Wakati tunamshukuru Mungu kwa kuwanusuru abiria waliokuwa wamepanda ndege ya ATCL iliyopata ajali Kigoma na kusikitika kuhusu hali mbaya ya kampuni/shirika hilo huu ni wasaa wa kuirejea mistari hii ya shairi la Issa Bin Mariam almaarufu kamaProfesa Issa G. Shivji na kujiuliza, je, kulikoni kurejea kwa twiga wetu?

Twiga Katoroka – Kajiheshimu

Nimemkosa,

Sikumuona.

Akisimama wima,

Kama askari,

Na kiburi chake.

Kwa heshima na taadhima,

Akiimba kwa sauti nyororo:

“Mabibi na Mabwana,

Nawakaribisha kwenye

ndege hii ya Serengeti,

ndege ya Shirika la Ndege la Taifa.”

Twiga kakimbia,

Kenda kwao.

Kwao upo?

Mahali pake mkiani

Peupeeeeee….!

Nyeupe ya rangi,

rangi ya ubaguzi.

Ninashindwa,

kumeza.

Mkate na mayai, yao:

Prepared and Packed

in Pretoria.

Nimeinamisha kichwa.

Ninatetemeka kwa aibu.

Nawaona kwa kuibia.

Dada zangu wawili,

Wanyonge.

Bila tashi wala tamaa.

“Here we’re

Carlesberg for you, sir.”

“na…na….naomba safari.”

“I…I…I’d like safari.”

“Sorry…er….”

Twiga katoroka,

Kenda na heshima zake.

(Kajiheshimu)

Katorokea wapi?

Mbuga zao,

Watalii wao,

Ndege yao.

Kibendera chetu!

“Jjambo!

Captain Roaming Rogue speaking.”

Buriani Twiga.

Kwaheri za kuonana.

Kama sio kesho,

Keshokutwa.

3 Aprili 2003

Comments Off on ATCL KULIKONI TWIGA WETU?