Miaka 10 iliyopita nikiwa nimekaa kwenye jukwaa la wageni waalikwa katika sherehe za uhuru wa Sudan ya Kusini, nilimwona mzee mmoja akitembea taratibu akiwa amepinda mgongo na kitambaa cheupe mkononi. Alikuwa akitembea uwanjani kuelekea jukwaani siku hiyo ambayo Jamhuri ya Sudan Kusini ilitangazwa kuwa huru. Shughuli za uhuru zilikuwa zimeanza na uwanja ulikuwa umejaa pomoni kukiwa na wakuu wa nchi na serikali kutoka bara zima la Afrika.
Uwanja ulikuwa kimya nadhani kwa bumbuwazi kwani kila mtu alikuwa amekaa lakini mzee huyu alikuwa akiendelea kutembea kuelekea jukwaani. Kulikuwa na kitambo. Mwendesha shughuli alitangaza kwa umma kuwa huyo anayetembea si mwingine bali ni Kenneth David Kaunda. Uwanja ulilipuka kwa kelele, nderemo na vifijo. Jukwaa Kuu la Marais na Mawaziri Wakuu wote walisimama kupiga makofi mpaka Mzee Kaunda alipoketi.
Ilikuwaje aingie uwanjani wakati Marais wote akiwemo Rais mwenyeji wameshaingia, lilibaki swali la wengi pale jukwaani nilipokuwa nimekaa. Baadaye nilifahamishwa na Maafisa wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Tanzania kuwa Mzee Kaunda alikuwa amefika muda ule kwani ndege yake ilichelewa. Mapokezi yake pale uwanjani yalionesha jinsi ambavyo wazee hawa walioanzisha na kuendesha vita ya ukombozi walivyobaki na heshima zao hata katika maisha yao ya ustaafu. Kwa Jamhuri ya Sudan Kusini, Rais mstaafu wa Zambia na Mwenyekiti wa pili wa Nchi Za Mstari wa Mbele kuhudhuria siku yao ya kuwa taifa huru ilikuwa ni heshima kubwa.
Miezi michache baadaye, mnamo mwezi Machi mwaka 2012 nilibahatika kuonana na Mzee Kaunda. Nilikuwa Lusaka kwa shughuli za kibunge na nililiomba Bunge la Zambia kuniombea nafasi ya kwenda kumsalimu. Alinipokea vizuri ofisini kwake na tukazungumza mambo kadhaa ya Afrika. Kwa hakika mazungumzo haswa yalikuwa ni maswali na majibu kuhusu maisha yake ya kupigania uhuru.
Ninakumbuka unapoingia tu ofisini kwake unakutana na picha ya yeye Kaunda, Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Jomo Kenyatta wakiwa uwanja wa ndege wa Nairobi nchini Kenya wakisubiri kuunganisha ndege kwenda Uingereza. Kaunda na Kenyatta walikuwa Mawaziri Wakuu wakati ule kabla ya nchi zao kuwa na mamlaka kamili maana zilikuwa bado zina utawala wa ndani na hazijawa huru. Tanganyika tayari chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ilikuwa imepata uhuru kabla ya kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nilimwuliza Mzee Kaunda kama anakumbuka picha ile ilipigwa lini, akaniambia ilikuwa Januari 1964. Walikuwa vijana watanashati wakiwa wanajiamini sana. Aliniambia kuwa muda ule Afrika ilikuwa ina matumaini makubwa sana. Akanieleza namna alivyokuwa na ukaribu wa kindugu na Mwalimu Nyerere na hata Mzee Kenyatta japo siasa zao hazikuwa zinashabihiana sana. Wote watatu sasa wametangulia mbele ya haki. Mzee Kenneth David Kaunda amefariki jana, Alhamisi tarehe 17 Juni 2021, Jijini Lusaka.
Kenneth Kaunda, almaarufu KK, alikuwa ni mwasisi pekee wa Nchi za Afrika Huru aliyekuwa amebakia hai. Kuna makosa yanayotokana na mazoea tu kusema kuwa Kaunda alikuwa mwanzilishi wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU). Zambia haikuwa nchi huru wakati ule OAU inaanzishwa Mei 25 mwaka 1963, hivyo sio Kaunda wala Jomo Kenyatta waliokuwa miongoni mwa viongozi waliotia saini mkataba wa OAU. Zambia ilijunga na OAU tarehe 26 Februari mwaka 1965.
