CUF-Maalim Seif Kuhamia ACT:Maswali Mengi Kuliko Majibu

Emmanuel Mohamed

Habari za Maalim Seif Sharif Hamad kutoka chama cha CUF kwenda ACT yawezekana ikachukuliwa kimazoea maana imeshakuwa kasumba kuwaona wanasiasa wakihama vyama. Isitoshe si mara ya kwanza kwa Maalim Seif kufukuzwa  katika chama kikubwa. Lakini tofauti ya Maalim Seif aliyefukuzwa CCM miaka ya 80 ambapo alilazimika kujenga vuguvugu lililokuja kuunda CUF ni tofauti na wa leo. Si haba leo anapohama huku tayari akiwa na uwanja mpana wa kuchagua chama cha kuhamia.

 Sasa ni kwa nini Maalim Seif na watu wengi waliokuwa wanachama wenzake wa CUF wanakata tanga la CUF na kupandisha tanga la ACT? Maalim Seif anatoka katika chama kikubwa chenye misingi na nidhamu ya chama na uzoefu wa kitasisi akihamia katika katika chama kidogo na kichanga. Wengine wanasema tembo kahamia kwenye kibanda. Kitasalimika? Pia wengine wanasema dodo limeokotwa kwenye mnazi. Litalika?

Nilisubiri kwa shauku kubwa kuona mapokeo yake leo pale kwenye ofisi za ACT na kumsikiliza kwa makini Maalim Seif; mosi, nikitamani aongea juu ya Muungano na hatima ya vyama vya siasa ili kujibu swali iwapo umefika wakati wa kutanua wigo wa siasa zake na wafuasi wake hadi bara? Pili, ili kujua ni kwa nini ‘CUF-Maalim’ ijiunge na ACT badala ya vyama vingine hasa chama kikubwa cha CHADEMA ambacho ilishirikiana nacho kupitia UKAWA kwenye uchaguzi wa mwaka 2015. Tatu, nilitaka kujua kama Maalim Seif ametoka CUF kama mtu au taasisi. Nne, kutaka kujua ACT itajiendesha kwa mfumo upi huko Zanzibar ambako ndipo medani kuu ya kisiasa ya Maalim Seif. Tano, nilitaka pia kujua ni jinsi gani ACT imejipanga kujihuisha kwenye baadhi maeneo ya Tanzania Bara ambayo, kihistoria, CUF imeota mizizi.

Ingawa maswali haya nilikuwa nayo kichwani, yalishabihiana kwa kiasi kikubwa na maswali kadhaa ya waandishi ya habari kwenye tukio la leo. Maalim Seif na Viongozi wa ACT walijaribu kuyajibu. Ufuatao ni muhtasari wangu wa baadhi ya maswali waliyoulizwa:


  Inasemekana umehamia ACT ili ugombee urais, je, ni kweli? Wafuasi wako wa CUF wanashusha na kuchoma bendera pamoja na kukwangua rangi majengo ofisi za CUF, huoni huo ni uharibifu? Huo msemo wa wafuasi wako wa ‘ulipo tupo’, hauoni unakuza siasa za mtu (personalities)? Ni nini maoni yako kuhusu siasa za taasisi (institutions)? Kwa nini baadhi ya wabunge hatuwaoni wakihama nawe? Pia inasemekana walikudekeza na kukufanya Sultani CUF, je, umejitayarisha na mazingira utakayokutana nayo ACT? Je, una lengo la kuuvunja Muungano toka moyoni?

Kama ilivyo ada, wanasiasa kutokuwa na majibu kamili siyo jambo la kushangaza. Lakini msikilizaji anaweza kudadavua maongezi yaliyojiri katika mapokezi hayo na hotuba zilizotolewa kupata majibu ya maswali. Majibu hayo yanaweza kuibua maswali zaidi.

