Kufundishia Kiingereza Nchini: Ni Kasumba Tu Inayodumaza Elimu!
Angalia Saa yako, unahesabu Saa kwa Kiswahili, lakini lazima
utakuwa umeirekebisha isomeke kwa Kiingereza!
Na Saidi Nguba
Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini huru, Nelson R. Mandela, aliwahi
kusema katika nukuu zake nyingi za busara, kwa Kiingereza:“If you talk
to a man in a language he understands, that goes to his head. If you
talk to him in his language, that goes to his heart.” Kwa tafsiri
yangu, ya Kiswahili: “Ukizungumza na mtu neno katika lugha
anayoielewa, linamuingia kichwani. Lakini ukizungumza naye katika
lugha yake, linamuingia moyoni mwake”.
Mbunge, Profesa Kulikoyela Kanalwanda Kahigi, ambaye ni mtaalamu wa
lugha, akizungumza katika mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, bungeni mjini Dodoma Agosti
mwaka 2011 alisema: “Lugha ni nguzo ya msingi ya kujenga uzalendo.
Vinginevyo utajengaje uzalendo kwa kutumia lugha ya kukopa ya
kigeni?”.
Profesa Kahigi aliongeza: “Tunawafundishia vijana wetu kwa Kiingereza.
Je, tunawapa maarifa vijana wetu au tunawafurahisha mabwana zetu?”.
Hii ndiyo hali ilivyo nchini Tanzania, tuna kasumba ya Kiingereza,
lugha ya kigeni na lugha ya kikoloni. Mpaka sasa, miaka 50 ya Uhuru
wa Tanzania Bara, uamuzi haujafanywa wa kuitumia Lugha hii adhimu ya
Kiswahili kufundishia nchini katika ngazi zote, pamoja na kuwa lugha
hiyo ina vigezo vyote vya kukidhi kazi hiyo. Hii haina maana kukipuuza
Kiingereza, ambacho watu wengine hapa nchini wanakiita kuwa ni
“Kiswahili cha Dunia”. Ni vizuri Kiswahili kifundishwe vizuri,
kitumike kufundishia na Kiingereza pia kifundishwe vizuri kama lugha
na liwe ni somo la lazima kwa kila mwanafunzi kuanzia darasa la
kwanza, hadi Sekondari, ili wanafunzi wote, wakifika kidato cha nne,
kwa mfano, wazungumze na kuandika lugha hiyo kwa ufasaha mkubwa.
Kasumba imefikia kuona jambo hili kuwa ni kitu cha kawaida. Kwa mfano,
ukimuuliza mtumiaji wa Kiswahili, je, sasa saa ngapi? Atakujibu, sasa
ni saa 6. Lakini mwambie aangalie alivyorekebisha saa yake. Utaona
mshale, badala ya kuwa katika sita, uko kwenye namba 12, kama vile
walivyozoea Waingereza, kwa mfumo wao wa kujua wakati. Saa 6 ya
mchana, kwa Kiswahili, Kiingereza siyo “Six o’clock” ni “Twelve
o’clock”!
Kiingereza ni Lugha siyo Elimu
Swali la kujiuliza: Je ni kwa nini basi tunaendelea na kasumba hii ya
kukipa kipaumbele Kiingereza na kupata kigugumizi cha kukitumia
Kiswahili kufundishia katika ngazi zote?
Ubishi unaoenea kwa kasi ni kuwa Kiingereza ni “Lugha ya Kimataifa” na
kwamba kwa kufundishia, vijana wetu watakuwa na elimu inayolingana
kimataifa. Pili, kwa vile hakuna vitabu vya kutosha vya Kiswahili,
ukilinganisha na vya Kiingereza, kufundishia Kiswahili, ni tatizo.
Sababu zote hizi zinamfurahisha zaidi Mwingereza tu.
Ukweli ni kwamba Kiingereza ni lugha tu na mtu anaweza akajifunza, na
kwa utaalamu wa kisasa wa kufundisha lugha na nyenzo zilizopo, hata
kwa miezi mitatu mtu anaweza akakielewa na kuzungumza. Lugha siyo
elimu, isipokuwa ni chombo cha kusaidia kutolea elimu. Elimu ni uwezo
mkubwa wa kuelewa na kugundua mambo, ili hayo unayoyaelewa na
kuyagundua yatakusaidia kuleta mageuzi katika maisha yako na ya
binadamu wengine, kutoka kiwango fulani na kwenda kiwango cha juu
zaidi chenye kuleta manufaa na tija. Ili elimu nayo itolewe kwa vizuri
zaidi ni lazima lugha ya kufundishia iwe ile ambayo anayefundisha na
anayefundishwa wote wanaifahamu vizuri. Pili, hakuna vitabu vya
Kiswahili nchini kwa sababu havina soko. Mara uamuzi wa kufundishia
Kiswahili utakapochukuliwa, basi vitabu vya Kiswahili vitakuwa
biashara kubwa na vitaanzishwa hata “viwanda” vya kufyatua vitabu vya
elimu mbalimbali kutoka lugha za kigeni na kuwa vya Kiswahili.
