DEMOKRASIA NA KATIBA MPYA
NCHINI TANZANIA
MAONI KUHUSU KATIBA MPYA
Kutoka kwa: M.M. Mulokozi [Januari 2013]
Profesa Mstaafu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
S.L.P. 35110, Dar es Salaam: [tamulokozi50@yahoo.co.uk]
Wakati
tunajadili utungaji wa Katiba mpya ya Tanzania, ni vizuri tukatafakari kwanza
misingi itakayotuongoza katika kuandaa
maudhui ya Katiba hiyo. Katika waraka huu napenda kutoa mawazo machache
kuhusiana na suala hilo. Napendekeza misingi ifuatayo:
–
Kujenga umoja na utambulisho
wa kitaifa
–
Kupanua uhuru na haki
za msingi za raia
–
Kupanua demokrasia
–
Kuweka mfumo wa uwazi
wa utawala na uongozi, na kudhibiti ufisadi
–
Kuimarisha uchumi na
uzalishaji
–
Kujenga umoja na
ushirikiano wa kikanda,na hatimaye Umajumui wa Afrika nzima.
Kabla
sijajadili misingi hiyo nizungumzie kidogo suala la mchakato wa kuandaa Katiba.
Katiba ni chombo chenye mamlaka juu ya kila mtu na kila chombo katika jamii.
Katiba lazima itawale mamlaka zote – kuanzia kwa Rais hadi kwa balozi wa nyumba
kumi, hadi kwa mtu binafsi. Katiba sharti itawale asasi zote, kuanzia kwa
Bunge, hadi mahakama, polisi, asasi za kiraia na kidini, n.k. Ndiyo maana
haifai kwa Katiba kuamuliwa na vyama vya siasa, ambavyo ni vikundi vyenye maslahi
maalumu ndani ya Katiba hiyo.
Kujenga Umoja na Utambulisho wa Kitaifa
Katiba
yoyote ile ya nchi huwa na jukumu la kujenga utaifa na utambulisho wa Taifa
linalohusika, na hivyo kuchunga na kulinda usalama na uzalendo wa Taifa hilo.
Ndiyo maana katiba za mataifa mengi hutaja mipaka ya nchi, Bendera ya Taifa,
Wimbo wa Taifa, Lugha ya/za Taifa, na lugha nyingine rasmi kama zipo. Katiba za
baadhi ya nchi, hutaja hata hati za maandishi za lugha yao, na vipengele muhimu
vya utamaduni wa Taifa, kama vile dini, mila, na kadhalika. Katiba ya sasa ya
Tanzania inataja baadhi ya mambo haya, lakini si yote. Kwa mfano, haitaji Lugha
ya Taifa!
Kujenga
utambulisho na utaifa ni pamoja na kujenga umoja wa kitaifa, kuweka misingi
imara ya umoja inayokubalika kwa wananchi wote wa makundi na matabaka yote, kujenga
uzalendo, mapenzi ya nchi, na moyo wa kuwa tayari kuitetea na kuifia nchi
ikibidi.
Ni wazi
kwamba suala la kuruhusu uraia wa nchi mbili au zaidi ambalo linapigiwa debe
sana hivi sasa na baadhi ya watu inabidi litazamwe kwa kuzingatia msingi huu wa
uzalendo na maslahi ya Taifa: Mathalan, itakuwaje iwapo raia wa Marekani [au
nchi nyingine], ambaye pia ni raia wa Tanzania, atatumwa na Rais wake wa
Marekani na kupewa nyenzo zote kuja kututawala na kutekeleza matakwa ya nchi
yake [ya Marekani] hapa kwetu? Utamzuiaje? [Haya tayari tumeyaona katika baadhi
ya nchi]. Hatusemi kwamba kiongozi asiyekuwa na uraia wa nchi ya kigeni hawezi
kutumiwa na nchi hiyo kutekeleza maslahi yake katika nchi anayoiongoza.
Tunawafahamu viongozi vibaraka wengi waliotumiwa hivyo. Tunachosema hapa ni kwamba tusiwarahisishie
maadui zetu mchakato wa kupata vibaraka miongoni mwetu.
