MASWALI

1. Jambazi
amekamatwa au Jambazi limekamatwa?

2. Dawa imepakwa
au Dawa lilipakwa?

3. Jino
ilivunjwa au Jino lilivunjwa?

4. Makala
yameandikwa au Makala iliandikwa?

5. Mada
yametolewa au Mada imetolewa?

*KWA NINI?
(ELEZA TAFADHALI)

MAJIBU

1. Jambazi
amekamatwa au Jambazi limekamatwa? amekamatwa kama bado

kidhana unamuona
ni mtu ila kama kidhana umemvusha kuwa jitu basi

limekamatwa

2. Dawa imepakwa
au Dawa lilipakwa? me na li hapa si suala la ngeli ni

suala la wakati
me ni uliopita sasa hivi na li ni uliopita kabisa

3. Jino
ilivunjwa au Jino lilivunjwa? jino lilivunjwa ni sahihi hiyo

ni ngeli ya j/l

3. Makala
yameandikwa au Makala iliandikwa? nadhani ili/imeandikwa ila

sina hakikka

4. Mada
yametolewa au Mada imetolewa? nadhani imetolewa ila sina maelezo
 

– Demere

 

Ifuatayo ni
nukushi toka katika makala ya Ahmed Rajab yaliyochapishwa katika
Raia Mwema la 326, Desemba 4, 2013:

Katika mhadhara
huo amesema mengi Ngũgĩ yasiyo na ubishi na amempa sifa nyingi Mwalimu Julius
Nyerere, sifa anazostahiki kupewa kwa jinsi alivyokifanya Kiswahili kuwa lugha
ya taifa. Lakini lazima nibishane naye Ngũgĩ kwa kudai kwamba kwa Nyerere
kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa “Hatimaye, Kiswahili kikawa na kwao.”


Hapo kidogo Ngũgĩ
ameteleza. Siku zote Kiswahili kimekuwa na kwao. Hakijatimliwa kikenda
uhamishoni. Wakoloni walikuja wakakikuta kwao, wakaondoka, na wakakiacha huko
huko kwao. 


Na kwao ni kule
ambako wenyeji wake wanasema “vita hivi” na “vita vya” nasi wasemao “vita hii”
au “vita ya”.  Ni wale wale wasemao “makala haya” na si wasemao “makala
hii”. Na wasemao kwa inadi “makala hii” basi na waendelee na kusema “maradhi
hii” badala ya “maradhi haya” kama kisemwavyo Kiswahili huko kwao.

Kwa vile neno
“makala” liko katika ngeli ya JI/MA basi huwa “makala manana”. Na “kitabu
chanana”/ “vitabu vyanana”; “nyumba nyanana”, “ndizi nyanana” na “tabia
nyanana”.


Huko kuliko kwao
Kiswahili humsikii mtu akisema “dhehebu”; wenye lugha yao wanajua kwamba madhehebu
yanaweza kuwa mamoja kama makala yalivyo mamoja au mengi. Pia wanajua kwamba
hakuna neno “dhumuni” bali ni “madhumuni”.


Huko ambako
Kiswahili ni kwao wafuasi wa madhehebu ya Shi’a huitwa “Mashia” na humsikii mtu
kuwaita “Washia”.  Akiwa mmoja huitwa “Shia” nasi “Mshia”.


Vivyo hivyo kwa
wafuasi wa madhehebu ya Suni. Waswahili wanawaita “Masuni” na si
“Wasuni”.  Kule ambako Kiswahili ni kwao mtu atauliza: “Yule ni Suni au ni
Shia?” Humsikii mtu akiuliza: “Yule ni Msuni au ni Mshia?”


Mwalimu Nyerere kweli
amefanya kazi kubwa ya kukinyanyua na kukisambaza Kiswahili katika taifa zima.
Lakini si sahihi kamwe kusema kwamba kwa kufanya hivyo “Hatimaye, Kiswahili
kikawa na kwao.” Kiswahili siku zote kimekuwa na kwao, ila katika huko
kusambazwa kwake Kiswahili kimedakwa na wengine wanaokifanya kuwa ni chao. Hilo
si jambo baya, la kujiweza kwa kujipa uwezo wa kuisarifu lugha nyingine
ilimradi wasijaribu kutuweza. Wasikipotoshe Kiswahili chetu kwa kukisema
tusivyokisema wenyewe Waswahili.  


 http://www.raiamwema.co.tz/ngũgĩ-waswahili-na-nyerere#sthash.63e6P8hj.dpuf

– Sabatho 

Kama nimemuelewa
Ahmed Rajab (nimeinukuu barua pepe yake hapo juu), makala yapo/ipo kwenye ngeli
ya Ji/Ma, na kama kweli yako/iko humo kwa nini basi ‘umoja’ na ‘wingi’ wake
unafanana na hivyo ku(ya/i)fanya (ya/i)onekane ipo kwenye ngeli inayotumia
‘hii’ na ‘hizi’? 

