Hapa inakulazimu uwe na akili iliyotulia mno, ili kufumbua fumbo la mshairi huyu, venginevyo atakuacha patupu:
Kimbunga mji wa Siyu, kilichowahi kufika
Si kwa yule wala huyu, ilikuwa patashika
Kimeing’owa mibuyu, minazi kunusurika
Nyoyo zilifadhaika.Yalizuka majabali, yakabirukabiruka
Zikadidimia meli, ngarawa zikaokoka
Kimbunga hicho kikali, mavumbi hayakuruka
Nyoyo zilifadhaika.Nyumba kubwa za ghorofa, siku hiyo zimeruka
Zikenenda kwa masafa, kufikia kwa kufika
Vibanda vayo malofa, vyote vikasalimika
Nyoyo zilifadhaika.
Kimbunga gani hung’oa mibuyu minene na minazi membamba inabaki wima? Meli zinazama, ngarawa zinabaki zinaelea! Ghorofa zinapeperushwa ila vibanda vinabaki salama, na hata vumbi halipeperuki.
Ikiwa bado unatafakari shairi hilo, hebu nikujulishe. Huyo ndiye Haji Gora Haji. Juni 11, mwaka huu wa 2021, wapenzi wa fasihi ya Kiswahili walimpoteza gwiji huyo. Alifariki dunia katika kisiwa cha Unguja na kuzikwa kwao kisiwa cha Tumbatu, Zanzibar.
Hizo ni beti chache tu kutoka katika shairi lake la Kimbunga. Yeye ni mshairi, mtunzi, muimbaji, mwandishi, msimulizi wa hadithi ndefu na fupi. Kwa maneno mengine, marehemu Haji Gora alikuwa gwiji wa magwiji katika fasihi za Kiswahili.
Mwanzo wa Maisha Yake
Haji Gora alizaliwa kijiji cha Kokoni katika kisiwa cha Tumbatu mwaka 1933. Tarehe rasmi inabaki kitendawili kilichokosa jibu hadi leo. Tumbatu ni kisiwa chenye utajiri wa magofu ya kale zaidi visiwani Zanzibar. Ni mwendo wa nusu saa kwa boti kutoka fukwe ya Kaskazini mwa kisiwa cha Unguja.
Alipokuwa na umri wa miaka mitano, familia yake ilihamia Mkunazini, Unguja Mjini. Alipofika umri wa kwenda skuli, hakubahatika kupelekwa. Badala yake akasoma madrasa tu.
Familia yake ni kama familia nyingi za zamani. Hazikuipa umuhimu sana elimu ya skuli. Alijifundisha mwenyewe kusoma na kuandika kwa msaada wa mmoja wa marafiki zake wa utotoni.
Alipokuwa barobaro ndipo akajiingiza katika kazi ya uvuvi, kazi ya Baba yake. Kimsingi uvuvi ndio kazi ya asili katika familia yake na kwa wakaazi wa Tumbatu kwa ujumla. Wakati akiendelea na kazi hiyo, alijiunga na kikundi cha ngoma ya Zige, kwao Tumbatu. Mara kwa mara akienda huko kutumbuiza kisha anarudi mjini. Hii ni aina ya ngoma ambayo wahusika hushindana kwa kutunga mashairi ya kulumbana na kujibizana, mbele ya hadhira. Zige haikumuingizia pesa nyingi, ila hakuiacha.
Ilipofika miaka ya 1950 wakati akiwa kuli katika bandari ya Malindi, Mji Mkongwe baada ya kuacha uvuvi, alianza kuimba taraab. Aliimba katika kikundi cha Michenzani Club, kikiongozwa na Bakar Abeid. Pia aliimba katika kikundi cha Mlandege na Gulioni. Mashairi yake pia yalitumika katika kikundi maarufu wakati huo cha Nadi Ikhwan Swafaa.
Ametunga nyimbo nyingi katika vikundi hivyo. Waswahili wana msemo wao maarufu; “Mke Hapigwi Kwa Fimbo.” Haji Haji Gora alinidokeza kwamba msemo huo unatoka kwa baba yake.
Maajabu ya Haji Gora Haji
Mwandishi mkongwe wa habari visiwani Zanzibar, Ally Saleh, ambaye ameandika kitabu cha Maisha ya Haji Gora: Msanii Atakayedumu Milele kilichochapishwa mwaka 2016 alipata kuniambia mwaka 2018:
Haji Gora ni kifurushi kamili. Katunga nyimbo, mashairi, tenzi, hadithi fupi na ndefu pia kaimba. Watu wenye uwezo kama wake ni wachache mno duniani
Licha ya uwezo huo, maajabu ya maisha yake ya kifasihi andishi na simulizi ni kwamba hakuwahi kusoma hata darasa moja la elimu dunia, zaidi ya elimu ya dini, yaani madrasa. Imezoeleka kuona wanafasihi wakimaliza shahada zao vyuoni. Na hata wale ambao hawajafika kwenye shahada huwa angalau wamesoma hata elimu ya msingi. Naweza kusema ni nadra kukuta mwanafasihi aliyezikusanya fasihi andishi na simulizi lakini hakusoma hata chekechea.
