Kuna mjadala mkubwa unaoendelea hivi sasa nchini Tanzania miongoni mwa wananchi, wanaharakati, wasomi, na wanasiasa. Ni mjadala kuhusiana na hitaji la katiba mpya. Lipo kundi la wale wanaodhani sasa ni muda muafaka kwa Tanzania kuwa nayo. Pia wapo wale wanaoamini kwamba waraka huo sio muhimu sana kuliko upatikanaji wa haki za msingi za kijamii. Wapo na wadau wanaobainisha kwamba tatizo wala sio katiba mpya, bali namna ya kuyatekeleza yaliyomo kwenye katiba; kwa kitaalamu wanaita ukatiba.

Makundi haya yanaendelea kunyukana kwenye majukwaa mbalimbali ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii. Binafsi sitaki kujihusisha na kundi lolote kati ya haya matatu. Kupitia safu hii, ningependa kuibua hoja nyingine ambayo mpaka sasa sijaona ikijadiliwa kwa mapana na marefu licha ya umuhimu wake.

Hoja yangu inajikita kwenye dhana ya katiba kama uwanja wa mapambano ya kitabaka kati ya walionacho na wasionacho. Dhana hii kuhusu katiba inajengwa na ukweli kwamba katika jamii yapo makundi yenye maslahi tofauti, na muda mwingine kinzani.

Tabaka la wasionacho, au kama wanavyojulikana hapa Tanzania, walalahoi, linawajumuisha wafanyakazi, wakulima, wavuvi, machinga, bodaboda na kadhalika. Hawa wanahitaji katiba kujikomboa. Wakati huo huo wale walionacho, au walalaheri, wakiwemo watu wenye mitaji na wanasiasa wa pande zote mbili, upinzani na chama tawala, wanahitaji katiba kuhakikisha maslahi yao yanadumishwa kwa kuhakikisha mfumo uliopo wa kiuchumi-siasa unaendelezwa.

Kwa maoni yangu, mjadala kuhusu katiba mpya hauwezi kuachwa kuathiriwa na mgongano wa kitabaka niliougusia hapo juu. Hivyo, ni muhimu kutambua haya madai ya katiba mpya ni kwa maslahi ya kundi gani, wasionacho au walionacho?

Maslahi ya walalahoi yanaweza kuonekana kupitia hofu zao kuhusu mfumo wa uchumi unaowafukarisha wakati kwa walalaheri maslahi yao ni kuona nafasi yao kisiasa-uchumi inaendelea kudumishwa kupitia mfumo uliopo wa kibepari. Huu mvutano wa kimaslahi baina ya matabaka haya mawili kwenye jamii ni vema ukawekwa wazi katika mjadala huu wa katiba. Je, kwa hali iliyopo ni tabaka lipi litashinda?

Kwa vyovyote vile, tabaka tawala – linalojumuisha watawala waliopo madarakani na wapinzani wanaouwania utawala – litafanikiwa, kwa kuwa mawazo na nguvu za tabaka hilo ndizo zinatawala jamii kwa sasa. Kwa hiyo, walalahoi – na hata walalahai – wanaweza wakawa kama daraja tu la kufikia katiba mpya. Na hii inatukumbusha zaidi kuwa katiba ni mapambano ya kitabaka, sio kitu huru tu hivyo tunapaswa kuwa makini katika kujadili.

Ni kweli Watanzania wanahitaji Elimu ya Katiba?

Kama nilivyosema kwenye hoja iliyopita, katiba ni mapambano ya kitabaka. Katika mapambano hayo kundi la walalaheri linatumia mbinu mbalimbali za kuweza kuwafanya walalahoi wasiweze kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa katiba. Mbinu mojawapo ni elimu na nyingine ni ile mlalahoi akihitaji huduma ya maji au umeme, walalaheri wanamwambia hilo sio suala la katiba ni suala la wizara au halmashauri.

Kwa mfano, wapo watu wanaodhani kuwa katika mchakato wa katiba mpya, sharti kwanza ‘wananchi wa kawaida’ – yaani walalahoi – wapewe elimu kuhusu katiba. Wanaona walalahoi wapo kimya na hawajui uzito na maana ya katiba. Lakini wanasahau kuwa kwa mwananchi mlalahoi kufahamu katiba sio lazima awe amekariri vifungu au misamiati ya kisheria iliyopo kwenye katiba.

Profesa Issa Shivji aliwahi kusema mwananchi akisema hana barabara, hapati matibabu hospitali, na hana masoko ya mazao yake, hapo maana yake anazungumzia katiba, sio lazima aoneshe kuwa ibara fulani mimi siipendi au ibadilishwe. Suala la kubadilisha au kutengeneza hivyo vifungu sio la mwananchi moja kwa moja. Ni jukumu la waliopewa dhamana ya kutengeneza au kuyaweka maoni hayo ya wananchi kwenye katiba.

Hivyo, kwa makundi yote yaliyo mstari wa mbele katika mjadala wa katiba mpya ni muhimu watambue kwamba hoja ya elimu inapaswa kutafakariwa zaidi ya watu kujua ibara au maandishi ya katiba.

Katiba ni Mwarobaini?

