Kutoka 1995 Kuelekea 2015
“Ukitulia vizuri ukaangalia mbele na nyuma utaona kwamba katika jamii yetu tuna tabia ya kuchukia watu wenye uwezo, hasa wa kiakili. Tangu tukiwa mashuleni watu wanaonyesha uwezo mkubwa darasani na wanaofanya sana bidii huwa wanachukiwa na kutengwa. Hilo linaendelea hadi katika jamii na linajionyesha waziwazi pale ambapo huwa tunajikuta tunachagua bora viongozi na kuwaacha wale wanaoonekana wana uwezo. Mtu anayeonekana ana uwezo atapigwa vita kila kona hadi ‘aishe’ kisiasa. Ni nadra katika jamii yetu mtu mwenye uwezo sawasawa akapenya katika uongozi. Ndivyo alivyokwama SAS [Salim Ahmed Salim], na ndilo jambo analohangaika nalo ZZK [Zitto Zuberi Kabwe] na yeye amekuwa na ngozi nzito kweli kweli!!” – Dakta Kitila Mkumbo, 19 Machi 2013
Chambi Chachage
Wale wanaosahau yaliyopita wamehukumiwa kuyarudia.
Hayo si maneno yangu, ni ya mchambuzi mmoja mahiri. Japo aliyasema zamani
bado yanatulenga sisi leo.
Yaliyotokea kati ya mwaka 1993 na 1995 yanafanana na
yanayotokea sasa kati ya 2013 na 2015. Hebu tujikumbushe. Baada ya Tanzania
kuurejesha mfumo wa vyama vingi, nyota ya kisiasa ya Augustine Lyatonga Mrema
ilianza kung’aa kwa kasi ya ajabu. Wivu ulitanda ndani ya chama tawala.
Wananchi walionekana kumkubali sana hasa alipokea akitoa siku 7 za utekelezaji
wa maazimio yake dhidi ya uhalifu na wahalifu.
Rais Ali Hassan Mwinyi alimpa rungu pale alipounda nafasi ambayo haikuwepo kabla, yaani Unaibu Waziri Mkuu. Mrema akapachikwa jina
la ‘Fagio la Chuma’, la kufagia takataka zote za ufisadi nchini. Wapinzani wake
wakadai yote ni kiini macho, wengine wakadiriki kusema hata anatumia hizo siku
7 za vitisho kudai rushwa.
Hakika Mrema alibobea katika kile ambacho wachambuzi
wa masuala ya kisiasa wanakiita ‘populism’, wakimaanisha siasa ya kukong’a
nyoyo za watu kiasi kwamba hata wengine wanakuwa wafuasi wako tu bila kutafakari wewe
ni nani na unasimamia nini hasa.
Nakumbuka enzi hizo nikiwa mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari Azania kuna siku tuliambiwa twende kwenye viwanja vya Jangwani kuhudhuria tukio
kubwa la Kiserikali. Wakati viongozi wengine wakiwa ndani ya magari yao yaliyojulikana kama ‘mashangingi’ wakikodoa macho nje, Mrema alikuwa akitembea kwa miguu huku amezungukwa na watu wa kawaida na wanafunzi.
Huyo ndiye alikuwa Mrema wa kuelekea 1995.
Alipotofautiana na wenzake kwenye serikali ya chama tawala, akalazimika kutoka
na kuingia kwenye upinzani. Japo wapo waliodai kuwa alitumwa kwenda kuvunja
upinzani, tulichokiona ni hali ya kuweweseka ambapo ilibidi muasisi wa chama
tawala, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aingie dimbani kujaribu kutafuta ‘mgombea
safi’ ambaye angalau ataweza kuikoa nchi kutoka katika janga la kitaifa la ufisadi na
kukabiliana na mpinzani wao mkuu. Kwa taabu sana Benjamin William Mkapa
akamshinda Mrema.
