Mvutano mkali kati ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Dk. Wilbroad Slaa, na Waziri wa Utawala Bora, Philip Marmo, unazidi kupamba moto. Hoja ya Marmo ni kuwa Slaa anakiuka taratibu na Kisheria kwa kuwa na nyaraka za siri za Serikali. Kwa upande wake, Slaa anasema Marmo ndio anakiuka sheria kwa kuficha nyaraka za kifisadi.

Mgongano wa hoja zao unadhihirisha kuwa haki ya ya Kikatiba ya wananchi kupata taarifa muhimu zinazohusu masuala muhimu kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 18bado ina tafsiri tete. Hii inatokana na ukweli ni vigumu kujenga hoja kuwa Slaa anavunja sheria kwa kuwa hakuna sheria inayosema ufisadi ni siri za Serikali – au ipo?

Mjadala uliozuka kuhusiana na suala hili ni vyema ukaendelea ili kupanua wigo wa uelewa wetu kuhusu haki yetu ya kupata taarifa. Maswali ya kujiuliza ni kuhusu uzito wa Kisheria wa hoja hizi:

“Sisi tulimuonya [Slaa] kuwa asiendelee kuchukua nyaraka bila kufuata utaratibu ili asije kupata matatizo mbeleni. Huwezi kujitetea kuwa umevunja nyumba na kuiba kwa sababu una njaa, kwa hiyo ufisadi isiwe sababu ya kutofuata Sheria za nchi…Dk. Slaa ni Mbunge ambaye anafahamu Sheria na yeye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa hivyo ni rahisi akafuata taratibu zilizopo na akapata nyaraka anazohitaji kuliko kutumia njia zisizo halali… Sote tunapinga ufisadi lakini lazima tufuate sheria” – Philip Marmo

“Wanataka kunikamata mimi eti kwa kupata nyaraka za Serikali lakini anayestahili kukamatwa ni Waziri Marmo ambaye anaficha wizi na ubadhirifu kwa kisingizio cha siri za Serikali. Mimi nimetoa vielelezo vya wizi, hivi wizi na ubadhirifu vinahusiana vipi na Sheria ya siri za Serikali?`” – Dk. Wilbroad Slaa