Dondoo: Prof Ngugi wa Thiong’o aliutoa mhadhara huu kwa lugha ya Kiswahili jambo ambalo kwa mujibu wa Dakta Martha
Qorro hakuwahi kulifanya kabla kwenye mihadhara yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Tuliupata mhadhara
huu katika ‘hard copy’ na kutokana na umuhimu wake tumeamua kuuchapa upya ili watu
wengi wanufaike nao. Kama kutapatikana makosa yoyote yale yaliyojitokeza wakati
wa kuuchapa upya, ni yetu.

 

Ado Shaibu,

Mwendeshaji wa ukurasa wa  “Kitabu Nilichosoma”

(https://www.facebook.com/KitabuNilichosoma
)

0653619906

 

WASOMI, LUGHA ZA ULAYA NA AFRIKA: KATI
YA KUJIWEZA NA KUWEZWA

 

Ngugi wa Thiong’o

Katika mhadhara huu, nataka kuangalia na
kufafanua, kwa ufupi tu, uhusiano wa kitaaluma kati ya lugha za Afrika na
Ulaya, na hasa Kiingereza. Jambo hili ni muhimu katika wakati huu, ambapo nchi
nyingi za Afrika zinasheherehekea miaka hamsini tangu zipate uhuru wake toka utawala
wa kikoloni.

Msomi, au mwanataaluma wa aina yeyote
ile, si kitu kipya kwa Afrika: Kila jamii, za leo au za kale, zilikuwa na
wasomi au wanataaluma wake. Tunalitumia hili neno “msomi” kwa maana ya mtu
anayeshughulika na fikra. Yawezekana kwamba msomi huyo huenda akawa ana ujuzi
mwingine; lakini kazi yake kuu inayojitokeza ni matokeo ya kujishughulisha
kwake na fikra. Katika kundi hili wanaingia pia waganga wa kimwili na kiroho,
wahunzi (au wafua vyuma), wajenzi, na mafundi wengineo.

Watu kama hawa walikuwa miongoni mwa
wajenzi wa utamaduni wa Misri, Uhabeshi, Zimbabwe, Songhai, na kwingineko. Kati
ya hao, alikuwamo pia mshairi  ambaye
alichanganya ujuzi wa historia, maadili na utabiri. Afrika ya Magharibi , mtu
kama huyo aliitwa “griot”. Uswahilini kulikuwa na washairi wengi waliokuwa
viongozi wa fikra, na ambao wameendelea kuweko karne baada ya karne. Kitabu alichokihariri
Abdilatif Abdalla  na kuchapishwa na
shirika la Mkuki na Nyota, kiitwacho Kale ya Washairi wa Pemba: Kamange na Sarahani kina majina ya wachache kati
ya hao. Miongoni mwao wakiwemo Fumo Liyongo wa Bauri (Karne ya kumi na mbili);
Zahidi Mgumi (karne ya kumi na nne); Muyaka bin Haji; Sud bin Said Al-Maamiriy;
Kamange na Sarahani (wote ni karne ya kumi na tisa); na wengineo walioishi
katika karne ya ishirini.

Washairi kama hawa  walikuwa ni sauti ya jamii zao, na pia
watetezi wa haki. Ni muhimu kueleza hapa kwamba washairi-wasomi kama hao-  tangu
hizo zama za ustaarabu wa Misri, mpaka katika ustaarabu wa Waswahili – walitumia
lugha za jamii zao. Yaani wasomi wa kabla ya kuvamiwa na utawala wa kikoloni,
walikuwa wameshikamana na mizizi ya jamii zao.

Leo nataka kuzungumza, kwa ufupi tu, kuhusu
msomi Mwafrika wa zama zetu. Yaani msomi aliyekwenda shule za kisasa, na kupata
elimu yake kwa kupitia lugha za ulaya. Kuna nyuso mbili za msomi kama huyu,
ambazo zinapingana; na pia kuna  mihula
miwili iliyopita ambayo pia inapingana.

