Na Muhanyi Nkoronko

@MuhanyiSenior

Utangulizi

Jana Waziri wa Afya wa Tanzania alitangaza kuongezeka tena kwa wagonjwa wenye virusi vya corona hadi kufikia 6. Taarifa hizi kwa kiasi kikubwa zilinishtua sana, nikaingiwa na woga kuwa tunakwenda kufa wote. Wasiwasi ulinizidi nilipofikiria mrundikano wa watu Kariakoo, kwenye mabasi ya mwendokasi na daladala.

Tahadhari mbalimbali zinachukuliwa na umma unajulishwa. Waziri Mkuu amekwishatangaza kuwa vyuo vyote, shule za msingi na sekondari kufungwa. Wanafunzi wametakiwa kusalia majumbani kwa muda wa siku 30 ili kupunguza kasi ya virusi vya ugonjwa huo uitwa COVID-19.

Kuingia kwa ugonjwa huu kumesababisha kwa kiasi fulani umma kuwa na taharuki na wasiwasi mwingi. Taharuki hii inaweza kupelekea kuongezeka kwa maambukizi hivyo kuathiri utolewaji wa huduma za afya na kijamii nchini kwa mujubi wa dhana ya #DhibitiMlipuko (#FlattenTheCurve). Ili kutoathiri udhibiti wa mlipuko ni muhimu kuendelea kuutuliza umma na kuondoa taharuki na kuongeza juhudi za pamoja kujikinga na ugonjwa huu.

Sababu za Taharuki

Mosi, taarifa mbalimbali za vifo duniani kupitia vyombo vya habari huweza kuleta taharuki. Kwa mfano, siku ya Jumatano nchini Italia kuliripotiwa maambukizi mapya mengi na vifo 475 kwa siku. Jambo la msingi kwa umma ni kuelewa kuwa kuna njia nyingi rahisi za kujikinga na maambukizi na kuzuia vigo. Pia kuna habari njema za kuongezeka kwa jitihada ya kutafuta chanjo na hata tiba.

Pili, fikra potofu kuwa kila anayeumwa ugonjwa huu ni lazima afariki. Ukweli ni kuwa watu wengi wanaoumwa ugonjwa huu hupona na hurejea katika maisha ya kila siku. Kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali nchini, hadi kufikia leo asubuhi, wagonjwa 88,465 walikuwa wameshapona duniani kote huku wagonjwa 140,071 wakiwa katika hali nzuri. Ni jukumu la viongozi na jamii kwa ujumla kuutuliza umma juu ya ugonjwa huu maana unazuilika na kudhibitika pale tahadhari za mapema zinapochukuliwa na wote. Ni muhimu pia kuelewa ni namna gani kirusi hiki kinasambazwa na ni kundi lipi lipo katika hatari zaidi kuathirika na virusi hivi kama wazee, watu wenye historia ya magonjwa ya muda mrefu na watu wenye kinga dhaifu. Tunapaswa  kujikinga ili kuwakinga wengine.

Tatu, fikra za kukosekana ama kuadimika kwa bidhaa muhimu za kujikinga na vifaa kinga. Ni wazi kuwa mahitaji ya vifaa kinga yameongezeka sana hivyo kupelekea watu waliokosa mahitaji hayo kuwa wako hatarini zaidi. Hili ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa bidhaa na vifaa muhimu hazihohodhiwi na watu wachache. 

Mambo ya Kuzingatia

Ni muhimu kuelewa mambo ya msingi ili kupunguza maambukizi na kujikinga na virusi vya corona. Pata taarifa sahihi. Epuka kusambaza uvumi na taarifa zisizo sahihi. Linda afya ya mwili wako. Kula chakula bora kilichoandaliwa katika hali ya usafi.  Nawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka. Usijishike usoni.

Weka akiba ya vyakula muhimu na vifaa kinga. Lakini haimaanishi umalize kila kitu sokoni na dukani kwa maana wengi wanahitaji pia. Hili litatusaidia kuondokana na taharuki isiyokuwa na lazima.

Hitimisho

Tusitaharuki. Ugonjwa huu sio mwisho wa maisha. Maisha lazima yaendelee. Kilicho muhimu ni kuzizingatia jitihada zetu za kijamii na za kiserikali kujikinga na kudhibiti maambukizi. Tuwe watulivu.