UMAJUMUI WA AFRIKA: KURUNZI LA
MAPAMBANO YA WANYONGE

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Mirengo finyu

Juma
lililopita niliandika makala yaliyokemea itikadi finyu za ukabila (wa makabila,
maeneo na  wa ki-nchi), udini na ukaburu
(wa uzawa na wa kiumri). Nilisema kuwa itikadi hizi finyu zimelenga kuwagawa
wanyonge ili kwa kupitia dini zao, umri wao, jinsia zao, makabila yao au nchi
zao wajione wao ni sawa na watu wanaowanyonya na kuwafukarisha. Itikadi finyu
hizi huzalishwa na kuenezwa na watu wa tabaka la juu ili kukwepesha wanyonge
wasiungane na kuanzisha mapambano ya kitabaka. Katika makala ya juma hili,
nitaelezea itikadi pana inayopaswa kuongoza mapambano ya wanyonge wa Afrika.

Sehemu
kubwa ya watu wetu ni maskini. Umaskini huo si wa asili, si wa kuzaliwa nao.
Asili haikuumba matajiri na maskini. Umaskini ni zao la mfumo unaowafukarisha
wengi, na kuwatajirisha wachache. Kwa hiyo kama tukiamua kusema kuwa ufukara
huzalishwa na mfumo kristo basi matajiri wote waitwe wakristo na mafukara wote waitwe
waislamu. Hivyo vita iwe ni maskini dhidi ya matajiri bila kujali majina yao au
madhehebu yao. Kama umaskini huzalishwa na jinsia basi kila maskini aitwe
mwanamke na kila tajiri aitwe mwanaume, na minyukano ya kitabaka iendelee.
Hali kadhalika kama umaskini huzalishwa na Tanganyika (Muungano) basi matajiri
wote waitwe Watanganyika na mafukara waitwe Wazanzibari bila kujali
walikozaliwa au wanakoishi, kisha vita dhidi ya wanaowafukarisha iendelee.

Itikadi ya wanyonge

Itikadi
pekee itakayowaunganisha wanyonge bila kujali dini, vyama, jinsia, rangi, umri
au nchi ni itikadi ya Umajumui wa Afrika (pan-Africanism).
Itikadi hii haikuzaliwa barani hapa. Ilizaliwa ughaibuni, miongoni mwa watu
weusi, ambao walipelekwa katika nchi za Amerika kama watumwa. Hata baada ya
kukomeshwa kwa biashara ya utumwa, weusi hawa hawakutambuliwa kama binadamu.
Walibaguliwa. Walinyanyaswa. Walikandamizwa. Walinyimwa fursa za kupiga kura,
kumiliki mali, kujiendeleza kielimu, n.k. Wapo waliodiriki kusema kuwa utumwa
ulikuwa bora kwani watumwa walilishwa na hata kupewa matibabu walipougua ili
waendelee kuzalisha. Kadri weusi hawa walivyobaguliwa, kunyanyaswa na kukandamizwa
ndivyo walivyogundua udhaifu wao. Udhaifu huo ulitokana na rangi za ngozi zao –
ngozi nyeusi! Hivyo rangi ya ngozi zao ikazalisha itikadi ya kupigania usawa na
kupinga ubaguzi wa rangi katika nchi za Magharibi.

Umajumui ukazaa utaifa

Ni
baada ya vita kuu ya pili ya dunia ndipo itikadi ya Umajumui wa Afrika
ilipochukua sura mpya, sura ya kulikomboa bara la Afrika. Hii ilitokea katika
kongamano la tano la kimajumui lililofanyika katika mji wa Manchester, nchini
Uingereza mwaka 1945. Kati ya waliohudhuria walikuwepo pia Kwame Nkrumah na
Jomo Kenyatta.  Wito ukatolewa kwa
Waafrika kupigania uhuru wao toka kwa wakoloni, na kisha baada ya uhuru
kupatikana kuliunganisha bara la Afrika ili kuunda dola moja lenye nguvu.

Kwa
nini kuiunganisha Afrika? Kwa sababu mipaka iliyounda vinchi ambavyo leo
tunavitukuza haikuwekwa na Waafrika. Iliwekwa na wakoloni kwa madhumuni ya
kugawana bara letu ili wapore rasilimali zetu bila kuingiliana. Na wakoloni walipoligawa
bara hili, hawakuitisha kura ya maoni kwa wenyeji ili kujua kama jamii ya
Wamasai au Wajaluo wangekubali kugawanywa katika nchi mbili tofauti. Kwa hiyo
wakati wa harakati za ukombozi ajenda ilikuwa uhuru na umoja.

