Dada wa Kazi: Upumzike kwa Amani Salome Zacharia (17)

Na Jacqueline Halima Mgumia

Dada wa Kazi (DwK), Salome Zacharia, alikuwa na miaka 17 tu, alipochapwa na kuteswa na mwajiri wake huko mjini Arusha mpaka kufariki dunia, mwezi Machi, 2020.

Mwenyezi Mungu amrehemu.

Natumia jina la “Dada wa Kazi” japo hata asili au maana yake siijui. Niombe radhi kwa hilo, maana kwa sasa nina fundo wala siwezi kusubiri kuanza kutafuta maana ya jina la dada wa kazi. Siku zijazo nitatafuta maana yake, labda itatoa mwangaza wa kuelewa zahama zinazowakuta wasichana wa kazi za ndani na mahusiano yao na waajiri wao. Pia nafasi zao na maisha yao ndani ya nyumba za waajiri wao. Labda yaweza ikawa ndio chanzo cha kuvuliwa utu na thamani yao. Sijui. 

Ila kwa sasa nianze kwa kusema, siyo utu, wala uungwana kumpiga msichana wa kazi kwa sababu yoyote ile! Eti kaiba, kasema uongo, hajaaga, sijui ana kiburi au kaunguza mboga. Wewe ni nani? Kumpiga mtu mpaka anatoa damu! Na wala nafsi yako haishtuki? Mbaya zaidi, kipigo hicho kinarekodiwa na kusambazwa mitandaoni kama vile funzo kwa wasichana wengine! Kweli?

Naandika haya nikiwa na huzuni moyoni, kufuatia video niliyoiona leo ikizunguka mitandaoni, ikimuonesha Salome akiwa anapigwa na mwajiri wake ambaye yeye haonekani kwa sura bali sauti yake inasikika. Eti wanamwonesha Salome akiwa anaadhibiwa kwa wizi! Salome anaonekana akiwa amechoka kwa kupigwa na kujaribu kutoa maelezo ambayo hayaeleweki. Amechoka na kujawa na taharuki machoni, lakini kipigo hakimwachi. Wala kashfa ya maneno haipungui. Kakaa chini kwenye godoro linaloonekana lina matone ya damu. Anahema na kugugumia huku mgongo wake ameugemeza ukutani. Juu amevaa fulana ya pinki na chini, sketi ya rangi ya udongo. Kwenye fulana yake mkono wa kushoto kulikuwa na matone ya damu ambayo yalikuwa yanatoka katika kucha zake. Pia sehemu ya mapaja na mikono yake yalikuwa yamevilia damu. Fimbo zinasikika na mara sauti yenye ukali na kejeli inauliza na kufoka!

Mwajiri: Haya hela yangu iko wapi? Legeza na hayo macho kama unazimia. Hela yangu iko wapi?

DwK: Hela yako? (Salome anauliza kwa mshangao na uchovu)

Mwajiri: Mhmmm

DwK: Ipo pale chini

Mwajiri: Ya nini?

DwK: Chini

Mwajiri: Eeh! Chini ya nini? (kimya) Chini ya nini?

DwK: Chini

Mwajiri: Chini ya nini?

DwK: Chini ya pale nani hii….

Salome hatoi jibu la kueleweka. Mwajiri anaghafilika na anaendelea kumchapa Salome ambaye bado anashindwa kueleza kwa ufasaha pesa iko wapi. Baadaye taarifa za ziada zinasambaa zikionesha kwamba Salome alishutumiwa kwa kuiba shilingi 50,000 ambazo kumbe zilikuwa ni sehemu ya shilingi 100,000 zilizoibwa na mtoto wa mwajiri na nusu yake kugawiwa Salome. Mtoto wa mwajiri alikiri kuiba pesa hiyo na akaadhibiwa kidogo. Lakini Salome alichelewa kukiri labda kwa kuwa hakuwa ameiba, au kwa kuwa hela ilikuwa haipo maana binti wa mwajiri alieleza alipompa Salome hiyo pesa aliituma Singida kwa mama yake. Inasemekana baada ya kipigo, hicho, Salome alifungiwa ndani kwa siku mbili bila chakula wala huduma. Hali yake ikawa mbaya na kukimbizwa hospitalini ambapo umauti ulimkuta. 

Matukio ya namna hii katika jamii ya kitanzania yameanza kuwa mengi japo siyo kwa kiwango cha Salome, mengine yakiwa chini ya mateso yake na mengine zaidi. Naandika kwa sababu nimeshahadithiwa na kushuhudia mateso ya kupigwa kwa wafanyakazi. Nakumbuka siku moja jioni, wadada wa kazi wawili wa jirani walinitembelea kwa dharura. Baada ya maongezi marefu, msichana muongeaji akamwambia mwenzake, fungu aone. Kuangalia, lo, jicho la kulia lilikuwa jekundu na amevimba shavuni. Yule binti akaniambia, “unaona! anampiga mara nyingi tu! Anambamiza ukutani anavyotaka!” Ilinilazimu kwenda kuongea na mwajiri wake ambaye aliona aibu na kukiri kutorudia. Ila matokeo yake alimfukuza kazi yule binti. Siku nyingine, nilimsikia mwajiri mmoja katika maongezi ya kijamii akisema, “kale kabinti kaliniuzi, nikakachapa vibao!”

