Sitaomboleza

 

Rafiki yangu, kamaradi Henry Mapolu

Sijaja kukuzika

Sijaja kukuaga

Sitaomboleza

Sitabubujika

 

Nimekuja na marafiki zetu

Na makamaradi wetu

Kupokea mchango wako

Kujikumbusha mfano wako

Ewe kamaradi!

Unatukumbusha mengi ya usafi, sio ya ufisadi

 

Uhongo wa kisiasa uliukata,

Ukaenda wilayani

Udisi wa Mzee Ruksa haukufarijisha,

Ukauficha ukayani

Aha! hili halikuwa geni kwako

Kwani ulijiuzulu Uzuoni,

Ukaenda Urafikini

 

Mwito wako kuinua uelewa wa proletari

Hukujali kutunikiwa uzamili wa profesari

Ulituachia mabepari-chipukizi

Wakicheza ngoma ya ulimbikizi

 

Tumefika kukuenzi

Kwa fikra na mawazo yako

Kwa mtazamo na msimamo wako

Na waledi usiotetereka

Uaminifu usiopingika

 

Wapo kina Adamu na Zakia

‘Bakileki na Bgoya

Karimu na ukarimu wake

Na Kashiwaki namuona pake

 

Wapo pia Joe na Jenerali

Sio wa wanajeshi

Wa waandishi-wacheshi

Sitaki niwasahau Mwami na mwenzie Masanja

 

Eti wakijidai wanasosolojia viranja

 

 

Qorro wa Karatu

Amefuatana na Msoma Salumu

Aliyekuwa anatusalimu

‘Venceramos! A luta continua’

Ndio kamaradi: A luta continua

 

Amekuja pia Rameshi

Vijana wakimtania ‘wa Bangladeshi’

Na mwandishi mwenzio Nizari

Aishio nchi-kavu Kariakoni

Akijitambulisha orijino wa nchi-Visiwani

 

Namuona mheshimiwa Liundi, balozi

Akipambana na mawimbi ya machozi

Na Mzee Butiku amekaa majanini

Unakumbuka tulivyomsumbua ujanani?

 

Nimemuona rafiki yako wa siku zile za Kivukoni

Mzee wetu, mzee Ngombale wa Kiliwani

Alikuwa anakuulizia juzijuzi

Nipashe za Kamaradi Henry asiye na upuuzi

 

Sikuwa na ujasiri wa kumkumbushia

Barua yako ya wazi ulomrushia

Uonjo mkali wa kalamu yako katili

‘Ewe kamaradi wangu wa prolitari

Usikubali kupigwa teke na siasa za jemadari’

 

Kamwe sitosahau unyekekevu na utulivu wako

Kiburi uliepuka kama tauni, jazba zilikuwa geni kwako

Nilipotunga hadithi ya Amina na kijana mwanafalsafa

Nilikuwa nakuwazia wewe na usawa wa yako falsafa

 

Shati nje ya suruali, na ndara za kanda mbili

Ukiishi katika risachi fleti namba mbili

Yenye kuta pasi picha wala pambo

Isipokuwa Mzee Maksi na madevu yake ya majigambo

 

Ndugu yangu, rafiki yangu, Kamaradi Henry – mbele sitaenda

Nakuachie salamu za kamaradi chipukizi Sabatho Nyamsenda:

‘Afrika imepoteza mmoja wa makamanda muhimu

katika vita dhidi ya mfumo huu dhalimu …’.

 

Issa bin Mariam

02/02/2011

 

Ndugu zangu,

Henry Mapolu ameaga dunia, juzi Jumapili jioni.

Ni kati ya waanzilishi wa Chama cha USARF na jarida la Cheche katika chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya 60. Kwa mliopata kitabu cha “Cheche” mtakuta makala / taarifa zake.

Kwa mliosoma kitabu cha Walter Rodney “How Europe Underdeveloped Africa”, mtakuta ametoa shukrani kwa watu wawili: Karim Hirji na Henry Mapolu.

Prof. Shivji anamwelezea Henri Mapolu kama ifuatavyo:-

Henry alichagua kuwa upande wa wanyonge mapema katika maisha yake tukiwa sote Chuo Kikuu, na kushiriki katika vuguvugu la mwamko wa nadharia na itikadi ya Ujamaa kwa mtazamo wa Kimaksi. Baada ya kufuzu shahada ya uzamili, bila kusita, Henry akaacha kazi yake ya uhadhiri chuoni na kujiunga na Kiwanda cha Urafiki kama Afisa Elimu ili aweze kutoa mchango wake kwa kuamsha uelewa wa wafanyakazi na wavujajasho juu ya hali yao halisi. Mimi binafsi ninafarijika kwamba niliwahi kufanya kazi naye kuandika, kukusanya na kuhariri makala ambayo yalichapishwa katika kijitabu kiitwacho ‘Vuguvugu la wafanyakazi Nchini Tanzania’. Maandishi ya Henry Mapolu yataendelea kuwa nyenzo mojawapo katika mapambano ya wavujajasho dhidi ya mfumo katili wa ubepari.

Issa Shivji

30/01/2010

Hakika Afrika imepoteza mmoja wa makamanda muhimu katika vita dhidi ya mfumo dhalimu wa ubepari / ubeberu.

MAPAMBANO YA KUBOMOA NGOME YA UBEBERU YANAENDELEA

Sabatho Nyamsenda

 

  1. Mbele February 2, 2012 at 8:25 pm

    Nimeshtuka kupata taarifa hii. Nilipoingia Chuo Kikuu Dar kama mwanafunzi, mwaka 1973, ndipo nilipoanza kumwona na kumsikiliza Henry Mapolu. Alikuwa mmoja wa wanaharakati waliotupa changamoto sisi vijana. Wanaharakati wengine walikuwa akina Issa Shivji, Mahmoud Mamdani, Yash Tandon, Dan Wadada Nabudere, Walter Rodney, Grant Kamenju, Josaphat Kanywanyi, Frank Mbengo, Gilbert Gwassa, Haroub Othman, Walter Bgoya, Kingunge Ngombale Mwiru, na wengine zaidi, kutoka Tanzania, Afrika Kusini, Uganda, na kadhalika. (Kwa vile nimemtaja Kingunge, napenda tu kusema kuwa Kingunge Ngombale Mwiro wa leo si yule wa miaka ile, alipokuwa Kivukoni)

    Tulijifunza mengi kutoka kwa wote hao. Henry Mapolu alibobea sana kwenye suala la wafanyazi na uongozi wa wafanyakazi. Kazi aliyoifanya, pamoja na wanaharakati wenzake, ilitupa motisha sisi vijana wa TANU Youth League, na baadhi yetu tulikuwa tulijiunga na naendesha jarida la "Maji Maji," ambalo lilikuwa ndio mrithi wa "Cheche." Kuondoka kwake kunatuachia pengo kubwa, ila mchango aliotoa ni hazina itakayoendelea kuwepo.

    Natoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki. Mungu awape nguvu ya kustahimili kipindi hiki kigumu, na amweke marehemu mahali pema Peponi. Amina.

Comments are closed.