Wasomi Waafrika walioshiriki katika
mapambano dhidi ya ukoloni, walizichukua hazina zilizokuwamo kaika lugha za
kigeni, na wakazipeleka hazina hizo katika lugha za Afrika na kuzitajirisha. Katika nchi iliyoitwa Gold Coast
(ambayo leo inaitwa Ghana) kulichapishwa taarifa katika gazeti lililoitwa The Gold Coast People la tarehe 30
Novemba 1893. Taarifa hiyo iliwahimiza wasomi Wafante wa wakati huo kushukuru
kwamba ‘’Wafante wanaona fahari kuwa Wafante, na hawaoni aibu kujiita majina
yao ya kienyeji; wala kuzungumza kwa lugha zao; wala kuonekana wamevaa mavazi
ya kikwao.’’[1]  Badala
ya kuwa Waafrika-Wazungu, walitaka kuwa wasomi Waafrika wastaarabu.[2] Mawazo kama haya pia yalielezwa na
wasomi wa Afrika ya Kusini wa karne ya kumi na tisa. (Wasomi wa Lovedale n.k).
Hapa Afika ya Mashariki tuna mfano wa mshairi wa Tanzania, Shaaban Robert, na ule msemo wake maarufu, “Titi la mama li tamu, jingine halishi hamu.”

Baada ya Ghana kupata uhuru wake ,
mwaka 1957, Kwame Nkrumah hakuchelewa kuanzisha Kituo cha Lugha za Afrika. Na
vile vile akaanzisha magazeti ya lugha za Kiafrika. Katika hotuba yake ya ufunguzi wa
kongamano la kwanza la kimataifa la Wanataaluma wa Afrika lililofanyika Accra
mwaka 1962, Kwame Nkurumah alieleza matumaini yake kwamba kongamano hilo
litakuwa ni hatua muhimu kulifanya bara la Afrika kujithamini, na kuthamini
historia na utamaduni wake; na kwamba lugha za Afrika zitachukua nafasi muhimu.

Nkrumah alilirudia tena suala hilo
mwaka mmoja baadaye, alipokuwa akifungua taasisi ya Taaluma za Afrika ya
Kwanza. Kwake yeye , suala la taaluma na uendelezwaji wa lugha za Afrika
halikuwa ni suala la kuwekwa pembeni; bali aliamini kwamba lugha za Afrika ni
lazima zichukue nafasi ya kati, kwa sababu zilikuwa ni kiungo muhimu katika
taaluma, maendeleo na uhusiano wa Afrika na Waafrika wanaoishi nje ya Afrika.
Nkrumah hakutaka Afrika ijitenge kilugha na sehemu nyingine za dunia, kwani
aliijua nafasi na faida ya lugha nyingine za dunia kama vie Kiarabu,
Kiingereza, Kifaransa na Kireno.

Wakati ambapo watu wengine waliziona
lugha za Afrika kuwa ni duni katika pepo ya Kiingereza, Nkrumah aliziona lugha
za Afrika kuwa zina thamani na nafasi sawa na lugha nyingine duniani katika
kuijenga pepo ya pamoja. Kitu muhimu ni kwamba Nkrumah hakusema kwa maneno tu,
lakini alihakikisha kwamba kuna nyenzo za kufanyia kazi hiyo na kulitimiza
lengo hilo kwa vitendo. Lakini serikali za kijeshi zilizoipindua serikali ya Nkrumah
ziliibadilisha sera hiyo na huku baadhi ya Waghana wa tabaka la kati
wakishangilia. Waghana hao hawakutaka kuzuiliwa kuipanda ngazi ya kuwapeleka
kwenye pepo ya lugha ya Kiingereza.

