Mapenzi Mubashara: Mama Sele, washa!
Muhidin J. Shangwe
Lakini leo nililielewa tofauti.
Nitarejea tangazo hilo kwa nukuu ambazo si rasmi bila kupotosha maana/ujumbe. Nafanya hivi kwa sababu, mosi, sikumbuki neno hadi neno kwenye tangazo husika (lakini nakumbuka ujumbe), pili, nina jambo nataka kulieleza.
Ningeweza kusubiri hadi tangazo hilo lirushwe tena ili ninukuu kiufasaha lakini nina dukuduku ambalo siwezi kusubiri kulisema. Hivyo mniwie radhi pale ambapo sijanukuu kwa ufasaha.
Kwenye tangazo hili inasikika sauti ya mwanaume mwenye lafudhi ya Kichaga. Anaitwa Baba Sele.
Baba Sele anamtaka mkewe, Mama Sele, awashe redio ili asikilize kipindi cha Leo Tena. “Mama Sele, washa!” anasikika mwanaume huyo kwa takribani mara tatu, akirudia rudia wito wake huo.
Wakati wote huo Mama Sele anaonekana kutoelewa mumewe anataka nini. “Niwashe nini?” anahoji. Kisha analalamika, “Niwashe nini jamani? Si unaona nafua nguo, na kule mtoto analia? Au kwa sababu bado sijapika chakula?”
Baba Sele yeye hana habari, anaendelea tu, “Mama Sele, washa!” Mwisho, Mama Sele anagundua mumewe anamtaka awashe redio ili tu asikilize kipindi cha Leo Tena! Mama Sele anawasha redio na mumewe anafurahi!
Tangazo hili linaweza kuonekana ni la kawaida tu. Na wengi hubaki kucheka lafudhi ya Kichaga ya Baba Sele – na inawezekana kabisa aliyetengeneza tangazo alilenga hilo tu. Hata Baba Sele haongei kwa ukali kwa maana ya kuamrisha.
Lakini kuna kitu cha ziada, na kinahusu taswira inayojengwa na tangazo husika. Ni taswira ya mfumo-dume.
Baba Sele amewasilishwa kama mwanaume ambaye “amekaa tu.” Unaweza kusema ni mwanaume ambaye akiwa nyumbani hana kazi zaidi ya kuketi kwenye sofa au kivulini na msuli wake, miguu juu, huku akisikiliza redio.
Mama Sele kwa upande wake ni kila kitu. Ni mfua nguo. Ni mbembelezaji mtoto. Ni mpishi. Na kama hiyo haitoshi, ni mwasha redio!
Ni hivi: Mama Sele afue nguo, abembeleze mtoto anayelia, bado aamuriwe kuwasha redio na mumewe ambaye tangazo linajenga taswira amekaa tu!
Hii si taswira ngeni kwenye familia zetu na jamii yetu kwa ujumla. Na huwa tunathubutu kusema hayo ni majukumu ya mama! Mtazamo huu ni hasi na hauendani na zama tulizo nazo.
Hizi ni zama ambazo, wakati Mama Sele anafua, Baba Sele alitakiwa ambembeleze mtoto, na pengine aingie jikoni kupika ili Mama Sele akimaliza kufua afike mezani wale. Au kama Mama Sele yu apika jikoni, basi Baba Sele afue nguo na/au ambembeleze mtoto.
Ni zama za kusaidiana majukumu majumbani na kwingineko. Na haya ndiyo Mapenzi Mubashara (Kaulimbiu ya Siku ya Wapendanao kama inavyochagizwa na Clouds Media Group).
Tangazo hili, kisanii, linaakisi jamii yetu ilivyo. Na ndiyo maana wengi wetu hatuoni kasoro hii ninayoieleza hapa. Lakini vyombo vya habari na sanaa kwa ujumla vina jukumu kubwa zaidi ya kuelezea tu jamii yetu ilivyo. Ni jukumu la kwenda mbele zaidi na kutafuta suluhisho, na pia kusema hili ni sahihi na lile si sahihi.
Sanaa na vyombo vya habari haviwezi kujificha nyuma ya kivuli cha kufichua tu yanayojiri kwenye jamii. Vinatakiwa vituongoze katika namna ya kuleta mabadiliko chanya ya kifikra.
Kuelezea tu namna jamii ilivyo bila kuonesha njia sahihi ni kupigia chapuo mila na desturi mbaya au zilizopitwa na wakati.