Kufutwa kwa POAC: Anne Makinda adhibitiwe au tusahau uwajibikaji nchini

Zitto Kabwe

Katika mkutano wa Kumi wa Bunge la
Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Spika wa Bunge ndugu Anne Makinda
alitangaza mabadiliko kadhaa ya muundo wa Bunge katika Kamati mbalimbali za
Bunge. Moja ya maamuzi ya Spika yalikuwa ni kufutwa kwa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Mashirika ya Umma ambayo inajulikana kwa kifupi kama POAC. Maamuzi haya
yameleta sintofahamu kwa wananchi wengi na wafuatiliaji wa masuala ya Bunge na
Uwajibikaji katika nchi yetu. Ni muhimu tufahamu uundwaji wa POAC ulitokana na
misingi gani?

Baada ya Tanzania kuingia kwenye
zoezi la Ubinafsishaji, mashirika mengi ya Umma yaliuzwa na mengine kufa
kabisa. Wakati huo kulikuwa na chombo kinaitwa SCOPO (Standing Committee on
Parastatal Organisations) kwa madhumuni ya kusimamia uendeshaji wa Mashirika ya
Umma. Bunge lilikuwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na kamati hiyo
ilifutwa mwaka 1997 kufuatia hatua za ubanifsishaji na ukweli kwamba Mashirika
ya Umma hayatakuwapo na hivyo hapakuwa na haja ya kuwapo kwa kamati hiyo.
Mwenyekiti wa mwisho wa Kamati hiyo alikuwa ni Mzee William Shelukindo wakati
huo akiwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Mwaka 2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali alifanya mkutano wa Uwajibikaji na kueleza Taifa kuwa
kimsingi Mashirika ya Umma bado yapo na mahesabu yao, kwa kuwa hayaangaliwi, ni
mabaya sana na fedha za umma zinapotea. Pia alieleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ibara ya 143(5) inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali kutoa taarifa za Ukaguzi za Mashirika ya Umma (Public
Authorities and Other Bodies). Hivyo aliomba Bunge liunde Kamati ya Bunge ya
Mashirika ya Umma ili liweze kupokea, kujadili na kutoa maelekezo kuhusu
mahesabu ya Mashirika ya Umma na kusimamia ufanisi wa Mashirika ya Umma. Vile
vile alishauri Kamati hiyo isimamie sera ya 
Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma. Spika wa Bunge wa wakati huo,
kupitia Kamati aliyoiunda chini ya Job Ndugai (wajumbe wengine walikuwa Dkt. Willibrod Slaa, Beatrice Shelukindo, Hamad Rashid Mohammed na Nimrod Mkono)
wakaunda Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Kanuni za Bunge za
Mwaka 2007. Kamati ya POAC iliundwa rasmi mwaka 2008 mwezi Februari. Nilipewa
dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati hii. Sababu za kuanzishwa kwa
kamati ya POAC bado zipo.

Majukumu ya POAC yaliainishwa na
sehemu ya tatu ya nyongeza ya nane ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007,
kanuni ya 115 (13)(a-e). Majukumu hayo ni pamoja na kushughulikia mahesabu
yaliyokaguliwa ya Mashirika ya Umma, kuainisha maeneo sugu ya matumizi mabaya
ya fedha za Umma, kutathmini ufanisi wa Mashirika ya Umma na kufuatilia
utekelezwaji wa sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya Umma. Kuanzia mwaka 2008
Mdhibiti na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali amekuwa akitoa taarifa za
mahesabu ya mashirika kama Katiba ya nchi inavyomtaka na sheria ya ukaguzi ya
mwaka 2008. Sheria hii imeitaja kamati ya POAC kama moja ya kamati zenye
majukumu ya kuwasilisha Bungeni taarifa ya mwaka ya mahesabu ya Mashirika ya
Umma.

