Jasper “Kido” Sabuni
Siku ya juzi, majira ya mchana, Tanzania ilitangaziwa rasmi juu ya uwepo wa virusi vya corona. Hali ya sintofahamu na taharuki nayo ikajitokeza. Mitandao ya kijamii ilifurika jumbe na vibonzo mbali mbali kuhusiana na mgeni corona. Njia mbalimbali za tahadhari zilitolewa na elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa huo imeendelea kutolewa.
Wakati yote hayo yakifanyika, nilipata kujionea mapicha picha. Jioni hiyo ya jana nilionana na mtu, wakati wa mazungumzo naye, pembeni alikuwa na kitakatishi mkono (hand sanitizer). Kabla ya hapo, ofisi niliyokuwepo waliagiza kununuliwa kwa vitakatishi (sanitizer) kwa ajili ya wafanyakazi. Aliyetumwa alirudisha taarifa kuwa wakubwa wa kazi, wafanyabiashara, waliona na kuitumia vyema fursa ya wimbi la wahitaji na hivyo kuongeza bei maradufu, chini ya kaulimbiu mujarab ya dimandi endi saplai (demand and supply).
Hapa kule niko naenda kuonana na ndugu zangu kadhaa kipande cha Mwenge Mpakani nikakutana na mandugu kadhaa wamevaa viziba uso (maski). Haki vile nilijihisi niko Wuhan ghafla. Huyo, nimefika ninakoenda nimesalimiana na mandugu, Bi Mkubwa kanipa tano (ndio tunavyosalimiana kila siku), wengine tumepeana mikono, ila dada yangu akagoma hata kunisogelea, akaishia kunipungia. Kweli damu nzito kuliko maji, lakini corona nzito zaidi, hadi sista akanichinjia baharini salamu ya kugusana.
Tukiwa tunaendelea na mazungumzo nikawa ninawatizama wale mandugu waliokuwa na viziba uso. Mmoja alinifurahisha sana, japo sio kwa uzuri. Alinyanyua kiziba uso akafikicha pua, akaipandisha miwani aliyokuwa amevaa na akafikicha kidogo macho alafu akajiziba tena. Kabla ya hapo, yeye na wenzake wananyanyuka na kuingia mara kwa mara kwenye duka lao, ambao wao walikuwa wameketi nje. Wote waliovaa viziba uso na wasiovaa wanashika mlango huo huo, bila tahadhari yeyote ile katika sehemu hiyo ya mlango.
Muda ulivyozidi kuyoyoma, ilibidi tuagane. Ndugu zangu hao wakasema wao wanaita Uber, hawataki msongamano wa daladala, kujiepusha na corona. Hapo nikakumbuka jibu la mtu mmoja Twitter aliyeuliza, “Kwani Arteta [Kocha wa Arsenal] alipanda daladala la wapi hadi akaupata [ugonjwa wa corona]??” Nikawaacha wao wakiendelea na utaratibu wao wa Uber mimi nikaenda kupanda daladala, wakati naondoka niliwaambia wacha nikapambane na Corona ya Umma wakati wao wakijishughulisha na Corona Private.
Kwenye daladala hapo ndio kulikuwa na vituko kupitiliza. Tunafika Mwenge, watu kituoni wamejaa, gari za Bunju zilikuwepo mbili lakini watu hawazitaki hizo wakakimbilia daladala yetu iliyokuwa na nafasi. Wakapanda abiria kadhaa, konda akaja kujaribu watu warudi nyuma lakini watu waligoma kusogeleana, nje napo watu hawataki kuingia. Walibaki kusubiri gari nyingine ambayo haijajaza. Dereva vunga na wewe, nje konda ita abiria wapi… watu wamegoma, hawaitaki corona.
Ndani ya daladala, paliibuka zogo. Mdada wa watu alihamaki aliposhikwa na mtu aliyekuwa nyuma anataka kupita. Kaka wa watu akaomba msamaha, kisha akaomba wapishane. Yule dada kwenye kumpisha alikuwa ameshika bomba na kwenye kusogea nyuma, mkono wake uliteleza kwenye bomba na akaenda kushika maeneo yale yale nyuma alipokuwa ameshika yule kaka. Hapo nikajiuliza ni nini haswa yule dada alikuwa anaogopa, kushikwa moja kwa moja ilihali kama ni hatari ya corona alikuwa nayo kwani bomba lile lile linashikwa na abiria wengi. Isitoshe wakati wa kupanda pale Mwenge walipigana vikumbo haswa.