Nchini Kenya, mapambano dhidi ya
ukoloni yalipelekea kuanzishwa kwa magazeti ya lugha za Kiafrika. Jomo Kenyatta
aliwahi kuwa mhariri wa gazeti mojawapo kama hilo, lililoitwa Muguithania. Baadaye aliandika kitabu
kwa Kikikuyu kiitwacho Kenya Bururi wa
Ngui;
yaani, Kenya, Nchi ya Migogoro. Hiki kilikuwa ni nyongeza ya kitabu
chake alichokiandika kwa Kiingereza, Facing Mount Kenya. Serikali ya
kikoloni ikayapiga marufuku magazeti hayo ya lugha za Kiafrika , na baadhi ya
wahariri wake wakalazimika kukimbilia uhamishoni na wengine wakafungwa jela.

Baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961,
Mwalimu Julius Nyerere akakifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa. Hatimaye,
Kiswahili kikawa na kwao. Naye akaonyesha mifano kwa vitendo. Baadhi ya hotuba
zake muhimu alizitoa kwa Kiswahili; na baadhi ya maandishi yake yakatafsiriwa kwa
Kiswahili. Na hata akazitafsiri kwa Kiswahili tamthilia mbili za William
Shakespeare-Julius Kaizari(Julius
Caesar), na Mabepari wa Venisi
(Merchants of Venice).

Wasomi kama hawa waliutumia ujuzi wao
wa Kiingereza kuzizidishia uwezo jamii zao tofauti kabisa na Waafrika wa tabaka
la kati la baada ya uhuru! Hawa ni wale ambao baadhi yao wameshika madaraka ya
serikali, na ambao wamekuwa ni mateka wa lugha za ulaya.

Miaka kadhaa iliyopita, nafikiri miaka
mitatu iliyopita, bunge la Kenya huru lilipiga kura kuzipiga marufuku lugha za
Kiafrika zisizungumzwe katika maeneo rasmi, kwa mfano maofisini. Kichekesho ni
kwamba bunge hilo halingekuwako kama si kwa sababu ya wafanyakazi na wakulima
wadogo wadogo wanaozungumza lugha hizo za Kiafrika kuingia msituni na
barabarani ili kupambana dhidi ya serikali ya kikoloni. Bila shaka bunge hilo
halikuona kwamba mizizi yake inatokana na lugha za Kiafrika, bali inatokana na
lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo za Ulaya. Sheria hiyo haijapitishwa kwa
sababu tu Rais hakuitia sahihi.

Lugha imekuwa ni medani ya mapambano ya
fikra. Lakini ninalotaka kulizungumzia hapa ni kwamba lugha ni uwanja wa
mapambano baina ya utumwa na harakati za kujikomboa na kujipa uwezo. Historia
ya lugha, ameandika Tom Paulin, mara nyingi huwa ni hadithi ya kutamalaki na
kupora; ni hadithi ya kuziteka ardhi na kuziweka katika mamlaka ya walioziteka;
au kuwalazimisha watu kufuata utamaduni fulani.[3]

 

Lugha, haidhuru iwe inatumiwa ndani au
nje ya maeneo ya taaluma, imekuwa ni uwanja wa vita –  katika hali zote  -baina ya
mtawala na mtawaliwa, hasa katika enzi za ukoloni. Katika hali kama hizo, lugha
imekuwa ni silaha ya kutamalaki au ni silaha ya kupinga kutamalakiwa, sawa na
silaha kama upanga. Kwa hakika, vita vikali zaidi vimepiganwa, na vinaendelea
kupiganwa katika eneo hili.

Mshairi mmoja wa Kiingereza, Spencer,
aliyeishi zama moja na Shakespeare, na ambaye aliandika kitabu maarufu, The Faerie Queen, aliueleza vizuri umuhimu
wa kutumia silaha ya lugha katika kutamalaki. Katika mwaka 1599, aliandika
kwamba, “imekuwa ni kawaida kwa anayetamalaki kuidharau lugha ya  anayemtamalakiwa na kumlazimisha kwa kila njia
huyo anayemtamalaki kujifunza lugha yake (mtamalaki).” Spencer aliyaandika
maneno haya katika kitabu chake A View of the Present State of Ireland. Katika kitabu hicho alitetea kupigwa marufuku
mfumo wa majina ya watu wa taifa la Ireland – kitendo ambacho lengo lake lilikuwa
ni kuzifuta kabisa kumbukumbu za taifa hilo. Udhibiti wa mfumo wa majina ya wananchi wa Ireland ulikuwa ni njia kuu iliyotumiwa na Waingereza kuitamalaki
Ireland.