Kilichofuata baada ya 1995 ni kudidimia kwa kilichokuwa
chama kikuu cha upinzani. Hali ilikuwa tate na tete kwenye mkutano wa chama hicho mjini
Tanga ambapo taa zilipozimwa, vurugu kubwa ilitokea. Mtafaruku huo ulisababisha
na kupelekea uwepo wa kambi ya Mrema na ya Mabere Marando. Mwisho wa siku wote
waliondoka chamani.
Wapo wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanaodai kuwa kila
uchaguzi mkuu unapokaribia chama kilicho kikuu cha upinzani kinahujumiwa na
chama kingine kinapandishwa. Kwa mantiki yao, 1995 chama cha upinzani
kilichokuwa kwenye chati ni NCCR-Mageuzi
ila ilipofika 2000 ikawa ni CUF. Mantiki hiyo inaendelea kudai hicho nacho
kikahujumiwa 2005 na hivyo kupelekea kupanda kwa CHADEMA mwaka 2010.
Mgogoro unaondelea sasa ndani ya CHADEMA unaonekana,
kwa mantiki, hiyo kuwa ni sehemu ya kutekeleza mlolongo huo wa kuhujumu chama
kikuu cha upinzani kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Safari hii shutuma hizo zimelengwa
kwa mwanasiasa machachari mwenye mvuto na ushawishi mkubwa, Zitto Zuberi Kabwe.
Sasa glovu zimevuliwa na pambano kati ya wapinzani wa“mwanasiasa huyu nguli“,
kama rafiki yake Dakta Kitila Mkumbo anavyomtambulisha, liko wazi baada ya
kufichwafichwa kwa maneno ya kisiasa kuwa ‘Hakuna Mgogoro wowte CHADEMA’.
Mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya Jamii – Twitter, Facebook, Jamii Forum, Mwananchi News n.k. – inadhihirisha kuwa Zitto anakubalika sana
miongoni mwa vijana na wanaharakati walioko kwenye asasi huru za kiraia (NGOs/CSOs). Kwa wengi
wao anaonekana ni mkweli na mzalendo anayeweka maslahi ya taifa mbele kuliko
maslahi yake binafsi na ya chama chake. Pia kuna makundi ya vijana wasomi,
wakiwemo wale waliopoteza na walioanza kupoteza imani naye kutokana na sakata la DOWANS na
suala la Kamati ya Madini aliyounda Rais Jakaya Mrisho Kikwete (Kamati ya BOMANI), ambayo sasa
yemerudisha/yanarudisha imani yao kwa mwanasiasa huyu hasa baada ya kukataa posho na kuanza kuongoza vita dhidi ya posho pamoja na kusimamia kidete harakati za kurejesha mabilioni ya fedha zilizofichwa Uswizi na kwingineko.
Tatizo kubwa ni kuwa makundi yaliyopo CHADEMA nayo kwa
kiasi kikubwa yanaakisiwa katika makundi haya ambayo yanajumuisha vijana ambao
wanadai hawana chama ila ni wazalendo. Kwa kiasi fulani hali ya zile siasa za
‘populism’ inajionyesha ndani na nje ya chama kikuu cha upinzani hivyo hata kusababisha iwe vigumu kupata uchambuzi
ambao ni huru.
Jambo hili linasikitisha hasa ukizingatia kuwa jamii yetu inawategemea vijana walio kwenye asasi huru za kiraia na vyuo vikuu pamoja na
wahitimu wake walio kwenye sekta binafsi, wawe tayari kuweka pembeni siasa za
kishabiki/kinazi na kuchambua masuala haya kwa uwazi na uhuru bili kujali kama
mtu au watu wao ndio wanahusika.