Hata kwenye huo
mfano wa (ma)dhehebu na (ma)dhumuni ambao Mwanazuoni mmoja humu aliwahi
kuushikilia bango nao unaleta utata maana hata watu wa madhehebu ya Mwanazuoni
huyo wanajiita Wasabato ilhali, kama kweli Ahmed yuko sahihi na kama
nimemuelewa vizuri, wanastahili kuitwa Masabato? Ama kweli “Kiswahili kina
kwao” na “Kiswahili kina wenyewe”!
 

– Chambi

Pamoja na
kukubali kwamba watu wanafanya makosa mengi ya Kiswahili na hasa hawafuati
sheria za sarufi vizuri, nadhani ni muhimu kukubali pia kwamba lugha zote
zinabadilika.  Kwa kutoa mfano mmoja tu, katika Kiingereza kutokana na
msukumo wa jinsia utakuta kwamba mara nyingi watu wanatoa sentenso kama hii
(hasa wanapoongea)

When a person is
sick, they go to hospital. 

Badala ya when a
person is sick he or she goes to hospital.  Ili kukwepa kutaja he na she
wanatumia wingi … they.

Kuna mifano
mingi ya aina hiyo.

Sasa lini
tunang’ang’ania sheria ifuatwe na lini tunakubali mabadiliko.

Wafaransa, kama
Waswahili, wanakuwa prescriptive.  Wanajaribu kudhibiti matumizi ya lugha
na kukataza matumizi mengine (sijui wanafanikiwa kiasi gani, kwa mfano Academie
Francaise inajaribu kuzuia maneno ya Kiingereza

Upande mwingine
Waingereza ni descriptive.  Iwapo neno au lugha fulani imeshaanza kutumika
na wengi, wanaiweka kwenye kamusi n.k. 

Wengine wanasema
ndiyo maana Achebe alivuma alivyovuma (licha ya kupigwa vita na wahafidhina wa
lugha) wakati Ahmadou Kourouma ambaye aliafirikisha kifaransa kama Achebe
alivyofirikisha kiingereza alishuhudia kupigwa marufuku kwa vitabu vyake vya
kwanza kama Les soleils d’independence

– Mabala

Richard Mabala
neno ‘aliafirikisha’ nalo limeshaingizwa ama? Nimelipenda! Inanikumbusha vile
Kiswahili cha mtaani kilivyo ’embrace/adapt’ neno ‘change’ na kuzua  neno
‘a(li/me/ta)nichenjia’…

– BeeJay

Neno hili
lilizaliwa leo.  Natafuta hakimiliki tehe tehe tehe

– Mabala

Anachokizungumza
Ahmed Rajabu siyo Kiswahili bali ni lahaja ya Kiswahili aipendayo yeye. Ndiyo,
zipo lahaja lakini kamwe zisiitwe Kiswahili cha wenyewe bali lahaja tu. Mimi
humchukulia Ahmed kama mpotoshaji wa Kiswahili Sanifu bila yeye mwenyewe kujua,
kwa kudhani tu yuko sahihi. Anatumia sauti pekee kujenga hoja kuliko mantiki.
Nitamjibu hiyo makala yake.

– Matinyi

Hata Kiingereza
kina lahaja, na walau lahaja kadhaa zinakubalika, japokuwa kile cha Malkia ndio
kinaitwa kiingereza sanifu. Nadhani anachosisitiza Rajab ni kwamba usanifishaji
wa Kiswahili uliambatana na uingizaji wa miundo/maumbo ambayo hayaendani na
miundo/maumbo asili ya lugha husika. 

Pengine cha
kufurahisha ni kwamba lahaja iliyochukuliwa na kufanywa kuwa lahaja sanifu ni
ya huko huko kwa akina Rajab. Je, yeye kama mswahili mzawa hana haki ya
kulalamika pale anapoona lugha yake inapotoshwa? Ukisoma kamusi za Kiswahili
zilizoandaliwa na taasisi za Zanzibar au hata maandiko ya Kiswahili mengi toka
visiwani utagundua namna Kiswahili chao kinavyotofautiana na hiki
tunachojifunza huku. Kamusi moja niliyoiona hata jina lake lenyewe
lilinishangaza: Kamusi LA Kiswahili. Huku tungetumia YA.

