Tazama ni jinsi gani inavyopendeza kuona Rais wetu akisoma kwa makini, tena mbele ya kadamnasi, ripoti ya Afrika kuhusu namna ya kutimiza Malengo ya Maendeleo ya Milenia kabla ya 2015. Picha hii iliyopigwa huko Misri kwenye mkutano wa AU iliupamba ukurasa wa mbele wa gazeti la Majira la jana na Tovuti ya Magazeti ya Serikali. Picha hii imenikumbusha mahojiano/taarifa ya Dk. Asha-Rose Migiro (pichani) wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje kuhusu moja ya ziara za Rais kule USA. Mama Migiro aligusia kuwa pamoja na kubanwa sana na ratiba ya ziara, Rais alitafuta upenyo na kwenda katika mitaa ya huko ughaibuni kununua vitabu.

Tukio hili pia limenikumbusha ila dhana ya ‘Kilongola’ ambayo iliingizwa katika misamiati yetu pale Bungeni na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kabla kulazimika kujiuzulu Kutokana na lile sakata la Richmondgate, Dk. Ibrahim Msabaha. Kwa ufupi, Kilongola ni mtu anayewaongoza wenzake katika jambo fulani muhimu. Tena kama anavyosisitiza Jenerali Ulimwengu katika makala yake ya Kazi ya ‘Kilongola’ kuonyesha njia, huwa inakuwa vyema mtu huyo akiwaongoza wenzake kwa vitendo na sio kwa maneno tu.

Tanzania yenye utamaduni wa kusoma inawezekana. Rais wetu anaonyesha njia. Risala zake zinadhihirisha ni kiasi gani Rais na wasaidizi wake wana utamaduni wa kusoma. Rais ndiye Kilongola wa kuivunjilia mbali ile dhana mgando ya kwamba ukitaka kumficha Mwafrika jambo fulani basi liweke katikati ya kitabu, yaani, kwenye maandishi. Tumuunge mkono. Na kama vitabu tulivyovitumia darasa la kwanza enzi zile vinavyotukumbusha, tusome kwa furaha!