Unyonyaji wa ‘wamjini’ dhidi
ya ‘wavijijini’ – Tusisahau jambo hili

Zitto Kabwe, Mb

Mnamo tarehe 12 Septemba, 2012 niliandika makala iliyochapwa kwenye
magazeti mawili nchini, Raia Mwema na Tanzania Daima. Makala hiyo ‘Mafukara milioni 30, Mabilioni 30’ ilikuwa inaonyesha namna ambavyo mfumo wa uchumi wa
nchi yetu ni wa kinyonyaji. Kwamba wakazi wa mijini wanafaidi zaidi rasilimali
za nchi kuliko wakazi wa Vijijini. Vilevile nilieleza kuwa mfumo wa uchumi wa
Tanzania ni wa kifisadi na ufisadi unafaidisha kikundi kidogo cha watu mijini
au wenye tabia za kimjini na hivyo kukosesha huduma za msingi za wananchi wengi
waishio vijijini. Mwanazuoni kijana Sabatho Nyamsenda ameandika uchambuzi wake
mzuri kuhusu makala hiyo kama ‘Tangazo la Coca Cola na wito wa Zitto dhidi ya Vizito’ ambapo amejaribu kuonyesha kuwa masikini wa mijini ni sawa tu na
mafukara wa vijijini. Sikubaliani naye. Nitatumia Azimio la Arusha kuboresha
hoja yangu na pia mfano halisi wa Mwalimu wa Kalinzi, Kigoma dhidi ya Mwalimu
wa Miburani, Temeke.

Muono wangu unathibitishwa na mambo matatu. Kwanza ni kuongezeka kwa
kasi kwa tofauti ya kipato kati ya walionacho na wasionacho ambapo sasa kuna
kundi dogo la watu ni matajiri sana na kundi kubwa sana ni mafukara sana.
Nilionyesha kuwa asilimia 30 ya Watanzania wanamiliki asilimia 75 ya Pato la
Taifa. Pili, nilionyesha kuwa kasi ya kupunguza umasikini nchini inaonekana
mijini kuliko vijijini ambapo katika kipindi cha miaka 16, umasikini wa watu wa
Dar es Salaam, kwa mfano, umepungua kwa asilimia 12 wakati umasikini vijijini
umepungua kwa asilimia 2 tu. Tatu, nimeonyesha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa
vijijini ipo chini ya wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa kutokana na sekta ya
Kilimo ambayo inaajiri asilimia 75 ya Watanzania imekuwa ikikua ‘flatlining’
kwa asilimia 4 wakati Uchumi wa nchi umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 7
katika muongo mmoja uliopita.

Nilionyesha kuwa tabaka la chini la watu wa mijini ni masikini kwani
wamepewa fursa za kuweza kuondokana na umasikini wakati watu wa vijijini ni
mafukara kwani mfumo kwa makusudi umewanyima fursa. Kimombo ninasema watu wa
tabaka la chini la mijini ni ‘poor’ na watu wa vijijini ni ‘impoverished’.
Azimio la Arusha limeonyesha muono kama huu na lilionya kutosahau mwono huu
katika andiko lake. Ninanukuu.


“Vile vile mkazo wa fedha na wa viwanda unatufanya
tukazanie zaidi maendeleo ya mijini. Tunatambua kuwa hatuwezi kupata fedha za
kutosha kuleta maendeleo katika kila kijiji na ambayo yatamfaa kila mwananchi.
Tunajua pia kuwa hatuwezi kujenga kiwanda katika kila kijiji ili kisaidie
kuleta maendeleo ya fedha na viwanda katika kila kijiji; jambo ambalo tunajua
kuwa haliwezekani. Kwa ajili hiyo, basi, fedha
zetu huzitumia zaidi katika miji na viwanda vyetu pia hujengwa katika mij
i.
Na zaidi ya fedha hizi huwa ni mikopo. Japo zijenge shule, hospitali, majumba
au viwanda ni fedha za mikopo. Hatimaye lazima zilipwe.

Lakini ni dhahiri kwamba
haziwezi kulipwa kwa fedha zinazotokana na maendeleo ya mijini au maendeleo ya
viwanda. Hazina budi zilipwe kwa fedha tunazopata kutokana na vitu tunavyouza
katika nchi za nje
. Kutokana na viwanda vyetu
hatuuzi na kwa muda mrefu sana hatutauza vitu vingi katika nchi za nje. Viwanda
vyetu zaidi ni vya kutusaidia kupata vitu hapa hapa ambavyo mpaka sasa
tunaviagiza kutoka nchi za nje. Itapita miaka mingi kabla ya kuweza kuuza
katika nchi za nje vitu vinavyotokana na viwanda vyetu. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba fedha tutakazotumia kulipa madeni haya ya
mikopo ya fedha kwa maendeleo na viwanda mijini hazitatoka mijini na wala
hazitatokana na viwanda. Zitatoka wapi, basi? Zitatoka vijijini na zitatokana
na KILIMO
. Maana ya ukweli huu ni nini? Ni kwamba wale wanaofaidi
maendeleo yanayotokana na fedha tunazokopa sio kwa kweli watakaozilipa
. Fedha zitatumika zaidi katika
miji lakini walipaji watakuwa zaidi ni wakulima.