Suala
la utamaduni sharti lipewe uzito kikatiba, maana bila utamaduni hakuna Taifa,
na njia ya uhakika ya kumdhibiti na kumtawala mtu ni kumteka kitamaduni na
kiakili. Hapa suala la lugha sharti lipewe uzito unaostahiki; lugha ya Taifa –
Kiswahili – ipewe nafasi muhimu kikatiba, na lugha za kijamii na za kigeni
tunazozihitaji zisisahaulike. Katiba itaje wazi kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya
Taifa na lugha rasmi ya kwanza, na Kiingereza ni lugha rasmi ya pili; Katiba ielekeze
kwamba itatungwa sheria mahsusi itakayofafanua nafasi, dhima na matumizi ya
lugha ya Taifa na lugha nyinginezo katika jamii.
Kupanua Uhuru na Haki za Raia
Katiba
inapaswa kulinda uhuru na haki za raia, ambazo ni pamoja na haki za kuishi, kuheshimiwa
kama binadamu, kufanya kazi na kupata malipo ya haki kwa kazi hiyo, kupewa
pensheni ya uzeeni, kujumuika, kusafiri, kuishi popote, kuabudu au kutokuabudu.
Haki za lugha na utamaduni pia zinahusika hapa. Na haki hizo lazima ziwe ni kwa
raia wote bila kujali jinsi, kabila, rangi, dini, cheo, umri au nasaba. Katiba
ya sasa inatoa haki hizo kwa kiasi fulani; Katiba ijayo ingefaa isisitize na
kufafanua zaidi haki hizi za msingi.
Kumtaja Mungu katika Katiba
Hapa
tunaweza kueleza kuwa pendekezo la Jaji Mstaafu Samatta katika kongamano moja
kuwa Katiba mpya itaje “Mwenyezi Mungu” halikubaliki kwa sababu linakwenda
kinyume na uhuru wa kuabudu tunaouzungumzia. Kwa kuwa Katiba tayari inatoa
uhuru wa kuabudu, hakuna sababu ya kuufunga uhuru huo kwa kuuhusisha na imani
fulani maalumu – zile zinazozingatia dhana ya “Mungu.” Ni vyema Katiba iendelee
kutofungamana na imani ya dini yoyote.
Kupanua Demokrasia
Katika
ulimwengu wa sasa na ujao utawala wa kidemokrasia hauepukiki. Hivyo tunahitaji
Katiba inayotambua haki na haja hiyo ya kujenga na kuimarisha demokrasia. Demokrasia
tunayozungumzia hapa ni demokrasia pana inayojumuisha wananchi wote wa makundi
yote; hatuzungumzii demokrasia ya vyama vya siasa tu. Katiba yetu ya sasa, kwa kiasi kikubwa, inajikita katika demokrasia ya
vyama badala ya demokrasia ya Umma. Labda hili linahitaji ufafanuzi zaidi:
Miaka kadha
iliyopita makundi mbalimbali ya wanasiasa yalianza kufanya kampeni ya kutaka
majimbo ya uchaguzi yaongezwe ili “kuimarisha” uwakilishi na demokrasia. Tulishuhudia
madiwani wa halmashauri mbalimbali wakipitisha maazimio ya kuongeza majimbo ya
udiwani na ubunge. Baadhi ya wabunge na vyama vyao vilevile walipendekeza
majimbo mapya yaanzishwe. Kampeni hiyo ilifanikiwa kwa kiasi fulani, na majimbo
mapya kadha yaliundwa, japo ilitolewa tahadhari kuwa jengo la sasa la Bunge
mjini Dodoma halina nafasi ya kuongeza wabunge wengi. Msingi wa kampeni hii ni
dhana potofu kuwa demokrasia maana yake ni kuwa na wawakilishi wengi wa vyama katika bunge na mabaraza ya
madiwani.
