WASOMI KAENI PEMBENI, WANYONGE SHIKENI HATAMU!

 

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

 

Katika
makala yangu ya juma lililopita, nilifafanua chimbuko la itikadi ya Umajumui wa
Afrika na kubainisha kuwa ndiyo inayopaswa kuongoza mapambano ya wanyonge.
Makala yaliishia kwa kuwahamasisha wanyonge wote wa Afrika kuungana na
kupambana kwa pamoja bila kujali dini zao au makabila yao, vyama vyao au kazi
zao, maeneo yao au nchi zao, jinsia zao au umri wao. Kwa kufanya hivyo
hawatakuwa na cha kupoteza isipokuwa minyororo yao, minyororo inayowafanya
waendelee kuwa mafukara huku jasho lao na rasilimali zao zikiwatajirisha
mabeberu wa nje pamoja na mawakala wao wa humu ndani.

 

Lakini
je, wanyonge wataungana vipi? Na ni nani wa kuchukua jukumu hilo la
kuwaunganisha wanyonge ili wapambane na mfumo dhalimu wa ubepari, ambao kwa
sasa umechukua sura ya uliberali mambo-leo? Makala ya juma hili yamelenga
kujibu maswali hayo.

 

Ni jukumu la wasomi

Kama
nilivyoelezea juma lililopita, kati ya silaha za thamani ambazo wanyonge
waliporwa mara baada ya uhuru ni itikadi ya Umajumui wa Afrika. Itikadi hii
iliondolewa mikononi mwa wanyonge na kuwekwa mikononi mwa watawala. Na watawala
wengi hawakuwa tayari kusalimisha mamlaka ya nchi zao ili kuunda dola la
Muungano la Afrika kwa sababu mamlaka ya kidola ndiyo yaliyowapa fursa za
kuishi katika anasa za kitajiri pamoja na kuwatumikia mabeberu.

 

Kwa
hiyo, si ajabu kwamba viongozi wenye mtazamo wa kimajumui waligeukia makundi
mbadala katika jamii zao na kuwapatia jukumu la kuongoza harakati za kujenga
umajumui wa Afrika. Kwa upande wa Nkrumah, pamoja na kuendelea kuwashawishi
viongozi walioingia madarakani, alivigeukia pia vyama vya wafanyakazi na
taasisi nyingine zilizowaunganisha wananchi, na kuvihamasisha kuongoza juhudi
za kuiunganisha Afrika.

 

Nyerere
pia, hasa baada ya mwaka 1965, aliona kuwa kundi pekee lenye uwezo wa kuongoza
juhudi za kuubadili uzalendo/utaifa (nationalism)
kuwa Umajumui wa Afrika (pan-Africanism)
ni kundi la wanazuoni, na hasa wanafunzi na walimu wa vyuo vikuu. Hii ni kwa
sababu wao wana muda wa kutosha kufanya uchambuzi kwani hawabanwi na shughuli
za uzalishajimali ama utawala.

 

Lakini
pia ni kwa sababu vyuo vikuu, kwa tafsiri ya Nyerere, ni vitovu vya mijadala,
tafiti na maandiko, ambayo huwafanya wasomi “wasimame katika kweli kama
wanavyoiona, bila kujali yale yatakayowatokea wao binafsi”. Ndio maana pia
Mwalimu alikipenda sana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani), ambapo
alikwenda mara kwa mara kushiriki katika mijadala na wasomi.

 

Lakini wasomi ni sehemu ya unyonyaji

Mwalimu
aliwakabidhi wasomi mikoba ya kuongoza mapambano ya Kimajumui tarehe 13 Julai
1966 alipotoa hotuba katika uzinduzi wa Chuo Kikuu cha Zambia. Lakini mwezi
Oktoba 1966, Mwalimu alikumbana na maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam wakipinga kulazimishwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa miaka miwili, huku
wakipokea asilimia 40 tu ya mishahara yao. Asilimia 60 zingekuwa ni mchango wao
katika ujenzi wa taifa.

Katika
tukio hilo, Mwalimu aliukata mshahara wake kwa asilimia 20 na kisha kuwaambia
wanafunzi:

 

 Mamishahara
ya anasa haya ndiyo yaliyojenga kasumba hii kwa wasomi, wote! Mimi na ninyi. Sote tumo katika tabaka la juu la wanyonyaji… Kila mmoja katika nchi hii
anadai hisa yake. Kila mmoja isipokuwa mkulima maskini. Atadaije? Hajui lugha
hiyo… Ni nchi ya aina gani hii tunayoijenga?