Ukiwauliza kosa ni nini unapata majibu ya kuwashambulia kama vile, “hawa wasichana vichwa maji” au “mcharuko.” Pia mara nyingi unapata majibu ya kujihami yakidai wamejitahidi kuongea kwa upole na upendo nao lakini wasichana hao wameshindwa kujifunza na kubadilika; wengine huenda mbele zaidi kuonesha ukarimu wao kuwa wanawalipa mshahara mnono, wanakula chakula pamoja nao, wanawatibu wakiwa wanaumwa na hadi kuwapa zawadi za nguo zao lakini hawana shukrani au hawaoni thamani ya utu wao. Lakini kimsingi, sijawahi kusikia sababu yoyote ya msingi ya – na wala siamini kuna sababu inayolazimisha mtu – kupigwa au kutukanwa kwa kufanya makosa ya kibinadamu haswa katika umri wa ukuaji, kati ya miaka 14 hadi 18, ambalo ndilo rika la wasichana wengi wa kazi.

Si kwamba madada hawakosei. Najua wanakosea tena sana tu, na sisi kama waajiri tunakosea tena kwa kiwango kikubwa tu. Nayasema haya mimi kama mwajiri wa wasichana wa kazi kwa miaka 13 sasa. Ndani ya muda huo nimeajiri wasichana wapatao 7 wenye umri upatao kati ya miaka 18 hadi 40. Niliyekaa naye zaidi ni kwa miaka mitano, ambaye mimi na majirani zangu tulipatana naye na hadi kumwandalia harusi alipoamua kuolewa. Si kwamba alikuwa tofauti. Labda damu zetu zilipendana au alikuwa na uvumilivu mkubwa kwangu. Wengi waliofuata niliishi nao kati ya mwaka mmoja hadi miwili tu. Kila mmoja na changamoto zake na raha zake. Walinikera na mimi nikawakera. Hivyo tukatafuta namna na kuvumiliana mpaka tamati yetu ilipofika. Katika kipindi hicho hicho kuna kumbukumbu nyingi za furaha kwangu, kwa mwanangu, na hata kwa wasichana hao.

Yupo pia ambaye alikaa kwa siku moja, akachoka ndani ya masaa 48 kwani matarajio yake ya kazi ilikuwa ni mtoto mmoja. Kwa bahati mbaya siku aliyokuja alikuta watoto wapatao sita ndani ya nyumba waliokuja kumtembelea mwanangu. Kufika tu, alitakiwa kuwaangalia na kuwapikia wakati nikiwa nimeenda kazini. Niliporudi jioni aliniuliza kwa uwazi, “dada sikujua kuna watoto wengi hivi?” Na mwanangu bila kujua, akajibu, “kila wiki marafiki zangu huja hapa na kulala.” Hakuwa tayari kuwaangalia watoto wale. Akaaga akaenda zake. Kwa hakika hiyo ilikuwa ni haki yake maana hayo ya kuangalia watoto wa ziada hayakuwa makubaliano yetu ya awali yaliyomfanya kuvutiwa kuja kufanya kazi kwangu.

Hivyo, napoamua kuandika makala haya, uzoefu wa kukaa na wasichana ninao ila kila kukicha nimegundua kuna changamoto kubwa sana ya maisha yetu ya nyumbani na wasichana wa kazi. Kuna mahali kuna tatizo, na kutupasa kutafakari. Sisi kama waajiri, wanawake, na walezi kwa wakati huo huo. Hapo bado sijazungumzia changamoto za wanaume na wasichana wa kazi. Zipo nyingi, lakini kwa leo naziweka kando. Nazungumzia nafasi ya dada wa kazi ndani ya nyumba, na madhara yake katika familia nzima iwapo haki yake inakandamizwa. 

Ukifanya tathmini ya juu juu kupitia maongezi ya mitandaoni na maongezi ya mitaani, naweza kusema tatizo la ukosefu wa ajira halipishani kwa umaarufu na changamoto za wasichana wa kazi. Kila kukicha wasichana wanaacha kazi na waajiri wanatafuta wasichana, huku malalamiko yakizidi kuongezeka. Wapo wanaolalamika wasichana wa siku hizi hawashikiki. Wengine wanatoa maangalizo ya malezi mabaya ya wasichana kwa watoto. Wapo wanaodhani utendaji wa kazi wao umeporomoka. Pia wapo wanaowalaumu waajiri, kwamba wengi wetu hatuna utu na huwafanyisha kazi wasichana zaidi ya vijakazi. 