Hata hivyo, kutokana na ukweli kuwa KK alikuwa mstari wa mbele katika harakati za uhuru wa bara la Afrika na kwamba uhuru wa Zambia ulipatikana muda mfupi baada ya kuanzishwa kwa OAU ni rahisi sana kufanya kosa hilo. KK pia alikuwa ni muumini mkubwa wa Umoja wa Afrika. Alishiriki karibu mikutano yote ya OAU na kuwa Mwenyekiti wake mwaka 1970 kufuatia Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi uliofanyikia Jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Zambia ilipata uhuru nyakati ambazo nchi za kusini mwa bara la Afrika zilikuwa zimeanza harakati za ukombozi dhidi ya utawala mkongwe wa Ureno katika nchi za Msumbiji na Angola na vile vile utawala dhalimu wa kibaguzi wa makaburu huko Afrika ya Kusini na Namibia. Licha ya kwamba Zambia ilizungukwa na nchi nyingine zilizokuwa huru kama vile Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo – DRC) na Malawi, ni nchi mbili tu zilizopakana na Zambia ndizo zilikuwa na utawala ambao ni rafiki. Hizi ni Tanzania na Botswana.
Malawi chini ya Hastings Kamuzu Banda ilikuwa karibu na utawala wa makaburu wa Afrika Kusini na Zaire ilikuwa inatumiwa na nchi za magharibi dhidi ya juhudi za ukombozi. Zambia ilikuwa katika wakati mgumu sana kwa kuwa ni nchi isiyo na bahari. Ilitegemea mizigo yake kupitia bandari za Beira au Nacala nchini Msumbiji iliyokuwa chini ya Ureno na kusafirishwa kupita Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe) ambayo ilikuwa imekaliwa na mlowezi Ian Smith. Hapa ndipo uongozi wa Rais Kaunda ulikuwa na majaribu makubwa – kulinda maslahi ya nchi yake kwa kushirikiana na tawala dhalimu au kusaidia vyama vya ukombozi na kuondoa ukoloni barani Afrika. Alichagua la pili, kwa gharama kubwa sana.
Rais Kaunda, Rais Nyerere na Rais Obote wa Uganda walikutana katika Mkutano Mkuu wa Chama cha UNIP [United National Independence Party] kilichokuwa kinatawala Zambia na kuanzisha Klabu ya Mulungushi kwa malengo ya kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kuendesha nchi zao na kuimarisha vyama vyao. Bahati mbaya Rais Obote alipinduliwa na Idi Amin mwaka 1971 hivyo wakabaki wawili tu.
Katika moja ya vikao vya Kaunda na Nyerere walimwalika Rais Seretse Khama wa Botswana na hapo ndipo kwa mara ya kwanza jina ‘Nchi za Mstari wa Mbele’ lilianza kusikika, yaani Frontline States. Kikao cha kwanza kilifanyika Lusaka na Mwalimu Nyerere akawa Mwenyekiti wa Kwanza wa Frontline States kinyume kabisa na utamaduni wa Rais wa nchi mwenyeji kuwa Mwenyekiti. Mark Chona, msaidizi maalumu wa Rais Kaunda katika masuala ya ukombozi ananukuu namna Rais Nyerere alivyokuwa mwenyekiti:
Ilikuwa ni suala la kuwatoa jela wapigania uhuru wa Zimbabwe, mkutano wa kwanza ulikuwa mwezi Oktoba nikiwa nimetumwa Cape Town na KK alitaka kuwapa mrejesho wenzake Rais Nyerere na Rais Khama. Walipokaa Mwalimu akasema “Oh! Kenneth, wewe ni mwenyeji. Naomba uwe Mwenyekiti” na KK akasema “Hapana, Mwalimu; ongoza kikao, mimi ni mwenyeji tu.” Kikao cha pili kilipofika, Mwalimu alimtaka tena Kaunda awe Mwenyekiti na Kaunda akasema “hapana, hapana, kikao cha kwanza uliongoza vizuri sana, endelea tu kuongoza vikao.
Hivyo ndivyo Mwalimu Nyerere aliendelea kuwa Mwenyekiti wa Nchi za Mstari wa Mbele mpaka mwaka 1985 alipomaliza uongozi wake na Mzee Kaunda akachukua uenyekiti mpaka aliposhindwa Urais katika uchaguzi wa Zambia wa mwaka 1991.