Wataalamu wamekwishathibitisha
Uwezo wa Kiswahili kufundishia ili hatimaye elimu ikue kwa kiwango
kikubwa nchini na kujenga taifa la kujitegemea badala ya kuendelea
kuwategemea wengine kwa kila kitu, siyo mahitaji ya kisiasa, bali ni
jambo linalowezekana na lililothibitishwa na wanataaluma wa elimu na
wa lugha pia.
Profesa John Kiango, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati anamkaribisha Waziri Mkuu Mizengo
Pinda kuzindua Taasisi mpya ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Julai 26, 2009, alisema: “Nikiwa mtaalamu wa lugha, napenda
nichukue nafasi hii, kukuhakikishia kuwa Kiswahili kinaweza, na
kikipewa nafasi kitaleta mageuzi ya kitaalamu na kiugunduzi nchini.”
Anaongeza:“Tafiti zimebaini kuwa nchi zote zilizo na ugunduzi asilia
ambao siyo ule wa kuiga ni zile zinazotumia lugha zao. Nchi
zinazotumia lugha za kigeni katika kutolea elimu zimebaki kuwa
watumiaji wa teknolojia zilizogunduliwa mahali pengine, teknolojia
ambazo tunauziwa kwa bei mbaya sana.”
Hatutaki tu kuuona ukweli. Kwa mfano, ukimuandaa mtaalamu wa Kilimo
hadi anapata shahada, akija kuwa Bwana shamba kijijini, je elimu yake
atawapatia wale wakulima kule vijijini kwa lugha gani? Kiingereza,
alichojifundishia au kwa lugha ambayo walengwa wanaielewa? Kwa vile
madhumuni ya elimu ni kwa watakaobahatika kuipata wawagawie maarifa na
huduma wengine, kwa nini sasa tunalazimika hapa hapa nchini ambako
tuna lugha yetu, kuifundisha elimu hiyo kwa lugha ya kigeni na ya
kikoloni? Kama elimu utaipata kutoka China, ni dhahiri lazima
kujifunza kwa Kichina.
Katika kitabu “Focus on fresh data on the Language of Instruction
debate in Tanzania and South Africa” kilichoandikwa na Brigit Brock-
Utne, Zubeida Desai na Martha Qorro, mwaka 2006, ikiwa ni sehemu ya
matokeo ya tafiti za LOITASA (Language of Instruction in Tanzania and
South Africa) ambayo ni Mradi wa NUFU (The Norwegian Programme for
Development Research and Education) ulioanza mwaka 2001 na
unaomalizika mwishoni mwa mwaka 2011, imebainishwa jinsi lugha ya
Kiingereza ilivyokuwa tatizo katika ufundishaji kwenye shule za
Sekondari nchini Tanzania.
Utafiti wa LOITASA ulifanywa katika shule mbili za Sekondari kwa
kutumia utaratibu wa kufundishia somo la Baiolojia – darasa moja kwa
Kiingereza na darasa jingine kwa Kiswahili. Kwa mujibu wa kitabu
hicho, katika darasa lililokuwa linafundishiwa Kiingereza, wanafunzi
walionekana kutochangamka na hawakuelewa kilichokuwa kinaendelea,
wakati lile la Kiswahili, wanafunzi walikuwa wanachangia kwa uelewa wa
hali ya juu na ukawepo mjadala wenye tija baina ya mwalimu na
wanafunzi.
Tume ya Rais ya Elimu, iliyojulikana kuwa Tume ya Makweta (mwanasiasa
na mwanataluma mashuhuri nchini) ilitoa mapendekezo ya kutaka
Kiswahili kitumike katika ngazi zote, hatua kwa hatua, kuanzia kidato
cha kwanza mwaka 1985 na Chuo Kikuu kuanzia mwaka 1992. Mapendekezo
hayo mpaka sasa hayajatekelezwa.
Mapema tangu mwaka 1953, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi
na Utamaduni (UNESCO), lilitoa azimio lililosema, pamoja na mambo
mengine, ni vema hasa kwa elimu ya msingi kwa watoto wadogo,
kuwafundisha kwa lugha wanazozielewa vizuri na hasa lugha za mama zao.