Kama alivyoeleza Tiny Crowley katika
kitabu chake, War of Words: The Politics of Languages in Ireland 1537-2004, wavamizi mbalimbali wa Ufalme wa
Uingereza walipitisha sheria kadhaa zilizokuwa na madhumuni ya kuilinda lugha ya
Kiingereza isiingiliwe na kuathiriwa na lugha ya Ki-Ireland, Ki-Gaeli (Gaelic).
Moja ya mfululizo wa sheria hizo ni sheria ya Kilkenny ya mwaka 1369, baada ya
Uingereza kuiteka na kuikalia Ireland. Kwa mfano, amri mojawapo ya sheria hiyo
ilitishia kwamba serikali itamnyang’anya ardhi yake Mwingereza yeyote au
mwananchi yeyote wa Ireland ambaye atazungumza na mwenzake kwa lugha ya kwao,
kinyume na sheria hiyo.[4]
Kwa hiyo Spencer aliyaandika maneno yake hayo kutokana na sheria hiyo, ambayo
inaonyesha haikufaulu kama ilivyotarajiwa. Kwani kama ingekuwa na athari
yoyote, Spencer asingekuwa na haja ya kutaka sheria hiyo itekelezwe baada ya
zaidi ya miaka mia mbili kupita.Yeye Spencer mwenyewe alikuwa ni
Mwingereza mlowezi (au setla) katika sehemu ya Munster. Mmojawapo wa majirani
zake alikuwa ni mlowezi mwenzake kutoka Uingereza, Walter Raleigh-ambaye ndiye
aliyeanzisha makao ya walowezi Virginia, Amerika.

Inawezekana kwamba hakukuwako na
uhusiano wa moja kwa moja baina ya yaliyotokea Ireland wakati huo na yale
yaliyowakumba Waafrika waliochukuliwa kwa nguvu kutoka Afrika na kwenda
kufanywa watumwa katika mashamba ya Marekani yaliyomilikiwa na walowezi
waliokuja baada ya kina Walter Raleigh. Hata hivyo, katika mashamba hayo
Waafrika waliotiwa utumwani hawakuruhusiwa kuzungumza kwa lugha zao. Hata
mawasiliano ya kutumia ngoma pia yalikatazwa. Vilevile, hawakuwa na ruhusa ya
kutumia majina yao ya Kiafrika. Na Waafrika waliopatikana wakizungumza lugha
zao waliadhibiwa na hata wengine kuuliwa. Lengo la yote hayo lilikuwa ni lile
lile: kuwasahaulisha uhusiano wao na kwao walikotoka.

Japan nayo ilifanya kama hivyo baada ya
kuitamalaki Korea: iliwalazimisha Wakorea kutumia lugha ya Kijapani na mfumo w
Kijapani wa kupeana majina. Sera hiyo ilitupiliwa mbali baada ya Japani
kushindwa vita ya pili ya dunia. Lakini athari ya sera hiyo ingali ipo: Mpaka
hivi karibuni, ndani ya Japan kwenyewe, wenye asili ya Korea walilazimika kuwa
na majina ya Kijapani. (Shahidi wa hili ni Esther W. Dungumano, Mkurugenzi wa
uhusiano wa kimataifa wa Chuo hiki cha Dar es Salaam. Yeye anakichapa Kijapani kama yuko Tokyo!)