Kama ambayo Profesa Shivji husema, ni umajumui wa
Afrika (pan-Africanism) ndio uliozaa
uzalendo/utaifa (nationalism).
Nkrumah aliporejea Ghana hakwenda kupigania uhuru wa Ghana. Alianza kwa
kupigania uhuru wa Afrika Magharibi. Lakini kwa sababu za kimkakati, ilibidi
kukomboa koloni moja moja na baadae kuziunganisha nchi huru. Ndio maana hata
katiba ya Ghana ilikuwa na kifungu kisemacho kuwa Ghana itakuwa tayari
kusalimisha mamlaka (sovereignty)
yake kwa dola huru la Muungano la Afrika. Hata Nyerere alikuwa tayari
kuchelewesha uhuru wa Tanganyika ili nchi za Afrika Mashariki zipate uhuru
zikiwa zimeungana.

Wanyonge
walipoporwa itikadi yao                

Nimekwisha kutoa hoja ya kwamba itikadi ya umajumui
wa Afrika ilikuwa ni itikadi ya kuwakomboa wanyonge. Ilikuwa ni itikadi
iliyowaunganisha wanyonge ili wapambane na kuishinda mifumo yote kandamizi na
ya kinyonyaji. Kati ya mwaka 1900 na 1945 itikadi hii ilikuwa ya kupinga
manyanyaso na ubaguzi dhidi ya watu weusi katika nchi za Magharibi. Kati ya
mwaka 1945 na 1960 itikadi hii ilichukua sura ya ukombozi, lengo likiwa ni
kulikomboa bara la Afrika toka katika ukoloni, na hatimaye kuunganisha ili
kujenga nchi moja. Lengo la uhuru lilitimia, la umoja limebaki kuwa ndoto.

Je, kwa nini nchi huru za kiafrika zilishindwa
kuungana? Viongozi walioingia madarakani walinogewa na madaraka na hivyo kuwa
na maslahi katika kutukuza vi-nchi walivyorithi kutoka kwa wakoloni. Nkrumah
tayari alikuwa ameliona hili na akawaonya viongozi wenzake kuwa Afrika kama
Afrika isingeungana katika miaka ile ya 1960 basi ingekuwa ngumu kuiunganisha.

Nkrumah aliwaonea huruma wanyonge wa Afrika kwani
ndio wangeendelea kuwa kitoweo cha mabeberu. Wakulima na wafanyakazi
wangeendelea kulipwa kiduchu, huku wakikosa huduma bora za afya, elimu na maji,
ilhali mataifa ya kibeberu yakiendelea kuneemeka kwa rasilimali na malighafi
kutoka Afrika. Viongozi wasingekuwa na cha kupoteza kwani waliendelea kuneemeka
na kodi za wanyonge pamoja na “makombo” ya mabeberu.

Jaribio la mwisho la kuwashawishi viongozi wa Afrika
kuungana mara moja lilifanyika mwaka 1965 katika mkutano wa Umoja wa nchi huru
za Afrika uliofanyikia mjini Accra, nchini Ghana. Hoja ya Nkrumah ilikataliwa
tena, na mwaka uliofuatia Nkrumah alipinduliwa katika mapinduzi yaliyopangwa na
kusimamiwa na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA).

Kati ya watu walioongoza upinzani dhidi hoja ya
Nkrumah alikuwa ni Nyerere. Nyerere alitaka Afrika iungane kwa kupitia
mashirikisho ya kikanda na baadae mashirikisho hayo ndiyo yaungane kuunda dola
la Afrika. Lakini Nkrumah alitaka nchi zote za Afrika kusalimisha mamlaka yao
mara moja na kuunda dola moja. Kwa hiyo, Nkrumah na Nyerere walitofautiana juu
ya njia za kuunda dola moja la Afrika. Lakini wote walitaka Afrika iungane.

Wapinzani wa Nkrumah walidandia hoja ya Nyerere
wakijidai kuiunga mkono, lakini lengo lao likiwa kukwamisha kila jitihada za
kuiunganisha Afrika. Mwaka 1997, akihutubua halaiki ya watu nchini Ghana,
Nyerere alikiri kuwa pengine Nkrumah alikuwa sahihi. Ilikuwa rahisi
kuiunganisha Afrika katika miaka ya 1960 kuliko ilivyo sasa. Kisha Mwalimu
akasema kuwa mara baada ya Mkutano wa Accra, kuna rais mmoja aliyemfuata na
kumshukuru kwa kuipinga hoja ya Nkrumah. “Yaani siamini kama narudi nchini
kwangu nikiwa bado mkuu wa nchi. Nimefurahi sana”, kiongozi huyo alimtamkia
Mwalimu. Na hapo ndipo Mwalimu alitoboa siri ya jeshi la watu wenye maslahi ya
kukataa Afrika isiungane:

Ukichukua
idadi ya nyimbo za taifa, bendera na pasi za kusafiria za nchi mbalimbali, na
watu wenye stahiki ya kupigiwa mizinga 21, hapo hujazungumzia mawaziri,
mawaziri wakuu na mabalozi, utapata jeshi zima la watu wenye nguvu na ushawishi
walio na maslahi ya kuifanya Afrika iendelee kugawanyika. Hicho ndicho Nkrumah
alichokutana nacho mwaka 1965
”.

