Tumepotea
njia


Pendekezo la kitabu cha mkusanyiko wa
mashairi

Na: demere
kitunga, juni 19, 2012

1. Utangulizi

Kwa kipindi cha miongo miwili hivi, nchi
yetu inapita katika msukosuko mkubwa. Kuanzia nyakati tulizoahidiwa kufunga
mikanda kwa miezi 18 katika miaka ya 80, baadhi ya watanzania hawakuifungua
tena na si ajabu wasiifungue kabisa wakati wa uhai wao. Lakini ingekuwa ni
kufunga mikanda kwa miaka 18 ukiwa na matumaini kuwa madhila yako ni sadaka kwa
vizazi vyako vya sasa na vijavyo, labda mzigo huo ungekuwa mwepesi kuubeba.
Lakini yale tuliyoambiwa na wanazuoni wenye uzalendo wakati tunakubali sera za
utandawazi ili angalau tupate bidhaa madukani, kuwa sera hizo hazitaifanya  hali kuwa nzuri kwa watu masikini kwani
ufunguaji milango ulioshinikizwa utawafanya wapoteze hata kile kidogo
walichonacho inajidhihirisha vema sana. Historia inatudai tuchukue hatua katika
kila nyanja, ili kuinusuru hali hii, kama si leo hata iwe kesho, keshokutwa au
mtondogoo. Nasi kama watu wa kalamu na fikra, hatuna budi kuutoa mchango wetu
kwa njia moja au nyingine. Watafiti na waandishi wameshaandika sana na
wanaendelea kuandika. Lakini haitakuwa ziada mbaya kama tutaweza kutoa juzuu
moja la ushairi unaokijadili kipindi hiki cha historia. Siku moja, siikumbuki
tarehe, tuliongea haya na Profesa Shivji kuhusiana na mkusanyiko wa ‘Summons’
uliohaririwa na Richard Mabala, kwamba mfululizo wake haujapatikana. Alinichagiza
niongoze mchakato wa kupata mkusanyiko mwingine kama ule katika muktadha wetu
wa sasa. Imenichukua muda kutafakari pa kuanzia, na leo nimeona pa kuanzia ni
hapa. Kutuma mwaliko, na kuomba mrejesho na maboresho.

2. Jina:
Tumepotea njia

Kwa kuanzia nimelipendekeza jina hilo
lakini linaweza kubadilika. Wengi, pamoja na mimi, tunapenda majina yenye
mwelekeo chanya, yanayotoa matumaini. Lakini katika lugha yangu ya kwanza, Chasu,
tuna msemo usemao ‘kupotea njia ndio kuijua’. Nami naamini kuwa hali iliyopo
sasa hivi ni ishara wazi kuwa tumepotea njia kama jamii, kama kizazi, na kama
taifa. Labda tukilikubali hilo, tutatumia fursa hiyo vilevile kuitafuta,
kuifuata na kuionyesha.

3. Utanzu:
ushairi

Napendekeza ushairi kwa kuwa ni utanzu
unaoweza kubeba mawazo mazito kwa maneno machache kuliko utanzu mwingine
ukiacha methali. Vilevile ni utanzu uliokita mizizi katika fasihi na utamaduni
wa mtanzania kwa miaka mingi. Utanzu huu pia hupokea na hupendeza unapokuwa na
sauti nyingi ndani ya juzuu moja.

4. Lugha:
Kiswahili

Japo maongezi yetu yalilenga ushairi kwa
lugha ya Kiingereza, napendekeza tuanze na Kiswahili kwa makusudi. Mkusanyiko
huu utakuwa mchango wetu katika mijadala na vitendo vya kupinga hali
inayoendelea kujitokeza miongoni mwa makundi ya watanzania ambao wengi wao
lugha yao ya mawasiliano ni Kiswahili. Hii ndiyo lugha ya umma wa mtanzania
hivyo kama hatua ya kwanza katika ‘mradi’ huu, napendekeza Kiswahili.


5. Idadi,
uwiano: [nakaribisha maoni]

6. Dhamira
kuu na ndogondogo: [nakaribisha maoni]

7. Washiriki:
Washairi wazalendo [rika na jinsia zote, waliobobea na chipukizi]

Kwa kuanzia
kufikiri, itategemea na idadi ya mashairi na kama itabidi kuzalisha majuzuu
mawili na iwe hivyo. Naamini baadhi yetu tuna mashairi tayari na mchakato huu unaweza
kutupa hamasa ya kuongeza mengine. Labda tuweke ukomo wa juu wa mashairi
tutakayochangia: napendekeza kila shairi lisizidi kurasa mbili na kwa kila
mchangiaji ukomo wa juu uwe mashairi 5 ambayo yanaweza yasichapishwe yote
kulingana na maoni yatakayojitokeza katika mchakato wa uhakiki na uhariri.

8Muda:

Uandishi—kukusanya:
Juni/Julai; Uhakiki na Uhariri: Agosti; Usanifu na Uchapishaji: Septemba/Oktoba—lengo
liwe kuchapishwa kabla ya Disemba

9. Njia:

i) Ukusanyaji: Michango itumwe kwa
mhariri ambaye atapendekeza mpangilio na kutoa maoni ya kiuhakiki, na
kuyakabidhi kwa kamati ya uhariri.

ii) Uhakiki na uhariri: Mhariri
ataomba wachangiaji kupendekeza majina matano ya washairi na wahakiki wa
ushairi kuwa wajumbe wa kamati ya uhariri. Kila mwanakamati atapatiwa
mkusanyiko mzima aupitie na kutoa maoni ya uhakiki na kushauri kuhusu mpangilio
na mapengo yanayohitajika kujazwa. Kila mchangiaji atapewa maoni binafsi kuhusu
mashairi yake na mrejesho wake utazingatiwa katika hatua ya mwisho ya
uhakiki/uhariri. Kisha mswada wa juzuu la kwanza utasambazwa kwa wachangiaji
wote ambao mashairi yao yameingia ili kupata maoni yao. Mhariri ataratibu mirejesho
na kamati itapitia mirejesho yote kabla ya kuupitisha mkusanyiko kuwa
mswada.  

Uiii) Uchapishaji: Wachapishaji
rafiki na wapenzi wa fasihi watakaribishwa kuupokea mswada kwa uchapishaji kwa
masharti kuwa wataweza kuuzalisha kwa wakati uliopangwa—na kama ndivyo mkataba
utafanyika wenye kuzingatia makubaliano hayo.

11   Mrabaha:

Wachangiaji watakubaliana jinsi watakavyogawana mrabaha. Mapendekezo
ni kuwa tuwe na jambo fulani ambalo tutataka fedha zitakazopatikana zichangie[maoni
zaidi yanakaribishwa].

Demere Kitunga < demeredye@gmail.com >

Mkahawa wa Vitabu Soma