 

Katika
kutafakari nukuu hiyo ya Mwalimu, tunaweza kujiuliza swali moja: kama Mwalimu
alijua kuwa wasomi, kama walivyo watawala, ni sehemu ya wanyonyaji, je, kwa nini
aliwakabidhi jukumu adhimu la kupigania Umajumui wa Afrika na kuongoza
mapambano ya wanyonge?

 

Ndipo likaja Azimio

Ifahamike
kwamba maandamano yale ya wanafunzi yalimfanya Mwalimu autafakari mfumo mzima
wa nchi yetu, kitu kilichomfanya agundue jinsi wanyonge (wakulima na
wafanyakazi wa ngazi za chini) walivyokuwa wamesahaulika katika nchi hii. Ili
kurejesha matumaini ya wanyonge ndipo Mwalimu akaja na Azimio la Arusha ambalo
ndilo  lingekuwa silaha ya wanyonge dhidi
ya wanyonyaji na waporaji wa ndani na nje ya nchi. Lakini Azimio lenyewe pia,
kama ilivyotokea katika itikadi ya Umajumui wa Afrika, lilikabidhiwa kwa
watawala ili walitekeleze. Hawa, kwa kushirikiana na mabeberu, walitumia kila
mbinu kulihujumu na hatimaye kulizika. Pengine nikipata wasaa huko mbeleni
nitaandika kwa kirefu juu ya Azimio na jinsi lilivyohujumiwa na hatimaye
kuuawa.

 

Hebu
turejee kwa Mwalimu na wasomi. Mwalimu alichukua hatua madhubuti ya kuubadili
mfumo wa elimu ili uendane na siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Aliwahimiza wasomi
kuutumikia umma bila kudai malipo ya ziada. Fedha za kuwasomesha zililipwa na
wanyonge, hivyo wasomi walipaswa kuwatumikia wanyonge kwa uadilifu mkubwa na
kupigania maslahi ya wanyonge.

 

Kwa
upande wa walimu, wao walikuwa na nafasi ya pekee ya kuleta mapinduzi katika nchi hii.
Akihutubia mkutano wa walimu toka nchi nzima mwaka 1969, Mwalimu aliwasihi
walimu kuzalisha wanamapinduzi na sio vimashine. Kipimo cha utumishi wao
kingekuwa ni vijana wenye kujiamini, wanaokataa unyonyaji, dhuluma na
ukandamizwaji; vijana wapigania usawa na wanaofanya kazi kwa bidii na maarifa
ili kukabiliana na changamoto zinazowakumba wao na jamii nzima. Mwalimu
aliwataka walimu kuachana na kasumba ya kikoloni ambayo ilikuwa ikipima usomi
wa mtu kwa kutumia karatasi (vyeti), kiasi kwamba mtu asipopata cheti hajioni
kama amesoma.

 

“Wasomi mmetusaliti”

Je,
wasomi wametimiza jukumu hilo la kuongoza mapambano ya wanyonge? Katika makala
yangu ya wiki jana, wasomaji walionitumia maoni walilalamika kuwa sisi wasomi
tumewasaliti wanyonge kama ilivyo kwa wanasiasa. Nitanukuu ujumbe kutoka kwa
mmoja wa wasomaji hawa aliyejitambulisha kwa jina la Alawi Ugama wa Tandika, Dar
es Salaam:

 

Hatuna cha kupoteza isipokuwa minyororo
yetu, ni kweli mwalimu. Je, ni nani wa kutuunganisha ikiwa nyie wenye dhamana
hiyo tayari ni mabepari? Ndio. Maana wasomi wenye pesa na wanasiasa mpo kwenye
fungate! Maskini mnyonge aende wapi
?”

 

Hicho
ndicho kilio cha wanyonge, kwamba wasomi tumewasaliti. Ni kilio cha haki, na ni
cha kweli tupu. Sisi walimu wa vyuo vikuu (hatupendi kuitwa walimu, tunataka
tuitwe wahadhiri) tumesaliti jukumu letu la msingi. Wengi wetu tumekuwa
makahaba wa kitaaluma (academic
prostitutes
) kwa kuwa tumeamua kuuza usomi wetu sokoni ili kujiongezea
kipato. Wengi hatufanyi tafiti za mambo yanayowahusu wanyonge mpaka kuwe na
malipo, na tumejikita kutoa ushauri-elekezi (consultancies) kwa makampuni ya kibepari, serikali (zinazotawaliwa
na vibaraka na waporaji) au asasi za kiraia ambazo nyingi pia hutegemea
ufadhili wa mabeberu na kujidai zikiwapigania wanyonge huku zikiwarudisha
utumwani. Haiyumkiniki kuwa wahadhiri wa vyuo vikuu wakiteuliwa katika vyeo vya
serikalini hujiingiza katika uozo na upuuzi ule ule ufanywao na watawala. Mfumo
unaowafukarisha wanyonge, ndio unaotufaidisha sisi wasomi.