Mtazamo
huu wa kimajimbo kuhusu uwakilishi unadaiwa kutokana na mfumo wa Westminster,
yaani mfumo wa bunge la Uingereza. Hii ni kweli kwa kiasi fulani tu. Waingereza
wana utaratibu wa uwakilishi wenye historia ya karne nyingi za mapambano ya
kitabaka na kikatiba kati ya mamwinyi, mabwanyenye, watwana na wafanyakazi, na
kati ya ufalme wa England na falme za Wales, Scotland na Ireland, ambazo kwa
pamoja zinaunda Ufalme wa Muungano wa Uingereza (UK). Baada ya miaka mingi ya
kupambana na kumwaga damu, na baadhi ya viongozi na wafalme kukatwa vichwa,
hatimaye Waingereza walikubaliana kuwa na bunge lenye chemba au mabaraza mawili
ili kuzingatia maslahi ya pande zote. Mabaraza hayo ni lile la Mamwinyi (House of Lords) na lile la Makabwela (House of Commons). Wajumbe wa Baraza la
Mamwinyi hawachaguliwi na wananchi, na hujumuisha mamwinyi wenye kumiliki ardhi
kubwa na viongozi wakuu wa kanisa la Uingereza. Wajumbe wa Baraza la Makabwela
huchaguliwa majimboni.
Mapambano
ya kudai demokrasia nchini Uingereza vilevile yaliibua vyama vikuu viwili, kile
cha Conservative (chenye kuwakilisha
maslahi ya mamwinyi na mabwanyenye), na kile cha Labour (ambacho awali – siyo sasa – kiliwakilisha maslahi ya
matabaka ya wazalishaji – wafanyakazi, vibarua, n.k.). Siku za karibuni, mwaka
1988, kimezuka chama kingine kikuu cha tatu, Liberal Democrats, ambacho
kimetokana na muungano wa vyama vidogo viwili vya Liberal Party na Social
Democratic Party; hicho ni chama cha kiliberali cha mrengo wa kati. Vipo
vyama vingine vidogo vidogo lakini havina athari kubwa kiutawala. La muhimu
kufahamu kuhusu mfumo huu wa Uingereza ni kwamba vyama vyote vinavyoshika
utawala huendeleza takriban sera zilezile za uchumi, utaifa na mambo ya nje, na
hakuna hata kimoja kwa sasa kinachowakilisha maslahi ya mnyonge. Jingine la
kukumbuka ni kwamba mfalme au malkia wa Uingereza ni nguzo mojawapo ya Bunge la
Uingereza, kama alivyo Rais hapa kwetu.
Hivyo,
madai ya kwamba Tanzania inafuata mfumo wa Westminister yana walakini, maana
hayasemi ukweli wote. Hata hivyo, kuna jambo moja la Westminister ambalo
Tanzania na nchi nyingi za Jumuiya ya Madola zinaling’ang’ania, nalo ni
uwakilishi na utawala kupitia katika vyama. Huu ni utaratibu ulioletwa kwetu na
nchi za Magharibi, nasi tukaupokea na kuukubali bila kuusaili. Lakini je,
utaratibu huu unahakikisha kuwapo kwa mfumo bora wa uwakilishi wa makundi yote
ya wananchi?
Jibu ni
kwamba utaratibu huu hautuhakikishii uwakilishi wa kweli kwa sababu zifuatazo:
Kwanza, wawakilishi wote sharti watoke katika vyama rasmi vya siasa
vilivyosajiliwa. Kwa kuwa vyama vinawakilisha itikadi na maslahi ya wanachama
wake, hususani viongozi, hatuwezi kudai kuwa aghalabu vinawakilisha itikadi na
maslahi ya wananchi. Kwa hakika
uzoevu umeonesha kuwa takriban vyama vyote nchini Tanzania vinatetea itikadi
ileile ya ubepari na uliberali, hivyo vinawakilisha kundi lile lile la
mabwanyenye au wamiliki mali kiuchumi (hata kama katika maandiko yake rasmi
vinadai kufuata sera ya “Ujamaa na Kujitegemea”, “Nguvu ya Umma” n.k.). Tofauti
yao iko katika njia na mbinu zao za kulifikia lengo hilo la ubepari. Haya
yanadhihirika tunapoangalia sera na manifesto zao. Hali hii ni tofauti na ile
ya Chama cha TANU/CCM kabla ya Azimio la Zanzibar la 1991, ambapo utetezi wa
Umma na makundi ya wazalishaji ulikuwa ni nguzo mojawapo ya itikadi, sera na utendaji wa chama-tawala. Kwa ufupi, ukiritimba
wa vyama katika siasa unaua demokrasia badala ya kuijenga.
