Serikali Tatu na Zimwi Likujualo
Hatimaye
Jaji Warioba amelihutubia
Bunge Maalum la Katiba. Ule mzozo wa nani aanze kuhutubia kati yake na Rais
Kikwete sasa ni historia. Kwa umahiri mkubwa Mwenyekiti huyu wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba amekong’a nyoyo za wanaotaka Serikali Tatu.
Hata
baadhi ya wapinzani wa zimwi hili tusilolijua sasa wamemgwaya Waziri Mkuu huyo
wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyopanga hoja zake na
za Tume yake. Tayari wengine wameshabadili mtazamo na sasa wanaamini kuwa lile
zimwi tulijualo la Serikali Mbili limetula vya kutosha. Sasa tunahitaji Zimwi
mbadala.
Hakika
mwanataaluma huyo aliyebobea katika sheria alijipanga vilivyo. Pengine sehemu
pekee ya kupangua hoja zake ni matumizi ya maneno haya: “Tathmini ya Tume.” Ni vigumu kujua wapi
maoni ya wananchi yanaishia na wapi tathmini au maoni ya Tume, ama vinara wa
Tume, yanaanzia. Ni Zimwi lenye vichwa vingapi hasa raia tunalitaka?
Hapa tunaongelea wanatume
ambao kwa namna fulani waliakisi tofauti za kimtazamo za wananchi.Pamoja na hayo mbinu yao ilikuwa ni hii: “Hata tulipopata matatizo ya kufikia uamuzi kwa suala
lolote hatukukimbilia kupiga kura. Tulijifungia kwenye vikundi vya watu wenye
mawazo kinzani na mwisho tukafikia maridhiano na muafaka. Dira yetu ilikuwa
Maslahi ya Taifa. Hatukupiga kura hata mara moja kwa jambo lolote wala kuwa na
mawazo mbadala. Kila Ibara iliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo
ninaiwasilisha katika Bunge Maalum la Katiba, inaungwa mkono na kila mmoja
wetu.”
Hayo aliyoyanena Jaji yanatukumbusha uchambuzi huu wa
Profesa Shivji ambaye amekuwa mwiba mchungu kwa Tume: “Baada ya kuisoma
Rasimu kwa kina, mimi nadhani kwamba masharti mengi ya Rasimu na muundo wake
mzima ni matokeo ya mivutano mikali katika Tume. Bahati mbaya hatuna mwenendo
wa majadiliano ya Tume wala taarifa yao rasmi, hata taarifa ya awali. Lakini
usomaji wangu wa awali unaniambia kwamba Rasimu hii ni maelewano kwa maana ya compromise,
na sio mapatano, au mwafaka, kwa maana ya consensus. Nijieleze kidogo.
Katika maelewano au compromise, pande zinazokinzana hatimaye
zinakubali kwa shingo upande ili kutokwamisha maamuzi. Pande zote zinapata
kidogo na kupoteza kidogo, na kila upande huwa na mkakati wake wa kupata zaidi
katika duru ya pili. Kwa hivyo, maelewano kamwe hayawezi kuwa kwa moyo safi.
Maelewano au compromise, yanazaa uamuzi legelege. Mapatano au consensus,
kwa upande mwingine, ni maafikiano yanayofikiwa baada ya mjadala mrefu, kila
mmoja akilenga kuthibitisha hoja yake na kwa njia hii kusadikisha wenzake
kwamba hoja yake ni sahihi. Baada ya kufikia uamuzi wa mwafaka, kila mmoja
anatoka akiwa ameridhika na amefurahi. Katika compromise, kila mmoja
anatoka amenuna. Ni wazi kwamba huwezi ukapata mwafaka fastafasta.
Lazima utachukua muda.”(Ukurasa wa 7-8, “Utatanishi
na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba Mpya: Mhadhara wa Kuaga Kigoda cha
[Taaluma cha] Mwalimu [Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam]” Mwaka 2013).
Hakuna ubishi hapo kwenye
hilo la msongo wa muda maana uchaguzi mkuu wa
2015 umekaribia. Jaji kwa namna fulani naye kaligusia katika hotuba pale
aliposema: “Tume imekamilisha kazi yake kwa muda ulipangwa kutokana na kazi
nzuri ya Sekretarieti. Wakati Wajumbe wa Tume walipokuwa wanakusanya maoni
mikoani, Watumishi wa Sekretarieti waliofuatana na Wajumbe, walifanya kazi kwa
muda mrefu sana, hata siku za mapumziko. Walikuwa wa kwanza kuamka na wa mwisho
kwenda kulala.” Hakuna kulala hadi kieleweke, ndivyo tusemavyo mtaani na kwa
kiasi kikubwa hakukuwa na kulala hadi Zimwi tusilolojua lieleweke. Kabla ya
hapo ilibidi lieleweke kwa wanatume.
