Chambi Chachage

@udadisi


Tumetangaziwa kuwa kesho tarehe 13 Oktoba 2020 Rais wa Tanzania, Dakta John Magufuli, atatuongoza sisi Watanzania wazalendo kupokea mgawo wa ~ shilingi bilioni 100 kutoka kwa kampuni ya dhahabu ya Barrick/Twiga. Hakika ni ni jambo la kufurahia na kufurahisha. Lakini nilipoliona tu tangazo hilo niliyakumbuka makala niliyoyaandika hivi karibuni kuhusu jinsi ya Kuhadaa Halaiki kwa Takwimu za Madini.


Msingi wa makala hayo ambayo baadhi ya wasomaji hawakuupata haukuwa kudai kuwa takwimu za madini siyo halisi ama kupima ni za uongo au ukweli. Ilikuwa ni kuonesha kuwa takwimu zina sayansi yake lakini pia zina siasa zake. Ndiyo maana kuna kipindi niliandika pia makala yaliyohoji: Sayansi au Siasa ya Utafiti wa Twaweza?


Sasa leo nataka tena kuzirejea takwimu zetu za mapato ya dhahabu kama ambavyo zimekuwa zikitolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) mara kwa mara. Ukitazama picha ya kwanza hapo chini utaona mwelekeo wa mauzo ya dhahabu nje ya nchi katika kipindi cha mpito kutokea Awamu ya Nne kwenda Awamu ya Tano ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ni dhahiri kuwa mauzo yalipungua kutoka Dola za Kimarekani milioni 1,457.9 mwaka 2014 hadi milioni 1,266.7 mwaka 2015 na kupanda kidogo hadi milioni 1,364.4 mwaka 2016 bila kufikiwa kwa kiwango cha juu cha awali cha mwaka 2014.


Kwa kawaida, sababu za mapato yatokanayo na uuzaji wa dhahabu nje ya nchi kupanda au kushuka ni nyingi tu, kwa mfano, soko la dunia, utashi wa wawekezaji na jinsi serikali husika inavyosimamia mauzo. Hapa kilicho muhimu ni kutambua kuwa utoaji na tafsiri za takwimu zozote hutegemea sana namna ambavyo zinawasilishwa mathalan kwa kuonesha vipindi vifupi vifupi au/na virefu. Vipindi vifupi ni rahisi sana kuonesha mafanikio makubwa mno kama yapo. Ila vipindi virefu ni halisia zaidi kwa maana vinakuonesha mwelekeo wa miaka mingi.

Picha ya kwanza hapo chini ambayo imetolewa mwaka huu inaonesha pia kipindi kifupi cha miaka mitatu ila wakati wa Awamu ya Tano. Ni picha nzuri yenye mvuto mkubwa hasa kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 28 ya mwezi huu wa Oktoba 2020. Kwa nini? Kwa sababu inaonesha mabadiliko makubwa sana yaliyo chanya kati ya mwaka 2018 ambapo mapato yatokanayo na uuzaji wa dhahabu nje yalikuwa Dola za Kimarekani milioni 1,446.4 na yakaruka hadi milioni 1,785.3 mwaka 2019 na kufikia hadi milioni 2,728.7 mwaka huu wa 2020. Na tena hayo mamilioni ni mabilioni!


Msomaji, kama wewe ni mdadisi kama mimi utakuwa unajiuliza, ziko wapi takwimu za mwaka 2017? Sijaziona kwenye kabrasha la BOT la Agosti 2017 ambalo ndilo huwa linapaswa kutoa takwimu za kufikia Julai 2017. Ukiziona naomba unijulishe. Kama kweli hazipo labda ni kwa kuwa huo ndiyo muda ambao sakata kati ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli na Kampuni ya Barrick lilikuwa limepamba moto hata kusababisha kutungwa kwa sheria mpya, sakata ambalo wanaharakati na wanazuoni wetu wamelichambua kwa kina kwenye hizi makala zao:Watanzania Kizimbani: Jinsi Kampuni za Madini Zilivyojipanga Kuiangamiza Tanzania (Sabatho Nyamsenda); How good is the deal between Barrick and the Government of Tanzania? (Danstan Kweka)State Participation in Mining Investment: Will Tanzania witness Optimal Benefits? (Lucy Linus)On Criticism of HakiRasilimali and ACT-Wazalendo (Thabit Jacob).


Picha hiyo hapo chini kutoka kwenye kabrasha la BOT la mwezi Agosti 2019 inaonesha miaka miwili tu, yaani haituoneshi ule wa tatu – mwaka 2017. Hili linaibua maswali ambayo majibu yake inawezekana yapo kule kwenye yale majedwali mengi ya BOT hasa yale ya kwenye programu ya Excel tovutini. Ila kwa msomaji ambaye ni mdadisi zaidi kazi kwako kulinganisha picha hii hapa chini na hiyo picha hapo juu.

Lakini kwenye kabrasha la Novemba 2018 la BOT kuna takwimu za mwaka za hadi kufikia mwezi Oktoba 2017 kama zinavyoonekana kwenye hiyo picha hapo chini. Usiniulize kwa nini linaonesha miaka miwili tu siyo mitatu kama zile zingine. Kilicho muhimu ni kujiuliza kwa nini taarifa kama hii ya mwaka 2017 haipewi kipaumbele kwenye taarifa tulizooneshwa mwaka 2019 na tunazooneshwa mwaka huu wa 2020? Je, ni kwa sababu hapo tunajionea kupungua kiasi kwa mauzo ya nje kutoka la Dola za Kimarekani milioni 1,549.4 mwaka 2017 hadi milioni 1,528.6 mwaka 2018. Wafukunyuzi watakuambia kupotezea huko kwenye takwimu za sasa eti kisa huu ni mwaka wa uchaguzi.

Wadadisi wa mambo ndiyo maana tulipouona mwaliko wa kuongozwa kesho na Rais kupokea gawiwo (la faida) kutoka kwa ile ile kampuni ya ‘kibeberu’ ya dhahabu tuliyoingia nayo ule ubia tukajua ni yale yale. Yale ya kushawishiwa kama siyo kupumbazwa au hata kuhadaiwa kwa mng’aro mzuri wa takwimu za madini. Lakini hatuwezi kuwa Tomaso asiyeamini, hivyo kesho tutadamka kwenda kupata mshiko wetu.

 Tupo tunaotamani takwimu za madini ziachwe tu zijieleze zenyewe kwenye maisha yetu ya kila siku. Tunataka dhahabu inayoonekana kwenye majedwali ya BOT ya takwimu za ‘akaunti ya mizania ya malipo ya nje na ndani’ (balance of payment) ikitoka kwenye dola za Kimarekani milioni 1,288.4 mwaka 2014 hadi milioni 2,215.1 mwaka 2019 ziachwe zijisemee zenyewe kwenye kuutokomeza umaskini wa kipato cha watu. Lakini zikiachwa tu bila kampeni nani ataziamini?


Na bila tafakuri tunduizi nani atajua si kila king’aacho ni dhahabu?