Pili,
mfumo wetu wa ukiritimba wa vyama unahakikisha kwamba hatuwezi kuwa na wagombea
binafsi, ambao labda wangewakilisha makundi yaliyosahaulika, na hatuwezi kuwa
na wawakilishi wa kweli wa Umma.
Wawakilishi wachache wa sasa wanaojaribu kuutetea Umma aghalabu wanajikuta
wakikemewa na hata kuenguliwa na vyama vyao, maana wanaonekana kuwa ni waasi wa
tabaka lao au vyama vyao.
Uwakilishi wa Majimbo dhidi ya Uwakilishi wa
Umma
Uwakilishi
wa majimbo si uwakilishi wa Umma ndani ya majimbo hayo, bali ni uwakilishi wa
kundi au makundi fulani maalumu, ndani ya jimbo, kulingana na itikadi ya chama kinachohusika,
na nguvu (ya ushawishi na fedha) ya wapiga kura wanaohusika. Aghalabu makundi
hayo yanayowakilishwa na maslahi yao kutetewa ni yale ya tabaka tawala –
mabepari, mabwanyeye, mafisadi na matajiri wa aina mbalimbali. Makundi ya
wakulima na wafanyakazi huwekwa pembezoni, yaani maslahi yao ya msingi hugusiwa
mara chache sana, hasa wahusika wanapohitaji kura zao.
Kuongeza
majimbo, basi, hakutaimarisha demokrasia kwa maana ya kuimarisha utetezi au
sauti ya wanyonge; sana sana kutaimarisha utetezi wa matabaka yaleyale ya wenye
mali. Na hilo ndilo lengo kuu lisiloelezwa la mfumo wa Westminster. Ili
kurekebisha hali hii tunahitaji kubuni mfumo tofauti wa uwakilishi badala ya
kuiga ule wa nchi za Magharibi.
Hivyo
pamoja na uwakilishi wa majimbo, ambao unawachukulia watu wote katika jimbo
kuwa wenye hali, maslahi na malengo sawa, tunahitaji pia uwakilishi wa makundi
maalumu ya kijamii. Makundi hayo ni yale yenye maslahi maalumu ya kiuchumi, kijamii,
kiitikadi au kitabaka. Hapa tunaweza kuorodhesha machache:
- Wakulima
- Wafugaji
- Wavuvi
- Wachimba migodi
- Wafanyakazi wa viwandani
- Wafanyakazi wa serikali
- Wafanyakazi wa mashirika
- Walimu (wa shule za msingi na sekondari)
- Wahadhiri, wakufunzi na maprofesa wa vyuo
- Weledi na wataalamu wengine (k.m. madaktari, wahandisi,
n.k.) - Askari wa Jeshi la Ulinzi, JKT na Jeshi la Kujenga
Uchumi - Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza
- Usalama wa Taifa
- Walemavu
- Wanawake
- Vijana
- Wasanii
- Wazee na wastaafu
- Wanafunzi wa msingi na sekondari
- Wanafunzi wa vyuo/vyuo vikuu
- Vikundi vya kidini – Waislamu, Wakristo, Wanajadi,
Wahindu/Wabudha, Wayakinifu (wasioamini), n.k. - Vyama vya ushirika (vya wakulima, wafanya biashara)
- Wachuuzi wadogowadogo
- Wanyabiashara wa kati (wenye maduka)
- Watoa huduma (mahoteli, bima, ushauri, n.k.)
- Mabepari/wafanya biashara wakubwa wa viwanda na
madini (k.m. kupitia Chamber of Commerce) - Wakulima wakubwa.
Haya ni
baadhi tu ya makundi ya kijamii ambayo nimeweza kuyaainisha. Bila shaka yapo
mengine. Baadhi ya makundi, k.m. lile la madhehebu ya dini, yatahitaji
wawakilishi zaidi ya mmoja – kila dhehebu na mwakilishi/wawakilishi wake, bila
kusahau wanajadi, ambao aghalabu huwa wanabaguliwa. Makundi ya wakulima na
wafanyakazi nayo yanahitaji wawakilishi wengi; vivyo hivyo kundi la wanawake.