Kumbukumbu ya Rais Kaunda haswa ni ukombozi wa Afrika. Wakati wake Zambia ilihudumia vyama vya ukombozi, kutatua migogoro ya vyama hivyo, kuvisaidia kifedha na kuwaandaa kwa ajili ya kutawala nchi zao. Kutokana na haya, Zambia ilishambuliwa na Ian Smith na ndege za Afrika Kusini na hata wakati mmoja kulikuwa na tishio la Zambia kumalizwa kwa bomu la nyuklia ambalo inasemekana lilikuwa linatengenezwa na Afrika Kusini.
Katika kukabiliana na kuifanya Zambia kutotegemea bandari za Msumbiji na Afrika Kusini ndio Rais Kaunda na Rais Nyerere waliamua kuomba msaada China ili kujenga Reli ya TAZARA [Tanzania-Zambia Railway]. Reli hiyo pia inajulikana kama Uhuru Railway (Reli ya Uhuru). Vile vile inasemekana kuna wakati Zambia nayo ilianza matayarisho ya kuunda bomu la nyuklia ili kupambana na Afrika Kusini.
Nchi za Mstari wa Mbele ziliendelea kuongezeka kila uhuru ulipopatikana. Kwanza Angola na Msumbiji mwaka 1975 kisha Zimbabwe mwaka 1980 na hivyo kufikia nchi sita. Kazi kubwa ilikuwa ni kukamilisha ukombozi wa Afrika Kusini na Namibia ambazo zilikombolewa mwaka 1991 kwa Namibia na mwaka 1994 kwa Afrika Kusini. Mzee Kenneth Kaunda alikuwa mbele kabisa katika kukamilisha kazi hii kubwa ambayo iligharimu damu nyingi za wananchi wa nchi yake.
Rais Kaunda pia alifanya maamuzi yaliyoleta sintofahamu kati yake na viongozi wenzake katika Nchi za Mstari wa Mbele au kushawishi wenzake kufanya maamuzi kinyume na OAU. Mambo matatu yanakumbukwa zaidi. Moja ni kuhusu kuitambua Biafra kama nchi huru kutoka katika Shirikisho la Nigeria. Uamuzi huu ambao ulifanywa na nchi nne tu za Afrika – Zambia, Gabon, Ivory Coast na Tanzania – ulileta zogo kubwa katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika.
Tanzania iliitambua Jamhuri ya Biafra Aprili 13 mwaka 1968 na Zambia ilifanya hivyo mwezi mmoja baadaye, Mei 20 mwaka 1968. Nimepata kuhadithiwa na kiongozi mmoja mstaafu wa Tanzania ambaye wakati huo alikuwa Balozi na alihudhuria Mkutano Mkuu wa Tano wa OAU Jijini Algiers, Algeria mwezi Septemba mwaka 1968 ambao ulijadili suala la Biafra. Rais Kaunda alitukanwa na kushambuliwa na marais wenzake kiasi cha kukimbia mkutano ule. Rafiki yake Mwalimu Nyerere hakuhudhuria na badala yake alimtuma Makamu wa Rais, Rashidi Mfaume Kawawa. KK aliendelea kuamini katika Biafra kwa muda mrefu kiasi cha kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Kiongozi wa Biafra Kanali Chukwuemeka Odumegwu Ojukwu mwezi Novemba mwaka 2011.
Jambo la pili ni kuhusu kutambuliwa kwa uhuru wa Angola kupitia MPLA [Movimento Popular de Libertação de Angola]. Uhuru huo ilioupata mwaka 1975 kutoka kwa Ureno ulitokana na vita ya ukombozi ambapo kulikuwa na vyama vitatu vya ukombozi – MPLA cha Augustino Neto, UNITA [National Union for the Total Independence of Angola] cha Jonas Savimbi na NFLA [National Liberation Front of Angola] cha Holden Roberto. Kwa kuwa uhuru wa Angola ulitokana pia na mazungumzo baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Ureno (na mazungumzo haya yaliendeshwa na Zambia), hapakuwa na chama cha ukombozi ambacho kilikuwa kimelishika Jiji la Luanda. Hivyo, Umoja wa Afrika uliingilia kati kwamba chama gani kikabidhiwe uhuru.
Umoja wa Afrika uligawanyika mapande bila upande wowote kuwa na kura nyingi. Katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika jijini Addis Ababa mabishano yalikuwa makubwa na Rais Kaunda alitoa hotuba ya kuonesha mwelekeo wa kuunga mkono UNITA ya Savimbi, jambo ambalo lilimkasirisha sana Mwalimu Nyerere na ujumbe wa Tanzania. Hivyo, Mwalimu Nyerere hakutoa hotuba yake isipokuwa maneno machache kumjibuRais wa Senegal, Léopold Sédar Senghor kuhusu UNITA na MPLA.