Katika bara la Afrika, baada ya
kulivamia na kulitamalaki, Wafaransa, Waingereza na Wareno, walifuata sera kama
hizo. Ingawa wakoloni hao hawakuzipiga marufuku lugha za Kiafrika, lakini
waliziteremshia hadhi yake ya kuwa lugha zenye uwezo, maarifa na kuwa ni
kitambulisho cha wenye lugha hizo. Hata kama waliziruhusu lugha hizo kutumiwa
katika mfumo wa elimu, ilikuwa ni katika hatua za mwanzo mwanzo tu kabla ya
wanafunzi kugeuzwa na kuwa wasemaji wa Kiingereza au Kifaransa. Siijui sheria
yeyote ya utawala wa kikoloni iliyopiga marufuku majina ya Kiafrika. lakini kutokana
na athari za mamlaka ya kiutamaduni, karibu kila Mwafrika aliyepata elimu ya
kisiasa ameliambatanisha jina la kizungu katika jina lake la kiafrika. Sera za
kikoloni kuhusu lugha zilikuwa zinaendeleza sera za vita ya kutamalaki kwa
kutumia mbinu za kilugha.

Kulikuwa na muingereza mmoja: jina lae
ni Macauley. Yeye alikuwa ameajiriwa  katika kampuni ya British East India ambayo ndiyo ilikuwa inatawala India. Yeye ndiye
aliyependekeza sera za kutumia kiingereza kwa kuwasomesha  badala ya kihindi au Sanskrit .Yeye alisema “lazima
tuwe na kikundi cha wahindi ambao kwa rangi ya ngozi ni Wahindi lakini kwa
akili ni Waingereza. Kikundi hiki kitakuwa kati yetu  na umma tunaoutawala.” Fikra kama hizi ndizo
zilipelekwa kwa makoloni mengine ya waingereza. Kikundi au tabaka ambalo kwa
ngozi ni Waafrika, kwa ubongo ni Waingereza.

Bara la Afrika linaendelea kuteseka na
kudhalilika kutokana na kutamalakiwa kilugha. Uhuru wa kisiasa tulioupata labda
umeikomboa miili yetu tu, lakini haukuzikomboa bongo zetu. Na hayo ndiyo
matokeo ya kutamalakiwa kilugha kwa muda mrefu.

Kutokana na hali hiyo, hivi leo bara la
Afrika kuna mgawanyiko mkubwa baina ya Waafrika wenye elimu wa tabaka la
kati  na Waafrika wengine kwa jumla. Na
hilo ndilo lengo la ukoloni. Tukiurudia ule mfano tuliotoa wa kwamba lugha ni silaha
ya kivita – imekuwa ni kana kwamba majemedari waafrika wameshikwa mateka katika
kambi ya adui. Na nisemapo “Majemedari”, simaanishi serikali zetu tu; bali
ninamaanisha tabaka zima la wasomi. Na hakuna hata mmoja katika sisi anayeweza
kujigamba kwamba hakuathirika na huko kukubali kushindwa kwetu au kuendesha
maisha yetu kisomi na kitaaluma na huku tukiendelea kuwa mateka.

Kwa sababu hiyo ya kuwa sisi ni mateka
tunalazimishwa kulitazama bara la Afrika kama kwamba sisi ni wageni hapa. Nyanja
kadha wa kadha za elimu yetu kuhusu Afrika zimejikita katika ule mfumo wa
kikoloni wa aliyeko nje akiangalia ndani. Tunakusanya elimu  na maarifa mengine ya humu barani Afrika  na kwa msaada wa waafrika wenyeji, halafu
tunaficha elimu na maarifa hayo katika lugha ya Ulaya kwa faida ya wale tu
wanaofahamu lugha hiyo. Yaani tunaendelea kuvikusanya vito vya thamani vya
kisomi na kuviweka katika majumba ya makumbusho (Archives) ya lugha ya Ulaya. Jamii
ya wasomi Waafrika – walioko nje na ndani ya bara la Afrika – wamesalimu amri na
wamekubali hali hii kwamba ni hali ya kawaida.

