Afrika katika mapambano
hayo. Lakini baada ya uhuru kupatikana, tabaka hilo likafanya kinyume na hivyo:
likazitumia lugha za Afrika kuzipa uwezo lugha za Ulaya.
Wakati wa
mapambano dhidi ya ukoloni, Waafrika waliokuwa na elimu walikuwa ni wasasi
katika msitu wa lugha za kigeni. Baada ya uhuru, wasomi hao wakawa ni mateka na mahabusu
katika gereza la lugha za Ulaya. Tunalofanya sisi wasomi wa tabaka hilo ni
kuikusanya elimu na maarifa yetu na kuyafungia katika majumba ya makumbusho na
makavazi ya lugha za Ulaya. Hii imekuwa ndiyo hali ya kisomi ndani na nje ya
Afrika.
Katika
makongamano ya taaluma za Afrika, nimepata mara kadha wa kadha kuuliza swali
hili: Ni wasomi wangapi kati ya waliohudhuria, ambao wamepata kuandika angalau
maandishi mamoja kwa lugha yoyote ya Afrika? Huwa hakuna hata mtu mmoja
anayeinua mkono! Maana yake ni kwamba maarifa na ujuzi wetu kuhusu Afrika huwa yanapitia kwenye kichujio cha lugha za
Ulaya na misamiati yake.
Labda
hoja yangu hii itaeleweka vizuri zaidi tukiliuliza swali hili kivingine:
Unaweza kumpata Profesa wa Historia ya Italia, au Utamaduni wa Italia, ambaye
hajui hata neno moja la Kitaliani? Au kumpata Profesa wa Utamaduni wa Ujerumani
na Historia, ambaye hafahamu Kijerumani?
Mamlaka
za kikoloni, kama zilivyokuwa hapo zamani, huenda zikawa haziko tena barani
Afrika; lakini Ulaya inaendelea kuyatamalaki mabongo. Matokeo yake yamekuwa ni
kuzikumbatia kwa nguvu kabisa lugha za Ulaya, na kuzikana lugha za Afrika:
Kuukumbatia ugeni, na kuukimbia uzawa
wetu. Hii ndiyo hali ya bara la Afrika
hivi leo.
Kwa
hakika, tatizo hili si tatizo la Afrika pekee bali ni tatizo linalotokea kila mahali palipokuwa na utawala wa kikoloni;
na pia ni tatizo la walionyimwa uwezo na
nafasi katika jamii. Msingi wake umechimbwa kutokana na dhana ya kwamba lugha
zinaweza kuhusiana kwa mujibu wa viwango vyake tu. Yaani twaweza kusema kuwa ni
mfumo wa kilugha wa ki-Darwin , ambapo mwenye nguvu humvamia mnyonge ili apate
kuendelea kuishi.
Fikira ya
kwamba lugha yangu na utamaduni wangu ni bora kuliko wako, inaonyesha kama
kwamba ndiyo hali iliyoko duniani, licha ya kwamba kuna huo unaoitwa utandawazi.
Sina haja ya kuzungumza kwa urefu kuhusu historia ya maumivu na uchungu – kwa
mfano, mauaji, au mauaji ya halaiki – ambayo yanaweza kutokea iwapo
tutazitazama lugha na tamaduni kwa mtazamo huu. Hata hivyo, mahusiano baina ya
watu, vikundi vya jamii, na rangi za watu, au maeneo mbalimbali ya dunia,
yanaendelea kutazamwa kwa mujibu wa vyeo na daraja. Baadhi ya watu wanaamini
kama kwamba lugha zao ni lugha takatifu, yaani ni lugha anazozungumza Mungu. Lakini, kwani ni lazima lugha ziwe na uhusiano
unaotegemea viwango na daraja zao?
Lugha na
tamaduni zinafaa zihusiane kimtandao. Mtandao unategemea mfumo wa “Nipe, nikupe”. Sawa na mfumo wa daraja.
Daraja linalotumika huwa ni la kuwavusha wa huku na kule; si la kuwavusha watu
wa upande mmoja tu. Likitumiwa hivyo, halitakuwa daraja tena.
Kwa
hivyo, tuendelee kujenga madaraja baina ya lugha na tamaduni mbalimbali, bila
ya kujali ukubwa au udogo wao. Na hili linahitaji kuziendeleza harakati dhidi
ya wanaotamalaki mabongo ya wengine. Nimepata bahati ya kuwa na mimi nimo
katika harakati hizi. Na harakati hizi zinaniunganisha na juhudi za mamilioni
ya watu wengine duniani wanaopigania haki za lugha, kwa msingi wa kwamba kila
lugha na kila utamaduni una uwezo wa kutoa na kupokea. Mshairi wa Kiingereza,
John Donne, alitunga akasema:
No man is
an island,
Entire of
itself,
Every man
is a piece of the continent,
A very
part of the main…
Any man’s
death diminishes me,
Because I
am involved in mankind,
And
therefore never send to know for whom the bell tolls;
It tolls
for thee
Twaweza
kusema maneno kama hayo kuhusu lugha na tamaduni mbalimbali: Kwamba hakuna
lugha auutamaduni ambao ni kama kisiwa; zinategemeana. Kuzifanya lugha
chache zikatawala na kuzidunisha lugha nyingine duniani ni kama kuichukua
okestra ya Wagner ukaipunguza ala, na kuzibakisha ala chache tu za aina moja,
na zenye sauti zinazofanana. Kifo cha utamaduni na lugha yoyote kinaidunisha
okestra ya binadamu wote duniani.
Ikiwa
heshima hii ninayopewa leo na Chuo Kikuu hiki kitukufu itasaidia kuikumbusha dunia
kwamba mapambano ya kupigania lugha yanaendelea, basi naipokea kwa shukurani
nyingi. Kwani uhai wa kila lugha na utamaduni duniani unaitajirisha okestra
hiyo ya binadamu.
Ahsanteni
sana.
[1]Jina lake ni Danny
Durant.
[2]Hotuba ya kupokea Digrii ya Heshima ya
Uzamifu, Chuo Kikuu cha Bayreuth, Ujerumani, tarehe 5 Mei, 2014, iliyotolewa
kwa Kiswahili. Imefasiriwa na Abdilatif Abdalla kutoka Kiingereza.