Naweza kuongezea kuwa hicho ndicho kinachoikumba
nchi yetu sasa. Hata zinazoitwa kero za Muungano kwa kiasi kikubwa zinahusu
mamlaka/matakwa ya wanasiasa kuliko maslahi ya moja kwa moja ya wananchi wetu.

Kwa ufupi, ajenda ya umajumui wa Afrika iliporwa
toka mikononi mwa wanyonge na viongozi wa Afrika walioingia madarakani baada ya
uhuru kupatikana. Katika kupigania uhuru, itikadi hii ilitumika kuwahamasisha
wanyonge dhidi ya ukoloni. Mara baada ya uhuru kupatikana itikadi hii ikahamia
mikononi mwa viongozi walioshika madaraka. Suala pana la ukombozi wa wanyonge
likafinyangwa na kubakia kuwa kamradi kadogo ka kuziunganisha nchi za Afrika.
Na hata ajenda ya kuiunganisha Afrika pia ikaondolewa mikononi mwa wanyonge na
kuwa ni suala la watawala walioingia madarakani. Taratibu, wanyonge wakaanza
kuisahau itikadi yao ambayo ingeongoza mapambano dhidi ya watawala wakatili,
waporaji na vibaraka ndani ya nchi, na mabeberu wa nje ya nchi.

Wanyonge
waidai itikadi yao

Nimalizie kwa kusema sio kila nchi za kiafrika
zinapoanzisha ushirikiano, au hata zikiwa na lengo la kuungana zinakuwa
zimeongozwa na itikadi ya Umajumui wa Afrika. Sasa hivi, kwa kuwa nchi za
kibeberu zimeamua kushirikiana, basi zinazitaka nchi za kiafrika pia kuanzisha
ushirikiano wa kiuchumi. Mabeberu wanataka kuendelea kuzipora nchi hizi kwa
pamoja. Kwa mfano, nchi za Umoja wa Ulaya sasa zinaingia mikataba ya ushirikiano
wa kiuchumi (economic partnership agreements [EPAs]) na Jumuiya za kikanda za
Afrika ili kurahisisha uporaji wa rasilimali za Afrika. Jumuiya ya Afrika
Mashariki pia imo. Huwezi kuiita jumuiya hii kuwa ni ya kimajumui.

Lengo la itikadi ya umajumui kama ilivyopiganiwa na
Nkrumah na Nyerere halikuwa kujenga nchi moja tu. Tunajenga nchi moja ili
iweje? Lengo lilikuwa ni kujenga nchi moja ili kupambana na waliotupeleka
utumwani, waliopora rasilimali zetu na kuwachinja babu na bibi zetu, walioligawa bara
letu na kulitawala. Biashara ya utumwa, ukoloni na hata ubaguzi wa rangi ni
sura tofauti tofauti za dubwasha liitwalo ubepari. Kwa hiyo, kadiri ubepari
unavyobadili sura ndivyo itikadi ya umajumui inavyotakiwa kubadili sura ili
kupambana nao.

Kwa hivi sasa ubepari umechukua sura ya uliberali
mambo-leo, mfumo ambao unatumiwa na mabeberu pamoja na vibaraka wao wa ndani
kupora rasilimali za wanyonge kwa kisingizio cha uwekezaji na ubinafsishaji.
Viwanda vyetu vimeuzwa kwa bei ya kutupa, nyumba za serikali zimeporwa, dhahabu
inatolewa karibu na bure na watawala wakipewa vyandarua wanashangilia kama
“mazuzu”. Ardhi pia inaporwa. Huduma za afya, elimu na maji sasa ni bidhaa:
huna pesa huzipati. Wanaofeli mitihani ni watoto wa maskini katika shule za kata.
Mambo haya yanatokea huku Bara, yanatokea visiwani. Yanatokea Tanzania, Kenya,
Misri, na hata Afrika Kusini. Wanaoumia ni wanyonge wote bila kujali dini zao
au makabila yao, jinsia zao au umri wao, maeneo yao au nchi zao. Ni itikadi ya
Umajumui wa Afrika pekee ndiyo inaweza kuongoza mapambano ya wanyonge dhidi ya
mabeberu na vijibwa wao wa ndani. “Wanyonge wote unganeni. Hamna cha kupoteza
isipokuwa minyororo yenu!”

Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana
kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com