Hapa
tunazungumzia uwakilishi wa kweli wenye kuzingatia vikundi amali na vikundi
maslahi, sio ule wa vyama vya siasa ambao unazingatia maslahi ya kundi moja au
mawili tu. Wagombea wa ubunge kupitia makundi ya kijamii wasilazimishwe kupitia au
kuungwa mkono na chama chochote cha siasa, na wachaguliwe kidemokrasia ndani ya
makundi yao kulingana na taratibu zitakazowekwa.
Bunge
la sasalina wabunge wengi sana wa kuteuliwa na Rais, wakiwamo mawaziri na
wamaziri wadogo. Hali hii inapunguza udhibiti wa Bunge kwa serikali. Aidha,
mawaziri ama wanalazimika kupendelea majimbo yao katika mipango ya maendeleo ya
wizara zao, ama hawapati nafasi ya kutosha ya kushughulikia matataizo ya
majimbo yao. Hivyo inapendekezwa Mawaziri wasiwe wabunge wa kuchaguliwa; wateuliwa
na Rais kulingana na sifa zao za kitaaluma na kiutendaji tu.
Kama
mfumo huu utafuatwa, itawezekana kabisa nusu ya wabunge wote wakawa ni
wawakilishi wa makundi-maslahi badala ya vyama vya siasa. Hii ina maana kwamba
idadi ya wabunge wa majimbo, na hivyo idadi ya majimbo, itabidi ipunguzwe ili
kutoa nafasi kwa wabunge wa makundi. Aidha, wagombea Urais wanaopata asilimia
10 au zaidi ya kura zote wawe ni Wabunge wa Kitaifa ndani ya vyama vyao. Pendekezo
langu ni kwa kila wilaya kuwa jimbo moja tu la uchaguzi. Hivyo, kwa wilaya kama
150 zilizopo sasa, tutakuwa na majimbo 150 na wabunge wa vyama wasiozidi 150.
Wakiongezwa wabunge wengine kama 100 wa makundi tuliyoyataja, na 50 wa kitaifa
na kiwadhifa (k.m. mawaziri), tutakuwa na jumla ya wabunge 300. Wanatosha
kabisa.
Kuweka Mfumo wa Uwazi wa Utawala na Uongozi,
na Kudhibiti Ufisadi
Katiba
kwa vyovyote itaelezea na kufafanua mfumo wa utawala na uongozi kuanzia ngazi
za juu [Rais na Baraza la Mawaziri] hadi zile za chini, mihimili ya dola
[Bunge, Mahakama na Serikali] uhusiano wa mihimili hiyo, na mgawanyo wa
madaraka kati yao. Hili halina utata sana; la muhimu ni kuweka uwiano mzuri
unaofafanua wazi ni chombo kipi ni kikuu zaidi – serikali au Bunge? Hapa
tungependekeza utamalaki wa Bunge juu ya mihimili mingine [pasina kuingiliana
bila shaka] utiliwe mkazo. Hatimaye, Bunge nalo liwajibike kwa wananchi, ambao
ndio waliolichagua.
Uzoevu
wa miaka ya karibuni unaonesha kuwa uongozi unapochanganywa na ubepari au
biashara ya binafsi maslahi ya Umma hutelekezwa kwa minajili ya kuendeleza
maslahi ya binafsi. Muungano huu wa siasa na biashara huzaa ufisadi, ukiwamo
wizi wa kura au kung’ang’ania madaraka, ambao hatimaye huvuruga na hata
kukwamisha maendeleo ya nchi, na hali hiyo isipodhibitiwa huweza kusababisha
vurugu, mauaji na hata mapinduzi ya serikali.