Mwandishi wa habari mbobezi na mwanasheria, Jenerali Ulimwengu alikuwepo Addis Ababa akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Afrika na alipata kunihadithia kuwa hali ilikuwa mbaya sana. MPLA waliamua kuingia Luanda na kutangaza uhuru baada ya Ureno kuacha ombwe kwa kubwaga ‘instruments of power’ [hati za madaraka]. Jenerali ambaye alikuwepo Luanda siku ya uhuru hawezi kuisahau siku hiyo kutokana na Tanzania kuonekana haina msimamo licha ya kumtuma Makamu wa Rais, Aboud Jumbe Mwinyi katika sherehe zile. Mpaka mauti yanamkuta Mzee Kaunda, suala la yeye na Jonas Savimbi na UNITA bado ni jambo ambalo halikueleweka kabisa.
Jambo la tatu ni suala linalohusu nchi yake. Rais Kaunda aliadhibiwa vikali na serikali ya walowezi wa Rhodesia na makaburu wa Afrika Kusini kiasi kwamba uchumi wa Zambia ulianguka kabisa. Alikuwa amefunga mpaka wa kusini lakini TAZARA haikuwa inaweza kusafirisha mbolea na bidhaa nyingine kuingia nchini. Wananchi walianza kumlaumu kwa siasa zake za kusaidia ukombozi bila kuangalia maslahi ya nchi yao.
Kinyume na makubaliano na viongozi wenzake na pia kinyume na ahadi yake kuwa “hatafungua mpaka hadi Zimbabwe ipate uhuru” KK aliamua kufungua mpaka wake na Zimbabwe. Katika kikao cha Nchi za Mstari wa Mbele ugomvi mkubwa ulitokea kati ya marais Samora Machel wa Msumbiji, Agostinho Neto wa Angola, Kenneth Kaunda wa Zambia na Julius Nyerere wa Tanzania. Mzee Joseph Butiku, Katibu wa Rais wakati wa Mwalimu Nyerere, amerekodiwa akisema mkutano ule ulikuwa ni moja ya mikutano migumu kabisa kuhudhuria akiwa na Rais Nyerere. Butiku anasema:
Katikati ya kikao viongozi walianza kulia. Sisi wasaidizi kazi yetu ni kuchukua kumbukumbu za maongezi. Mimi niliandika tu, marais wanalia!
Hatimaye Zambia iliachiwa kuendelea na mpango wake. Maamuzi magumu yaliyowafanya viongozi walie na KK kulaumiwa yalimkuta Rais Samora Machel mwaka 1984 katika Mkataba wa Nkomati na utawala wa makaburu. Yeye naye alikutana na lawama kiasi cha Mwalimu Nyerere ‘kumfukuza’ alipokuja kumpa mrejesho.
Mzee Kaunda alimaliza ngwe yake ya uongozi kwa somo kubwa kwa demokrasia ya Afrika pale alipokubali kushindwa uchaguzi na kukabidhi madaraka ya Urais kwa Frederick Chiluba mwaka 1991. KK alikuwa ni kiongozi asiye na makuu kiasi kwamba alipomaliza urais hakuwa na pa kukaa. Rais aliyeingia baada yake alimsumbua sana na hata kumsweka jela kwa kosa la uhaini.
Aligoma kula akiwa jela mpaka ikabidi Mwalimu Nyerere kwenda kumwona. Ndipo akaacha mgomo wake. Ilikuwa ni Rais wa tatu wa Jamhuri ya Zambia, Dkt. Levy Patrick Mwanawasa aliyerudisha hadhi ya Baba wa Taifa kwa Rais Kaunda. Pia akampa stahiki zake zote kama Rais Mstaafu ambapo ameendelea kuzipata mpaka mauti yalipomkuta.
Katika kitabu cha Development as Rebellion: A Biography of Julius Nyerere, Prof. Issa Shivji, Prof. Saida Yahya-Othman na Dkt. Ng’wanza Kamata wanaeleza namna Rais Kaunda alivyoshangazwa na ubovu wa barabara kwenda Butiama. Alishangazwa kiasi cha kudhani dereva aliyekuwa anampeleka alikosea njia kwani barabara ya kwenda kwa Rais haiwezi kuwa mbovu kiasi kile. Yeye Rais Kaunda anashangaza zaidi kwani hakuwa hata na nyumba yake binafsi ya kuishi baada ya kumaliza Urais kwa sababu alitoa utumishi wake wote kwa nchi yake ya Zambia kiasi hakujiwaza binafsi.