Hao wanatume
walipoeleweshwa, ama kueleweshana, ndipo yakafikiwa ‘maelewano’ haya bila hata
kupiga kura: “Hiyo haina maana kwamba kila mmoja wetu ameacha imani yake,
itikadi yake na msimamo wake. Kuna mambo ambayo kila mmoja wetu amebaki na
imani yake na msimamo wake. Kwa mfano, kwenye suala la Muungano tupo tunaoamini
muundo unaofaa ni Serikali Moja, tupo tunaoamini Muundo wa Serikali Mbili, tupo
tunaoamini Serikali Tatu na tupo tunaoamini Muungano wa Mkataba. Tunachoamini
wote kwa pamoja ni umuhimu wa kuendelea kuwepo na kudumu kwa Muungano. Baada ya
kuwasikiliza wananchi, dira yetu imekuwa ni maslahi ya Taifa na siyo maslahi ya
makundi yetu au nafsi zetu. Nawashukuru sana wajumbe wenzangu wa Tume kwa
kusimamia misingi ya kiutendaji ambayo imetuwezesha kukamilisha kazi hiyo.”
Hiyo Sentensi ya mwisho ya Jaji hapo inatukumbusha tena msongo wa muda kuelekea
2015.
Hatua ambayo ilibidi
ifuatie kabla ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba hawajapigana vikumbo kuhusu Zimwi tulijualo dhidi ya tusilolijua ndiyo hii ya hotuba ya takribani saa nne
aliyoitoa Jaji. Ni hotuba ya kuelewesha na si ya kuwasilisha rasimu. Ya
kuwaelewesha nini? Kutuelewesha ‘maoni’ ambayo Jaji anayaiita “Tathmini ya
Tume.”
Hatuna budi sasa kuzirejea
kwa kina sehemu ambazo hayo maneno ya “Tathmini ya Tume” yanatumika kama rungu
kutuelewesha kuhusu Zimwi tusilolijua: “Tathmini ya Tume ni kwamba siyo rahisi
mambo haya kutekelezwa chini ya muundo wa Serikali mbili.” Je, wananchi wangapi
tuliulizwa kuhusu urahisi huo? Na kitu kutokuwa rahisi ina maana hakiwezekani? Na
hizo jitihada za kuyarahisisha hayo mambo, kadri muda unavyokwenda na
changamoto mpya zinavyoibuka, ambazo hotuba imezianisha katika sehemu ya 147 na
148 ndio mwisho wa safari? Zimwi la Serikali Tatu ndio mwarobaini?
Hapo kwenye sehemu ya 127
ya Hotuba kuna hitimisho hili: “Kwa hiyo, tathmini ya Tume ni kwamba Muundo wa
Serikali moja hauna uhalisia.” Hitimisho hilo linatokana na uchambuzi huu: “Njia
pekee ambayo ingefanya maendeleo ya Zanzibar yapewe uzito sawa na mambo ya
Tanzania Bara ni kuyaweka mambo yote ya Zanzibar chini ya Serikali ya Muungano,
yaani kuwa na Serikali Moja. Lakini kama nilivyosema, wakati wa kukabidhi
Rasimu kwa Marais wetu, Muundo wa Serikali Moja una changamoto nzito. Waasisi
waliona matokeo ya Muundo huo ni Zanzibar kumezwa na Tanganyika. Tume ilipokuwa
inakusanya maoni, wananchi wengi, hasa Zanzibar, walionyesha hofu hiyo ni kubwa
sana hivi sasa kuliko ilivyokuwa mwanzoni.”
Wameonaje kuwa Zimwi la Serikali Moja tusilolijua halina uhalisia ila la Serikali Tatu tusilolojua ndilo lina uhalisia?
Hapana shaka Jaji ana jibu.
Linapatikana kwenye sehemu ya 133: “Tume ilitafakari kama kuna uwezekano wa
kuyarudisha mambo yaliyoondolewa kwenye orodha kufuatia muafaka wa 1994, lakini
tathmini ya Tume ni kwamba kufanya hivyo ni kuzua mgogoro upya kwani itaonekana
mamlaka (autonomy) ya Zanzibar yanaingiliwa. Wakati Tume ilipokuwa inakusanya
maoni, wananchi wengi wa Zanzibar kutoka makundi yote mawili, yaani wale
waliotaka Muungano wa Serikali Mbili na wale waliotaka Muungano wa Mkataba,
wote walipendekeza mambo mengi yaondolewe kwenye Orodha ya Muungano. Wale
waliotaka Muungano wa Mkataba walitaka mambo yote yaondolewe kwenye Orodha ya
Mambo ya Muungano isipokuwa suala la ulinzi. Wale waliotaka Muundo wa Serikali
mbili walitaka mambo yote ya uchumi yaondolewe kwenye Orodha ya Mambo ya
Muungano. Katika hali hiyo, kuyarudisha mambo ambayo hivi sasa yako chini ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hata kama siyo kikatiba, kunaweza kuleta
mgogoro wa kisiasa.” Kama “msingi wa Muungano”, kama sehemu ya 175 ya hotuba
inavyosema, ni Hati/Makubaliano ya Muungano (Articles of Union) ya mwaka 1964
yaliyokuwa na mambo ya Muungano 11 kwa nini ishindikane kuyapunguza kikatiba baada
ya kuongezwa maradufu kinyemela? Si ndicho hicho Wazanzibari wamekuwa
wakikidai?