Hili ni
jambo ambalo inabidi lishughulikiwe katika Katiba. Mathalan, Katiba itenganishe
biashara na uongozi, itaje itikeli (ethics)
za uongozi, na iwe na vifungu vyenye kuwabana wanaoiba au kuchakachua kura
[watu binafsi na vyama]. Mimi ningeshauri wizi au uchakajuaji wa kura wakati wa
uchaguzi uchukuliwe kuwa kosa la uhaini. Kadhalika, Katiba iweke kikomo cha
muda wa uongozi wa ngazi na kada zote za viongozi, siyo kwa Rais tu. Siku hizi
nafasi za uongozi zimekuwa ni ajira ya kudumu badala ya kuwa fursa tu ya
kuhudumia Umma kwa zamu. Tumefikia hatua ya baadhi ya watu kuandaa mazingira ya
kuhakikisha kuwa wao, wake/waume zao, watoto na hata wajukuu zao wanarithishana
uongozi. Hivyo ningependekeza wabunge na madiwani waongoze kwa vipindi
visivyozidi vitatu kwa mfululizo [yaani miaka 15]. Aidha, kiongozi anayefanya
makosa makubwa au ambaye chombo anachokiongoza kinasababisha matatizo
yanayotokana na uzembe, ufisadi, uongozi hafifu, n.k. alazimishwe na Katiba
kujiuzulu uongozi.
Kujenga na Kuimarisha Uchumi na Uzalishaji
Hakuna
Taifa lolote duniani linaloendelea bila kujenga uchumi na uzalishaji, ambao ni
pamoja na kuendeleza kilimo, viwanda, teknolojia, n.k. Hapa inabidi kuwa
waangalifu; Katiba ikiruhusu umiliki holela wa njia kuu za uzalishaji kama
ardhi , migodi na viwanda vikubwa, ikiizuia serikali kushiriki katika masuala
ya “biashara” na “uzalishaji” hata pale ambapo maslahi ya Taifa yanahusika,
itakuwa ni kikwazo badala ya kuwa kichocheo na nyenzo ya kukuza uchumi na
kuleta maendeleo. Katiba sharti iweke uwiano mzuri kati ya uzalishaji holela wa
watu au makampuni binafsi na ule unaoongozwa au kusimamiwa au kumilikiwa na
serikali kwa manufaa ya nchi. Tusijidanganye: Hata nchi zilizoendelea sana
kibepari kama Japan, Marekani na Uingereza bado zina sekta ya Umma. Ni vizuri
Katiba ikaainisha maeneo ambayo serikali itawajibika, pekee au kwa ubia,
kuyaendesha. Hapa nafikiria maeneo kama miundo-mbinu mikubwa kama ya reli,
barabara na usafiri wa meli na ndege, viwanda vikubwa vya msingi [vya chuma,
utengenezaji wa mitambo mikubwa, mashine, n.k.], nishati, maji, uhifadhi wa
mazingira, elimu, utafiti, na uendelezaji wa teknolojia, na sekta muhimu za
utamaduni [kama vile Makumbusho, Makavazi, lugha, fasihi na vitabu], na baadhi
ya maeneo ya sekta ya Fedha.
Kujenga Umoja na Ushirikiano wa Kikanda na
Hatimaye Umajumui wa Afrika Yote
Katiba
izungumzie, kwa mtazamo chanya, suala la umoja na ushirikiano wa kikanda, na
kuweka misingi ya kuiwezesha Tanzania kuunda Shirikisho na nchi nyingine za
ukanda huu, na hatimaye kushiriki katika Shirikisho la Afrika Nzima. Msingi huu
ulikuwamo katika Katiba ya TANU tangu miaka ya 1950, na ni msingi muhimu
tunapofikiria maslahi ya Tanzania na Afrika ya sasa na baadaye. Tutake
tusitake, usalama wa Tanzania kama Taifa na nchi umefungamana na hatima ya
ukanda huu na bara zima la Afrika.
Hivyo
Katiba mpya itaje suala la Shirikisho na Umajumui wa Afrika kama lengo na dira
mojawapo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MUHTASARI WA MAPENDEKEZO
Ili
kutekeleza mawazo tulioyoyaeleza hapo juu, tunapendekeza:
- Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ibadilishwe ili iwe na mtazamo mpya usiokuwa wa ki-Westminster; - Katiba itaje alama zote za Utambulisho wa Utaifa wa
Mtanzania, ambazo ni pamoja na lugha ya Taifa – Kiswahili. - Katiba ikatae Uraia wa Nchi Mbili.