Hakika kizazi cha kwanza cha viongozi wa Afrika kilikuwa ni kizazi cha dhahabu. Sidhani kama Afrika itapata viongozi wa aina ya Kenneth David Kaunda tena. Mungu amlaze Mzee wetu mahala pema peponi.
Hamba Kahle KK. Salaam kwa Nyerere, Bibi Titi, Samora, Josina, Winnie, Mandela, OR Tambo, Lumumba, Neto, Mondlane, Hani, Chitepo, Marcelino na wengine waliotoa damu, jasho na muda wao kutukomboa.
Thanks for this story
Nimesoma makala haya kwa shauku. Uchambuzi mfupi na wa kweli ktk taazia hii. Viongozi vijana mbapaswa kuiga mfano huu wa kujikana na kuwatumikia watu badala yake
Shukrani sana Zitto,na pole kwetu kwa msiba mzito huu wa shujaa wetu Dr Kenneth Kaunda
Ahsante sana Ndugu Zitto
Ningeshangaa kama usingeandika Tanzia hii nzuri. Shukrani sana Zitto na poleni sana wananchi wa Zambia.
Kazi nzuri, ZZK
Asante sana ZZK kwa article iliyoshehemu maudhui ya kutufundisha na kutujuza juu ya wapigania uhuru wa bara tukufu la Africa.
Seconded.
William Shao.
Thanks for this useful information and R.I.P KK
Beautiful piece Mwami Ruhyagwa.
‘Marais wanalia’ inasema mengi sana juu ya hawa wazee wetu mababa wa mataifa yetu.
Mungu awajalie pumziko lenye heri.
Nakushukuru sana Mh.Zito hakika umenena maisha ya viongozi wetu wapigania Uhuru ni fumbo kama la Imani umenena Zito tusubiri tuone kama kufikiri kungaliko.
Àskofu Muhagachi
Kadri ukiendelea kusoma btn lines, unaweza kutaka andiko lisiishe, makala nzuri..
Hakika Ni Habari Nzuri Mnoo…
Nimejifunza Mengi Sana Mengine Hata Sikua Nayajua..
Asante Sana kaka Zitto Zubery
Afrika ilibahatika kuwa na viongozi waliopenda wananchi wao kulioko hata wao wenyewe,rest in peace the father of the nation.
Hongera sana zitto zuber kabwe kwa historical background ya mzee KK
Nimesoma makala haya kwa shauku. Uchambuzi mfupi na wa kweli ktk taazia hii. Viongozi vijana mbapaswa kuiga mfano huu wa kujikana na kuwatumikia watu badala yake
Hakika, kweli ni kizazi cha dhahabu
Watu mpk wanalia cyo mchezo kbsaa
Ni uzalendo wa kitaifa
Hakika wewe ni hazina ya nchi hii.
Umenikumbusha mengi niliyokwisha kuyasahau ingawa wakati Niko shule ya msingi nilipenda kuyafuatilia.
Afrika haitapata tena kizazi cha viongozi wa Aina ya Kaunda
Pole Zambia, pole Afrika
Oooh Hawa walikuwa watoto kweli wa kiafrika, Afrika inajivunia Sana watu wa aina hii kuzaliwa katika ardhi yake.
Kazi imebaki kwetu vijana mliotuacha kuendelea kuipambania Afrika hasa dhidi ya umaskini ili nasi tuache mchango chanya juu ya ustawi bora wa jamii zetu.
Hakika nimepata elimu kubwa juu ya mambo ya kale. ahsante sana Zitto Zuberi Kabwe. Hakika musomi Ni yule anayesoma kuliko aliesoma. Karibu Tabora
Kiongozi zitto kabwe ,tunashukuru kwa article hii iliyojaa Mambo mazuri yakujifunza juu ya wazee wetu haya ,waliotumia maisha yao kwa ajiri ya ukombozi barani afrika , Rip mzee Keneth Kaunda
Umejitofautisha sana na wanasiasa wengi. Mtu asipokuelewa kwa kipaza sauti,atakuelewa kwa kalamu yako.
I can wait to read your books soon.
Makala nzuri. Asante kwa muda wako Ndugu ZZK kuandika na kukumbushia historia tamu na adhimu kupitia tanzia hii.
Sijaona tanzia (iliyoandikwa na yeyote hasa katika Udadisi) kuhusu Mwanazuoni Prof. Mwesiga Baregu. Wish to read one.