Mwezi Septemba mwaka jana, kulikuwa
na kongamano kubwa mjini Leeds Uingereza. Kongamano hilo lilihudhuriwa na zaidi
ya wataalam mia tano kutoka Afrika na Ulaya. Nikawauliza wataalam waliohudhuria: Ni wangapi kati yao waliandika angalau
kitabu kimoja tu kwa lugha yeyote ya kiafrika? Hakuna hata mmoja aliyeinua
mkono! Je, aliyeandika nakala moja tu kwa lugha ya Kiafrika? Hakuna hata mmoja
aliyeinua mkono! Je, aliyeandika ukurasa mmoja tu kwa lugha za Kiafrika? Hapo ikainuliwa
mikono mitatu! Mikono mitatu tu!! – katika kongamano kubwa kama hilo
lililohudhuriwa na wasomi na wataalamu wa kiwango cha juu wanaojishughulisha na
taaluma za bara la Afrika. Niliuliza maswali kama hayo nchini
Nigeria, Kenya, Zambia, Ghana mbele ya hadhira ya Waafrika mashuhuri. Matokeo
hayakuwa tofauti na haya!

Labda hoja yangu itaeleweka vizuri
zaidi lau tutaliuliza swali hilo kwa namna tofauti: Unaweza kumfikiria Profesa
wa Historia au Utamaduni wa Italia, ambaye hafahamu hata neno moja la
Kitaliani? Au Profesa wa Historia ya Ufaransa asiyejua Kifaransa. Au Profesa wa
Kigiriki au Kilatini ambaye hazifahamu lugha hizo? Bila shaka utajibu kwamba
hilo si jambo la kawaida. Lakini inapohusu taaluma za Afrika, hali hiyo
imegeuzwa na kuwa ya kawaida. Huu ni mzaha, kama si upumbavu! Bara kubwa kabisa
duniani – kubwa kuliko mabara ya Ulaya, Amerika na China yakikusanywa
pamoja – kutendewa hivi!

Hali hii ni lazima ibadilishwe. Na hili
litawezekana tu iwapo kutakuwako na ushirikiano baina ya asasi za
taaluma-  ambazo zitakubali na zitakuwa tayari kufuata mbinu tofauti za kutafutia
elimu; na wachapishaji – ambao watakubali kuwa na mikakati tofauti ya
uchapishaji; na wasomi ambao watakuwa tayari kuzidisha juhudi zao ili
kulifanikisha lengo hili.

Lakini kuna  mshirika mwingine ambaye ni muhimu pia. Naye
ni serikali; serikali zenye sera za kuliendeleza na kuzikuza lugha za Afrika.
Tusisahau kwamba wanaoziendesha serikali hizo, wao wenyewe wamefinyangwa na
asasi za kitaaluma. Labda kama wakati walipokuwa wanafunzi misimamo yao ya
kuendesha serikali ingekuwa imekabiliwa na changamoto, huenda wangeibuka kuwa
majemedari walio tayari kuongoza wakiwa ni watu huru wanaotaka kutafuta mbinu
nyingine za kupigana na kuelewa, badala ya kuwa ni mateka. Lakini hakuna
mabadiliko makubwa yanayoweza kupatikana ikiwa serikali zinashinikizwa kufanya
shughuli zake bila ya kutoka nje ya mipaka iliyowekwa na wanaotamalaki.

Kuna dalili chache za matumaini ya
kwamba mambo huenda yanabadilika, na kwamba Kiswahili kiko mstari wa mbele.
Kufaulu kwa Kiswahili nchini Tanzania ni matokeo ya wasomi wa aina ya kwanza
tuliowataja; yaani wale waliochukua kutoka lugha za Ulaya kile walichoweza, na
kukihifadhi katika lugha za Afrika. Tumeshamtaja Mwalimu Julius Nyerere. Kama
tunavyojua, yeye alihitimu katika vyuo vikuu viwili maarufu vya wakati wake – Makerere
na Edinburgh. Aliposhika uongozi wa taifa hili, aliweka sera  – kwa nadharia na
kwa vitendo – za kukipa Kiswahili hadhi na uwezo.[5]
Urithi mkubwa wa Nyerere ni wa lugha; kutuachia mfano wa kuonyesha bila shaka
kwamba lugha za Kiafrika zina uwezo  wa
kukua na kukuza fikra kama lugha zingine za dunia. Heshima tunayoweza
kumkumbuka nayo ni kukiendeleza na kukikuza Kiswahili mpaka kiwe moja  ya lugha za dunia.