- Majimbo ya ubunge na udiwani yapunguzwe; kila
wilaya iwe ni jimbo moja tu la ubunge (kwa upande wa Zanzibar itabidi
mfumo wa wilaya urekebishwe kwa kuzingatia hali hii mpya). Uwakilishi
zaidi utokane na vikundi vya kijamii tulivyovitaja. - Chama kinachopata angalao 50% ya wabunge wote wa
majimbo kiunde serikali; kama hakuna chama kilichopata 50% ya wabunge,
iundwe serikali ya mseto; - Mawaziri wasiwe wabunge wa majimbo; waingie Bungeni
kwa sababu ya nyadhifa zao tu, na wathibitishwe na Bunge; - Mawaziri na wabunge wengine wa kiwadhifa wasiwe na
haki ya kupiga kura wakati bunge linapofanya maamuzi; - Pasiwe na wabunge wa kuteuliwa na Rais au chombo
kingine, isipokuwa wale wa kiwadhifa. - Wagombea Urais wanaopata 10% au zaidi ya kura zote
wawe Wabunge wa Kitaifa papo hapo. - Mbunge/Diwani ashikilie wadhifa huo kwa vipindi
vitatu tu vya mfululizo. Anaweza kugombea tena baada ya kukaa nje ya
Bunge/Baraza kwa angalao kipindi kimoja. - Wakuu wa wilaya wachaguliwe na wananchi wa wilaya zao
kwa kura ya siri kupitia katika vyama vya siasa, na wawajibike kwa
wananchi hao. - Katiba iweke kanuni ya uwiano wa kijinsia katika
uwakilishi. - Mamlaka ya Rais, ambayo kwa sasa ni makubwa mno na
hayasailiwi popote, yapunguzwe. Mathalan, Baraza la Mawaziri lithibitishwe
na Bunge, watendaji wakuu wa asasi na mashirika ya Umma wateuliwe na
Mabaraza au Halmashauri za mashirika hayo, na Katiba iruhusu Rais kushitakiwa
kwa makosa anayoyafanya [aweze kushitakiwa akiwa bado na wadhifa huo au
baada ya kustaafu]. - Katiba isitaje Mungu au Miungu yoyote katika kifungu
chochote, bali itoe tu uhuru wa kuabudu. - Haki ya kufanya kazi, na stahiki ya pensheni na
mafao ya haki kwa wastaafu iingizwe katika Katiba. - Mgawanyo wa mikoa na wilaya usifanywe na Rais au
serikali peke yake, bali upendekezwe na serikali na kuthibitishwa na
Bunge. - Mgawanyo wa Majimbo ya Uchaguzi upendekezwe na Tume
ya Uchaguzi na kuthibitishwa na Bunge. Hii itaepusha mwenendo tunaouona
sasa wa watu maalumu kuundiwa majimbo ya ubunge au udiwani. - Mwanasheria Mkuu wa serikali apendekezwe na Rais na
kuthibitishwa na Bunge. - Pawe na Tume Huru ya Uchaguzi na isiteuliwe na Rais
bali iteuliwe na Bunge kwa kuzingatia Sheria itakayotungwa kwa ajili hiyo. - Pawe na Tume Huru ya kushughulikia maslahi na mafao
ya viongozi wakuu, wakiwamo Wabunge. Maamuzi ya Tume hiyo yaheshimiwa na
Bunge na Serikali. Hii itapunguza mwanya wa viongozi na wansiasa kujilipa
mafao na marupurupu yalisiyolingana na hali ya uchumi wa nchi. - Katiba itaje mji mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ili kuondoa utata uliopo sasa ambapo Dodoma inashindana na Dar es
Salaam kubeba majukumu ya “mji mkuu” na hivyo kutoa mwanya kwa warasimu na
mafisadi kuitumia hali hiyo tata kwa manufaa yao. - Azma ya kuleta Shirikisho la Afrika Mashariki na
hatimaye lile la Afrika iwemo katika Katiba.
Naamini
kuwa utaratibu wa aina hii, iwapo utatekelezwa, utahakikisha uwakilishi halisi
zaidi wa wananchi, maana wawakilishi watatokana na wananchi wenyewe katika
makundi yao ya kikazi na kimaslahi. Hivyo utetezi utakuwa ni wa dhati, mawaziri
watawajibika kwa Bunge la Umma, na ukiritimba wa vyama hautakuwapo.