Je, Profesa Shivji ana Sura Mbili za
Usaliti wa Kitaaluma?


Ndugu Mhariri


Naandika makala
haya kwa sababu moja tu nayo ni kubainisha UONGO ulioandikwa kwenye gazeti la
Raia Tanzania (gazeti dada na hili) na mwandishi wa makala aliyejitambulisha
kwa jina la Joseph Mihangwa. Mihangwa ameandika makala mbili katika gazeti hilo
kwa nyakati tofauti na yote yamebeba ujumbe wa uongo na matusi mazito juu ya kile anachodai kuwa ni ‘sura
mbili za usaliti wa kitaaluma wa Profesa Shivji kuhusu Muungano’. Aidha, uongo na
matusi hayo mazito vimerudiwarudiwa (neno kwa neno) na Mihangwa katika makala
yake ya tarehe 5 Aprili 2014 (ukurasa wa 10) na tarehe 10 Aprili 2014 (ukurasa
wa 12-13).
Katika makala hayo, Mihangwa
anahitimisha kwa kusema kwamba  Shivji
amesaliti taaluma yake na kwa hivyo ni  “mamluki wa kujitakia”.
Hali hii imenishangaza na kunisononesha. Sitajikita kwenye matusi kwa sababu
msingi wa mijadala yenye manufaa ni hoja na siyo matusi.


Mihangwa ametumia
mtindo wa uandishi unaofanana kwa kunukuu maneno kutoka kwenye kitabu cha
Shivji (2008) kiitwacho “Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika-Zanzibar”.
Amenukuu sehemu ya aya mojawapo iliyomo katika kitabu hicho cha Shivji  ( angalia ukurasa wa 209 ) na kutumia nukuu
hiyo kuandika uongo.


 Nukuu iliyotumiwa na Mihangwa ni hii: “Firstly, the Articles of Union, which is
the constituent document of the Union, provided for three governments and that
the political association envisaged was a federation…The Articles did not
dissolve Tanganyika nor abrogate the constitution of Tanganyika. It was Act
(No. 22 of 1964) of the Tanganyika Parliament ratifying the Articles which
abrogated the constitution of Tanganyika. This was contrary to the Articles”.

Mihangwa mwenyewe
ameitafsiri nukuu hiyo  kwa kiswahili
kama ifuatavyo: ‘…mkataba wa Muungano ambao ni sehemu ya Hati ya Kikatiba ya
Muungano inasimika serikali tatu za Muungano, na kwamba Muungano wa kisiasa
uliokusudiwa ni wa Shirikisho. Mkataba wa Muungano haukufuta au kuuwa
Tanganyika wala kutangua au kubatilisha Katiba ya Tanganyika. Ni sheria ya
Bunge la Tanganyika lililoketi kuridhia Mkataba huo ndilo lililotangua na
kubatilisha Katiba ya Tanganyika kinyume cha Mkataba wa Muungano”.


Baada ya kusoma
kwa makini sehemu yenye nukuu hiyo (ukurasa wa 209), nimebaini kwamba maneno
yaliyomo kwenye nukuu hiyo siyo ya Shivji mwenyewe kama Ndugu Mihangwa
anavyodai katika makala yake bali ni sehemu ya muhtasari wa uchambuzi wa Shivji
wa hoja kuu za waraka unaodaiwa kuandaliwa na wanasheria wa Alhaji Aboud Jumbe
Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar,

kwa ajili ya kupelekwa katika Mahakama ya Katiba. Waraka huo, kwa mujibu wa
Shivji, ndilo chimbuko la mashtaka dhidi ya Mzee Jumbe mbele ya Halmashauri Kuu
ya Taifa ya CCM.
Profesa Shivji ameutumia waraka huo katika kitabu chake
kwenye sehemu anayochambua zahma ya kisiasa katika kipindi cha ‘kuchafuka’ kwa
hali ya siasa Zanzibar (1983-1984). 


Muhtasari wa Shivji kuhusu hoja kuu za
waraka huo unaanzia ukurasa wa 208 hadi 213 na kichwa cha habari cha sehemu
hiyo ni ‘Zanzibar’s case for three governments’.
 Tena hata kabla ya kuwasilisha muhtasari wa
hoja kuu za waraka huo, Shivji anaanza kwa kusema (angalia ukurasa wa 209):
‘Although the document is over 100 printed
pages, the thrust of the position taken by the authors, which was in effect
Jumbe’s position, may be summarized in two major points’. 
Anachosema hapa Shivji ni kwamba: ‘ Kwa
kuwa waraka una zaidi ya kurasa 100, msisitizo katika msimamo wa waandishi
  wa waraka huo, ambao ndiyo msimamo wa Jumbe,
unaweza kugawanywa
  katika hoja kuu
mbili’. Shivji anaendelea kuzijadili hoja hizo mbili. Uchambuzi huo unaanzia
ukurasa wa 209 hadi 213. Maneno yaliyonukuliwa na Mihangwa ndiyo hoja kuu ya
kwanza ya waraka huo unaochambuliwa na Shivji. Hoja mbili za waraka
uliochambuliwa na Shivji katika kitabu chake zinaakisi msimamo wa Jumbe kuhusu
hati za Muungano na muundo wa Muungano. Huo siyo msimamo wa Shivji.


Iweje sasa Mihangwa augeuze msimamo wa Mzee Jumbe na
wanasheria wake kuwa ndiyo MSIMAMO wa Shivji. Alichokifanya Mihangwa ni kunukuu
sehemu ndogo ya kitabu cha Shivji inayojadili msimamo wa Mzee Jumbe na kudai
kuwa huo ndiyo msimamo wa Shivji. Na kwa kutumia UONGO huo, aliousuka kwa
sababu anazozijua yeye mwenyewe, Mihangwa anamtusi Shivji kwa kumuita msaliti
wa kitaaluma. Wasomaji wa Raia Tanzania amueni: kati ya Shivji na Mihangwa,
nani msaliti wa kitaaluma?


Makala haya yameandikwa na Bashiru Ally na kuchapishwa
katika gazeti la Raia Mwema toleo  Na.
347 la Jumatano April 16 hadi Aprili 22,2014