Pia jambo la kushangaza kuona kwamba
Tanzania imezaa shirika la uchapishaji la Walter Bgoya [kama] shirika la Henry
Chakava, East African Educational Publishers, ambalo limekuwa na msimamo wa
kuchapisha vitabu kwa lugha za Afrika, zaidi maandishi ya Kiswahili ya kiwango
cha juu. Shirika hilo ni Mkuki na Nyota la nalo limechapisha tafsiri za
Kiswahili za vitabu vya karibu waandishi wote maarufu wa Afrika, ambavyo
viliandikwa kwa Kiingereza na Kifaransa.

Lakini, je, asasi za taaluma kwa ujumla
zinafuata nyayo hizi? Hata hapa kuna dalili za matumaini:
Hatua ndogo, ingawa yenye athari kubwa, imechukuliwa katika uwanja wa falsafa
kutokana na kuchapishwa kitabu kinachoitwa Listening to Ourselves, ambacho kimehaririwa na msomi mwenye asili mchanganyiko wa
Carribea na Kanada, anayeitwa Chike Jeffers (Kimechapishwa na State University of  New York ( SUNY)). Kitabu chenyewe ni
mkusanyiko wa insha kuhusu falsafa  ambazo zimeandikwa kwa lugha mbalimbali za
Afrika ya Mashariki na Afrika Magharibi -kwa mfano, Kiwolof, Kijaluo, Kiigbo,
Kiakan, Kikikuyu – na tafsiri zake kwa Kiingereza. Waandishi wa insha hizo, miongoni
mwao akiwemo hayati Emmanuel Eze, ni wanataaluma Waafrika maarufu
wanaoshughulika na falsafa; na ambao wanashikilia nyadhifa za uprofesa katika
vyuo vikuu vya nje ya Afrika. Hii ni mara yangu ya kwanza kuona maandishi kwa
lugha za Afrika, yaliyoandikwa na wanafalsafa wa zama zetu.

Msomi mwenye asili ya Carribea amelifanyia
bara la Afrika jambo ambalo ni la kwanza kufanywa. Kwa kufanywa jambo kama
hili, Jeffers ameingia katika orodha ndefu ya Wacarribea wenziwe waliolifanyia
kazi bara la Afrika; kwa mfano, Marcus Garvey, CLR James, George Padmore, W.E.
Du Bois, Walter Rodney, kwa kuwataja wachache tu.

Kitabu hiki cha Jaffers kinatukumbusha
lugha nyingine, ambayo haijatumiwa kwa mapana yake katika kuzipa uwezo lugha za
Afrika. Lugha yenyewe ni Tafsiri. Katika kitabu changu, Something Torn and New, nimeeleza kwamba tafsiri ni lugha ya lugha
mbalimbali. Hakuna utamaduni hata mmoja duniani ambao haukufaidika na tafsiri.
Kwa hivyo, hapana shaka kwamba tafsiri baina ya lugha za Afrika zenyewe kwa
zenyewe, na tafsiri baina ya lugha za Afrika na lugha nyingine za dunia,
zitazifaidisha tamaduni za Afrika na tamaduni nyingine za dunia. Vyuo vyetu vinapaswa
kuwa ni viwanda vya shughuli za kutafsiri maandishi ya lugha za kigeni kwa
lugha zetu Afrika.