Inasikitisha pale unapoona vijana wasomi/wanazuoni wakitoa misimamo na
maneno ya kishabiki hata kabla ya kusoma kwa undani tamko la Zitto na la Kitila,
kuyalinganisha na tamko la Kamati Kuu ya CHADEMA kama lilivyosomwa na
mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Antiphas Lissu. Vijana hao, wakiwemo wale
walio kwenye yale yanayoitwa ‘Think Tanks’ (Taasisi za Tafakuri), watatusaidia
sana kama watafanya uchambuzi wa kina wa matamko kama hayo na kuyalinganisha,
kwa mfano, na makala/maelezo/matamko mbalimbali ya zamani pamoja na mahojiano ya zaidi ya masaa 7 ambayo Zitto aliyafanya na Jamii Forum. Kwa kuwa Zitto na Kitila
wamehusishwa na wamekiri/wamedhihirisha kuhusiana, ingekuwa vyema pia kama watalaamau wetu wangefanya
uchambuzi wa maandishi ya Kitila katika mtandao wa Mabadiliko na wa Jamii Forum
na kutusaidia kuelewa kwa upana huo unaoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013 na hata ile iitwayo Ripoti ya Siri Juu ya Zitto Kabwe ambao nao unalitaja jina la Kitila.
Mpaka dakika hii pia sijaona vijana hao waliobobea,
walau kishahada, katika tasnia ya uchambuzi wa kisiasa, wakichambua kwa kina, kwa mfano,
kuingia ulingoni kwa mwanasheria aliyebobea, Lissu, kwenye pambano hilo dhidi
ya Zitto, jambo ambalo halijawahi kutokea waziwazi. Hata kitendo cha Kitila
kuipiga dongo Kamati Kuu ya CHADEMA kuhusu kile ambacho anakiita ni (pengine)
kupitiwa kwa kamati hiyo kinastahili uchambuzi wa kisiasa na si wa kisheria tu.
Kwa kudai kuwa Kamati hiyo ambayo ina wanasheria nguli
imemvua ujumbe wa Kamati Kuu ya Chama ilhali haina mamlaka hayo ambayo ni ya Baraza Kuu, moja kwa moja
Kitila anaigeuzia kibao kile kile ilichokitumia kuwapiga wao, yaani kuvunja Katiba
ya chama. Lakini pia inaonyesha utayari wa kupambana na mwanasheria Lissu
ambayo kwa wale tunaomjua, inahitaji kazi ya ziada hasa kama amejipanga na
ushahidi.
Pia suala la kuingia ulingoni kwa Mwanasheria Alberto Msandoambaye naye ni mwana-CHADEMA tena ni kiongozi katika ngazi ya udiwani
tena huko huko kwenye kanda ambayo inadaiwa kuhodhi uongozi wa CHADEMA nalo
linastahili uchambuzi yakinifu (rejea hizi salamu zake kwa Zitto na Godbless Lema). Je, huu ndio mwanzo wa kujitokeza waziwazi kwa
kundi ambalo mwanasheria Nyaronyo Mwita
Kicheere analiita “chadema yenye watu wenye fikra pevu”? Na, je, wachambuzi wetu waliochukua upande nao ni miongoni mwao? Kama ndio, wanaweza/wataweza kweli kufanya uchambuzi mpevu au watabakia kuwa wanatimu/mashabiki ambao msimamo wao unatabirika hata kabla hawajafungua mdomo kuongea au kuchukua kalamu kuandika?
Mimi binafsi uwezo wangu wa kuchambua masuala haya
unafungwa kwa kiasi kikubwa na mgogoro wa maslahi (conflict of interest) n.k.
Pengine wachambuzi wetu mahiri nao wana migogoro hiyo na labda ndio maana
wengine wameamua kuwa waumini wa ushabiki tu wa kisiasa (populism) au/na wajumbe wa timu za wahusika.
Kama ni hivyo, basi makala haya hayawahusu.
Ila kwa wale ambao hawana mgogoro na wasiofungamana na upande wowote, jamii iliyowalea na kuwasomesha inawadai wairudishie walau
kitu kimoja – uchambuzi huru wa hali ya kisiasa na wanasiasa Tanzania kutoka
1995 kuelekea 2015 kwa maana safari hii wananchi tunahitaji kufanya uchaguzi sahihi.