Hatutaitendea haki Tume
tusipoona utata huo kuhusu historia tete unaojidhihirisha zaidi kwenye sehemu
hii ya 157 ya Hotuba: “Kwa Ta[t]hmini ya Tume, Muundo wa Serikali mbili hauwezi
kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa Serikali mbili waliotuachia waasisi siyo
uliopo sasa. Umebadilishwa mara nyingi, wakati mwingine bila ya kufanya
mabadiliko kwenye Katiba. Waasisi walituachia Muungano wa Nchi Moja yenye
Serikali Mbili, na siyo Nchi Mbili zenye Serikali Mbili. Muundo wa Serikali
Mbili unaweza kubaki tu kama orodha ya mambo ya muungano haitapunguzwa bali
itaongezwa. La sivyo, Serikali ya Muungano itabaki na rasilimali na mambo ya
Tanzania Bara tu. Katika hali hiyo, pande zote mbili zitaendelea kulalamika.
Kwa upande, mmoja Zanzibar itaendelea kulalamika kwamba Tanzania Bara imevaa
koti la Muungano kwa faida yake, na kwa upande mwingine, Tanzania Bara
itaendelea kulalamika kwamba mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara na
rasilimali zake ndizo zimekuwa Muungano.” Hivi kweli hata wanatume waliokuwa
viongozi wa juu wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wakati wa kuongeza mambo ya Muungano hawakumbuka nia hasa ya/za
kufanya hivyo?
Haiwezekani tukachakachua
historia kirahisi namna hii na kusahau (kusema) kuwa Serikali Mbili ilikuwa pia
ni muundo tu wa mpito kuelekea kwenye Serikali nyingi chini ya Shirikisho laAfrika Mashariki. Hotuba ya Jaji imejikita kwenye mpito wa kuelekea kwenye
Serikali Moja ambao, kwa mujibu wa “Tathmini ya Tume”, hauna uhalisia. Na kama
kweli hauna uhalisia basi ina maana tumebakiwa na mwisho mmoja tu ambao
Muungano wa Serikali Mbili unaulenga, yaani Umoja wa Afrika (Mashariki). Na
tukisema huo nao hauna uhalisia basi hakuna mwisho mwingine zaidi ya kuvunjika
kwa Muungano. Lakini hotuba ya Jaji inajaribu kutabiri, ama kutuambia inajua,
hautavunjika.
Haijalishi nani amevunja
Katiba, kinachohitajika ni kuchukua hatua kuilinda. Lakini hotuba ya Jaji
inaendeleza utamaduni wa kulalamika kuhusu upande mmoja wa Muungano kuivunj kana
kwamba Katiba mpya itakuwa na kinga ya kujaribiwa kuvunjwa. Heri angetueleza,
kwa kutumia taaluma yake ya Sheria, kuhusu namna ya kukabiliana na uvunjaji huo
wa Katiba aliyoapa kuilinda. Na mashabiki wa mbadala wangeenda mbali zaidi na
mibadala kwa kutuonyesha namna ambavyo Mahakama ya Katiba, ambayo tayari
inaruhusiwa kuundwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa japo hatujawahi – labda kwa
sababu ya woga – kujaribu kuisimika, inaweza kutatua migogoro ya Muungano. Hata
mwasisi mmojawapo alishaacha kulimung’unyia maneno hilo suala:
Halafu tukizitazama takwimu
alizowasilisha Jaji zinaonesha kuwa Wazanzibari wengi wanataka Muungano wa
Mkataba: “Mchanganuo wa takwimu hizi unaonyesha kuwa wananchi waliotoa maoni
kuhusu muundo wa Muungano kwa upande wa Tanzania Bara, 13% walipendelea
Serikali Moja, 24% walipendekeza Serikali Mbili na 61% walipendekeza Serikali
Tatu. Kwa upande wa Zanzibar, 34% walipendekeza Serikali mbili na 60%
walipendekeza Muungano wa Mkataba, na 0.1% (watu 25) walipendekeza Serikali
Moja.” Ina maana ‘Muungano wa Mkataba’ ni sawa sawa kabisa na wa Serikali Tatu?
Kama si sawa kwa 100% hii haina maana tunalinganisha machungwa na matofaa?
Haishangazi tupo tunaosema
waasisi hawana majibu ya matatizo ya Muungano tuliyo nayo leo. Inabidi
tukabiliane na kero mpya wenyewe na ikibidi tutafute mbadala. Lakini tusiache
mbachao kwa msala upitao kisa umetuambia, ama kututabiria, kuwa kuifufua Tanganyikani kuiua na kuizika Tanzania. Nchi yetu bado changa. Mtoto akililia wembe?
Halahala mti na macho. Kwa
hakika hotuba hii inatukumbusha methali na misemo ya wahenga wetu walioona
mbali. Ndio wao waliosema Zimwi likujualo halikuli likakwisha.