Lakini mambo haya yanahitaji mshikamano
na ushirikiano mkubwa baina ya wasomi, wanataaluma, wachapishaji na
wanaotayarisha sera za elimu. Wasomi, walioko ndani na nje ya Afrika, ni lazima
waongoze njia na kushika nafasi zao za heshima za tangu jadi. Katika tamaduni
na historia zote za dunia, msomi amekuwa ni msaka njia. Na katika tamaduni
zote, wasomi kama hawa imewabidi kulipa bei ghali, wakati mwingine hata kwa
kupoteza roho zao. Na mimi nimelipa-  ingawa si malipo makubwa hivyo. Lakini
nimelipa; kufungwa gerezani, na hata kulazimika kuishi uhamishoni. Wasomi wa zama zetu wasiyakimbie mapambano.
Wasiukimbie uwanja wa vita.

 

Lakini  serikali na asasi zetu nyingine nazo ziache
kuvizika vichwa vyao kwenye mashimo ya huu unaoitwa utandawazi. Utandawazi
ulianza tangu karne ya kumi na saba wakati mwili wa Mwafrika ulipolazimishwa
kufanya kazi ya kitumwa katika mashamba. Na kazi hiyo ya kitumwa ikapelekea
kwenye utumwa wa kikoloni. Hivi leo, utandawazi unategemea maliasili ambayo
bado yanapatikana katika bara kubwa kabisa duniani-  Afrika. Serikali zetu
nyingi, na wanataaluma na wasomi wetu wengi, wanaishi katika njozi kwa
kufikiria. Kwamba ili kuishi katika tandawazi, ni lazima wapotelee kwenye lugha
ya Kiingereza.

Watu kama hao inawabidi waukumbuke
ukweli huu: Wao walitupa lafudhi ya Kiingereza; na sisi tukawapa njia ya
kutuingilia katika bara letu (They gave
us accent, We gave them access
). Katika karne za kumi na saba na kumi na
nane, waliuchukua mwili wa Mwafrika. Katika karne ya kumi na tisa na ishirini
walipata njia ya kuchukua shaba yetu, dhahabu yetu, almasi yetu; na sasa mafuta
yetu. Hivi leo, wakati ambapo tumeshughulika na kuzifanya lafudhi zetu za
Kiingereza kuwa bora zaidi za kupora mali ya bara letu.

Tusipoteze wakati wetu na nyenzo zetu
kwa kujibidiisha kuboresha lafudhi zetu za Kiingereza. Badala yake tutumie wakati
wetu mwingi zaidi na nyenzo tulizonazo, ili kuulinda utajiri wa Afrika kwa kila
hali. Lugha ni silaha ya kivita.

Tuyakumbuke maneno ya Shaaban Robert:
Titi la Mama li tamu, jingine haliishi hamu.

Tuseme hivi: ukijua lugha zote za
dunia, na hujui ya mama, wewe u mtumwa; umewezwa. Lakini ukijua lugha ya mama
na kuiongezea lugha za dunia, wewe wajiweza, yani umejiongezea uwezo. Lazima
tuchague baina ya kujiweza na kuwezwa na natumai Afrika itajichagulia kujiweza
badala ya kuwezwa.

Ahsante sana kwa kunisikiliza.

 


[1]
David Kimble, A Political History of Ghana, Oxford, 1963, uk. 518.

[2]
A.G.Hoplins, “R.B.Blaize: Merchant Prince of West Africa”, Tarikh, vol.1,
no.2, 1966.

[3]
Tazama kitabu chake, Empires of the World.

[4]
Tiny Crowley, War of Words: The Politics of Language in Ireland-1537-2004

[5]
Baadhi ya watu wana fikra ya kwamba lugha ya taifa inaweza kujengwa tu juu
ya makaburi ya lugha nyingine za Afrika.
Kuwa na lugha moja tu ya taifa kumelinganishwa na dhana ya ki-Ulaya ya
taifa-dhana ambayo ilibuniwa katika karne ya kumi na saba, mwanzoni mwa ubepari
wa kisasa na ukoloni.