Katika kujadili hili nakubaliana na Profesa Shivji ambae alitolea mfano wa nchi kadhaa zinazoaminika kuwa na katiba bora zaidi Afrika lakini ukitazama hali ya ndani katika nchi hizo ni ya kusikitisha sana. Hii inatupa picha kwamba haitoshi tu kutazama katiba pekee kama chombo kinachoweza kuleta mabadiliko ya mfumo wa maisha kwenye jamii.

Kenya na Afrika Kusini, nchi zinazotajwa kuwa na katiba bora barani Afrika, ni miongoni mwa nchi ambazo zinatajwa kuongoza kwa mauaji ya kiholela ya raia. Pia zinatajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye tofauti kubwa ya kipato na hali ya maisha baina ya walionacho ambao ni wachache na wasionacho ambao ni wengi.

Hii inatukumbusha kwamba ni lazima tutazame mgongano wa kitabaka uliopo na mahusiano ya uzalishaji mali kiujumla maana ndipo kilipo kiini cha matatizo ya kijamii. Bila ya kujadili mgongano wa kitabaka uliopo kwenye suala la katiba mpya tutakuwa kama tunatwanga maji kwenye kinu.

Kwa mfano, katiba iliyopo sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika ibara ya 11 inaeleza kuhusu haki ya kufanya kazi, elimu na nyinginezo. Lakini ukija kwenye mfumo wa uchumi katika jamii ambao una matabaka ya walalahoi na walalaheri, elimu bora inauzwa kwa wachache wenye uwezo wa kifedha. Elimu imekuwa biashara.

Kwa hiyo, sio suala tu la katiba inasemaje lakini lazima tutazame hiyo katiba ipo ndani ya tabaka lipi. Je, mfumo-tabaka unawajali wengi/walalahoi? Mfumo huo unaamini elimu si biashara bali ni haki ya asili ya kila mtu?

Ni nini kinahitajika?

Wapo wanaofikiri kwamba katiba ni zao la siasa tu, lakini ukweli ni kwamba katiba nayo ni zao la mfumo wa uchumi  unaotawala, ambao unatokana na mgongano wa kitabaka. Kwa maana nyingine, ni zao la siasa-uchumi. Ndio maana tukitaka kuangalia utekelezaji wa katiba hatuna budi kutazama pia mfumo wa uchumi unaoongoza.

Hata maoni mengi ya wananchi, hususan wavujajasho/walalahoi kupitia mijadala mbalimbali, yanaanzia kwenye mashaka yao juu ya hali ya uchumi. Wanajikita kwanza kwenye masuala kama ya ajira, afya, kilimo na mengineyo kabla ya kuhusisha na hali ya kisiasa. Lakini tabaka la wavunajasho/walalaheri lenyewe linasukumwa zaidi na maslahi ya kisiasa na ulinzi wa mali zao.

Kwa maana hiyo basi, katiba yenyewe si kani ya mabadiliko. Mabadiliko ya kweli siku zote yanaletwa na mapambano ya kujenga mfumo wa uchumi ambao unajali walio wengi.

Sasa katika mfumo wa uchumi wa kibepari hususan kwa nchi za pembezoni (zinazoendelea), hata katiba iwe bora kiasi gani haitaweza kuleta nafuu kwa jamii. Kwa nini? Kwa sababu mfumo huu uliopo wa kibepari umekuwa haugusi walio wengi/walalahoi kutokana na namna yake ya kuneemesha wachache/walalaheri kupitia ufukara wa wengi.

Hivyo, wadau mbalimbali kama wanaharakati wanapaswa kuliona hilo na kujadili mvutano uliopo ambao hauzungumzwi na makundi yote – mvutano wa walalahoi na walalaheri kuhusu maslahi ya katiba.

Walalahoi hawahitaji kuona maandishi ya katiba kama maneno matamu. Wanahitaji kuona kwa vitendo katiba ikifanya huduma za kijamii kuwa sio biashara, bali kuwa haki ya asili ya binadamu. Vile vile ukatiba wa aina hiyo utafanya umiliki wa ardhi usiamuliwe na pesa, upatikanaji wa matibabu usiamuliwe na pesa, upatikanaji wa elimu bora nao usiamuliwe na pesa, bali mahitaji haya yapatikane kwa kila binadamu bila kujali hali yake ya kiuchumi.

Lakini walalaheri hoja hii hapa juu sio ajenda kwao, kwa sababu wao ni wanufaika wa kuuzwa kwa elimu, afya, maji, na huduma nyingine za jamii.

Ni rai yangu kwamba, watu waelewe mjadala wa katiba ni muhimu lakini sio suluhu ya mwisho katika kumkomboa mwananchi. Hii ni kwa sababu katiba ni mapambano ya kitabaka, sio mkataba kati ya watawala na watawaliwa. Ndio maana nasema hakuna budi kupigania mfumo wa uchumi utakaoelekeza katika kutetea maslahi ya walio wengi/tabaka la walalahoi katika nyanja zote, na katiba kuwa sehemu tu ya hayo mapambano ya wavujajasho.

Hakimiliki

Udadisi imetumia vibonzo kwa hisani ya Mchora Katuni Masoud Kipanya.