ARVs Bandia:
Serikali itoe taarifa sahihi kulinda afya za watumiaji
Tumesikitishwa kupata taarifa kwamba watu 5,358
wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (VVU) waliokuwa kwenye matibabu wameacha kutumia
dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARVs), mkoani Dodoma.
Taarifa
kupitia vyombo vya habari na taasisi
mbalimbali kuhusu Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) kuacha kutumia dawa,
zimekuja kipindi ambacho wananchi na wadau wa UKIMWI wakitafakari hatma ya uchunguzi
wa sakata la kutengenezwa dawa bandia za ARVs. Dawa hizo aina ya TT-VIR toleo
namba (batch number oc.01.85) zilisambazwa katika mikoa ya Mara, Tanga na Dar
es Salaam tangu Mei, 2011.
Kuwepo kwa
ARVs bandia na taarifa juu ya WAVIU kuacha kutumia dawa kunadhihirisha udhaifu uliopo ndani ya mifumo na mamlaka za
serikali zilizopewa kusimamia ubora, uwepo na upatikanaji wa dawa. Sikika inaamini, pengine kuna uhusiano wa
karibu kati ya uwepo wa dawa hizo bandia nchini na WAVIU hao kuingiwa hofu na kuacha
kutumia dawa.
Tunaamini hayo
kwa kuzingatia ukweli kwamba suala la mgonjwa kutumia dawa kwa kiasi kikubwa
linategemea imani na utayari wa mhusika. Uwepo wa dawa
bandia ama zisizo na ubora unapunguza imani na hivyo kuweza kusababisha mgonjwa
kuacha kuzitumia na kupelekea kuathirika zaidi.
Sakata la
kuwepo kwa ARVs bandia lililochukua takribani miezi nane sasa, limekuwa na sura
tofauti hususan juu ya nani anahusika moja kwa moja baada ya kiwanda
kinachodaiwa kutengeneza dawa hizo Tanzania Pharmaceticals Industry (TPI)
kukanusha kuhusika na utengenezaji huku Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Bohari
Kuu ya Dawa (MSD) wakisisitiza kuwa dawa hizo zimetoka kiwandani hapo.
Sikika inathamini
na kutambua juhudi za serikali za kutekeleza taratibu za kisheria ikiwemo
ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara uliofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii kupitia TFDA. Hatua nyingine
iliyochukuliwa na serikali ni kukifungia kiwanda cha TPI kutokana na nyaraka
zilizokutwa MSD kuonesha kuwa TPI iliiuzia MSD dawa hizo. Serikali pia iliwasimamisha
kazi watendaji watatu wa MSD.
Usambazaji
na matumizi ya dawa aina ya TT –VIR 30 toleo namba 0C .01.85 pia ulipigwa
marufuku na serikali ilizitaka mamlaka za serikali za mitaa kupitia waganga
wakuu, kukusanya dawa hizo bandia kutoka
vituo vya huduma za afya na kwa wananchi, na kisha kuzirudisha MSD.
Kwa mujibu
wa taarifa zilizotolewa na MSD, takribani makopo 8,000 ya toleo hilo kati ya
zaidi makopo 12,000 yaliyosambazwa yalikusanywa. Hivyo kwa hesabu rahisi, kuna
takribani makopo 4,000 ambayo bado yapo kwenye mzunguko na ambayo hakuna
taasisi yenye uhakika wa yalipo makopo hayo; kwenye vituo vya huduma ama kwa
wananchi.
Serikali
ililifikisha suala la ARVs bandia kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) kwa
uchunguzi na hatua zaidi za kisheria. Lakini, pamoja na juhudi hizo za
serikali, Sikika hairidhishwi na kasi ndogo ya ufuatiliaji wa tatizo hilo
hususan muda mrefu unaotumika kupeleleza.
Kwa mujibu
wa taarifa kutoka ofisi ya DPP, jalada la kesi ya ARVs bandia limepokelewa na
linashughulikiwa ili kupata muelekeo wa nani ahusishwe na kwa kosa gani kabla
ya kuachia mamlaka husika jukumu la uchunguzi wa kina. Kwa maelezo ya ofisi hiyo, suala la ARVs bandia limechukua muda mrefu
(zaidi ya miezi miwili), tofauti na muda wa kawaida wa siku 14 unaotumiwa na
ofisi ya DPP kushughulikia kesi mbalimbali zinazofikishwa hapo, kutokana na uzito/unyeti
wa suala hilo.
Wakati
taratibu hizo za kitaalamu na kisheria zikiendelea, tunaishauri serikali kutoa
taarifa rasmi kwa wananchi juu ya dawa bandia (makopo 4,000) ambazo
hazijakusanywa. Je, ziko vituoni au zilishatumiwa na wananachi? Kama zilishatumiwa,
je serikali ina taarifa zozote juu ya waliozitumia dawa hizo? Je, kuna madhara
yoyote waliyopata kutokana na kuzitumia?
Kwa kutoa
taarifa sahihi, serikali itasaidia kuwatoa mashaka wanaotumia ARVs na
kuwajengea imani waendelee kuzitumia bila kuathiri afya zao. Sikika inaamini kuwa kuwepo kwa dawa zenye ubora
na uhakika kutaongeza imani kwa WAVIU kuendelea kuzitumia na kuimarika afya
zao.
Makala hii
ya Sikika imeandikwa na Aisha Hamis, Afisa Programu, Idara ya VV na UKIMWI.