Haji Gora visiwani Zanzibar alijulikana kwa jina maarufu “Mzee wa Kimbunga,” kutokana na hilo shairi lake la Kimbunga. Sitiari na mgongano wa maudhui katika kazi zake, ni baadhi ya mambo yanayomfanya kuwa wa kipekee mno. Ukimsoma atakutafakarisha kwa lazima, hadi umuelewe au utoke patupu.
Heshima na Umasikini
Mwaka 1994, Haji Gora alitoa kitabu chake cha kwanza, kwa jina hilo la shairi la Kimbunga, kilichochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka 1999 akatoa kitabu cha pili cha Utenzi wa Visa vya Nabii Suleiman bin Daud.
Baadae alitoa vitabu vitano vya watoto. Ulikuwa ni mradi wa hadithi fupi fupi za watoto. Vitabu hivyo vinatumika kwenye shule za msingi Tanzania Bara. Kitabu chake kingine kilichofuatia ni cha riwaya, iitwayo Siri ya Giningi, kilochochapishwa mwaka 2009 na TUKI.
Haji Gora ameshiriki pia katika matamasha ya mashairi katika miji kadhaa kama Medellin nchini Colombia na Rotterdam huko Uholanzi. Hali kadhalika ametunga kamusi la kwanza la lahaja ya Kitumbatu, kabla ya Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kutunga kamusi kama hilo.
Kipo na kitabu chake cha Shuwari kilichohaririwa na Flavia Aiello Traoré na Irene Brunotti, ambacho ni mkusanyiko wa kazi zake za kifasihi za zamani. Ameshatunga nyimbo na mashairi zaidi ya mia tano.
Kwa mujibu wa huyo mtoto wake aitwaye Haji Haji Gora, baba yake alitoa jumla ya vitabu kumi. Kitabu chake cha mwisho ni hicho cha Shuwari. Kilichapishwa nchini Ufaransa na kinapatikana mtandaoni.
Wale wanaoujua uwezo na heshima ya Haji Gora, mfano mwanataaluma na mfasiri wa fasihi za Kiswahili na Kiingereza, Nathalie Arnold Koenings, ambaye alimjua miaka mingi na kukutana naye, aliniambia:
Kazi za Haji Gora ni muhimu kwa lugha ya Kiswahili na lahaja ya Kitumbatu. Pia, ni hazina kubwa kwa jamii.
Hakika ni gwiji aliyeacha alama kubwa katika ustawi wa fasihi ya Kiswahili. Ila linalosikitisha ni kwamba mwenyewe ameaga dunia akiwa fukara. Mafanikio ya wanafasihi yanabaki kuwa kitendawili katika mataifa mengi ya Afrika. Haji Gora ameingia katika orodha ya wanafasihi waliofanya kazi kubwa lakini manufaa ya kazi zake imebaki kuwa “heshima” tu kwa wale wanaomjua.
Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa familia yake, mathalan, juu ya uwepo wa watu na taasisi ambazo zimekuwa zikitumia kazi zake bila mwenyewe kunufaika lolote wakati wa uhai wake. Miaka ya mwisho ya maisha yake, Haji Gora alikuwa anaishi Bububu, kisiwani Unguja, chini ya uwangalizi wa wanawe. Uzee na maradhi vilikuwa vikimsumbua. Mwaka 2018 Haji Haji Gora alinieleza hali ya baba yake kwa sentensi hizi:
Shughuli zote za utunzi zimekatika. Hawezi tena hata kutunga ubeti mmoja.
Haji Gora mwenyewe aliuzungumzia mwisho wa maisha ya wasanii katika shairi hili la Hupendwa baada ya Kufa lilipo katika kitabu chake cha Shuwari:
Kwengine ulimwenguni, msanii kichomoza
Hatiliwi maanani, wengi wao humbeza
Aingiapo mautini, ndipo kupendwa huanza
Humpenda kwa jeneza, na kumfukia dongo.
Mapenzi ya nyingi sifa, kwa msanii huanza
Ghafla baada kufa, mwema watamfanyiza
Watu hukaa misafa, kuliwania jeneza
Humpenda kwa jeneza, na kumfukia dongo.