Katika kipindi cha miaka mitano POAC
imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa umahiri na kwa kweli kwa uwazi sana
kuliko kamati nyingine zote za Bunge. Taarifa ya mwisho ya POAC katika Bunge
iliyowasilishwa katika mkutano wa saba wa Bunge, mwezi Aprili mwaka 2012
ulipelekea kutolewa kwa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo
ilisababisha mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri. Hatua hii ilikuwa ni
hatua muhimu sana katika kuweka mizizi ya utamaduni wa uwajibikaji nchini
kwetu. Wakati Kamati inajiandaa na Taarifa yake ya Mwaka 2012 kwenye Mkutano wa
Kumi na Moja, Spika ameivunja. Ikumbukwe maagizo ya mwisho ya Kamati ya POAC
yalikuwa ni kuzuia mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa mikopo kwa Serikali bila ya
kuwapo kwa mikataba. Hivi sasa Serikali imekopa zaidi ya shilingi 1.2 trilioni
kutoka mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa ajili ya miradi mbalimbali, mikopo hiyo
ya fedha za wafanyakazi haina mikataba yeyote na POAC iliona hatari ya fedha za
wafanyakazi kupotea na kuleta madhara makubwa kwa wastaafu nchini.

Katika maelezo yake Spika amesema
nchi nyingine duniani hazina kamati kama ya POAC. Nadhani waliomshauri Spika
waliamua kumdanganya na yeye akadanganyika. Nchi zote za Afrika Mashariki zina
Kamati ya kusimamia Mashirika ya Umma. Kenya inaitwa Public Investments
Committee, Uganda inaitwa State Corporations Committee na hata nchi nyingine
kama India ambazo zinafuata utamaduni wa kibunge kama wetu wanayo na wanaita
Public undertakings Committee. Nchini Afrika Kusini sio tu kuna Kamati ya
Mashirika ya Umma bali pia kuna Wizara inayosimamia Mashirika ya Umma (Ministry
of Public Entreprises). Kimsingi Kamati ya POAC ilipaswa kuongezewa nguvu zaidi
ili kufikia uwezekaji wa Serikali kwenye makampuni binafsi badala ya kuifuta.
Uwezekaji wa Serikali kwenye makampuni kama BP, AirTel, Kilombero Sugar, SonGas
n.k. hauna uangalizi wowote.

Uamuzi wa Spika wa Bunge kuifuta
Kamati ya POAC ni uamuzi unaorudisha nyuma juhudi za nchi kujenga asasi za
uwajibikaji, ni kinyume cha sheria ya ukaguzi wa umma inayotaja Kamati tatu za
Bunge za kusimamia fedha za Umma na ni kinyume cha Katiba ya nchi. Spika wa
Bunge anasema kazi za Kamati ya POAC zitafanywa na Kamati ya PAC; Tanzania ina
jumla ya Mashirika ya Umma 258 yenye thamani ya shilingi trilioni 10.2 mpaka
mwezi Juni mwaka 2012, hata kamati ya POAC ilikuwa haiwezi kushughulikia
Mashirika yote ya Umma katika mwaka mmoja, PAC itawezaje kusimamia Wizara za
Serikali, Mikoa na wakala za Serikali na wakati huo huo Mashirika ya Umma 258?
Kwa vyovyote vile Taifa linarudi miaka ya kabla ya 2008 ambapo Mashirika ya
Umma yalikuwa kichaka cha kuiba fedha za Umma. Hivi karibuni Kamati ya POAC
iligundua mtindo wa Wizara za Serikali kupeleka fedha Serikali kwenye Mashirika
na kutumia kifisadi ili kukwepa ukaguzi kwenye Wizara (Wizara ya Utalii
ilipeleka zaidi ya shilingi 600 milioni Bodi ya Utalii mwaka 2010/2011).
Ikumbukwe pia wizi wa EPA, MEREMETA na hata uuzaji holela wa baadhi ya mali za
Serikali kupitia ubinafsishaji ulifanyika nyakati ambazo Bunge halina kamati
inayosimamia Mashirika ya Umma.

Kwa vyovyote vile Spika wa Bunge
amedhihirisha namna ambavyo anafanya maamuzi bila kuzingatia maslahi ya nchi
wala kuzingatia historia ya uwajibikaji katika nchi. Namna mijadala ya Bunge
inavyoendeshwa, namna anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge
kibogoyo na namna anavyofanya maamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa
misingi ya uwajibikaji wa nchi. Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa
kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba
Mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la
wananchi liitwalo Bunge. Anne Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu
itaumia.