Jambo hili linafaa
kukumbukwa sana
, maana kuna njia nyingi za
kunyonyana. Tusisahau hata kidogo kwamba
wakaaji wa mijini wanaweza wakawa wanyonyaji wa jasho la wakulima wa vijijini. Hospitali zetu kubwa zote ziko katika
miji. Zinafaidia sehemu ndogo sana ya wananchi wa Tanzania. Lakini kama
tumezijenga kwa fedha za mkopo walipaji wa mkopo huo ni wakulima, yaani wale
ambao hawafaidiwi sana na hospitali hizo. Mabarabara
ya lami
yako katika miji, kwa faida ya wakaaji wa mijini na hasa wenye
magari. Kama mabarabaraba hayo tumeyajenga kwa fedha za mikopo walipaji ni
wakulima; na fedha zilizonunua magari yenyewe zilitokana na mazao ya
wakulima. Taa za umeme, maji ya mabomba, mahoteli na maendeleo mengine yote ya
kisasa yako zaidi katika miji. Karibu yote yametokana na fedha za mikopo na
karibu yote hayana faida kubwa kwa mkulima, lakini yatalipwa kwa fedha
zitakazotokana na jasho la mkulima.


Tusisahau jambo hili. Japo tunapotaja unyonyaji hufikiria mabepari, tusisahau kuwa bahari
ina samaki wengi. Nao hutafunana. Mkubwa humtafuna mdogo na mdogo naye humtafuna
mdogo zaidi. Katika nchi yetu twaweza kugawa wananchi kwa njia mbili. Mabepari
na Makabaila upande mmoja; na wafanyakazi na wakulima upande mwingine.
Pia twaweza tukagawa wakaaji
wa mijini upande mmoja na wakulima wa vijijini upande mwingine. Tusipoangalia
tutakuja kugundua kuwa wakaaji wa mijini nao ni wanyonyaji wa wakulima.” Azimio la Arusha,1967. (msisitizo ni wangu).

Azimio la Arusha limerudia zaidi ya mara moja “Tusisahau jambo hili” ama
“Jambo hili linapaswa kukumbukwa sana”. Tumesahau jambo hili. Licha ya kwamba
sisi wanasiasa wa kisasa tunaona Azimio la Arusha ni nyaraka “outdated” ipo
siku tutakumbushwa kwa njia ambayo hatutakuja kuisahau. Sitaki tufike huko.
Mwangwi wa “tusisahau jambo hili” lazima uendelee kutuonyesha kuwa kuna kazi ya
kufanya kuhusu Mafukara milioni thelathini wanaoishi kwenye vijiji vyetu.
Watanzania hawa wa vijijini hawana fursa za barabara, maji, umeme na hata
huduma za jamii kama wenzao wa mijini.

Nitatoa mfano mmoja kuonyesha tofauti ya Masikini wa mjini na Fukara wa
kijijini. Wakati nachaguliwa kuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini (jimbo la
vijijini) mwaka 2005, ilikuwa inamgharimu Mwalimu wa Shule ya Msingi Kalinzi
shilingi 15,000 kwenda Kigoma mjini kuchukua mshahara wake katika Benki ya NMB
kila mwezi. Mwalimu wa shule ya Msingi Miburani, Temeke atatumia shilingi 600
tu kwenda kuchukua mshahara wake katika Benki ya NMB tawi la Bank House
(angeweza kutembelea kwa mguu kwenda tawi la Temeke pia lakini tuchukulie alikuwa
na kazi mjini vilevile). Hawa ni walimu ambao ni daraja moja, wanalipwa
mshahara sawa lakini uwepo wa barabara (zilizojengwa kwa jasho la mkulima wa
kahawa wa Kalinzi) unampa unafuu huyu masikini wa Temeke, Dar es Salaam na
kumkandamiza katika ufukara Mwalimu wa Kalinzi, Kigoma. Mwaka 2010 barabara ya
lami ilifika Kalinzi. Barabara kubwa ya kwanza mkoani Kigoma toka Uhuru mwaka
1961. Hivi sasa Mwalimu wa Kalinzi anatumia shilingi 3,000 kwenda Benki. Ahueni
kubwa sana ambayo walimu wengi maeneo vijijini bado hawana. Ahueni aliyosubiri
miaka 40 kuipata.

Ukiangalia Bajeti ya Tanzania utaona namna ambavyo rasilimali kubwa ya
nchi inatumika kutatua changamoto za watu wa mijini na hasa Dar es Salaam.
Wabunge (ambao wengi wetu tunatumia muda mwingi sana Dar es Salaam) bila kujali
majimbo au mikoa yao hukasirikia sana, kwa mfano, foleni Dar es Salaam na
kuisukuma Serikali kutenga fedha zaidi za kujenga barabara za Dar es Salaam.
Sasa Dar es Salaam, kwa kutumia mabilioni ya fedha, zinajengwa barabara za
kupaa juu (flyovers). Umeme ukikatika Dar es Salaam, waandishi wa habari
wanaandika ‘nchi gizani’ bila kujali kuwa Watanzania wa Urughu kule Iramba  na wengine asilimia 83 ya Watanzania wapo
kwenye giza la kudumu. Zaidi ya fursa walizonazo, masikini wa mijini pia sauti
zao zinasikika. Mafukara wa Vijijini nadra kuwasikia.

Tusisahau jambo hili. Azimio lilisema.