Sasa, kama wataalamu wamekwishamaliza kazi yao na kuthibitisha kuwa
Kiswahili ni lugha inayojitosheleza kwa msamiati karibu katika kila
fani, mbona Kiswahili hakitumiki nchini katika kufundishia, hasa elimu
ya juu? Kwa nini?
Jibu la uhakika ni kwanza, matokeo na athari ya kutawaliwa na
Waingereza na hivyo kupandikiza ndani ya akili zetu hali ya
kutojiamini wenyewe, kuanzia katika lugha na hata katika maeneo
mengine. Kazi yetu ni kuwategemea wengine, wa nje tu. Pili, kasumba tu
ya kawaida kwamba Kiingereza ndiyo elimu na tatu ni kusita kuchukua
uamuzi.
Sera; Dira, hazitekelezwi
Sera ya Elimu ya Mwaka 1995 nchini inasema kuwa Lugha ya Kufundishia
ni Kiswahili na Kiingereza. Sera hiyo inafanyiwa mapitio, lakini
katika maandiko ya awali ya marekebisho yanayopendekezwa, haionekani
kwamba uamuzi unafanywa wa kukitumia Kiswahili katika ngazi zote.
Kwa mfumo wa sasa nchini, kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba,
lugha ya kufundishia ni Kiswahili, lakini kuanzia kidato cha kwanza
hadi kwenye vyuo, lugha ni Kiingereza. Ingawa ukweli ni kwamba hata
kwenye vyuo, mwalimu akiona haeleweki kwenye ukumbi wa mhadhara, huwa
anabadilisha lugha na anatumia Kiswahili na mara mambo yanabadilika na
kwenda vizuri.
Katika Sera imetamkwa rasmi kuwa: “Serikali itakuza elimu ya awali ya
watoto wenye umri wa miaka 0-6. Elimu hii itahakikisha kudumishwa kwa
maadili yetu kiutamaduni”. Lakini hali halisi ya sasa, ni tofauti na
tamko la Sera. Siku hizi kuna shule za binafsi nyingi zilizochipukia
zinazofundisha kwa Kiingereza, ziitwazo kwa Kiingereza “English-Medium
Schools”, hata kwa zile za elimu ya awali, tena nyingine ada ni lazima
kulipwa kwa fedha za kigeni, hasa za Kimarekani, Dola! Kwa msingi huo,
haitawezekana kuwa elimu hiyo “itahakikisha kudumishwa kwa maadili
yetu ya kitamaduni”, kama yenyewe inatolewa kwa lugha ya kigeni ya
kikoloni na kulipiwa kwa fedha za kigeni!
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, sehemu yake inasema: “Tanzania haina
budi ijijengee misingi ya kujitegemea inayotokana na mazingira ya
ukombozi wa kisakolojia, kifikra na kuweza kujiamini ili jamii iweze
kuamua kuliongoza gurudumu lake la maendeleo kwa lengo la kutosheleza
mahitaji ya msingi ya watu wote, wanaume, wanawake na watoto”. Je,
tutaliweza hilo kwa kufundishia lugha ya kigeni, ya kikoloni?
Ni siasa, uchumi na utamaduni
Karibu nchi zote duniani, zinatumia lugha zao kufundishia. Lakini
katika Afrika karibu nchi zote (isipokuwa Ethiopia, inayotumia lugha
yake ya Amharic na maandishi yake, pamoja na nchi za Kaskazini mwa
Afrika zinazotumia Kiarabu na maandishi yake) zinatumia lugha za
kigeni za Kiingereza, Kifaransa au Kireno, zilizorithiwa kutoka kwa
Wakoloni hao. Haishangazi basi kuwa miaka 50 sasa tangu ukoloni
uondoke, bado tunakuwa tegemezi kutoka kwa wakoloni hao.
Msomi B.F.P. Masele, katika makala yake yenye kichwa cha habari:
“Kiswahili au Kiingereza? Siasa na lugha muafaka ya
kufundishiaTanzania,” alikariri “janga” lilioikuta nchi ya Afrika ya
Madagaska iliyoamua mwaka 1975 kutumia lugha yake ya asili ya
Kimalagasi, inayofahamika na kutumika kwa ufasaha zaidi nchini humo,
katika nyanja zote za maisha ya watu, ikiwa ni pamoja na kufundishia
elimu ya awali hadi vyuo vikuu.
Kwa mujibu wa Masele, baada ya Madagaska kukumbwa na hali mbaya ya
kiuchumi, nchi ya Ufaransa, iliyokuwa ikiitawala zamani, ilishinikiza
kuwa Kimalagasi kifutwe kama lugha ya kufundishia au kutumika katika
shughuli nyingine rasmi kitaifa. Serikali, ikalazimika kukirudisha
Kifaransa kuwa lugha kuu Madagaska baada ya kupewa ahadi ya fedha
kutoka Ufaransa ili itatue matatizo yake ya kiuchumi. “Hili ni somo
muhimu sana kwa Tanzania na nchi zote zinazofanana nayo”, anasema
Masele.
