Taarifa kwa Vyombo vya Habari, April 09, 2013


Bunge lijadili ripoti za CAG kwa Uwazi


Sikika inapenda kuamini kwamba taarifa zilizochapishwa kwenye
magazeti mbali mbali kuhusu Bunge kutojadili ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mkutano huu wa 11, ama ‘zimenukuliwa vibaya’,
au aliyezitoa alikuwa hajawasiliana kikamilifu na viongozi wa juu wa Bunge.

Iwapo habari kwamba Bunge
halitajadili ripoti za CAG katika mkutano ni za kweli, basi Bunge limejitenga
na wananchi na pia limejipunguzia madaraka yake ya kuisimamia serikali kwa
niaba ya wananchi. Kwa lugha nyingine, Bunge litakuwa limewaasi wapiga kura
wake.

Takribani miaka kadhaa
mfululuzo, CAG amekuwa akilalamika kwamba serikali haitekelezi mapendekezo na
ushauri wake katika kusimamia vyema matumizi ya fedha za umma. Matatizo mengi
ambayo CAG amekuwa akiibua katika ripoti zake kuhusu matumizi ya fedha za umma
yamekuwa yakijirudia. Sikika inaamini kwamba kutojadiliwa kwa ripoti za CAG
bungeni kwa uwazi kunalenga kuficha mapungufu haya ya serikali.

Katika mkutano wa 10 wa
Bunge, tulishuhudia mabadiliko makubwa ya namna Bunge linavyoisimamia na
kuiwajibisha serikali, ambayo hata hivyo hayakutafuta baraka za wananchi.
Wananchi wameiajiri serikali na wameliweka Bunge kuisimamia na kuiwajibisha
serikali kwa niaba yao.  Bunge halina
mamlaka ya kujiondolea au kujipunguzia majukumu ambayo linatekeleza kwa niaba
ya wananchi bila kupata baraka za wananchi.

Katika mabadiliko hayo,
mojawapo ni hili la kutokujadili ripoti za CAG ndani ya Bunge. Kifungu cha 63.3.b cha Katiba ya JMT
kinalitaka Bunge kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge
wa kila mwaka wa bajeti. Mkutano huu wa sasa wa Bunge ni wa Bajeti.

Kipengele hicho cha Katiba
hakikutaja Kamati za Bunge bali Mkutano
wa Bajeti.
Hivyo hata kama ripoti hizi zitapitiwa kwenye Kamati za Bunge,
ni lazima, kwa mujibu wa Katiba zikajadiliwa kwenye Mkutano wa Bunge. Hapo
wabunge wote na wananchi watapata fursa ya kujua nini kilichojiri katika kila
ripoti ya CAG. Pia mjadala huo utanukuliwa katika kumbukumbu rasmi za Bunge
yaani Hansad ambayo iko wazi kwa wananchi kuipitia muda wowote.

Mabadiliko ya pili yalihusu
kubadilisha muundo na majukumu ya Kamati za Kudumu za Bunge. Katika mabadiliko
hayo, Kamati ya Mashirika ya Umma ilifutwa na baadhi ya majukumu yake
kuunganishwa kwenye kamati Hesabu za Serikali Kuu (PAC)

Majukumu ya Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC) ambayo hayakuhamishiwa kwenye Hesabu za Serikali Kuu (PAC)
ni lile la kushughulikia ubinafsishaji na pia jukumu la kufanya tathmini ya
mashirika ya umma. Majukumu haya mawili ni ya msingi kabisa katika kuwezesha
wananchi kujua kinachoendelea katika ubinafsishaji ambao umelalamikiwa sana
jinsi ulivyoendeshwa, na pia kujua ufanisi wa mashirika ya umma kwa ujumla.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi
kwamba mabadiliko yote mawili yalikusudia kuongeza usiri kwa namna serikali
inavyotumia madaraka na mali za umma, hivyo kulifanya Bunge kukosa mamlaka
yake, na kuwafanya wananchi kushindwa kuiwajibisha serikali. Pia inawezekana
Bunge limevunja Katiba kwa kujipunguzia majukumu yake kikatiba. Pia ni wazi
kwamba Bunge limeasi wananchi waliolichagua kwa kujivua jukumu la kuisimamia
serikali.

Sikika inalitaka Bunge
kurejea kwenye misingi ya majukumu yake kwa sababu majukumu hayo limepewa na
wananchi. Bunge halina mamlaka ya kujipunguzia majukumu ya msingi lililopewa na
wananchi bila ridhaa ya wananchi wenyewe. Iwapo Bunge linaamini lina mamlaka ya
kufanya mabadiliko hayo na kwamba ndiyo njia bora ya kuongeza uwajibikaji wa
serikali, litafute ridhaa ya wananchi kwanza.

Mwisho, Sikika inashauri
mijadala inayohusu ripoti za CAG, mapendekezo ya bajeti ya serikali, mapato na
matumizi, utekelezaji wa mipango na bajeti za mwaka uliotangulia lazima
zijadiliwe katika mkutano wa Bunge ulio wazi ili wananchi nao waone namna
wawakilishi wao wanavyotekeleza wajibu wao wa kusimamia fedha za walipa kodi.

Bw. Irenei Kiria

Mkurugenzi Mtendaji, Sikika, S.
L. P 12183 Dar es Salaam,

Simu: +255 222 666355/57, Nukushi:
2668015, Barua pepe: info@sikika.or.tz, Tovuti: www.sikika.or.tz