Miaka 10 iliyopita Udadisi ilitoa ujumbe usemao ‘Watanzania Wajizatiti/Wajidhatiti Twitter!’ Mtandao huo wa kijamii wa Twitter ulikuwa ndiyo kwanza una miaka minne toka uanzishwe. Kipya kinyemi. Upya huo ulileta hamasa na kuchochea mijadala mikali.
Sasa mwongo mmoja baadaye kuna kipya kingine. Kina jina lenye utata maana ukimuuliza mtu upo Clubhouse wapo wanaodhani ni ‘klabu’ ya kunywa vileo au ukumbi wa starehe za usiku. Hivyo, unajikuta inabidi ueleze kuwa huo ni mtandao mpya wa kijamii.
Orodha ya Watanzania waliokuwa sehemu ya mijadala ile ya mwaka 2011 Twitter ina wadau – wanasayansi, wasanii, wanasiasa, wajasiriamali na wenye fani zingine nyingi tu – ambao sasa mwaka huu wa 2021 wapo au wanaingia kwa kasi kwenye Clubhouse.
CH, kama Clubhouse inavyojulikana kwa kifupi, ilianzishwa mwaka jana. Sifa yake kuu ni kuwapa fursa watu wengi kutumia sauti zao badala ya maandishi kujadiliana kwenye vikundi. Kwa kutumia simu (janja) za viganjani, watu hujumuika kwenye ‘vyumba’ vya klabu tofauti kujadili masuala anuwai. Unaweza kutoka na kuingia wakati wowote kwenye chumba chochote kile kilicho wazi.
Hadi leo klabu ya Watanzania yenye ufuasi mkubwa kuliko zote ni ‘Kumekucha Tanzania’ ikiwa na wanaklabu 2400. Kila kukicha, kuanzia saa moja na nusu asubuhi katikati ya wiki au saa tatu asubuhi kwa siku za mwisho wa juma na sikukuu, wanakumekucha hujadili mada motomoto zilizojiri kwa mujibu wa vyombo vya habari. Magwiji wa sekta mahususi pia hujumuika kutoa ‘madini’.
Vilabu vingine vyenye vyumba vilivyo na mvuto mkubwa ni pamoja na ‘Sheria Poa’ cha saa 12 jioni kila Jumatatu na cha ‘Laws of Tanzania 101’ cha saa 12 jioni kila Jumanne. Kama majina yanavyoonesha, vilabu hivi hutoa mada na kujibu maswali tata na tete kuhusu sheria. Kwa mfano, kumekuwa na mijadala kuhusu sheria za kazi na za ardhi, masuala ya uraia pacha, na kesi za mirathi.
Wanateknolojia wetu nao wana vilabu kama ‘Girls in Tech Tanzania’, ‘African Women and/in Tech’, na ‘Tanzania Tech Corner.’
Biashara asubuhi, wahenga walinena. Na sisi tunaongezea, biashara mtandao. Clubhouse imewavutia wajasiriamali wanaoitumia vilivyo kutangaza na kuuza vitu mbalimbali kwa wanavilabu. Kwa kweli maua ya Rahab Krestinina kwenye hili hayana mfanowe!
Pia wajasiriamali hao wana vilabu, kama vile ‘Tanzania Businesses’ na ‘TZ Entrepreneurs Den’ , pamoja na vyumba mbalimbali vya ‘kufagiliana’/’kutangazana’. Pia magwiji wa ujasiriamali hufungua vyumba vya ‘kushirikishana’ mbinu zao za kijasiriamali.
Ndani ya Clubhouse pia utakutana na madokta kama Winluck Shayo, Maryam Amour na Francis Furia kwenye klabu ya Afya4All.
Raha utaipata utakapojiunga na klabu ya Mwandishi wa Furaha ya Ally Abdallah, bingwa wa ‘chemsha bongo’ na ‘tuliza moyo.’
Klabu ya aina yake ni pamoja na Mwanzo@Tanzania iliyofunguliwa na Ezekiel Lengaram. Ifikapo kila Jumanne saa moja usiku magwiji mahsusi kutoka ndani au nje ya nchi hualikwa na kufanya ‘mahojiano’ ya wazi na wanaklabu kuhusu fani zao. Klabu hii imefanikiwa kuwahoji ‘waalikwa’ kama Zuweina Farah, Craig McLeod, Salum Awadh, Jeff Barr, Carol Ndosi, na Ahmed Asas.
Twitter ilipoanza, Udadisi kwa kujitakia ilichelewa sana kujiunga. Safari hii iligomea mwaliko mwaka jana wa kujiunga Clubhouse ikidhani ni yale yale. Ila kama ilivyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu, onjeni nanyi muone (utamuwe). Basi imeshaonja na kuona kweli nyumbani Clubhouse kumenoga. Patamu hapo. Hivyo, nayo imefungua klabu ya Udadisi kujadili yanayojiri tovutini humu.
Idadi ya vilabu vya Watanzania inazidi kukua kama kalenda hii na picha hizi zinavyoonesha. Clubhouse ni kama Buffet, yaani mlo utoao fursa ya kuchagua tu aina mbalimbali ya vitu utakavyokula bila kikomo au chumba chenye milo anuwai. Ndani ya CH kuna vyumba vya muziki, sayansi, teknolojia, dini, tafakuri, michezo, utani, mazoezi n.k. Ingia tu humu https://www.clubhouse.com .
Thank you for great work Dr. Chambi. Samahani Kiswahili changu sio bora kuweka kuandika kwa Kirefu ila nashukuru na kukupongeza tena kwa website yako. Asante kwa kufeature mwanzo@Tanzania.
Well explained, nimeshadowload clubhouse kwenye simu yangu but sina mtu wa kunialika can you assist me with that pls🙏🏾🙏🏾🙏🏾🙏🏾
Safi, nitumie namba yako ya simu editor@udadisi.com nikutumie mwaliko.
Asante sana kwa kuendelea kujenga na kuelimisha jamii, Dr. Chambi! Shukran tena kwa kuipa nafasi klabu ya Mwandishi Wa Furaha.
Mh Ngoja nipakue
Asante kwa article. Mmesahau FPL TANZANIA. Room kwa wapenzi wa Fantasy Premier League waliopo Tanzania