Masele anaongeza: “Utekelezaji wa maamuzi ya matumizi ya Kiswahili
kufundishia katika ngazi zote za elimu umekuwa mgumu ingawa jambo
lenyewe liko wazi kiutafiti, kitaaluma, kipedagogia na kimantiki tangu
zamani. Ugumu unatokana na ukweli kwamba, ingawa Kiswahili ni suala
linalohusu lugha, mizizi yake ya fitina imejikita katika uwanja nyeti
wa siasa, huku siasa hii ikifungamana na masuala ya uchumi na
utamaduni. Bila ya kuichokonoa mizizi hii kutoka katika siasa, uchumi
na utamaduni ilikojificha, si tu itakuwa vigumu, bali haitawezekana
kukithamini Kiswahili”.
“Waafrika,” Masele katika makala hiyo amemnukuu mtaalamu mwingine
nchini, M.M. Mulokozi akisema: “ni watu wa pekee duniani waishio kwa
vitu vya kuazima; utamaduni wa kuazima, dini za kuazima, lugha za
kuazima, majina ya kuazima, teknolojia ya kuazima, fasihi/fani za
fasihi za kuazima, nywele na rangi za ngozi za kuazima, sanaa za
kuazima, mavazi ya kuazima, vyakula vya kuazima…vitu ambavyo wengi
wetu vinatufanya tuwe viumbe bandia, vichekesho vya dunia.”
Hivyo basi ni maoni yangu kuwa, kwa vile miaka 50 imekwishapita tangu
uhuru bila ya kukifanya Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia nchini
katika ngazi zote, maandalizi yaanze sasa kwa kufundishia Kiswahili
Sekondari na baadaye Chuo Kikuu. Kwa namna hii, utamaduni wetu
utaendelezwa, vijana wetu wanaopata elimu watajijua vizuri wanatoka
wapi na wanakwenda wapi na watakuwa na kitu cha kujitambulisha kama
taifa. Isitoshe elimu itapanuka mno na taifa litapata wataalamu
wanaoweza kujitegemea na wazalendo na hivyo utajengeka utamaduni wa
kuwaamini wataalamu wetu na siyo wa nje. Ikifikia hapo, kasi ya
maendeleo nchini itakuwa kubwa mno, kwa muda mfupi sana, kiajabu.
(mwisho)
• Saidi Nguba aliwahi kuwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti
yanayochapishwa kwa Kiswahili ya UHURU (2000 – 2004) na Mwananchi
(2004 – 2005). Hivi sasa ni Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu. Haya
ni maoni na mawazo yake binafsi.
Simu: 0754 -388418, Barua-Pepe: sanguba@gmail.com
Naomba niulize swali moja: kwani Afrika Kusini inalugha ngapi? Kama ni uzalendo basi nasi tuwafuate na kuruhusu lugha zinazoingia moyoni zinazoongelewa na makabila makubwa kama sehemu ya kujenga uzalendo(i.e. Kihaya,Kisukuma,Kichagga,na Kinyakyusa etc). Pili tukumbuke hili la lugha ya kikoloni halina mantiki maana kabla ya mkoloni Kiswahili haikua lugha ya taifa:hiyo iliketwa na mkoloni pia-kwanini tunabagua ukweli kwenye kujenga mada? Mwisho,je hicho kiingereza kwani kimetoka wapi: mbona hata huko uingereza nacho ni lugha ya kikoloni maana ilikopwa kwa waliowatawala. Jamani tuwe na fikra endelevu sio uzalendo wa kijinga!
☆Kiswahili kilikuwepo kabla ya Wakoloni kuja huku…!
☆Afrika Kusini, kama Zambia, Uganda, Zimbabwe n.k. wanatumia lugha za Makabila yao makubwa kwa kuwa hawana lugha moja inayowaunganisha. Hatuwezi kuwaiga, tutakuwa tunarudi nyuma na kuendeleza ulabila.
☆Taifa ni Lugha. Kama huna Lugha moja huna Taifa, ni vikundi tu vya Makabila. Tanzania, tumekwishafika pazuri kama Taifa, tuna Lugha Inayotuunganisha na siyo Taifa kwa Kijiografia kuzingatia mipakwa iliyowekwa na Wakoloni. Msimamo huo wa kuitetea na kuendeleza ma kuienzi Lugha yetu siyo “uzalendo wa kijinga”.