Mwenyekiti wa ACT, Yeremia Maganja, alijibu swali la kwanza la kwa nini ACT kwa mkanganyiko mkubwa wa lugha na maudhui. Ila ukimsikiliza kwa utulivu mkubwa unaweza kukokotoa mambo makubwa matatu. Mosi, Mwenyekiti alisema chama cha ACT kinaongozwa na Maganja Doctrine ambayo ni mchanganyiko wa itikadi, kwa lengo la kutanua demokrasia na kuleta mabadiliko ya kuondoa ukandamizaji wa wananchi. Hivyo, ACT ambayo inajitanabahisha na siasa za ujamaa wa kati, inaweza kabisa kufunga mbeleko na siasa za uchumaji, kama lengo ni kuunda Tanzania yenye usawa. Ingawa huu ni mwanzo mzuri, maongezi ya kina yanahitajika kuoanisha itikadi zao. Ukizingatia kuwa hii ni mara ya kwanza kwa baadhi yetu kuisikia Maganja Doctrine nachelea kusema pengine ilikuwa ni jitihada ya ACT kujioanisha kiitikadi na kile ambacho CUF hupenda kujitanabahisha nacho sana, hasa hapo zamani, kama itikadi yake, yaani Utajirisho. Hapa kilicho muhimu ni namna ambavyo Azimio la Tabora litatumika kuoanisha na kuiuza itikadi ya CUF/Utajirisho na ACT/Ujamaa katika uhuisho mpya wa ACT.

  Pia Mwenyekiti Maganja alisisitiza kuwa ujio wa CUF-Maalim umekuja wenyewe bila shurti. Suala hili lilikaziwa baadaye na Malim Seif aliposema ACT walituomba tuhamie kwao hatukuja. Ila tukafanya tathmini na mwisho tukaamua kuja Maneno ya Biblia kutoka kwenye sura ya 60 ya Kitabu cha Isaya mstari wa 22 nayo yalitumika kujenga hoja kuwa tukio hilo limetokea muda sahihi au mwafaka na kupelekea familia ndogo kuwa kubwa. Suala la kutafakari ni, je, muda sahihi ni muda gani hasa? Ni kipi hicho kimewezesha wanachama wa CUF kuhamia ACT sasa? Je, ni ugomvi wa CUF-Maalim na CUF-Lipumba tu? Au kuna masuala mengine nyuma ya pazia kuhusiana na mkono wa Chama-Dola, mtafaruku wa Chadema-Ukawa, na mchanyato wa Udini-Ukanda?

Kabla ya kuhitimiha hotuba yake, Mwenyekiti aliweka nadhiri akisema kuwa haki ambapo haipo, kwa pamoja tutapambana. Akitumia mfano wa jamii ya Wakurya, alitoa rai ya udugu wa ACT na CUF uwe ni wa kudumu. Alisema kuwa, kwao mkoani Mara watu huchanjiana, na kula damu, ili wadumu. Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe, alidhihirisha hili pale ambapo kadi za wanachama waanzilishi wa ACT, kama Profesa Kitila Mkumbo, waliokuwa wametoka zilipewa kwa wanachama wapya waliokuja kutoka CUF ambapo Maalim Seif alipata kadi nambari moja. Walipata kadi hizo zilizogombolewa kwa pesa na kulipiwa ada yenye fungamano la uwanachama wa miaka 10. Sasa mtu unabaki unajiuliza kwa nini umlipie mtu ada miaka 10? Je, hili lilikuwa ni suala la kuchangia chama na/au ishara ya kuonesha kuwa kiukweli huu ni muungano wa kitaasisi na kiungozi wa vyama viwili, hivyo, itarajiwe kuwa wanachama wapya watakuwa na nafasi za juu za uongozi katika ACT? Ama pia likuwa ni ishara ya kuwa watadumu muda mrefu?

Swali la kwa nini CUF-Maalim imejiunga na ACT lilijibiwa zaidi na Kiongozi wa Chama. Maalimu Seif na viongozi na wanasiasa waandamizi waliombatana nao, Zitto alisisitiza, wamejiunga ACT kutafuta namna ambavyo upinzani utaendeleza safari ya kudai haki na demokrasia katika Tanzania. Ukiwa kiongozi ulioko kwenye nyoyo za wananchi, alisema, hawawezi kukutupa. Zitto pia alitumia fursa hiyo kuzungumzia somo ambalo ambalo viongozi vijana wanalipata kutokana na uzoefu huo wa Maalim Seif wa kujenga imani kwa watu wanaokupa dhamana ya uongozi maana wao wana uwezo wa kufanya lolote ili kufika wanakotaka kufika.