– Sabatho

Hata mimi hii
makala niliipenda maana kwa sasa hususan kuna upotoshaji mkubwa unaendelea kwa
minajili wa kudai hiki Kiswahili cha bara hiki cha Unguja na hata wengine
kudiriki kukitukuza zaidi Kiswahili kilichonukuliwa na wakoloni wamisonari kuwa
ndio sahihi zaidi kuliko kile kinachofundishwa na waliozaliwa na lugha yao.
Alimradi….

– Salma

Kwa mujibu wa
hayo makala uliyoyapenda, unatakiwa useme “mimi hayo makala
niliyapenda”

– Chambi

Ndo upotoshaji ninausema suala hapa si makala bali ni wakati ambao tayari nishauanisha kwa kusema niliipenda na kumbuka unaweza kutumia hii/hizi!?

– Salma

Watu wa visiwani
wanaweza kuwa na Kiswahili chao na wengine wakawa na cha kwao pia. Hata
kiingereza cha Marekani, Canada, Australia, Uingereza hakifanani. Lakini hapa
ninachokiona ni madhara ya kutokienzi Kiswahili, hatukitumii kujifunza maarifa
mashuleni na hivyo tunakidumaza. Fikiria wewe Mwanazuoni katika fani yako laiti
kama ungetumia Kiswahili wakati wote wa masomo yako leo hii ungekua na uelewa
mkubwa sana wa lugha. Ungekua na misamiati mingi na si rahisi kuafanya makosa
madogo madogo kama kuchanganya “R” na “L”, “kuua”
na “kuuwa” “kua” na “kuwa” nk. 

Sisi sote ni
wahanga wa kutoenzi Kiswahili!

– Shangwe

Kwanza,
Unguja kuna zaidi ya lahaja moja.

Pili,
wataalam wa Kiswahili wa kwanza wa Baraza la Afrika Mashariki walikuwa
Waswahili, siyo Wazungu.

Tatu,
hakuna miundo ya Kiswahili iliyojengwa na wakoloni.

Nne,
Ahmed Rajabu ana haki ya kulalamika na hata kulazimisha hoja kwamba yeye ndiye
mwenye Kiswahili chenyewe lakini hiyo haiifanyi hoja yake kuwa sahihi.

Tano,
kwa kutumia mfano neno “makala” ni vizuri tukakumbuka pi hili si neno
la Kiswahili bali ni la Kiarabu. Limeazimwa tu.

Lakini
pia, kwa kuheshimu mifano ya awali, kuwa Ahmed anasema kwa Kiswahili
 “sahihi” – – siyo sanifu naamini – – ilibidi tuseme Shia na
siyo Mshia. Pia Mashia na siyo Washia. Je, ni sahihi kusema “Islam”
badala ya “Mwislamu” au “Maislam” badala ya
“Waislamu”? Mimi kwangu haiji na wala haipo, sijui watetezi wa
Kiswahili cha wenyewe mnasemaje?

Lakini
pia, kwa kuheshimu maana inayobebwa na ngeli za JI/MA mjadala utakuwa mpana
zaidi. Zina mantiki yake na haipingiki kirahisi. Hakuna lugha isiyokuwa na
mantiki.

Kwamba
Kiingereza nacho kina lahaja kunasaidia nini katika mjadala huu, hebu nisaidie
hapo.

Pili,
lahaja si hoja; zipo kwenye kila lugha ila lahaja ni lahaja tu hata kama ina
historia ya kuibeba lugha fulani sanifu. Kwamba, Kiswahili Sanifu kilichomoka
kutoka kwenye Kiunguja hakukifanyi Kiunguja kuwa Kiswahili sahihi bali
kinabakia kuwa Kiunguja.

Hoja
hii ndiyo Wakenya hujidanganya nayo kuhusiana na Kimvita ambacho kiko mbali
zaidi na Kiswahili kuliko hicho ki-Ahmed Rajabu.

Kiunguja, Kimakunduchi, Kipemba, Kingazija, ni baadhi tu ya
lahaja zinazozungumzwa Unguja. Sasa tuzichukue zote tuziite Kiswahili cha
wenyewe? Ahmed anazunguka humu humu kwenye lahaja. Ni tatizo pia lililopo
kwenye Kiarabu ambapo Mwarabu Misri anadai chake ni bora zaidi na wa Sudan
anasema hivyo, lakini wote wanapoteana na cha Mauritania na cha Kuwait, n.k. na
wote hawa wanatofautiana na Kiarabu Sanifu ambacho wengine hukiita cha
Aljazeera na vyuo vikuu.

 —

Matinyi

MJADALA 

https://groups.yahoo.com/neo/groups/Wanazuoni/conversations/messages/23337