Mosi, nianze kwa kukiri, mimi kama mwajiri nina shida zangu nyingi inapokuja katika mkataba wangu wa kazi na wasichana wa kazi za ndani. Pili, ni masharti ya kazi ninayoyatoa kwa wasichana hao. Wapo walioshindwa kuwahi kuamka, na wale waliochelewa kurudi nyumbani. Wapo waliovunja vyombo na kuunguza mboga. Wapo waliokuwa wezi na kuvaa nguo zangu, na wapo waliopenda kuangalia TV na kupuyanga tu nikitoka. Kama mwajiri matukio yote haya yalipotokea, nimekuwa nikihamaki na kushikwa na hasira. Mara kadhaa nimerudi nyumbani na kukuta msichana wa kazi katoka bila ruhusa, au mara nyingine napigiwa simu kwamba mtoto kafikia kwa jirani kwa sababu dada hayupo nyumbani.

Niliwahi kupigwa bumbuwazi siku moja niliporudi nyumbani kwa ghafla na kukuta binti wa kazi kavaa nguo yangu. Nilipomuuliza akaniambia, mbona Kariakoo zipo nyingi tu? Na ipo siku msichana aliomba ruhusu kwenda kwa nduguze lakini alisahau nguo za kubadilisha nyumbani. Nikawapigia ndugu zake baada ya kumkosa hewani, cha kutisha hakuwa amelala kwao. Moyo ukanidunda nikihofia janga gani limemkuta. Inasemekana alilala kwa jirani. Kwa sababu zipi, siyo muhimu kwa sasa, ila siwezi kusema kwa hakika alilala wapi. 

Hakika wasichana wa kazi nao wana shida zao, tena nyingi tu. Ila nizionavyo mimi nyingi ni changamoto za ukuaji, makuzi na mazoea. Mosi, wasichana wengi wanatoka katika hali duni katika maeneo ya vijijini bila mafunzo ya kazi katika mazingira ya mjini. Hivyo, hujikuta wakilazimika kujifunza vitu vingi kwa haraka. Kuna wakati inakuwa vigumu kupokea maelekezo ya mwajiri na kuyazoea mazingira yao mapya kwa wepesi. Pia baadhi ya waajiri wanalalamika kuwa mabinti wanakula sana, wakati mwingine hadi vyakula vya watoto. Wengine wanalalamika kazi yao kuangalia TV na kuongea na simu muda mwingi. Ikumbukwe vitu hivi wengi wanakutana navyo kwa mara ya kwanza kwa mwajiri hivyo ni kawaida kwa binadamu kukamia kitu hadi mazoea. 

Pili, waajiri wengi wanalalamika wasichana wana viburi, watembezi, na wanapenda wanaume. Tukumbuke huo ndiyo muda wa ukuaji wa mwili kibailojia na wasichana hao hupitia mabadiliko makubwa sana ya kimwili na kiakili, hivyo, vitu hivyo havikosi kuwepo na huhitaji busara ya mtu mzima kumuonesha binti mwangaza. Wapo pia wasichana ambao ni wezi, wasiosema ukweli na wengine hutumia vitu vya matajiri wao. Lakini tumeshawahi kujiuliza kama huwa tunawafikiria wasichana hawa kama wanawake wanaokua na waotaka kupendeza? Au je tumeshawahi kufikiria kwamba hizi ni tabia ambazo zinaweza kukanyika?

Nadhani ninachotaka kusema ni kuwa kuchukua msichana wa kazi wa umri wa chini ya miaka 20, ni wajibu mkubwa kwa mwajiri. Wakati unataka akufanyie kazi, lazima ukumbuke huyu ni mtu huru. Siyo mfungwa wa kitwana. Kama mtoto ana hitaji muda wa kucheza na atafanya makosa, ndiyo sehemu ya makuzi. Kama ni msichana, atatamani wanaume na kutaka uhuru. 

Hivyo, jukumu la mwajiri, ni kujifunza ni namna gani ya kuishi na wasichana wa kazi, sio kwa kuwanyonya nguvu kazi tu, bali kuweka nyumba yako au ajira yako ijali makuzi ya mfanyakazi wako. Kama maofisini tunaongelea maendeleo ya mfanyakazi na haki zao, je, maendeleo ya dada wa kazi ni yapi na haki zake ni zipi? Kama ofisini tuna siku ya mapumziko ya wiki na likizo, dada wa kazi anapumzika lini? Iwapo ofisini kuna bima ya afya, je, wa kwako umemkatia?

Kimsingi, iwapo unaajiri msichana wa kazi chini ya umri wa miaka 20, wewe ni mwajiri mlezi. Tambua una nguvu ya kumjenga msichana huyo au kumbomoa. Mjenge ajengeke.