Ni dhahiri pia kuwa suala la muungano mpana wa vyama vya upinzani lilikuwa vichwani mwao hasa ukizingatia kuwa uhamaji huo haujatokea katika muktadha wa UKAWA na pengine kupelekea hofu kwamba utakuwa kikwazo. Kwa mfano, Zitto alikishukuru CHADEMA kwa kuipongeza ACT kwa ujio huo wa CUF-Maalim. Kutokana na changamoto na mitihani ambayo vyama vinakutana navyo sasa hivi, alisisitiza, tunahitaji kushirikina kwa pamoja.

Maswali ya kujiuliza hapa, ni: Je, katika siasa za kutoaminiana ACT, imejipangaje kushirikiana na vyama vingine hasa katika muktadha huo ambapo Maalim Seif hakujiunga na washirika wake wakuu wa UKAWA, yaani, CHADEMA? Yale madai ya kuwa kumekuwa na jitihada, za kupangwa au kutopangwa, za kuikuza ACT na kuishusha CHADEMA ili kupunguza upinzani kwa CCM yatajibiwaje katika muktadha huu cha chama kidogo kuhuishwa ghafla katika kipindi cha kuelekewa Uchaguzi Mkuu wa 2020? Katika mazingira ambayo CUF ilijengewa wasifu hasi wa kuwa chama cha kidini kutokana na kuonekana kuwa kina wafuasi wengi zaidi wa dini mojawapo, je, ACT ambayo nayo inaonekana ina mwelekeo huo huo imejipangaje kujenga taswira ya chama kisicho cha kidini ama cha kikanda hasa pale kanda inapohusishwa na dini?

Inaonekana CUF-Maalim ilifanya uchambuzi wa kina kujua wajiunge na chama gani na naamini nao walijiuliza baadhi ya maswali hayo hapo juu yanayonitatiza. Ambacho ningependa kujua ni namna ambavyo watayajibu maswali kwa sera na vitendo. Kwa mfano, katika majibu yake leo Maalim Seif nilimsikia akisema:

Wachambuzi walisema pa kwenda ni ACT wazalendo – nawatoa wasiwasi wanachama wa ACT wazalendo. Tujue kwamba tuna jukumu kubwa kwa wananchi. Wamechoka hawajui waende wapi. Tumekuja kuonesha njia. Tumekuja kuongeza nguvu, siyo kuiteka kwa kushika nafasi ya uongozi. Watanzania wajue wanachoomba iwapo wakikiunga mkono tutaleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi. Kutoa uhakika wa chakula, elimu, afya – ndio malengo ya wananchi wa bara na visiwani.

Huo wasiwasi wa kumezwa na/au ACT kuchukua zaidi taswira ya CUF-Maalim siyo jambo dogo. Ni suala ambalo ACT inapaswa kulishughulikia kwa umakini na stratejia ya hali ya juu. Pamoja na Maalim Seif kumsifia Zitto na viongozi/uongozi wake kwa kuwa na maono, ujasiri, na nidhamu ni ukweli usiopingika kuwa timu ya CUF-Maalim ndiyo ina uzoefu mkubwa wa kitaasisi katika hayo. Maalim Seif mwenyewe nilimsikia akilithibitisha hilo aliposema.


 Tulipokuwa CUF tulijitahidi kujenga taasisi. Ndio maana mimi naondoka nchini kwa miezi sita chama kinakwenda. Chama kina competent leaders. Tumekuja hapa kujenga taasisi. Wananchi wana mapenzi yao vile vile. Jiulize kwa nini wanipenda? Hajajikweza. Anybody is free to speak to Maalim Seif. Anatembelea watu katika vijiji vyao. Maalim ana-represent aspiration za watu. Niwe ndani au nje ya chama au serikali, nitaendelea kuwa na wananchi….Watu wanashusha tanga na wanapandisha tanga ili safari iendelee. Wanachama ndiyo rasilimali yetu. Ni chama masikini. Majengo siyo ya CUF tumekodishwa au kuazimwa.

Utaasisi wa CUF-Maalim unaweza kuwa mbaraka mkubwa kwa ACT. Lakini pia unaweza kuwa laana kubwa. Hivyo, changamoto ni kuhakikisha unakuwa ni mbaraka badala ya laana kwa kujenga chama ambacho taswira yake ya kitaasisi siyo wasifu tu wa ki-mtu na kidini wa mafahali wake wakuu wawili: Maalim Seif na Zitto.