 

Wanafunzi
tunaowazalisha pia ni sehemu ya tatizo. Wengi wao hawana ari ya kuwatumikia
wanyonge bali kutajirika. Shida yao kubwa wawapo vyuoni ni kupata vyeti ili
waingie sokoni kujiuza. Soko halihitaji watu wanaofikiri na kupinga unyonyaji,
bali “vimashine”, yaani watu wafanyao kazi kama mashine bila kuhoji anaefaidika
na jitihada zao.

 

Ikitokea
wanafunzi wetu wanadai mikopo ndipo hujiita watoto wa wakulima. Fedha ziingiapo
kwenye akaunti basi husahau kabisa kuhusu huyo mkulima. Wengi wao
hawajishughulishi kuandaa mijadala au tafiti kuhusu mustakabali na ukombozi wa
wanyonge. Ni nani anayejitanabaisha kinadharia na kwa vitendo na kundi la
wanyonge, na kulikana tabaka lake ili akapambane pamoja na hao wanyonge?

Hata
wajiitao “wanaharakati” katika vyuo, huwatumia wanyonge kama mtaji wa kisiasa
ili baadae wakagombee ubunge au kuteuliwa katika nafasi za ulaji. Ni nani
anayedadisi chanzo cha madhila ya wanyonge? Japo wanafunzi wetu wanapaswa
kubeba lawama za kukubali kuwa sehemu ya tatizo, lakini zigo kubwa la lawama
tunapaswa kulibeba sisi walimu kwa kushindwa kuzalisha wanafunzi wanamapinduzi,
wapingao ubepari na kupigania maslahi ya wanyonge kwa nadharia na vitendo.

 

“Hivyo kaeni pembeni”

Sina
hakika kama wasomaji walionitumia ujumbe walikuwa wamesoma maoni yaliyotolewa
na Jumuiya za Wanataaluma wa Vyuo vya Umma nchini juu ya rasimu ya katiba mpya.
Kati ya moja ya mapungufu makubwa ambayo wahadhiri wameyaona katika rasimu ni
kwamba haikutaja itikadi tunayopaswa kufuata. Kisha wakatoa pendekezo kuwa
rasimu ijayo itamke kuwa itikadi yetu ni “ubepari”, na kwamba serikali sharti
ichukue hatua madhubuti za kuitimiza itikadi hiyo. Hao ndio wasomi ambao
Mwalimu aliwakabidhi jukumu la kuongoza mapambano ya wanyonge.

 

Mwalimu
alishatuonya wasomi kuwa “kama ninyi
walimu msipowaongoza wanyonge wa Afrika, ikitokea siku akawepo mtu wa kuwaondoa
katika umaskini na mateso mtapaswa kukubali kukaa pembeni na mkubali kuongozwa
na jeshi la wanyonge wa Afrika. Na nitafurahi nikiwaona mkidharauliwa kwa
sababu mlikuwa viongozi wasiofaa
”.

 

Wanyonge shikeni hatamu

Uzoefu wa miaka 5o ya Uhuru umetuonyesha kuwa kati
ya kosa kubwa ambalo wanyonge wanaweza kulifanya ni kuwakabidhi wasomi na
watawala haki ya kuwaongoza na kuwatawala. Kitabaka, wasomi na watawala hawana
ugomvi kwani wana maslahi yanayofanana. Wote ni watumishi wa mabepari, na kazi
yao huwa ni kuwapa wanyonge matumaini hewa huku wakiwauza kwa mabepari.

 

Ninapozungumzia wasomi hapa nawagusa hata wale ambao
wanaongoza asasi za kiraia, makampuni ya kibepari (yawe ya serikali au
binafsi), vyama vya siasa au hata vyama vya wafanyakazi. Ukichukua mishahara
yao, magari yao, nyumba zao, makampuni yao, hapo hujazungumzia safari za ndani
na nje  ambazo zina posho za kujikimu
achilia mbali watoto wao katika shule za binafsi (ndani na nje ya nchi),
utapata jeshi la watu wenye maslahi ya kuuendeleza mfumo wa kibepari na hata
kufikia hatua ya kutamka kuwa “katiba itamke kuwa itikadi yetu ni ubepari”!
Kundi hili haliwezi kuongoza mapambano ya wanyonge. Hivyo, wanyonge sharti
wajiongoze wenyewe.

 

Nitakapopata wasaa katika siku za usoni, nitafafanua
kwa kina namna ambavyo wanyonge wanapaswa kushika hatamu katika mapambano kwa
kujenga mshikamano wa kitabaka na kuongozwa na itikadi sahihi!

 

Mwandishi
wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya
Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com