Yote ya yote nikafika ninakoenda, nikaingia sehemu ya kula. Kwenda kunawa, maji hakuna, nauliza, ninajibiwa maji yameisha. Kwa lugha nyengine wewe kula tuu bila kunawa. Nilifadhaika sana. Nikaenda kuchukua chakula cha kufunga badala yake nikaona sio tabu. Niko njiani lakini nikaanza kujiuliza nimekasirika nini… wale wadada maji wananunua na hivi sasa saa tatu usiku wapi wakanunue maji waniletee mimi. Maji walioyapangia kwa siku hiyo yameisha, nao wanatonga na bajeti (wanaenda na bajeti), sasa inakuwaje mimi na ma-corona ndio tuingilie bajeti?
Maswali kadhaa wa kadhaa nilipata kujiuliza. Wapo watu wanatuambia tunawe mikono, lakini Shirika la Afya (WHO)wanasema kuwa inabidi iwe kwa maji yanayotiririka (running water), je maji hayo tunayapata wapi kwenye hizi jamii zetu za kawaida zisizokuwa hata na mabomba ya umma. Ni kweli suluhu kuu ni usafi haswa wa mikono, lakini kwa maji yapi yaliyokuwepo bwerere na yanayotiririka katika jamii kwa umma wa Tanzania kujinawia kila inapobidi?
Ni dhahiri na kweli isiyofichika kuwa umma wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unajishughulisha na ujira wenye kuwapatia kipato cha kila siku. Sasa kwa hili la kuepuka kuchangamana ndipo linakuja swali la kwamba mtu atakula nini iwapo hatachangamana? Kuhusu usafiri wa umma, sisi watumiaji hatuna budi kuwasili kwa ndugu muajiri kama kweli tuna dhamira ya dhati ya kutunza vibarua vyetu, sasa ni vipi tutajiepusha na usafiri wetu pendwa na sisi sio watu wa Uber? Na hata ukiambia daladala zisipakize sana, vipi na konda naye tajiri amempunguzia hela ya kuwasilisha sababu ya corona? Na mwendokasi ukitoa angalizo wapakie watu wachache, ni namna gani utazuia watu kujiepushia kupakia hizo mwendokasi wakati waajiri hawana msalie mtume zaidi ya kazi, tena nao wajinadi kuendeleza sera na kaulimbiu ya #HapaKaziTuu.
Virusi hivi vina mahitaji makubwa sana kukabiliana navyo. Miongoni mwa mambo mengine, inasisitizwa kujiepusha na matumizi ya pesa ngumu na iwapo utatumia isiwe hela ya kudai chenji. Yani kama kwenye daladala uwe na hela kamili kwani kitendo cha hela kubadili mikono kinaongeza uwezekano wa kuwapo kwa ugonjwa huo. Lakini hali ikoje kwa umma wa Tanzania, je kwa mifumo yetu ya kianalojia tunaweza vipi kujinusuru na hii hali?
Kuhusu watu kufanya kazi kutoka nyumbani…je, ni kazi ngapi zinaweza kufanyika hivi? Na ni asilimia ngapi ya watu katika soko la ajira ndio wanufaika wa kazi hizo? Lakini vipi kuhusu utegemezi wa watu wengine kwa kundi la hao wanaoweza kufanya kazi kutoka nyumbani? Mfano, wauza chakula maeneo ya ofisi za Vodacom wataathiriwa kwa kiwango gani iwapo Vodacom itawaamuru wafanyakazi wake kufanya kazi tokea nyumbani? Ni familia ngapi zitakazoathirika kwa hatua hiyo na hatua nyingine za namna hiyo? Yapo maswali mengi sana ya msingi yanayoambatana na ugonjwa huu ambao binafsi ninauona kuwa ni Ugonjwa wa Kishua, uliokuja kwa ndege, lakini wenye hatari na athari kubwa kwa watu wa kawaida – wasio hata na hati ya kusafiria.
Kwa ujumla, ugonjwa huu unahoji zaidi mfumo wa kimaisha na kidunia uliokuwepo na unaowaweka watu wa hali ya chini katika hatari ya maisha kwani wao hawawezi kumudu gharama za vitakatishi wala hawana ujasiri na uwezo wa kuita Uber; sio wanufaika wa mifumo rafiki ya upatikanaji maji, usafiri na huduma nyingine za kijamii; wao sio wenye maamuzi wala uhakika wa maisha yao; na wao, licha ya matamanio yao, hawawezi kuishi maisha yenye staha.
Ikiwa corona huwa na madhara zaidi kwa watu wasio na mifumo imara ya kinga, ni matumaini yangu kuwa licha ya changamoto zetu za kiafya na kimwili, mifumo ya kinga ya umma wa Tanzania itakabiliana na virusi hivi. Na ni matumaini yangu kuwa ulimwengu mzima utatumia wasaa huu kutizama na kujitafakari na kuangazia kuhusu mfumo tawala wa kimaisha uliokuwepo wenye kuhatarisha maisha ya wengi.